|
Mheshimiwa Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akipokelewa na maua na Mheshimiwa Matilda Masuka, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Jamhuri ya Korea Kusini. Kushoto ni Ndugu Masuka, mume wa Balozi Masuka. |
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
ZIARA YA WAZIRI MAHIGA KOREA KUSINI KUKUZA DIPLOMASIA YA UCHUMI
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt.
Augustine Mahiga ameanza ziara ya kikazi ya siku tatu nchini Jamhuri ya Korea
Kusini yenye lengo la kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi baina ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Korea ya Kusini.
Mara
baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Incheon Mjini Seoul,
Mheshimiwa Waziri Mahiga amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa
Makampuni ya GS E&C Bw. Min Jeong na timu yake inayoshugulikia uwekezaji na
biashara nchini Tanzania.
Waziri
Mahiga aliyeongozana na Bw. Edwin Rutageruka, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara (TANTRADE) na
Bw. Geoffrey Mwambe, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji cha Tanzania alielezea utayari wa Tanzania
kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo kama ule wa ujenzi wa reli ya kisasa ya
viwango vya kimataifa wa “Standard Gauge
Railway” inayohusisha makampuni makubwa ya kimataifa.
Kwa
upande wake Mkurugenzi Jeong alielezea kuwa Kampuni ya GS E&C iliyojikita
kwenye ujenzi wa miundombinu ya viwango vya kimataifa, ufuaji na usambazaji wa
umeme, usafishaji wa mafuta n.k., sasa imejipanga pia kushiriki katika Ujenzi
wa SGR (kupitia ushirikiano na kampuni ya Uturuki (awamu ya 3-5), na Ujenzi wa Daraja
la Selanda.
Mbali
na mpango huo, kwa sasa Kampuni hiyo yenye makao yake makuu kwenye mji mkuu wa Korea
Kusini, Seoul, imeshiriki katika Mradi ya Umeme nchini Tanzania wa Dar-Arusha “Transmition
Line”.
Waziri
Mahiga alisisitiza nia ya dhati ya Serikali ya Tanzania katika kusimamia ujenzi
wa Reli ya Kisasa ya Viwango na kuhakikisha inakamilika kwa wakati. Vilevile
alitumia fursa hiyo kumuelezea Mkurugenzi Jeong na timu yake kuhusu mpango wa
uendelezaji wa ujenzi wa reli hiyo ya viwango kutoka Isaka hadi Kigali, mpango
ambao ulitangazwa na Waheshimiwa John Pombe Joseph Magufuli na Mheshimiwa Paul
Kagame, Rais wa Tanzania na Rwanda hivi karibuni.
Mheshimiwa
Mahiga alimhakikishia mkurugenzi huyo na kundi la makampuni anayoyaongoza, ushirikiano
wake na kumkaribisha kuwekeza zaidi nchini Tanzania kwenye miradi mbalimbali ya
umeme na miundombinu mingine.
Kampuni
ya GS E&C ni miongoni mwa makampuni kumi “Top Ten” yanayofanya vizuri zaidi nchini Korea Kusini inayokusanya
faida ya kiasi cha $10 bilioni kwa mwaka.
Mheshimiwa
Waziri Mahiga ambaye yupo nchini hapa kuanzia leo tarehe 30 Januari hadi tarehe
2 Februari, 2018, kufuatia mwaliko wa Mhe. Dkt. Kang Kyung-wha, Waziri wa Mambo
ya Nje wa Jamhuri ya Korea anatarajiwa pia kuzindua Kongamano la kwanza la
wafanyabiashara, kufungua majengo ya Ubalozi wa Tanzania na kufanya mazungumzo
maalum na mwenyeji wake Waziri Kang Kyung-wha.
Mheshimiwa
Mahiga atatumia sehemu kubwa ya ziara hiyo kukutana na kufanya mazungumzo na
makampuni makubwa yalikwisha onesha nia ya kuwekeza nchini Tanzania. Mwishoni
mwa ziara hiyo, Mheshimiwa Waziri Mahiga anategemewa kutembelea Chuo cha Taifa
cha Diploamasia cha Korea Kusini, kabla ya kurejea nchini Tanzania.
-Mwisho-
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Seoul,
Korea Kusini,
|
Mheshimiwa Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akisalimiana na wawakilishi wa kampuni ya GS E&C waliofika hotelini kwake na kufanya naye mazungumzo ya kikazi kwenye Mji Mkuu wa Jamhuri ya Korea, Seoul. Pichani wawili ni Mkurugenzi Mkuu wa Makampuni hayo Bw. Min Jeoung. |
|
Ujumbe wa Mheshimiwa Mahiga ukiongozwa na Mheshimiwa Matilda Masuka, Balozi wa Tanzania nchini Korea Kusini, Bw. Geoffrey Mwambe, Mkurugenzi Mtendaji wa TIC na Bw. Edwin Rutageruka, Mkurugenzi Mkuu wa TANTRADE wakiwa kwenye mazungumzo na wawakilishi wa makampuni ya GS E&C. |
|
Picha ya Pamoja |