Thursday, March 29, 2018
Wednesday, March 28, 2018
UBALOZI WA TANZANIA NCHINI UHOLANZI WASHIRIKI MAADHIMISHO YA SIKU YA MAJI DUNIANI
Wanafunzi wa Shule za Msingi mbalimbali
mjini Gouda,
wakishiriki matembezi huku kila mmoja akiwa amebeba mgongoni lita 6 za maji kila mmoja. |
Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi, Mhe.Irene Kasyanju
akikaribishwa Gouda na Bibi Rola Hulsbergen, Mwenyekiti wa Rotary Club ya nchini Uholanzi |
Meya wa
Wanafunzi wa Gouda,
Bi. Romaissa Magou (kulia) akimkabidhi Balozi Kasyanju mfano wa Hundi ya kiasi cha fedha kilichokusanywa baada ya matembezi hayo. |
Balozi Kasyanju na Bibi Hulsbergen
wakisikiliza kwa makini
shairi kuhusu Tanzania lililoandaliwa na wanafunzi wa Gouda. ===================================================== |
UBALOZI WA TANZANIA NCHINI UHOLANZI WASHIRIKI KWENYE MAADHIMISHO YA SIKU YA MAJI DUNIANI
YALIYOFANYIKA MJINI GOUDA, UHOLANZI TAREHE 21 MACHI 2018
Katika kuadhimisha Siku ya Maji Duniani, Manispaa ya mji wa Gouda nchini Uholanzi, kwa
kushirikiana na Taasisi za Rotary
na shule za msingi za mji huo zilimwalika Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi, Mhe. Irene Kasyanju kushiriki katika matembezi ya hisani maarufu kama Walking for Water yaliyoandaliwa kwa lengo la kuisaidia Tanzania katika kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa maji safi inayowakabili watoto katika nchi zinazoendelea.
Matembezi hayo yalishirikisha walimu, wazazi na wanafunzi wa shule za
msingi za mjini Gouda ambao walitembea umbali wa kilometa 6 huku kila mmoja akiwa amebeba
lita sita (6) za maji kuashiria kutambua changamoto kubwa ya ukosefu wa
maji safi inayowakabili watoto, hususan katika Nchi Zinazoendelea ikiwemo
Tanzania.
Maadhimisho ya Siku hii kwa mwaka huu, yalilenga kuisaidia Tanzania ambapo
sambamba na matembezi hayo, kiasi cha Euro 24,021.29 kutoka mji wa Gouda kilichangwa kwa ajili ya kusaidia miradi ya afya na ujenzi wa vyoo
inayoendeshwa katika Mikoa ya Tabora na Dodoma. Mhe. Balozi Irene Kasyanju
alikabidhiwa mfano wa Hundi ya kiasi hicho cha fedha kilichokusanywa kutokana
na michango ya Taasisi husika, wazazi wa wanafunzi na wadau mbalimbali.
Akipokea mfano wa Hundi hiyo Mhe. Balozi Irene Kasyanju, kwa niaba ya wananchi
na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alitoa shukrani za dhati kwa waandaaji,
wadhamini na hususan wanafunzi kwa matembezi pamoja na mchango huo mkubwa na
kueleza kuwa utasaidia kubadilisha maisha ya watoto na wananchi wa maeneo
husika kwa ujumla. Aidha, Mhe. Balozi Kasyanju alisisitiza umuhimu wa matumizi
makini ya maji kwani maji ni muhimu kwa viumbe pamoja na mimea.
Jumla ya kiasi cha Euro 360,000.00 kinatarajiwa kukusanywa kutokana na
michango iliyotolewa kutokana na matembezi kama hayo katika miji mingine ya
Uholanzi siku hiyo pamoja na Serikali ya Uholanzi kuisaidia Tanzania hususan
kwenye mikoa tajwa.