Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akipokea Hati za utambulisho kutoka kwa Balozi mteule wa Kenya hapa nchini Dan Kazungu Ikulu jijini Dar es Salaam leo Julai 30, 2018 |
Monday, July 30, 2018
Balozi Mpya wa Kenya nchini Mhe. Dan Kazungu akabidhi Hati za utambulisho
Saturday, July 28, 2018
TAARIFA KUHUSU MATOKEO YA AWALI YA NAFASI ZA AJIRA ZA SADC
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
KUHUSU MATOKEO YA AWALI YA NAFASI ZA AJIRA
KATIKA SEKRETARIATI YA SADC ZILIZOTANGAZWA
KWA MWAKA 2018
Sekretarieti ya SADC
ilitangaza nafasi 50 katika kada mbalimbali mwezi wa Mei, 2018. Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, Menejimenti na Utumishi ilitangaza
nafasi hizo kupitia vyombo mbalimbali vya habari.
Wizara inapenda kuutangazia
umma kuwa baada ya mchujo wa duru ya kwanza uliofanywa na Kikosi Kazi Maalum,
jumla ya waombaji 141 kati ya waombaji 1,472 wamepita katika uchambuzi wa
awali. Katika muktadha huo, Wizara inaweka orodha ya awali ya mchujo wa
Tanzania ya waombaji waliochaguliwa katika nafasi mbalimbali pamoja na jedwali lenye
kuonyesha idadi ya waombaji hao.
Wizara inapenda kuutaarifu
umma na waombaji wa nafasi za ajira zilizotangazwa na SADC kuwa taarifa zaidi
itatolewa Sekretarieti ya SADC kwa wale tu watakao kuwa kwenye orodha ya mchujo
wa duru ya pili (shortlisted) utakayofanywa na Sekretarieti ya SADC.
Aidha, tutakumbuka kuwa mwezi wa Mei, 2017 Sekretarieti ya SADC
ilitangaza nafasi 48 ambapo zoezi la usaili wake lilikamilika mwaka huu. Kwenye
nafasi 48, Tanzania imefanikiwa kupata nafasi tano za kimkakati. Nafasi hizo
zinaainishwa kama ifuatazo:
i.
Afisa Mwandamizi anayeshughulikia masuala ya
Sera na Mikakati ya Maendeleo, (Senior Officer - Policy and Strategy Development);
ii.
Afisa Mwandamizi Mipango anayeshughulikia
masuala ya Viwanda na Ushindani, (Senior Programme Officer - Industrialization and
Competitiveness);
iii.
Afisa Mipango anayeshughulikia masuala ya Ushuru
na Utaratibu, (Programme Officer
Customs and Procedures);
iv.
Afisa anayeshughulikia masuala ya Ufuatiliaji,
Tathmini na utoaji wa Taarifa, (Monitoring, Evaluation and Reporting Officer); na
v.
Afisa anayeshughulikia masuala ya Fedha na
Bajeti, (Finance Officer -
Treasury and Budget )
Tunawapongeza kwa dhati wote waliochaguliwa na
kufanikiwa kuingia kwenye orodha ya mchujo wa awali uliofanyika Tanzania kwa
mwaka 2018.
Aidha, kwa aina ya pekee, tunawapongeza maafisa
waliochaguliwa kwenye nafasi tano (5) zilizotajwa na tunawatakia kila la heri
katika mjukumu yao mapya sambamba na kuwasihi daima kukumbuka kuwa
wanaliwakilisha Taifa letu kwenye nafasi hizo.
Mwisho, Wizara inapenda kutaarifu kuwa
itaendelea kuzitangaza fursa kama hizi zitapojitokeza kupitia SADC na Jumuiya
zingine za Kikanda na Kimataifa ambazo Tanzania ni nchi mwanachama, kwa manufaa
ya watanzania wote. Hivyo, tunawaomba Watanzania wasikate tamaa na wasisite
kuwasilisha maombi ya ajira kama hizi pale fursa zinapojitokeza.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam,
27 Julai, 2018
Tuesday, July 24, 2018
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU ZIARA YA MKURUGENZI WA WFP NCHINI
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango
wa Chakula Duniani (WFP), Bw. David M. Baesley atafanya ziara ya kikazi nchini
kuanzia tarehe 25 Julai 2018 hadi tarehe 03 Agosti 2018. Ziara hiyo pamoja na
mambo mengine inalenga kuimarisha mahusiano mazuri yaliyopo kati ya Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na WFP.
Wakati wa ziara hiyo nchini, Bw. Baesley ataonana na kufanya
mazungumzo na viongozi mbalimbali wa kitaifa kwa lengo la kujadiliana nao
kuhusu maeneo ya ushirikiano kati ya WFP na wakulima wadogo kupitia mpango wa “Social Protection Programmes”; Mfumo wa
Serikali wa Usalama wa Chakula; na masuala ya Wakimbizi na Jamii zinazozunguka
hifadhi za wakimbizi pamoja na njia za kukabiliana na changamoto mbalimbali
zinazowakabili.
Bw. Baesley anatarajiwa kuwasili nchini tarehe 25 Julai,
2018 kwa ajili ya kuanza ziara hiyo.
Imetolewa
na:
Kitengo
cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dodoma.
24 Julai 2018
Balozi Mabumba awasisitiza Watanzania waishio nchini Comoro (TADICO) kuwekeza nyumbani
Balozi wa Tanzania Visiwani Komoro Mhe. Sylvester Mabumba alikutana na kufanya mazungumzo na uongozi mpya wa Diaspora ya Watanzania waishio Komoro (TADICO) tarehe 23 Julai 2018. Viongozi hao wapya walifika ofisi za Ubalozi kwa ajili ya kujitambulisha ambapo miongoni mwa mambo waliyojadili ni pamoja na kutoa ahadi ya kuinua Diaspora ya Watanzania waishio Comoro ambapo kwa muda mrefu Diaspora hiyo imeonekana kuwa nyuma kimaendeleo ikilinganishwa na Diaspora za nchi nyingine.
Kwa upande wake Mhe. Balozi Mabumba alichukua fursa hiyo kuwapongeza viongozi hao wapya waliochaguliwa pamoja na kuwatakia kila la kheri katika nafasi zao hizo mpya walizoaminiwa na Watanzania wenzao. Aidha, Mhe. Mabumba alisisitiza juu ya umuhimu wa wanachama kulipa michango ya uanachama na vilevile kuwaomba viongozi kuwa wasimamizi wazuri wa matumizi ya fedha za wanachama hao.
Katika hatua za kuhuisha chama hicho wajumbe walishauriwa pia kuwa wabunifu katika mikakati yao na vilevile waangalie njia gani bora za kuibua vyanzo vipya vya mapato badala ya kutegemea michango ya wanachama pekee. Pia Balozi Mabumba aliwahimiza viongozi hao kutosahau kuwekeza nyumbani na vilevile kuchangamkia fursa za biashara ambazo zinapatikana Tanzania na kuzitangaza Visiwani humo.
Viongozi wakiwa katika picha ya pamoja. |
Monday, July 23, 2018
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU ZIARA YA MHE. MKAPA NCHINI MSUMBIJI
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Maadhimisho ya Miaka 50 ya Mkutano wa Pili wa Chama Tawala
cha Msumbiji FRELIMO yatafanyika katika Jimbo la Niassa nchini Msumbiji tarehe
25 Julai 2018. Rais wa Jamhuri ya Msumbiji, Mhe. Filipe Nyusi alimwalika Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM),
Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kushiriki maadhimisho hayo. Kutokana na majukumu
mengine ya kitaifa Mhe. Rais Magufuli hatoweza kushiriki. Hivyo, kwa kuona
umuhimu wa mahusiano kati ya Tanzania na Msumbiji na umuhimu wa maadhimisho
hayo kwa historia ya nchi hizi mbili, amemteua Rais Mstaafu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Benjamin William Mkapa amwakilishe kwenye sherehe
hizo na ataambatana na Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (Bara), Mhe.
Philip Mangula.
Mahusiano kati ya Tanzania na
Msumbiji
Mahusiano kati
ya Tanzania na Msumbiji ni mazuri
na yamekuwa yakiimarika kila wakati. Mahusiano kati ya nchi hizi yalianza enzi za harakati za ukombozi dhidi ya ukoloni wa
Kireno nchini Msumbiji. Mahusiano hayo yalijengwa na waanzilishi wa mataifa
haya mawili, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Samora Moises
Machel na yameendelea kuwa mazuri siku hadi siku na kuendelezwa na Viongozi wote
Wakuu waliofuata wa nchi hizi mbili. Ziara za Viongozi wa ngazi
mbalimbali wa Serikali na vyama tawala vya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na FRELIMO
wameendelea kutembeleana na kudumisha uhusiano huo.
Ushirikiano
katika Chuo cha Diplomasia (Mozambique - Tanzania Centre for Foreign Relations
(CFR)
Chuo cha Diplomasia
(Mozambique-Tanzania Centre for Foreign Relations – CFR) kilichopo Kurasini
jijini Dar es Salaam ni moja ya alama
muhimu za ushirikiano kati ya Tanzania na Msumbiji. Chuo cha Diplomasia
kilianzishwa mwaka 1978, kwa makubaliano ya nchi za Tanzania na Mozambique.
Chuo hichi kilianzishwa kwa lengo la kutoa mafunzo kwa Maafisa wa Mambo ya Nje
kutoka katika nchi hizi mbili katika taaluma ya Mahusiano ya Kimataifa na
Diplomasia.
Awali, kabla ya
kubadilishwa kuwa Chuo cha Diplomasia, ilikuwa ni kituo cha harakati za
kupigania uhuru wa Msumbiji. Hivyo, katika harakati za Ukombozi kutoka kwa
wakoloni, wapigania uhuru wa kutoka Msumbiji wakiongozwa na Hayati Eduardo
Mondlane waliweka kambi chuoni hapo na kuanzisha chama cha Ukombozi cha FRELIMO
mnamo mwaka 1962. Mwaka 1970 Hayati Samora Machel alishika madaraka ya kukiongoza
chama hicho baada ya kuuawa kwa Mhe. Mondlane
Ushirikiano wa kiuchumi na
kibiashara
Tanzania na
Msumbiji zimeendelea kushirikiana katika masuala ya kiuchumi na biashara kwa
kuzingatia ujirani na muingiliano mkubwa wa wananchi wa nchi hizi mbili, hususan katika Mikoa ya Ruvuma na Mtwara kwa upande
wa Tanzania, na Majimbo ya Niassa na Cabo Delgado kwa upande wa Msumbiji. Tanzania na Msumbiji zinauziana bidhaa
mbalimbali za kilimo na viwandani.
Kadhalika kuna Makampuni makubwa
kadhaa ya Kitanzania yaliyowekeza mitaji mikubwa nchini Msumbiji. Vile vile, wapo Watanzania wanaomiliki
makampuni ya usafirishaji wa abiria na biashara za kati na ndogo. Ili kuhakikisha kuwa kunakuwepo
na misingi imara ya kuendeleza mahusiano mazuri yaliyopo kati ya nchi hizi
mbili, Tanzania na Msumbiji ziliamua kujenga Daraja la Umoja linaloziunganisha
nchi hizo kwenye mpaka wa Mto Ruvuma ili kuboresha na kuimarisha mahusiano ya
kiuchumi.
Mhe.
Mkapa na Ujumbe wake wanatarajia kuondoka nchini tarehe 24 Julai, 2018 na
kurejea tarehe 26 Julai, 2018.
Imetolewa
na:
Kitengo
cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dodoma.
23 Julai 2018
Naibu Katibu Mkuu wa Mambo ya Nje aongoza maadhimisho ya siku ya Taifa la Misri
Picha ya pamoja |