TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Finland
yaipongeza Tanzania vita dhidi ya Rushwa.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Finland, Mhe. Timo Soini.amepongeza
jitihada zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe. Dkt.
John Pombe Joseph Magufuli za kupambana na rushwa na kusimamia uwajibikaji.
Pongezi hizo alizitoa wakati alipofanya mazungumzo
na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt.
Augustine Mahiga ambaye yupo nchini Finland kwa ziara ya kikazi ya siku mbili
tarehe 25 na 26 Februari 2019.
Kwenye mazungumzo yao, Mawaziri hao wamesisitiza
umuhimu wa Tanzania na Finland kuboresha ushirikiano kwenye sekta mbalimbali
zikiwemo za biashara, uwekezaji, mafunzo ya ufundi, ajira kupitia sekta ya
misitu, ushirikiano katika majukwaa ya kimataifa kwa kuzingatia usawa, pamoja
na kuwajengea uwezo wanawake na watoto.
Aidha, Mhe. Soini
alitoa shukrani zake za dhati kwa Serikali ya Tanzania kwa kuendelea
kuhifadhi wakimbizi na mchango mkubwa katika usuluhishi wa migogoro inayozikabili
baadhi ya nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu. Hivyo, walikubaliana kuendelea
kushirikiana katika kukabiliana na changamoto mbalimbali za kiusalama ikiwa ni
pamoja na biashara ya madawa ya kulevya, biashara haramu ya kusafirisha
binadamu, na matishio ya ugaidi.
Kabla
ya mazungumzo hayo, Mhe. Balozi Mahiga alikutana na kufanya mazungumzo na Bw.
Sampo Suihko, Mkurugenzi Mkuu wa Chuo cha OMNIA Espoo ambaye alieleza utayari
wa Taasisi yake wa kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kubadilishana
uzoefu wa kutoa mafunzo ya elimu ya ufundi yanayoendana na soko la ajira.
Mhe.
Mahiga pia alifanya mazungumzo na Mhe. Matti Ahtisaari, Rais Mstaafu wa Finland
na Mwanzilishi wa Taasisi ya Utatuzi wa Migogoro. Mhe. Ahtisaari aliipongeza
Tanzania kwa kazi nzuri inayofanya katika utatuzi wa migogoro kwenye nchi za
Ukanda wa Maziwa Makuu na kusihi kuendeleza jitihada hizo kwa ustawi wa Dunia
nzima.
Vilevile,
Dkt. Mahiga alifanya mazungumzo na Bw. Jukka Kallio, Makamu wa Rais wa
Helsinki. Katika mazungumzo hayo, uongozi wa Bandari ya Vuosaari umeahidi
kushirikiana na uongozi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania katika kuboresha mifumo
ya kidigitali (Digitalization) itakayoongeza
ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam.
Katika
kuhamasisha uwekezaji wa viwanda nchini, Mhe. Waziri Mahiga alifanya mazungumzo
na Jumuiya ya Wafanyabiashara (Business
Finland) na Makampuni makubwa ya kibiashara nchini humo. Wafanyabiasha hao
walipongeza jitihada zinazoendelea kufanyika nchini Tanzania katika kuboresha
mazingira ya biashara na uwekezaji na
waliahidi kuwekeza na kushawishi makampuni mengine kuona umuhimu wa
kuwekeza nchini Tanzania.
Mhe.
Waziri anahitimisha ziara hiyo kwa kufanya mazungumzo na Bi. Anne-Mari
Virolainen, Waziri wa Biashara na Maendeleo wa Finland; Bw. Mauri Pekkarinen,
Naibu Spika wa Bunge la Finland, Bw. Juhan Damski, Mkurugenzi Mkuu wa
Taasisi ya Utabiri wa Hali ya Hewa ya
nchini Finland na baadaye kuzungumza na Kamati ya Mambo ya Nje ya Bunge la
Finland.
Imetolewa
na:
Kitengo
cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki,
Dodoma.
26 Februari
2019
|