Tanzania na India zimeahidi
kuendeleza uhusiano wa kidiplomasia pamoja na kushirikiana katika kuhakikisha kuwa na maendeleo
endelevu baina ya nchi hizo mbili.
Akihutubia sherehe za
maadhimisho ya 71 ya Jamhuri ya India, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) amesema kuwa Tanzania
na India ni ndugu na nchi hizo zitaendelea kushikiana katika kuhakikisha kuwa maendeleo
ya diplomasia ya uchumi baina ya nchi hizo yanakuwa kila wakati.
"Nchi ya Tanzania
na India zina uhusiano mzuri, imara na wa muda mrefu ulianzishwa na baba wa
Taifa Mwl. Julias Nyerere pamoja na Mahatma Gandhi. Na uhusiano huu umekuwa
ukisaidia kuimarisha maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa" alisema
Dkt. Ndumbaro
Dkt. Ndumbaro aliongeza
kuwa "sisi Tanzania na India ni ndugu, kwa hiyo basi tunawatakia sana kila
la kheri katika kuiletea India maendeleo…lakini pia tukumbuke kuwa maendeleo ya
India ni maendeleo ya Tanzania pia,"
Kwa sasa uchumi wa
India na Tanzania umezidi kukuwa na kuendelea kuimarisha mahusiano ya
kidiplomasia baina ya mataifa hayo. India imekuwa msharika mzuri wa maendeleo
nchini Tanzania katika sekta mbalimbali ikiwemo utalii, maji, afya, teknolojia
na elimu. Msaada wa India katika sekta ya maji hadi sasa, imeweza kusaidia
kusambaza maji safi na salama katika kwa jiji la Dar es Salaam pamoja na
upanuzi na uboreshaji wa mitambo ya maji Zanzibar.
Aidha, kwa upande wa
sekta ya elimu, Tanzania na India zimeshasaini makubaliano ya kushirikiana
kujenga kituo cha ufundi na pia msaada wa kuendeleza vyuo vikuu vya Zanzibar
ambavyo vinatoa ujuzi unaolengwa kuwaendeleza wanawake walio na elimu ndogo au
isiyo rasmi.
Kwa upande wake,
Balozi wa India chini Tanzania, Mhe. Balozi Shri Sanjiv Kohli ameishukuru
Serikali ya Tanzania kwa umoja na mshikamano ambao imekuwa ikionesha kwa India na
kusema kuwa umoja huo umekuwa ni chachu ya maendeleo kwa Tanzania na Taifa la
India.
"Napenda
kuwafahamisha kuwa umoja na mshikamano wetu umekuwa chachu ya maendeleo baina
ya mataifa haya mawili…..tukumbuke kuwa umoja ni nguvu na dhamira yetu ni
kushirikiana na mataifa yote duniani. Na dhamira yetu ni kuishi kwa amani umoja
na mshikamano ili kukuza uchumi wetu," Alisema Balozi Kohli
Aidha, Balozi Kohli
amebainisha kuwa Tanzania itaendelea kuwa ya kipekee kwa taifa la India kutokana
na mshikamano ambao imekuwa ikionesha kwa nchi ya India kijamii, kisiasa na
kiuchumi.
"India inajivunia
kuwa na uhusiano na mzuri na Tanzania ambao umewezesha mataifa haya kufanya
biashara, uwekezaji, kujenga uwezo, ujenzi wa miundiombinu pamoja na maendeleo
ya kiuchumi," ameongeza Balozi Kohli.
Balozi
wa India nchini Tanzania, Mhe. Balozi Shri Sanjiv Kohli akihutubia wageni
waalikwa (hawapo pichani) wakati wa maadhimisho ya miaka 71 ya Jamhuri ya India
yaliyofanyika mwishoni mwa wiki katika ofisi za Ubalozi wa India jijini
Dar es Salaam. Kulia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro.
|
Naibu
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro (Mb)
akiwasilisha hotuba yake wakati wa maadhimisho ya miaka 71 ya Jamhuri ya India yaliyofanyika katika ofisi za Ubalozi wa India mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam. Kulia kwake ni Balozi wa India nchini
Tanzania, Kohli
|
|
Baadhi
ya wageni waalikwa wakifuatilia/kusikiliza hotuba ya mgeni rasmi (Dkt.
Ndumbaro) hayupo pichani wakati wa sherehe za maadhimisho ya miaka 71 ya
Jamhuri ya India yaliyofanyika mwishoni mwa wiki katika ofisi za Ubalozi wa India jijini Dar es Salaam
|