MWONGOZO WA USAFIRISHAJI WA BIDHAA MUHIMU NA HUDUMA KATIKA NCHI ZA SADC KWA KIPINDI HIKI CHA JANGA LA VIRUSI VYA CORONA (COVID – 19)
23 APRILI, 2020, DODOMA
Tarehe 6 Aprili, 2020 ulifanyika Mkutano wa Dharura wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC). Mkutano huo ulijadili janga la mlipuko wa ugonjwa wa homa kali ya mapafu (COVID-19) unaosababishwa na virusi vya Corona. Mkutano huo ulihusisha Mawaziri wenye dhamana ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Fedha,Viwanda,Biashara, Utalii, Mambo ya Ndani na Uchukuzi, kutoka nchi 16 wanachama wa SADC ambazo ni Angola, Botswana, Malawi, Mauritius, Msumbiji, Namibia, Jamhuri ya Visiwa vya Ushelisheli, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Zambia.
Katika mkutano huo, Baraza la Mawaziri lilitoa mwongozo kuhusu Usafirishaji wa Bidhaa Muhimu na Huduma Katika Nchi za SADC katika kipindi hiki cha janga la Virusi vya Corona. Mwongozo huu utatumika katika kipindi hiki unalenga kupunguza safari zisizo za lazima na usafirishaji wa bidhaa ambazo ni za muhimu tu na unazitaka Nchi Wanachama kuzingatia na kutekeleza sera na miongozo mbalimbali iliyotolewa na inayoendelea kutolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO), Shirika la Forodha Duniani (WCO), Shirika la Usafiri wa Anga Duniani (ICAO) na Shirika la Usafiri wa Maji Duniani (IMO).
Kwa mujibu wa Muongozo huo Malori na magari yatakayoruhusiwa kusafirisha mizigo ni yale yatakayobeba bidhaa za Vyakula; Vifaa tiba na Dawa, vifaa binafsi vya kujikinga; Mafuta na makaa ya mawe; Pembejeo za kilimo; vifungashio, vipuri vya magari na mashine.
Raia wanaorejea katika nchi zao wanatakiwa kuzingatia sheria za nchi zilizowekwa za kupimwa na ikiwa atagundulika mgonjwa mwenye Virusi vya Corona, atatakiwa kutengwa kwa kuwekwa kizuizini kwa muda uliowekwa; Kupunguza idadi ya wasafiri katika mabasi na vyombo vingine vya usafiri; Kutumia miongozo ya WHO ya usafi katika vyombo vya usafiri, vituo vya mabasi na maeneo mengine ambayo mabasi yatasimama; Madereva/waendeshaji kutoa taarifa mbalimbali kuhusu njia za kupambana na COVID-19 kwa wasafiri katika lugha za wasafiri na; Kujaza fomu zinazohoji maeneo waliopita wasafiri na kuhakikisha fomu hizo zinawasilishwa kwa kituo cha maafisa afya.
Vyama vya wasafirishaji vinatakiwa Kushirikiana na maafisa afya kuandaa na kutekeleza programu ya uhamasishaji kwa wasafirishaji magari na waajiri wake;Kuwaelekeza madereva wa malori kujaza fomu maalum zinazoonyesha maeneo ambayo watapita, maeneo watakayosimama wakati wa safari na kituo cha mwisho cha safari ambazo zitawekwa katika ofisi za maafisa afya zilizopo mipakani ili kuweza kuwasiliana na kufuatilia madereva kwa uchunguzi;
Wasafirishaji magari wanatakiwa kushirikiana na Serikali kuangalia jinsi taarifa za gari zinavyoweza kutumika wakati wa kuifuatilia; Kuhakikisha madereva wanaovuka mipaka wanabeba sabuni na maji ya kunawa; Kuwaelekeza madereva kutobeba watu wasiohusika katika magari yao; Kuelekeza madereva wa malori kuzingatia umbali wa mita moja kati yao wakati wa safari; na; Kugawa vifaa maalum kwa wafanyakazi na waajiriwa ambao wapo katika mazingira hatarishi ya kupata maambukizi.
Madereva wa malori watalazimika kuweka bayana kituo cha mwisho cha safari yao na wanaaswa kusimama katika vituo maalum vilivyopangwa na endapo dereva au wahudumu wa chombo husika wataonesha dalili za kuugua COVID-19 lori hilo litalazimika kupitia hatua za usafishaji kabla ya kuruhusiwa kuendelea na safari, watoa huduma wa chombo hicho watengwa katika eneo maalum (Quarantine) au kupelekwa kituo cha matibabu kwa gharama zao; Mmiliki wa lori atalazimika kuandaa dereva na watoa huduma wengine ili kuwezesha bidhaa kufika mahali zilipokusudiwa.
Dereva na wasaidizi wake wakishusha mzigo watapaswa kukaa watengwa katika eneo maalum ( Quarantine) kwa siku 14 na kutofanya safari nyingine ya nje katika kipindi hicho na wataalamu wa afya waliopo mpakani mwa nchi husika watalazimika kuwasiliana kwa kina na wataalamu wa afya wa nchi mwenyeji wa lori husika ili kupata taarifa zitakazo saidia kuchukua hatua ya kuwatenga katika eneo maalum dereva na wasaidizi wake wakati wa kushusha au kupakia mzigo.
Vyombo vya usafiri wa majini kutoka nchi ambazo zipo hatarini zaidi katika maambukizi au zenye wasaidizi au abiria waliopo kwenye hali hatarishi zaidi ya maambukizi watalazimika kutengwa katika eneo maalum kwa siku 14 kwa gharama zao kabla ya kuruhusiwa kutoka eneo ambalo chombo hicho kilitia nanga na chombo kilichobeba abiria na wasaidizi walioathirika na COVID-19 hakitaruhusiwa kutia nanga.
Ndege zinazofanya safari katika maeneo mbalimbali zitalazimika kufuata hatua zote za usafishaji kwa kupuliziwa dawa na hatua zingine za kujikinga ambazo kila ndege iliyobeba abiria walioathirika au washukiwa wa COVID 19 inapaswa kuzipitia.
SADC ilikubaliana kuwa hakutakuwa na zuio dhidi ya wasafirishaji wa nje waliosajiliwa la kuingia nchi mwanachama endapo wanaendesha shughuli zao kwa kuzingatia taratibu, kanuni na sera za usalama za nchi husika.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali
WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI
|