Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax ameungana na familia, ndugu, jamaa na mamia ya waombolezaji katika mazishi ya aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Austria, Balozi Celestine J. Mushy yaliyofanyika nyumbani kwake katika Kijiji cha Sambarai, Tarafa ya Kibosho, Mkoni Kilimanjaro.
Akitoa Salamu za pole kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tax amesema Serikali inatambua mchango wa Marehemu Balozi Mushy katika sekta ya Diplomasia nchini na kwamba itauenzi na kusimamia yale yote aliyokuwa anayaamini katika kukuza na kuimarisha Diplomasia nchini.
Amesema marehemu ametoa mchango mkubwa katika kukuza diplomasia na kuimarisha uhusiano kati ya Tanzania na nchi mbalimbali na Mashirika ya Kimataifa.
Dkt. Tax amesema marehemu Balozi Mushy alikuwa Balozi wa kwanza kuhudumu katika Ubalozi mpya wa Tanzania nchini Austria, hivyo katika nafasi hiyo, aliweza kutekeleza vyema majukumu yake na kuimarisha uhusiano kati ya Tanzania na Austria na aliweza kutafuta na kuibua fursa za biashara na uwekezaji zilizopo nchini humo.
Ameongeza kusema Balozi Mushy aliweza kukuza na kuimarisha uhusiano kati ya Tanzania na Mashirika ya Umoja wa Mataifa yaliyopo Vienna, Austria, tangu ateuliwe kuwa Balozi wa Tanzania nchini Austria na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Ofisi za Umoja wa Mataifa Vienna.
“Kama ilivyo kwa Familia, Serikali, Watanzania na Dunia kwa ujumla tumepokea kwa mshtuko, simanzi na masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha Balozi Celestine Mushy. Mshtuko, simanzi na masikitiko yetu unatokana na ukweli kwamba kifo cha Balozi Mushy kimekuwa cha ghafla mno. Taifa bado lilikuwa linamhitaji sana,” alisema Dkt. Tax
Dkt. Tax amesema Wizara imeguswa na kifo cha Balozi Mushy kwani katika uhai wake alikuwa na mchango mkubwa kwa nchi katika maeneo mbalimbali.
Amesema Serikali imepoteza Kiongozi mnyenyekevu, mwenye upendo kwa watu wote, mchapakazi hodari, aliyejitoa kwa yeyote aliyehitaji msaada wake, na aliyekuwa na mchango mkubwa kwa Wizara na Taifa kwa ujumla.
Wakati huo huo, Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Kikwete aliyehudhuria mazishi ya Balozi Mushy amemuongelea marehemu kama mchapa kazi, mwenye weledi mkubwa na ambaye ameifanyia makubwa Tanzania.
“Nilimfahamu Balozi Mushy kama kijana hodari tangu alipoajiriwa katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa mwaka 1999, alikuwa kijana hodari, mchapa kazi na mwenye weledi. Ni kutokana na utendaji wake huo mzuri alipelekwa kama Afisa katika Ofisi ya Ubalozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa New York, Marekani.
Amesema Balozi Mushy alikuwa mbobezi na mahiri wa masuala ya diplomasia, lakini pia alikuwa mzalendo na alikuwa tayari kujitoa kwa ajili ya Tanzania na kuongeza kuwa hata alipoteuliwa na Rais Samia kuwa Balozi wa Tanzania Austria na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Ofisi ya Umoja wa Mataifa, Vienna niliona kuwa Mhe Rais amelenga mtu sahihi
Viongozi wengine walioungana na familia katika mazishi ya Balozi Mushy ni Naibu Waziri, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk, Katibu Mkuu, Balozi Joseph Sokoine, Menejimenti ya Wizara, mabalozi mbalimbali wanaoiwakilisha Tanzania Nje ya Nchi wakiongozwa na Amidi Mkuu na Balozi wa Tanzania nchini Uingereza Mhe. Dkt. Asha Rose Migiro, Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia, Mhe. Innocent Shiyo, Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mhe. Mahamoud Thabit Kombo, Balozi wa Tanzania nchini Misri, Mhe. Dkt. Emmanuel Nchimbi, Majaji, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo Nje, Ulinzi na Usalama Mhe. Vita Kawawa pamoja na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa Shaka Hamdu Shaka.
Januari, 2022 Marehemu Balozi Mushy aliteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Balozi wa Tanzania nchini Austria na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Ofisi za Umoja wa Mataifa Vienna.
Balozi Mushy alifariki dunia Desemba 12, 2022 katika ajali ya gari iliyotokea Mkata wilayani Handeni mkoa wa Tanga baada ya gari alilokuwa akisafiria kugongana na lori la mizigo na kuungua moto akiwa ndani.
|
Baadhi ya Viongozi mbalimbali waandamizi wa Serikali wakifuatilia ibada ya mazishi ya Marehemu Balozi Celestine Mushy wakati wa mazishi yaliyofanyika nyumbani kwake katika Kijiji cha Sambarai, Tarafa ya Kibosho, Mkoni Kilimanjaro. Katikati ni Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Kikwete. |
|
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akitoa salamu za Serikali katika mazishi ya aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Austria, Balozi Celestine Mushy yaliyofanyika nyumbani kwake katika Kijiji cha Sambarai, Tarafa ya Kibosho, Mkoni Kilimanjaro |
|
Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Kikwete akitoa salamu za pole kwa familia ya Marehemu Balozi Celestine Mushy |
|
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa Shaka Hamdu Shaka akitoa salamu za pole kwa familia ya Marehemu Balozi Celestine Mushy |
|
Mkurugenzi Idara ya Ushirikiano wa Kikanda katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Agnes Kayola akitoa salamu za pole kwa familia ya Marehemu Balozi Mushy |
|
Mwakilishi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa (DMC) katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Hellen Maduhu akieleza alivyomfahamu Marehemu Celestine Mushy |
|
Sehemu ya Uongozi wa Wizara ukifuatilia ibada ya mazishi ya Marehemu Balozi Celestine Mushy nyumbani kwake katika Kijiji cha Sambarai, Tarafa ya Kibosho, Mkoni Kilimanjaro |
|
Viongozi wa Dini wakiendelea na ibada ya mazishi ya Marehemu Balozi Celestine Mushy nyumbani kwake katika Kijiji cha Sambarai, Tarafa ya Kibosho, Mkoni Kilimanjaro |
|
Mjane na Watoto wa Marehemu Balozi Mushy wakifuatilia ibada ya mazishi ya Marehemu Balozi Celestine Mushy nyumbani kwake katika Kijiji cha Sambarai, Tarafa ya Kibosho, Mkoni Kilimanjaro |
|
Uongozi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki katika picha ya pamoja mbele ya jeneza lililohifadhi mwili wa Marehemu Balozi Celestine Mushy nyumbani kwake katika Kijiji cha Sambarai, Tarafa ya Kibosho, Mkoni Kilimanjaro |
|
Baadhi ya Mabalozi katika picha ya pamoja mbele ya jeneza lililohifadhi mwili wa Marehemu Balozi Celestine Mushy nyumbani kwake katika Kijiji cha Sambarai, Tarafa ya Kibosho, Mkoni Kilimanjaro |
|
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akiweka udongo katika kaburi la Marehemu Balozi Celestine Mushy wakati wa mazishi yaliyofanyika nyumbani kwake katika Kijiji cha Sambarai, Tarafa ya Kibosho, Mkoni Kilimanjaro |
|
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk akiweka udongo katika kaburi la Marehemu Balozi Celestine Mushy wakati wa mazishi yaliyofanyika nyumbani kwake katika Kijiji cha Sambarai, Tarafa ya Kibosho, Mkoni Kilimanjaro |
|
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Joseph Sokoine akiweka udongo katika kaburi la Marehemu Balozi Celestine Mushy wakati wa mazishi yaliyofanyika nyumbani kwake katika Kijiji cha Sambarai, Tarafa ya Kibosho, Mkoni Kilimanjaro |