Tuesday, February 28, 2023
TANZANIA KUANZA SAFARI ZA NDEGE MOJA KWA MOJA HADI SAUDI ARABIA
Tanzania inategemea kuanzisha safari za ndege za moja kwa moja hadi Saudi Arabia ambapo safari ya kwanza kati ya Dar es Salaam na Jeddah inatarajiwa kuanza tarehe 26 Machi 2023.
Hayo yamebainishwa katika mazungumzo ya Balozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia Mhe. Ali Mwadini na Meneja Mkuu wa Masoko, Kanda ya Kati wa Shirika la Ndege la Saudi Arabia Bw. Abdulrahman Alabdulwahab na kujadili maandalizi ya uzinduzi wa safari za ndege za moja kwa moja kati ya Tanzania na Saudi Arabia.
Katika mazungumzo yao viongozi hao pia walijadili mikakati ya kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania ili kuongeza idadi ya watalii na kurahisisha usafirishaji wa bidhaa za Tanzania hususan nyama na matunda.
Monday, February 27, 2023
EU YARIDHISHWA NA UBORESHWAJI WA HAKI ZA BINADAMU, UTAWALA BORA NCHINI
Balozi wa Umaoja wa Ulaya nchini, Mhe. Manfredo Fanti akitoa mchango wake wakati wa majadiliano ya kisiasa kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya. Majadiliano hayo yamefanyika leo Jijini Dar es Salaam |
Majadiliano ya kisiasa kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya yakiendelea Jijini Dar es Salaam |
Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika Nchi za Jumuiya ya Ulaya wakitambulishwa |
Picha ya pamoja |
Sunday, February 26, 2023
DKT. TAX APOKEA NAKALA ZA HATI ZA UTAMBULISHO ZA MABALOZI WA ZAMBIA, BRAZIL NA VATICAN
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) amepokea nakala za Hati za Utambulisho za mabalozi wateule wa nchi za Zambia, Brazil na Vatican.
Mhe. Waziri Tax amepokea nakala za Hati za Utambulisho za Balozi mteule wa Zambia nchini, Mhe. Mathew Jere, Balozi mteule wa Brazil nchini, Mhe. Gustavo Martins Nogueira na Balozi Mteule wa Vatican Nchini, Mhe. Askofu Mkuu Angelo Accattino leo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na mabalozi hao kwa nyakati tofauti Waziri Tax amewahakikishia ushirikiano kutoka Serikalini wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yao ya kibalozi hapa nchini. Pia Waziri Tax ametoa rai kwa mabalozi hao kuendeleza na kudumisha ushirikiano uliopo baina ya Tanzania na nchi zao.
“Tanzania na Zambia tumekuwa marafiki na ndugu wa muda mrefu, Serikali ya Tanzania itaendelea kushirikiana na Serikali ya Zambia katika sekta za biashara na uwekezaji kwa maslahi mapana ya pande zote mbili,” alisema Dkt. Tax
Balozi mteule wa Zambia nchini, Mhe. Mathew Jere ameahidi kuendelea kuimarisha ushirikiano baina ya Zambia na Tanzania katika sekta za biashara na uwekezaji, usafirishaji, pamoja na nishati.
Kwa upande wake Balozi Mteule wa Brazil, Mhe. Gustavo Martins Nogueira ameahidi kuwa Brazil itaendelea kushirikiana na Tanzania katika maeneo mapya ya kimkakati kwa manufaa ya mataifa yote mawili hususan kilimo, biashara na uwekezaji.
Naye Balozi wa Vatican nchini, mhe. Askofu Mkuu Angelo Accattino ameahidi kuendeleza kuimarisha ushirikiano mzuri uliopo baina ya Vatican na Tanzania.
Friday, February 24, 2023
SERIKALI YAWAHAKIKISHIA WAFANYABIASHARA MAZINGIRA SALAMA YA BIASHARA
Serikali imewahakikishia wafanyabiashara kutoka Nchi za Umoja wa Ulaya (EU) kuwa mazingira ya biashara na uwekezaji nchini ni salama, bora na rafiki.
Rai hiyo imetolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi alipofunga Jukwaa la Biashara kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya lililofanyika jijini Dar es salaam kuanzia tarehe 23 – 24 Februari 2023.
Dkt. Mwinyi alisema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekusudia kuweka mazingira bora ya biashara na uwekezaji kwa ajili ya kuvutia wawekezaji wengi kuja kuwekeza nchini.
“EU imekuwa mwekezaji mkubwa nchini Tanzania na imechangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la ufanyaji biashara kati yake na Tanzania, lengo la serikali ya Jamhuri ya Mungano wa Tanzania ni kukuza na kuendeleza sekta binafsi yenye nguvu, hivyo natoa rai kwenu kuwekeza kwa wingi kwani mazingira ni bora na salama,” alisisitiza Dkt. Mwinyi
Rais Mwinyi aliongeza kuwa Serikali imejikita katika kukuza uwekezaji kupitia sekta za kilimo, uchumi wa buluu, madini, usafirishaji, miundombinu, utalii na nyingine nyingi na kuwasihi wafanyabiashara wapatao 400 kutoka EU kuchangamkia fursa za biashara na uwekezaji zinazopatikana nchini.
“Napenda kuwahakikishia kuwa Serikali imejidhatiti kuweka mazingira yenye ushindani ya biashara na uwekezaji ikiwa ni mkakati wa kuendelea kuimarisha mazingira ya uwekezaji na biashara na kuhakikisha yanakuwa rafiki kwa wawekezaji,” aliongeza Rais Mwinyi.
Awali Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU) nchini, Mhe. Manfredo Fanti alisema Tanzania imejitahidi kuboresha mazingira, kuimarisha mahusiano ya nje na kuondoa vikwazo mbalimbali hivyo ni wakati muafaka kwa EU kufanya biashara na Tanzania kwakuwa mazingira ni mazuri na yanaridhisha.
“Mfano kitendo cha Benki ya Uwekezaji ya Umoja wa Ulaya (EIB) kurejea Tanzania na kufanya uwekezaji mkubwa wenye thamani ya Euro milioni zaidi ya 500 ni kutokana na Serikali kuboresha mazingira ya bishara na uwekezaji,” alisema Balozi Fanti
Balozi Fanti amewasihi wafanyabiashara wa Tanzania kupenda kukuza ujuzi ili waweze kuendeleza na kukuza biashara zao pamoja na uchumi wa Taifa kwa ujumla.
“EU kwa umoja wetu tutaendelea kuimarisha nguvu zetu kwa pamoja ili kuhakikisha tunaendelea kuwekeza na kukuza biashara kati yetu na Tanzania kwa maslahi ya mataifa yote,” alisema Balozi Fanti.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Kazi Uchumi na Uwekezaji Zanzibar, Mhe. Mudrick Ramadhan Soraga amesema Tanzania na Nchi za Umoja wa Ulaya zimekuwa na ushirikiano imara na wa muda mrefu na kwamba ushirikiano huo umesaidia kuendelea kushirikiana katika sekta mbalimbali za maendeleo kwa maslahi ya mataifa yote mawili.
Sehemu ya viongozi mbalimbali wakifuatilia Hotuba ya ufunguzi wa Jukwaa la Biashara kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya lililofanyika Jijini Dar es Salaam |
Baadhi ya Mabalozi wa Tanzania katika nchi za Umoja wa Ulaya wakifuatilia Hotuba ya ufunguzi wa Jukwaa la Biashara kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya lililofungwa Jijini Dar es Salaam |
Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Mhe. Grace Martin akichangia jambo wakati wa Jukwaa la Biashara kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya lililofungwa leo Jijini Dar es Salaam |
DKT. TAX AONGOZA UJUMBE WA TANZANIA MKUTANO WA 43 WA BARAZA LA MAWAZIRI WA EAC
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax, ameongoza ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa 43 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) uliofanyika jijini Bujumbura, Burundi tarehe 23 Februari 2023.
Mhe. Dkt. Tax ambaye ameshiriki Mkutano huo kwa mara ya kwanza tangu kuteuliwa kwake kwenye wadhifa huo, ameungana na Mawaziri wenzake wanaosimamia masuala ya Afrika Mashariki na Ushirikiano wa Kikanda katika Jumuiya hiyo kupitia, kujadili na kupitisha mapendekezo ya agenda mbalimbali zinazolenga kuboresha utendaji wa Jumuiya kwa manufaa ya Nchi Wanachama.
Miongoni mwa agenda zilizojadiliwa na kupitishwa na Baraza hilo ni pamoja na ripoti ya utekelezaji wa maazimio mbalimbali yaliyofikiwa na Baraza hilo kwenye vikao vilivyopita; taarifa kutoka Ofisi ya Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, taarifa ya utekelezaji wa program mbalimbali katika sekta za miundombinu, forodha na biashara, utalii na ajira; taarifa ya mwaka ya ukaguzi wa hesabu za jumuiya kuanzia mwezi Januari hadi Juni 2022 na ripoti ya kamati ya utawala na fedha.pamoja na kupitia na kupitisha ratiba ya shughuli za Jumuiya kwa kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi Juni 2023.
Kadhalika masuala mengine yaliyojadiliwa ni umuhimu wa kukitangaza Kiswahili duniani kwa kuanzisha vituo vya utamaduni wa lugha hiyo katika Balozi za Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki; na kutoa mwelekeo wa kuanza kutumika kwa lugha ya Kifaransa na Kiswahili katika uendeshaji wa shughuli rasmi za Jumuiya.
Awali akizungumza na Waandishi wa Habari Mwenyekiti kutoka Jamhuri ya Burundi ambaye pia ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Ezekiel Nibigira amesema kuwa Burundi kama mwenyekiti inaona fahari kuandaa Mkutano wa aina hiyo ambapo pia aliwakaribisha Mawaziri wenzake na washiriki wa Mkutano huo nchini humo na kueleza kuwa nchi hiyo imeendelea kuwa na amani na utulivu wakati wote.
Mkutano huo ambao umefanyika kwa siku tano , ulitanguliwa na vikao vya Wataalam na Makatibu Wakuu kutoka nchi wanachama viilivyofanyika kuanzia tarehe 19 hadi 22 Februari 2023.
Mbali na Mhe. Dkt. Tax ujumbe wa Tanzania pia uliwajumuisha Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhe. Mhandisi Godfrey Kasekenya, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Geophrey Pinda, Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine, Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Mhe. Jilly Maleko, Naibu Makatibu Wakuu akiwemo Bibi. Amina Khamis Shaaban Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango na Maafisa Waandamizi kutoka Serikalini.
Miongoni mwa majukumu ya Baraza la Mawaziri la Jumuiya ni kutunga sera za Jumuiya, kufuatilia na kufanya mapitio ya mara kwa mara juu ya utekelezaji wa program mbalimbali za Jumuiya kwa maslahi mapana ya Nchi Wanachama.
Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo inaundwa na nchi saba za Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imeendelea kuhakikisha wananchi katika nchi hizo wananufaika na Jumuiya hiyo hususan katika nyanja za biashara, ulinzi na usalama, viwanda, kilimo, miundombinu na huduma za kijamii.
Sehemu ya ujumbe wa Burundi wakishiriki mkutano |
Ujumbe wa Uganda na Sudan Kusin katika mkutano |
Ujumbe wa Kenya katika mkutano |
Ujumbe kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wakishiriki Mkutano |
Ujumbe wa Rwanda katika Mkutano |
Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Mhe. Dkt. Jilly Maleko akishiriki kikao cha kupokea na kujadili taarifa ya nchi kilichofanyika kabla ya kuanza Mkutano wa 43 wa Baraza la Mawaziri. |
Kikao kikiendelea |