Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Phillip Mpango amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Mkutano wa Dharura wa 21 wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambao umefanyika jijini Bujumbura, Burundi tarehe 31 Mei 2023.
Mkutano huo ambao ulitanguliwa na Mikutano ya Kamati ya Uratibu ya Makatibu Wakuu na Mkutano Maalum wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya hiyo, pamoja na mambo mengine umejadili hali ya Usalama Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambapo viongozi hao wameeleza kuridhishwa na juhudi zinazofanywa na Jumuiya katika kutafuta amani ya kudumu katika eneo hilo.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano huo, Rais wa Jamhuri ya Burundi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhe. Evariste Ndayishimiye amesema kuwa anawapongeza Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuendelea kuhakikisha Jumuiya ya Afrika Mashariki inaedelea kustawi kwa maslahi mapana ya wananchi wa nchi zao.
Amesema mara zote, Wakuu hao wa Nchi wameonesha utayari wa kutafuta suluhu ya haraka kwa changamoto za Jumuiya hiyo ikiwemo kushirikiana kwa pamoja katika kutafuta amani ya kudumu katika eneo la Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
“Nawapongeza viongozi wenzangu kwa utayari wenu wa siku zote katika kutafuta changamoto mbalimbali zinazoikabili Jumuiya yetu ikiwemo kutafuta amani ya kudumu katika eneo la Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Pia navipongeza vikosi vya Kanda vya Jumuiya ya Afrika Mashariki vilivyopo Congo kwa kuendelea kulinda amani katika eneo hilo la Mashariki mwa Congo” alisema Mhe. Rais Ndayishimiye.
Kadhalika Mkutano huo umemteua Jaji wa Makakama ya Rufaa ya Tanzania, Mhe. Omar Othman Makungu kuwa Jaji wa Kitengo cha Rufaa katika Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki. Mhe. Makungu anachukua nafasi ya Mhe. Jaji Sauda Mjasiri kutoka Tanzania ambaye amestaafu.
Vilevile, Wakuu hao wa nchi wamemteua na kumwapisha Jaji Kayembe Kasanda Ignace Rene kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kuwa Jaji wa Mahakama ya Divisheni ya Awali ya Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki.
Kadhalika Mkutano huo umeteua na kuwaapisha Naibu Makatibu Wakuu wawili ambao ni Bi. Annette Ssemuwemba Mutaawe kutoka Jamhuri ya Uganda kushika nafasi ya Naibu Katibu Mkuu anayesimamia Umoja wa Forodha, Biashara na Masuala ya Umoja wa Fedha na Bw. Andrea Aguer Ariik Malueth kutoka Jamhuri ya Sudan Kusini kushika nafasi ya Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Masuala ya Miundombinu, Sekta za Uzalishaji, Kijamii na Siasa.
Bi. Annette anachukua nafasi ya Mhandisi Steven Mlote kutoka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye mkataba wake wa kazi umemalizika na Bw. Malueth anachukua nafasi ya Mhe. Christopher Bazivamo kutoka Rwanda ambaye naye mkataba wake umefikia ukomo.
Mbali na Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Mpango mkutano huo pia umehudhuriwa na Rais wa Kenya, Mhe. William Ruto pamoja na Wawakilishi wa Marais wa Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Uganda na Sudan Kusini.
Mhe. Dkt. Mpango pamoja na ujumbe aliiongozana nao wakishiriki Mkutano Maalum wa 21 wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika jijini Bujumbura, Burundi tarehe 31 Mei 2023. |
Mkutano Maalum wa 21 wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ukiendelea jijini Bujumbura, Burundi tarehe 31 Mei 2023. |
Mhe. Waziri Bashungwa na Balozi Mbundi wakati wa mkutano |
Picha ya pamoja |