Nigeria imeoneshwa kuridhishwa na utendaji wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Kauli hiyo imetolewa na Balozi wa Nigeria nchini, Mhe. Hamisu Umar Takamawa alipokuwa akimuga Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk katika Ofisi Ndogo za Wizara baada ya kumaliza muda wake wa uwakilishi nchini.
Balozi Takamawa ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa jitihada zake za kuboresha Sera ya Mambo ya Nje pamoja na kuanzisha Tume ya kuboresha Haki Jinai nchini.
“Naipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi Imara wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kweli imefanya mambo ambayo nadhani mataifa mengine tunapaswa kuiga hususan masuala ya kuboresha haki jinai, hili ni jambo kubwa na jema ambalo taifa lolote lile linapaswa kuiga mfano huo hapa Tanzania,” alisema Balozi Takamawa
Kuhusu Sera ya Mambo ya Nje, Balozi Takamawa amesema kuwa kuboreshwa kwa sera hiyo kunatoa mwanga wa kuimarisha utekelezaji wa diplomasia ya uchumi, kuongeza wigo wa biashara za kimataifa, kuvutia uwekezaji wa mitaji na teknolojia kutoka nje katika sekta za kijamii na kiuchumi.
Pamoja na mambo mengine, Balozi Takamawa ameishukuru Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Serikali kwa ujumla kwa ushirikiano iliompatia wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yake hapa nchini.
Kwa Upande wake, Balozi Mbarouk amesema kuwa uhusiano wa Tanzania na Nigeria ni matunda yalijengwa kwa misingi imara ya viongozi wa mataifa haya mawili (Hayati Mwl. Julius Nyerere na hayati Dkt. Nnamdi Azikiwe) ambao umedumu kwa takriban miaka 60.
Kadhalika, Balozi Mbarouk alimpongeza Balozi Takamawa kwa kuimarisha misingi ya ushirikiano wa Nigeria na Tanzania wakati wa uwakilishi wake hapa nchini ambapo katika kipindi chake uhusiano uliimarika katika sekta mbalimbali hususan elimu, bishara na uwekezaji.
“Tanzania na Nigeria zimekuwa na ushirikiano mzuri kibiashara na wewe ni shahidi wa hilo, ambapo benki ya ‘United Bank of Afrika’ kutoka Nigeria imewekeza nchini, kadhalika Kiwanda cha kuzalisha Cement cha Dangote pia kimewekeza Tanzania na kutoa ajira…..huu ni Ushahidi tosha kuwa ushirikiano wa kibiashara kati ya Tanzania na Nigeria ni Imara,” amesema Balozi Mbarouk.
“Naamini kuwa ukiwa nchini Nigeria utakuwa balozi mwema wa Tanzania, nakutakia kila la kheri katika utumishi wako,” amesema Balozi Mbarouk
“Katika kipindi chako umeiwakilisha vyema Australia na kuonesha mafanikio makubwa ambayo yamefikiwa kati ya Tanzania na Australia.
Tanzania na Nigeria zimekuwa zikishirikiana katika sekta za elimu, utalii pamoja na biashara na uwekezaji.