Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Cosato Chumi (Mb)
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Cosato Chumi (Mb.) kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) ametoa wito kwa Watanzania waishio nje ya nchi (diaspora) kuchangamkia fursa ya kuwekeza nyumbani, akisema kuwa mchango wao ni nguzo muhimu ya maendeleo ya taifa.
Mhe. Chumi ametoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya uzinduzi wa Akaunti ya Mzawa, huduma maalum ya kifedha kwa diaspora iliyozinduliwa na Benki ya Absa Tanzania.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mhe. Chumi ameipongeza Benki ya Absa kwa ubunifu wa huduma hiyo ambayo inalenga kupunguza changamoto wanazokutana nazo Watanzania wanaoishi ughaibuni, hususan katika kupata huduma za kifedha, kutuma fedha, na kushiriki katika uwekezaji wa ndani.
“Akaunti hii ni suluhisho la changamoto za kifedha kwa diaspora. Inawaruhusu kufungua akaunti, kutuma fedha, kuwekeza, na kutumia sarafu 5 tofauti wakiwa popote duniani.” Amefafanua mhe. Chumi
Amefafanua kuwa mchango wa diaspora umekuwa ukiongezeka kila mwaka, akitaja kuwa mwaka 2022 pekee, Watanzania waishio nje walituma nchini fedha za kigeni zenye thamani ya zaidi ya Shilingi trilioni 1.4. Amesema fedha hizo zimechangia maendeleo ya sekta mbalimbali kama elimu, afya, biashara, na ujenzi wa makazi.
“Serikali inatambua nafasi muhimu ya diaspora. Ndiyo maana tumekamilisha mapitio ya Sera ya Mambo ya Nje inayojumuisha masuala ya diaspora, tumeanzisha mfumo wa kidijitali wa usajili wa diaspora, tumepitisha hadhi maalum kwa Watanzania wasio raia, na kuanzisha vitengo mahsusi serikalini vya kushughulikia masuala yao,” ameongeza Mhe. Chumi
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Absa Tanzania, Bw. Obedi Laizer, amesema huduma hiyo imebuniwa kwa kuzingatia maoni ya Watanzania waishio nje, na kwamba benki hiyo itaendelea kushirikiana na Serikali katika kukuza uwekezaji wa ndani na biashara jumuishi.
Hafla hiyo pia imehudhuriwa na Mkurugenzi wa Idara ya Diaspora katika Wizara ya Mambo ya Nje, Bw. Salvator Mbilinyi, mabalozi wastaafu, na wadau mbalimbali wa sekta ya kifedha na uwekezaji.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Cosato Chumi (Mb)
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. David Cosato Chumi (kulia) akiwa pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Absa Tanzania, Bw. Obedi Laizer (kushoto)
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Absa Tanzania, Bw. Obedi Laizer
Mkurugenzi wa Idara ya Diaspora katika Wizara ya Mambo ya Nje, Bw. Salvator Mbilinyi