Thursday, March 7, 2013

Waziri Mkuu wa Denmark awasili Mkoani Arusha kuendelea na ziara yake

Waziri Mkuu wa Denmark, Mhe. Helle Thorning-Schmidt akisalimiana na viongozi  mbalimbali wa Mkoa wa Arusha mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Mkoa huo akitokea Dar es Salaam. Mhe. Thorning-Schmidt yupo nchini kwa ziara ya siku nne kauanzia tarehe 5 hadi 8 Machi, 2013.


Mhe. Waziri Mkuu wa Denmark akiwa amefuatana na Mhe. Mary Nagu (Mb.), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na Uwezeshaji pamoja na Mhe. Magesa Mulongo, Mkuu wa Mkoa wa Arusha mara baada yakuwasili mkoani Arusha akitokea Dar es Salaam

Mhe. Thorning-Schmidt pamoja na wenyeji wake wakifurahia burudani kutoka moja ya kikundi cha ngoma ya Kimasaai iliyokuwepo Uwanjani hapo wakati wa mapokezi.


Mhe. Thorning-Schmidt akilakiwa kwa shangwe na baadhi ya kina mama wa Mkoa wa Arusha



Mhe. Waziri Mkuu wa Denmark kwa pamoja na Mhe. Waziri Nagu na Mkuu wa Mkoa wa Arusha wakipata picha ya pamoja na kikundi cha ngoma wakati wa mapokezi yake Arusha


Mhe. Thorning-Schmidt akisaini Kitabu cha Wageni mara baada ya kuwasili katika Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) iliyopo Jijini Arusha

Rais wa Mahakama ya ICTR, Mhe. Jaji Vagn Joensen akitoa taarifa fupi ya utendaji wa Mahakama hiyo kwa Mhe. Thorning-Schmidt (hayupo pichani)

Mhe. Thorning-Schmidt akizungumza na uongozi wa Mahakama ya ICTR (hawapo pichani) mara baada kupokea taarifa kuhusu utendaji wa mahakama hiyo.


Mhe. Thorning-Schmidt akiwa katika picha ya pamoja na uongozi wa Mahakama ya ICTR mara baada ya mazungumzo nao.  Wengine katika picha ni Mhe. Waziri Nagu (watatu kutoka kulia), Mhe. Mulongo (mwenye tai nyekundu) na Bw. Jacob Msekwa (kulia), Mwakilishi wa Balozi wa Tanzania katika nchi za Nordic ikiwemo Denmark.


Mhe. Waziri Mkuu, Thorning-Schmidt akivalishwa Vazi Rasmi linalovaliwa na kina mama wa Kimasai mara baada ya kuwasili katika Kijiji cha Wamaasai cha Lepurko kilichopo Wilayani Monduli.


Mhe. Waziri Mkuu, Thorning-Schmidt akisaini kitabu cha wageni  alipowasili kijijini Lepurko

Moja ya shughuli maalum iliyompeleka Mhe. Thorning-Schmidt kijijini Lepurko ni kuzungumza na kina mama na kusikiliza matatizo na changamoto mbalimbali wanazokutana nazo katika maisha yao ya kila siku kama anavyoonekana.

Mmoja wa kina mama katika Kijiji cha Lepurko akimweleza Mhe. Thorning-Schmidt matatizo yanayowakabili wanawake wa kikiji hicho ikiwa ni pamoja na uhaba wa maji na elimu bora kwa watoto wao.


Moja ya nyumba  maarufu kama "Boma" zilizopo kijijini hapo

Mhe. Thorning-Schmidt akimsikiliza mmoja wa watoto wa kike ambaye ni mwanafunzi katika kijiji hicho

Mhe. Thorning-Schmidt akihutubia wananchi (hawapo pichani) wa Kijiji cha Lepurko

Mhe. Thorning-Schmidt akiangalia bidhaa mbalimbali zinazotengenezwa kwa shanga na kina mama wa kijijini hapo

Mmoja wa kina mama wa Kijiji cha Lepurko akimvisha ushanga Mhe. Thorning-Schmidt

Sehemu ya Wananchi wa Kijiji cha Lepurko wakisikiliza kwa makini hotuba ya Mhe. Thorning-Shmidt (hayupo pichani) ambapo aliahidi kuwasaidia katika kutatua tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama.

Mhe, Thorning-Schmidt akitoka ndani ya nyumba "Boma" aliyoitembelea kijijini hapo.

Mhe. Thorning-Schmidt akiagana na Waziri Mkuu Mstaafu na Mbunge wa Monduli, Mhe. Edward Lowassa  mara baada ya kuhitimisha ziara yake katika kijiji cha Lepurko.

Wednesday, March 6, 2013

Waziri Mkuu wa Denmark awasili nchini kwa ziara ya kitaifa ya siku nne

Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akimkaribisha nchini Mhe. Helle Thorning-Schmidt, Waziri Mkuu wa Denmark mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere tarehe 05 Machi, 2013 kwa ziara ya kitaifa ya siku nne.

Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) (katikati), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa akiwa na Mhe. Mary Nagu (Mb), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na Uwezeshaji pamoja na Mhe. Said Meck Sadick, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam wakati wa mapokezi ya Waziri Mkuu wa Denmark.

Mhe. Helle Thorning-Schmidt, Waziri Mkuu wa Denmark akisalimiana na  Balozi Dora Msechu, Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika wakati wa mapokezi ya kiongozi huyo alipowasili nchini kwa ziara ya kitaifa ya siku nne.

Mhe. Thorning-Schmidt akiwa na Mhe. Rais Kikwete akiwafurahia akina mama  wa Dar es Salaam waliofika kumpokea mara baada ya kuwasili.
Mhe. Thorning-Schmidt akiwa na Mhe. Rais Kikwete wakati wakisikiliza nyimbo za mataifa yao zikipigwa kwa heshima ya kiongozi huyo

Mhe. Thorning-Schmidt akiwa na Mhe. Rais Kikwete.

Mhe. Thorning-Schmidt akiongozana na Jenerali Davis Mwamunyange kukagua Gwaride la Heshima lililoandaliwa kwa heshima yake.

Mhe. Thorning-Schmidt na Mhe. Rais Kikwete wakifurahia kikundi cha burudani kilichokuwepo uwanjani hapo wakati wa mapokezi ya kiongozi huyo


Tuesday, March 5, 2013

Hotuba ya Mhe. Rais Kikwete ya mwisho wa mwezi Februari 2013






HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA
TANZANIA, MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE,
KWA WANANCHI, 28 FEBRUARI, 2013
                                      
Utangulizi
Ndugu wananchi;
Namshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehma, kwa kutujalia uzima na kutuwezesha  kuwasiliana kupitia utaratibu wetu mzuri tuliojiwekea wa kufanya hivyo kila mwisho  wa mwezi. Leo nimepanga kuzungumza nanyi mambo matatu; yaani Mpango wa Amani, Usalama na Ushirikiano wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Uhusiano wa Waislamu na Wakristo na Matokeo ya Mtihani wa Kidato cha Nne.


Mpango wa Amani, Usalama na Ushirikiano wa
Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo

Ndugu Wananchi;
Tarehe 8 Februari, 2013 kule Addis Ababa, Ethiopia niliungana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mhe. Ban Ki-Moon, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Mhe. Nkosozana Dlamini Zuma na viongozi wa nchi 12 za Afrika Mashariki, Kati na Kusini kutia saini Mpango wa Amani, Usalama na Ushirikiano wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na jirani zake.  Pamoja na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo zilikuwepo nchi za Burundi, Rwanda, Uganda, Sudani Kusini, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya Kongo, Angola, Zambia na Tanzania ambazo ni jirani ya Kongo.  Nchi za Ethiopia, Msumbiji na Afrika ya Kusini pamoja na Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika zilitia saini kama wadhamini.  Ethiopia kwa nafasi yake ya kuwa Mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Afrika na Msumbiji kwa kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).  Nchi wanachama wa Mkutano wa Ukanda wa Maziwa Makuu ziliwakilishwa na Uganda ambayo ni Mwenyekiti wake wa sasa.  Afrika ya Kusini ilishirikishwa kwa kuwa taifa kubwa na  linalotegemewa katika ukanda wetu.

Mpango huu ni jitihada nyingine ya kusaidia Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo ipate amani ya kudumu.  Kama tujuavyo, tangu mwaka 1997 wakati wa vita vilivyosababisha kuondolewa kwa Rais Mobutu Seseseko mpaka sasa nchi hiyo rafiki na jirani haijapata amani na utulivu wa kudumu.  Kumekuwepo jitihada na mipango kadhaa ya kuleta amani ambayo hata hivyo baada ya muda fulani machafuko hutokea tena na mipango hiyo kuvurugika.  Inakadiriwa kuwa takriban watu milioni 5.4 wamepoteza maisha na watu wengi kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi yao.  Pia kumekuwepo na vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto pamoja na mali nyingi kuharibiwa au kuporwa.

Ndugu Wananchi;
Machafuko yaliyoanzishwa na waasi wa Kundi la M23 mapema mwaka wa jana ndiyo sababu ya kuwepo kwa Mpango huu wa sasa tuliotia saini kule Addis Ababa, Ethiopia tarehe 8 Februari, 2013.  Katika Mpango huo Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na jirani zake, Tanzania ikiwemo, tumekubaliana kutokufanyiana vitendo vinavyohatarisha amani na usalama wa nchi zetu.  Tumeazimia tusifanye hivyo ama moja kwa moja kama nchi au kwa kutumia watu wengine.  Aidha, tumekubaliana tusiruhusu watu au vikundi vya watu kutumia nchi zetu kuhatarisha usalama wa nchi nyingine.  Kimsingi tumekubaliana kuwa majirani wema.  Katika Mkataba huo, majukumu ya kila nchi yameainishwa vizuri pamoja na yale ya Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na Mashirika ya Kikanda hususan SADC na ICGLR.

Ndugu Wananchi;
Niliamua kukubali kushiriki na kutia saini Mpango ule kwa kutambua ukweli kwamba sisi majirani wa nchi ya Kongo tunao wajibu wa kusaidia kwa kile tunachoweza.  Wananchi wa Kongo wameteseka kwa muda mrefu mno hivyo kama Mpango huu utawasaidia kupata amani na usalama hatuna budi kuunga mkono.  Ni kwa misingi hiyo hiyo, tulikubali kuchangia kikosi kimoja katika Jeshi la Kimataifa la kulinda amani huko Mashariki ya Kongo kama ilivyoamuliwa na Mkutano wa Nchi za Maziwa Makuu mwezi Julai, 2012.  Uamuzi huo umeungwa mkono na Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika.  Umoja wa Mataifa umeamua Jeshi hilo liwe sehemu ya Jeshi la Umoja wa Mataifa la Kulinda Amani nchini Kongo (MONUSCO) jambo ambalo sote tumeliafiki.  Tumepeleka walinzi wa amani Darfur, Sudan na Lebanon, kwa nini tusipeleke Kingo.  Miaka ya nyuma tulishapeleka walinzi wa amani Liberia, Siera Leon na Eritrea.

Ni matumaini yetu kuwa Mpango huu mpya utatekelezwa kwa ukamilifu na kuzaa matunda yaliyokusudiwa.  Kama nchi jirani, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo yenye amani, usalama na utulivu ni jambo lenye maslahi makubwa kwetu.  Ina maana ya kutokuwa na wakimbizi kutoka nchi hiyo, uharamia katika Ziwa Tanganyika kutokuwepo na ustawi wa shughuli za kiuchumi na kibiashara kwa upande wetu na wao.  Ni chachu muhimu ya maendeleo ya Mikoa ya pembeni mwa Ziwa Tanganyika na Tanzania kwa jumla.


Uhusiano wa Waislamu na Wakristo

Ndugu wananchi;
          Jambo la pili ninalopanga kulizungumzia siku ya leo ni uhusiano wa Wakristo na Waislamu hapa nchini.  Kwa miezi kadhaa sasa tangu mwaka wa jana kumekuwepo na matukio kadhaa yanayosababisha mifarakano na kupandikiza chuki baina ya waumini wa dini ya Kikristo na Kiislamu.  Matukio ya kauli na vitendo vya kudharau dini za wengine, kunajisi vitabu vitakatifu vya dini hizo, kuchoma moto nyumba za ibada na mzozo kuhusu nani achinje.   Kumekuwepo  na matumizi mabaya ya radio na simu za mkononi na mifumo  mingine ya mawasiliano iliyoeneza maneno na ujumbe wa chuki na vitisho kwa waumini na viongozi wa dini zetu hizi kubwa hapa nchini.  Kauli na matendo hayo, katika baadhi ya maeneo yamekuwa chanzo cha uhasama na magomvi baina ya waumini na hatimaye kusababisha vifo kama ilivyotokea Buseresere Mkoani Geita na Beit-el-Ras, Zanzibar. 

Ndugu zangu;          
          Watanzania hatujawahi kuwa hivi, kumetokea nini? Miaka yote Watanzania ni watu tunaotambua na kuheshimu tofauti za dini zetu mbalimbali tunazoabudu.  Watanzania ni waelewa na kwa ajili hiyo tumekuwa tunavumiliana kwa tofauti zetu na ndiyo maana tumekuwa tunaishi pamoja kidugu, kwa umoja na kushirikiana kwa mambo yote yanayotuhusu maishani isipokuwa wakati kila mmoja anapoingia kwenye nyumba ya ibada kumuomba Mola kwa misingi na taratibu ya dini yake.

 Watanzania wa dini zote na makabila tofauti wanaishi nyumba moja, wanasoma pamoja, wanafanya kazi pamoja kwa udugu, upendo, umoja na ushirikiano.  Kuna koo na familia zenye watu wa dini tofauti, wengine Waislamu na wengine Wakristo.  Wapo Waislamu na Wakristo wameoana, wamezaa na wamejukuu na kila mmoja amebakia kuwa mfuasi wa dini yake.  Wapo pia ambao hawakuoa lakini wamezaa watoto na wanashirikiana kulea watoto wao.  Hayo ndiyo maisha ya Watanzania na hiyo ndiyo Tanzania yenye amani na utulivu tuliyozaliwa, kukua na kuishi.  Nawasihi sana Watanzania wenzangu, tuienzi na kuidumisha tunu hii waliyotujengea mababu zetu.

Ndugu Wananchi;
          Kuna wenzetu kwa sababu wanazozijua wao na kwa manufaa wanayoyajua wao wanataka kutuvurugia nchi yetu hii nzuri.  Tusiwape nafasi wachochezi hawa kwani hawatutakii mema na wala hawazitakii mema dini zetu na nchi yetu.  Sisi katika Serikali hatutasita kuwachukulia hatua wale wote wanaochochea chuki za kidini, wanaodharau vitabu vitakatifu vya dini nyingine na wanaokejeli dini nyingine.

Nimewakumbusha Polisi na mamlaka husika kote nchini wasifanye ajizi kwenye matukio ya namna hiyo.  Wawachukulie hatua stahiki wale wote wanaohusika.  Nimewataka wazingatie msemo wa Kiswahili usemao “ajizi nyumba ya njaa”.  Wachochezi wa mifarakano  na chuki za kidini wasipodhibitiwa ipasavyo wataleta maafa kwa Watanzania wasiokuwa na hatia.  Nimewakumbusha Wakuu wa Wilaya na Mikoa kama walinzi wa amani wa maeneo yao ya uongozi, watimize ipasavyo wajibu wao.  Pia nimewataka Polisi wakamilishe mapema upelelezi wa makosa ya vurugu za kidini na wahusika wafikishwe haraka kwenye vyombo vya sheria ili iwe fundisho kwa wengine.

Ndugu Wananchi;
          Naendelea kuwasiliana na viongozi wa dini kuzungumza nao juu ya wajibu wao maalum wa kuhakikisha kuwa wafuasi wao hawawi chanzo au sehemu ya tatizo na mifarakano miongoni mwa waumini wa dini mbalimbali nchini.  Hali kadhalika naitumia nafasi hiyo kuwakumbusha umuhimu wa kuzungumza na wenzao wa upande mwingine kutatua tofauti au matatizo yanayoathiri uhusiano mwema baina yao.

Ndugu Wananchi;
          Kuna msemo maarufu usemao “mjenga nchi ni mwananchi na mbomoa nchi ni mwananchi”.  Naomba tuwe wajenga nchi na kamwe tusikubali kuwa wabomoa nchi.  Hivi tukiibomoa nchi yetu tutakwenda wapi? Tutaishi wapi?  Tusikubali kugeuka wakimbizi ndani ya nchi au nje ya nchi yetu.

Kwa mara nyingine tena, napenda kutumia nafasi hii kuwapa mkono wa pole makanisa, familia, ndugu na jamaa wote wa Mchungaji Kachila na Padri Mushi.  Sote tunafahamu machungu waliyonayo kwa kuondokewa na wapendwa wao.  Serikali na wapenda amani wote nchini wapo pamoja nanyi katika kipindi hiki kugumu.  Vile vile natoa rambirambi zangu nyingi kwa waumini wote wa Kanisa la Pentekoste Assemblies of God na Kanisa Katoliki Tanzania kwa kuondolewa ghafla na viongozi wao. Tuzidi kumwomba Mwenyezi Mungu azipumzishe kwa amani roho za viongozi wetu.  Amin.


Matokeo ya Mtihani wa Kidato cha Nne Mwaka 2012

Ndugu wananchi;
Tarehe 18 Februari, 2013 Baraza la Mitihani la Taifa lilitangaza matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne ya mwaka 2012.  Wanafunzi 397,132 walifanya mtihani huo na kati ya hao, waliofaulu ni 126,851 yaani sawa na asilimia 34.5.  Wanafunzi  240,903 ambao ni sawa na asilimia 65.5 hawakufaulu mtihani huo.  Kwa ulinganifu, matokeo hayo ni mabaya kuliko matokeo mengine ya mtihani huo ya miaka ya hivi karibuni.

Mwaka 2011, jumla ya wanafunzi 336,782 walifanya mtihani huo na waliofaulu walikuwa asilimia 53.6 na ambao hawakufaulu kabisa walikuwa asilimia 46.4.  Mwaka 2010 jumla ya wanafunzi 352,045 walifanya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne, asilimia 50.4 ya wanafunzi hao walifaulu  na asilimia 49.6 ya wanafunzi hawakufaulu. 

Ndugu Wananchi;
          Matokeo ya mitihani ya kidato cha nne mwaka 2012, yameshtua na kufadhaisha watu wengi nchini na kwa sababu stahiki kabisa.  Kwanza, kwamba kiwango cha kufaulu kimeporomoka sana, tena ghafla, kutoka asilimia 53.6 mwaka 2011 hadi asilimia 34.5 mwaka 2012.  Hili ni anguko la asilimia 19.1 ambalo, kwa kila hali, ni kubwa sana.  Pili, kwamba hata shule zinazofahamika kuwa na historia ya kufaulisha vizuri kama vile seminari, shule za watu binafsi, za mashirika ya dini na sekondari kongwe za Serikali ambazo hazina matatizo kama ilivyo kwa zile sekondari za Kata, nazo safari hii hazikupata mafanikio kama ilivyo kawaida yao.  Nazo zimejikuta zikiwa na idadi ya vijana waliopata daraja la kwanza, la pili na la tatu ikipungua wakati  waliopata daraja la nne na waliofeli wakiongezeka. 

Isitoshe na kiwango cha ufaulu wa vijana umepungua pia.  Mwaka 2010 wanafunzi 10 bora wote walikuwa wamefaulu daraja la kwanza la alama  au pointi 7.  Mwaka 2011 katika wanafunzi 10 bora wanane walipata daraja la kwanza kwa alama  7 na wawili alama 8.  Mwaka 2012 katika wanafunzi 10 bora, watatu walipata daraja la kwanza kwa alama 9, watatu alama 10  na wawili alama 11.    

Ndugu Wananchi;
Haya ndiyo mambo yanayozua maswali kwa watu wengi yanayohitaji kupatiwa majawabu ya uhakika.  Kulikoni mwaka 2012?  Ndiyo msingi wa uamuzi wa Waziri Mkuu, Mhe. Mizengo Pinda, kuamua kuunda Tume ya kuliangalia suala zima la mitihani ya mwaka 2012 na matokeo yake.  Hali hii haijawahi kutokea katika miaka ya hivi karibuni.  Ni suala muhimu sana kwa maendeleo ya nchi yetu, hivyo lazima ukweli wake ujulikane kwa uhakika.  Hii itawezesha Serikali na wadau wengine kuchukua hatua stahiki kurekebisha mambo mapema iwezekanavyo ili hatimaye mambo yawe mazuri siku za usoni.  Tusipofanya hivyo mambo yanaweza kuwa mabaya zaidi na lawama zinaweza kuwa kubwa zaidi kwa Serikali.

Ndugu Wananchi;
          Hivi sasa kunatolewa mawazo lukuki kuhusu sababu za kwa nini matokeo yamekuwa mabaya.  Wapo wanaodhani kuwa lipo tatizo katika utungaji wa mitihani, usahihishaji wake au kutoa maksi kwa watahiniwa.  Wapo wanaodhani walimu hawawajibiki ipasavyo au baadhi yao kutokumudu masomo wanayofundisha.  Wapo wanaofikiria kuwa wanafunzi hawako makini katika kufuatilia masomo na wazazi hawajali kufuatilia maendeleo ya watoto wao shuleni.  Wapo wanaoinyooshea kidole Serikali kwa sera, mitaala na uwekezaji usiokidhi mahitaji ya maendeleo  ya elimu.  Wapo wanaofikiria kuwa Serikali kushindwa kuongeza mishahara ya walimu kwa asilimia 100 kama walivyotaka imechangia.  Orodha ni ndefu, ali mradi kila mtu ana mawazo yake.  Na sisi katika Serikali hatuwezi kuwa tunadhani kwa sababu tunayo dhamana maalum.  Lazima tujue ukweli kwa uhakika na ndiyo maana kuna umuhimu wa Tume.  Naomba kila mtu mwenye mawazo yake ayafikishe kwenye Tume hiyo hapo itakapoundwa ili tupate jawabu muafaka la tatizo hili.

Ndugu Wananchi;
          Napenda kuwahakikishia kuwa sisi katika Serikali tumetoa kipaumbele cha juu sana kwa elimu na kwamba hakuna upungufu wa utashi kwa upande wangu na wenzangu wote Serikalini.  Ndiyo maana tumeguswa sana na matokeo haya.  Bajeti ya elimu ya shilingi trilioni 3.6 ambayo ni sawa na asilimia 24 ya bajeti yote ya Serikali ndiyo kubwa kuliko zote.  Kwa ajili hiyo imetuwezesha kuendelea kukabili mahitaji na changamoto za upanuzi mkubwa wa elimu ya sekondari na elimu ya juu.  Bado hatujazimaliza changamoto zote na kwamba bado tuna kazi kubwa mbele yetu, lakini mafanikio yanaendelea kupatikana.  Tutaendelea kutoa kipaumbele cha juu kwa elimu mpaka hapo itakapofikia mahali kwamba matatizo makubwa yatakapokuwa yamepungua sana.
 
Hitimisho
Ndugu Wananchi;

         
Mungu Ibariki Tanzania!
Mungu Ibariki Afrika!
Nashukuru kwa kunisikiliza!


Activities in the Ministry of Foreign Affairs


Hon. Bernard K. Membe (MP), Minister for Foreign Affairs and International Co-operation in a three-way discussion yesterday together with H.E. Klaus Peter-Brandes (center), Ambassador of Germany to the United Republic of Tanzania and H.E. Dianna Melrose (left), British Ambassador to the United Republic of Tanzania in his office in Dar es Salaam. 

Hon. Bernard K. Membe (MP) in a tête-à-tête meeting with H.E. Klaus Peter-Brandes (center), Ambassador of Germany to the United Republic of Tanzania yesterday in his office in Dar es Salaam.

H.E. Ambassador Ali Ahmed Saleh (left), Ambassador of the United Republic of Tanzania to Oman exchanging views with Ambassador Dora Msechu (right), Director of the Department of Europe and Americas, Ms. Grace Shangali (2nd right), Assistant Director of the Department of Europe and Americas and Ambassador Celestine Mushy (2nd left), Director of the Department of Multilateral Cooperation in the Ministry of Foreign Affairs. 

H.E. Ambassador Ali Ahmed Saleh, Ambassador of the United Republic of Tanzania in Oman in a candid photo with Mr. Togolani Mavura (right), Private Assistant to Hon. Minister Bernard K. Membe (MP), Minister for Foreign Affairs and International Co-operation. 



All photos by Tagie Daisy Mwakawgo 



TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI




TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Waziri Mkuu wa Denmark, Mhe. Helle Thorning-Schmidt anatarajiwa kuwasili nchini tarehe 05 Machi, 2013 kwa ziara ya kitaifa ya siku nne. Ziara hiyo ya Mhe. Thorning-Schmidt inafuatia mwaliko wa Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mhe. Thorning-Schmidt ambaye anatarajiwa kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere tarehe 05 Machi, 2013 saa 12:45 jioni atapokelewa na mwenyeji wake, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete.

Akiwa hapa nchini, Mhe. Thorning-Schmidt atafanya mazungumzo rasmi na Mhe. Rais Kikwete tarehe 06 Machi 2013 na baadaye kwa pamoja na Mhe. Rais Kikwete watakutana na Waandishi wa Habari, Ikulu, Dar es Salaam.

Aidha, siku hiyo hiyo ya tarehe 06 Machi 2013, Mhe. Thorning-Schmidt atatembelea Meli ya Kijeshi ya Denmark ya Iver Huitfeldt ambayo imetia nanga katika Bandari ya Dar es Salaam  tarehe 1 Machi, 2013 na kuzungumza na Mabaharia katika meli hiyo.

Mhe. Thorning-Schmidt pia anatarajiwa kutoa Mhadhara katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam siku hiyo ya tarehe 6 Machi, 2013 kuhusu Elimu na Maendeleo kabla ya kushiriki Dhifa ya Kitaifa iliyoandaliwa kwa heshima yake na Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete,  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ikulu, Dar es Salaam.

Mhe. Thorning-Schmidt ataondoka Dar es Salaam tarehe 7 Machi, 2013 kuelekea Arusha ambako ataendelea na ziara yake kwa kutembelea maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR), Kijiji cha Wamaasai cha Lepurko na kukutana na Waandishi wa Habari.

Akiendelea na ziara yake Mkoani Arusha tarehe 8 Machi, 2013 Mhe. Thorning-Schmidt atatembelea Shamba la Kahawa linalomilikiwa na Bw. Christian Jespen lililoko pembezoni mwa Bonde la Ngorongoro na baadaye anatarajiwa kutembelea Hospitali ya Wilaya ya Mbulu.

Aidha siku hiyo hiyo, Mhe. Thorning-Schmidt anatarajiwa kutembelea Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambapo atakuwa na mazungumzo na Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, Dkt. Richard Sezibera. Mhe. Thorning-Schmidt pia atatembelea Kituo cha Mafunzo kinachofadhiliwa na Serikali ya Denmark cha Mellemfolkeligt Samvirkes, MS-TCDC kilichopo Usa River.

Mhe. Thorning-Schmidt anatarajiwa kuondoka hapa nchini tarehe 08 Machi  2013 kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kurejea nchini kwake Denmark.


IMETOLEWA NA: WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA, DAR ES SALAAM.
04 MACHI, 2013



Monday, March 4, 2013

Membe holds talks with EU Delegation


Hon. Bernard K. Membe (MP), Minister for Foreign Affairs and International Co-operation, listens carefully to H.E. Filiberto Cerian Sebregondi, Ambassador and Head of European Union Delegation in the United Republic of Tanzania, during their meeting today in his offices in Dar es Salaam.  Hon. Membe held talks with the EU Delegation, that included a political consultation within the framework of Article 8 of the European-Africa Political Dialogue. 

Ambassador of Germany to Tanzania, H.E. Klaus Peter-Brandes (right), together with the new British Ambassador to Tanzania, H.E. Dianna Melrose (center), and Ambassador of France to Tanzania, H.E. Marcel Escure were also in attendance during the meeting with Hon. Membe. 

Hon. Membe listening to H.E. Klaus Peter-Brandes ( 3rd right), Ambassador of Germany to the United Republic of Tanzania. 

Ambassador Celestine Mushy (left), Director of the Department of Multilateral Cooperation, Ambassador Dora Msechu (center), Director of the Department of Europe and Americas and Ms. Grace Shangali (right), Assistant Director of the Department of Europe and Americas were also in present for the Tanzania Delegation during the Meeting between Hon. Membe and the European Union. 



All photos by Tagie Daisy Mwakawago 



Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Kimataifa azungumza na Balozi mpya wa Uingereza hapa nchini

Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Celestine Mushy, akimkaribisha Wizarani Balozi mpya wa Uingereza hapa nchini, Mhe. Dianna Melrose alipofika kuzungumza naye kuhusu masuala mbalimbali ya ushirikiano wa kimataifa ikiwa ni pamoja na maandalizi ya mkutano wa 39 wa G8 unaotarajiwa kufanyika nchini Uingereza mwezi Juni, 2013.

Balozi Mushy akiwa katika mazungumzo na Mhe. Balozi Melrose.
Balozi Mushy katika mazungumzo na Balozi Melrose huku Bw. Julian Chandler, Naibu Balozi wa Uingereza akifuatilia mazungumzo hayo.

Mhe. Balozi Melrose akimweleza jambo Balozi Mushy wakati wa mazungumzo yao.


Balozi Mushy akifafanua jambo kwa Balozi Melrose huku Bw. Chandler(kushoto) na Bw. Amos Tengu (kulia), Afisa kutoka Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa wakisikiliza kwa makini.








Saturday, March 2, 2013

Naibu Katibu Mkuu akutana kwa mazungumzo na Mwakilishi wa Brazil katika WTO

Balozi Rajabu Gamaha, Naibu Katibu Mkuu katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa akiwa katika mazungumzo na Balozi Roberto Azevedo, Mwakilishi wa Serikali ya Brazil katika Shirika la Biashara Duniani (WTO) lenye Makao yake Makuu mjini Geneva, Uswisi, alipofika Wizarani tarehe 2 Machi, 2013 kwa ajili ya kuwasilisha ujumbe maalum. Balozi Azevedo pia ni mgombea wa nafasi ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo.

Mhe. Balozi Azevedo akiwa na ujumbe aliufuatana nao  wakimsikiliza Balozi Gamaha (hayupo pichani) wakati wa mazungumzo yao. Kulia kwa Balozi Azevedo ni Mhe. Fransisco Carlos Luz, Balozi wa Brazil hapa nchini.

Balozi Gamaha akiendelea na mazungumzo na wageni wake.

Balozi Gamaha akimsikiliza Balozi Azevedo wakati wa mazungumzo yao.

Balozi Azevedo akiendelea na mazungumzo na Balozi Gamaha. Wengine katika picha ni Balozi Celestine Mushy (kushoto kwa Bal. Gamaha), Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Bw. Lucas Mayenga (kulia), Afisa katika Idara hiyo.


Balozi Gamaha akifafanua jambo kwa Balozi Azevedo wakati wa mazungumzo yao

Mhe. Fransisco Carlos Luz (wa kwanza kulia), Balozi wa Brazil hapa nchini pamoja na wajumbe wengine kutoka Brazil wakimsikiliza Balozi Gamaha (hayupo pichani) alipozungumza nao
Wajumbe wote kwa pamoja wakimsikiliza Balozi Gamaha.
 

Balozi Gamaha akiagana na Balozi Azevedo mara baada ya mazungumzo yao.

Picha ya pamoja.


Friday, March 1, 2013

Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Kimataifa azungumza na Balozi wa Indonesia hapa nchini

Balozi Celestine Mushy, Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa akizungumza na Mhe. Zakaria Anshar, Balozi wa Indonesia hapa nchini kuhusu masuala mbalimbali ya ushirikiano wa kimataifa.

Mhe. Balozi Anshar akifafanua jambo kwa Balozi Mushy wakati wa mazungumzo yao
 Balozi Mushy (katikati) na Bw. Lucas Mayenga (kulia), Afisa katika Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa wakimsikiliza Balozi Anshar.

Balozi Mushy akipitia moja ya nyaraka alizokabidhiwa na Balozi Anshar walipokutana kwa mazungumzo.

Balozi Mushy akiagana na Balozi Anshar mara baada ya mazungumzo yao.

Mhe. Membe akutana kwa mazungumzo na aliyekuwa Katibu wa Baraza la Mawaziri la Japan


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.), akizungumza na  aliyekuwa Katibu Mkuu wa Baraza la Mawaziri wa Japan, Bw.Osamu Fujimura alipofika na ujumbe wake Ofisini kwa Mhe. Waziri leo ambapo walizungumzia masuala mbalimbali ya ushirikiano kati ya Tanzania na Japan ikiwemo maandalizi ya Mkutano wa Tano unaohusu Ushirikiano kati ya Japan na Afrika (TICAD V) utakaofanyika nchini humo mwezi Juni 2013.

Mhe. Membe akiendelea na mazungumzo huku ujumbe kutoka Japan ukimsikiliza.

Mhe. Membe akimsikiliza Bw. Fujimura wakati wa  mazungumzo yao.

Mhe. Masaki Okada (kulia), Balozi wa Tanzania hapa nchini akimsikiliza Mhe. Membe (hayupo pichani) wakati ujumbe kutoka Japan ulipomtembelea Mhe. Membe ofisini kwake. Wengine katika picha ni Balozi Mbelwa Kairuki (katikati), Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Bw. Khatib Makenga, Afisa katika Idara hiyo.


Mhe. Membe akiwa katika picha ya pamoja na Bw. na Bibi Fujimura (kushoto) na Mhe. Masaki Okada (kulia), Balozi wa Japan hapa nchini mara baada ya mazungumzo.