Thursday, October 23, 2014

Fly Dubai yazindua rasmi safari zake nchini.

Ndege ya Shirika la Ndege la Fly Dubai ikiwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Kambarage Nyerere ikiwa katika uzinduzi wake uliofanywa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano) Mhe. Samia Suluhu, Ndege hiyo itafanya safari zake za moja kwa moja kutokea Dubai mpaka Dar es Salaa, Kilimanjaro, Mwanza na Zanzibar.
Watatu kutoka kushoto ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano) Mhe. Samia Suluhu, na wapili kutoka kushoto ni Balozi mdogo wa Tanzania, Dubai Omar Mjenga, wakwanza kushoto ni Spika wa Bunge Mstaafu Mhe. Pius Msekwa na wakwanza kulia ni Bajeti meneja wa Fly Dubai wa nchini Tanzania Bw. Riyaz Jamal wakiitazwa Ndege ya Fly Dubai ilipokuwa inawasili.  
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano) Mhe. Samia Suluhu akisalimiana na Makamu wa Mkuu wa kampuni hiyo, Sudhir Screedharan mara baada ya kuwasili na Ndege hiyo katikati ni Bajeti meneja wa Fly Dubai Tanzania Bw. Riyaz Jamal.
Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati Balozi Simba Yahaya akisalimiana na Bw. Screedharan   
Balozi Mdogo wa Tanzania, Dubai Omar Mjenga akisalimiana na Bw. Screedharan
Mhe. Suluhu akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Ndege hiyo itakayoanzisha safari zake moja kwa moja kutokea Dar es salaam mpaka Dubai 
Wakwanza kushoto ni Bw. Shabani Baraza akimwakilisha Balozi wa Tanzania UAE, wa pili kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Kituo cha Biashara katika Ubalozi Mdogo wa Tanzania, Dubai, Bw. Cleophas Luhumbika Watatu kutoka Kushoto ni Afisa Mambo ya Nje Bw. Hangi Mgaka pamoja na wajumbe wengine wakimsikiliza Mhe. Suluhu
Makamu Mkuu Bw. Screedhana (wakwanza kulia), wa kwanza kushoto Balozi Mdogo Mhe. Mjenga na (katikati) ni Bw. Riyaz Jamal wakimsikiliza Mhe. Waziri alipokuwa akizungumza.  
 Makamu wa Mkuu wa kampuni hiyo, Sudhir Screedharan akizungumza katika hafla hiyo mara baada ya uzinduzi wa safari za Ndege ya Shirika lake la Fly Dubai, alisema safari za ndege zao zinatumia ndege mpya za kisasa aina ya Boeing zipatazo 100.  
Wajumbe mbalimbali wakimsikiliza Bw. Screedharan alipokuwa akizungumza
Balozi Mdogo wa Tanzania, Dubai akizungumza na kuushukuru uongozi wa Fly Dubai kwakukubali kuanzisha safari za moja kwa moja kutokea Dar es salaam mpaka dubai, Balozi mdogo Mjenga alisema kwa kuanza kwa safari ya ndege hiyo inategemewa kuongezeka kwa idadi ya Watalii nchini kutokea Milioni 1 kwa mwaka mpaka Milioni 2, fursa za ajira kwa Watanzania.
Sehemu ya wajumbe wengine wakimsikiliza Balozi Mdogo.
Picha ya pamoja

Picha na Reginald Philip


==============================================================


Na Reginald Philip

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano) Mhe. Samia Suluhu (Mb.) ameupongeza Uongozi wa Shirika la Flydubai la Dubai kwa kuanzisha safari za ndege za moja kwa moja kati ya Dubai na Dar es Salaam, Kilimanjaro, Mwanza na Zanzibar kwa gharama nafuu.

Akizindua huduma hiyo kwa niaba ya Makamu wa Rais, Dkt. Mohamed Gharib Bilal, jijini Dar es Salaam, Jumatano tarehe 22 Oktoba, 2014, Mhe. Suluhu alimwambia Makamu Mkuu wa Shirika la Flydubai, Bw. Sudhir Sreedharan, kuwa  kuja kwao Tanzania kutafungua njia za kiuchumi na nchi nyingine za Kiafrika.

Alisema kuanzishwa kwa huduma hiyo pia kutatoa fursa ya ajira kwa watanzania, na akawahimiza wananchi kuchangamkia fursa hizo.

Shirika hilo, ambalo ndege zake zina bei nafuu- kutokea Dar es salaam kwenda dubai na kurudi (DSM-DXD-DSM) kwa bei ya dola za Kimarekani 399 tu (budget Airline) litafanya safari zake kati ya Dar es salaam, KIA na Zanzibar. Baadae, shirika hilo litaongeza safari zao kutokea Mbeya kuelekea Dubail.

Katika hafla hiyo ya uzinduzi iliyoandaliwa na shirika la Flydubai kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Kambarage Nyerere, Mhe. Suluhu aliipongeza Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, kwa kuratibu uanzishwaji wa safari za bei nafuu kupitia kwa Balozi  Mdogo wa Tanzania nchini Dubai, Mhe. Omar Mjenga, ambaye alihudhuria hafla ya uzinduzi.

Baada ya Dar es Salaam, hafla nyingine ya uzinduzi ilifanyika Zanzibar baadaye hiyo jana, Mgeni rasmi alikuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi.

-Mwisho-

AU yawatunuku Dkt. Salim na Balozi Mbita Tuzo za Juu za Mwana wa Afrika



Waziri Mkuu Mstaafu, Dkt. Salim Ahmed Salim akipokea Tuzo ya Juu ya Umoja wa Afrika ya Mwana wa Afrika kwa Mwaka 2014 kutoka kwa Kamishna wa Amani na Usalama wa Umoja wa Afrika, Mhe. Balozi Smail Chergui. Tuzo hiyo  ilitolewa mjini Arusha pembezoni mwa Warsha ya Tano ya Ngazi ya Juu kuhusu Amani na Usalama Bararani Afrika iliyoandaliwa na Umoja wa Afrika inayoendelea mjini humo. Tuzo hiyo pia imetolewa kwa Balozi Mstaafu na Mpigania Uhuru Mahiri Barani Afrika, Balozi Hashim Mbita. Tuzo hizo zimetolewa kwao kutokana na mchango mkubwa walioutoa Barani Afrika na kwa Umoja wa Afrika ambapo Dkt. Salim alikuwa Katibu Mkuu wa saba wa OAU kuanzia mwaka 1989 hadi 2001. Kwa upande wake Balozi Mbita alikuwa Katibu Mtendaji wa Sekretarieti ya Ukombozi Barani Afrika chini ya OAU kuanzia mwaka 1974 hadi 1994 ilipomaliza kazi yake baada ya Uhuru wa Afrika Kusini.
Balozi Chergui akimkabidhi Cheti cha Tuzo hiyo Dkt. Salim
Dkt. Salim akipongezwa na Balozi Chergui
Balozi Chergui akimkabidhi Tuzo ya Juu  ya Umoja wa Afrika ya Mwana wa Afrika ya Mwaka 2014, Binti wa Balozi Hashim Mbita, Sheila Hashima Mbita ambaye aliipokea Tuzo hiyo kwa niaba ya Baba yake ambaye hakuweza kufika kutokana na matatizo ya kiafya.
Balozi Chergui akimkabidhi Cheti Bi. Sheila Hashim Mbita kwa niaba ya Balozi Mbita

Balozi Chergui akimpongeza Bi. Sheila Hashim Mbitaaliyepokea Tuzo kwa  kwa niaba ya Balozi Mbita
Ujumbe wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwemo Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia, Balozi Naimi Aziz wakipiga picha ya pamoja na Dkt. Salim Ahmed Salim na Bi. Sheila Hashim Mbita mara baada ya kukabidhiwa Tuzo hizo.

Dkt. Salim akipongezwa na Balozi Augustine Mahiga huku Rais Mstaafu wa Cape Verde (kulia) akushuhudia.
Dkt. Salim akipongezwa na wajumbe mbalimbali waliokuwepo wakati wa hafala ya utoaji Tuzo.
Dkt. Salim katika picha ya pamoja na Balozi Naimi Aziz
Dkt. Salim katika picha ya pamoja na Bi. Zuhura Bundala, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

Balozi Aziz katika picha ya pamoja na Bi. Sheila Mbita
Balozi Aziz akiwa na Balozi Mahiga katika picha ya pamoja na Bi. Sheila Mbita.



Tuesday, October 21, 2014

Warsha kuhusu Amani na Usalama Barani Afrika yafunguliwa rasmi Mjini Arusha

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mohammed Gharib Bilal akifungua rasmi Warsha ya Ngazi ya Juu kuhusu Amani na Usalama Barani Afrika iliyoandaliwa na Umoja wa Afrika. Tanzania imepata heshima ya kuwa mwenyeji wa Mkutano huo unaofanyika  Jijini Arusha kuanzia tarehe 21 hadi 23 Oktoba, 2014 na itawahusisha Wajumbe Maalum, Wasuluhishi, Mabalozi na Wataalam wa masuala ya Amani. Kaulimbiu ya warsha hiyo ni "Silencing the Guns-Owning the Future" na inalenga kujadili changamoto za usalama Barani Afrika na kutafuta suluhisho la kudumu kwa changamoto hizo.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) akiwa pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia, Mhe. Naimi Aziz wakifuatilia hotuba ya ufunguzi wa Mkutano wa Tano wa Amani iliyotolewa na Makamu wa Rais,  Mhe. Dkt. Bilal (hayupo pichani)
Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Salim Ahmed Salim (kushoto) kwa pamoja na aliyewahi kuwa Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Mataifa na  Msuluhishi wa Mgogoro wa Syria, Dkt. Lakhdar Brahim wakisikiliza hotuba ya Mhe. Dkt. Bilal (hayupo pichani)

Sehemu ya Wajumbe wakifuatilia hotuba hiyo akiwemo Mwakilishi wa Umoja wa Ulaya hapa nchini, Mhe. Filberto Ceriani Sebregondi (kushoto)
Balozi Mstaafu Augustine Mahiga (kushoto) na Mhe. Sirpa Maenpaa wakifuatilia hotuba ya ufunguzi. Balozi Mahiga aliwahi kuwa Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia.
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bi. Zuhura Bundala akiwa na Balozi Mstaafu Walidi Mangachi wakati wa warsha hiyo ya amani na usalama.

Mwenyekiti wa Warsha hiyo ambaye ni Kamishna wa Amani na Usalama wa Umoja wa Afrika, Balozi Smail Chergui nae akizungumza wakati wa Warsha hiyo.
Wajumbe wakati wa ufunguzi wa warsha.
Sehemu nyingine ya wajumbe wakati wa warsha iliyojadili masuala ya amani na usalama Barani Afrika
Wajumbe zaidi
Warsha ikiendelea na wajumbe wakifuatilia kwa makini
Warsha ikiendelea
Waziri Membe akitoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali wakati wa mahojiano na waandishi wa habari kuhusu Warsha hiyo ya Amani na Usalama Barani Afrika. Picha zote na Rosemary Malale
=================================================

Na Ally Kondo, Arusha.



Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mohammed Gharib Bilal amesema kuwa, licha ya machafuko yanayoendelea hivi sasa katika Bara la Afrika, nchi za Afrika hazina budi kuunganisha nguvu ili ziweze kukabiliana na changamoto mpya zinazoibuka ambazo zinatishia amani, usalama na utulivu wa Bara hili.  Changamoto hizo ni pamoja na ugaidi, uharamia, biashara haramu ya silaha ndogo ndogo na nyepesi, biashara ya dawa za kulevya, na biashara haramu ya binadamu.

Hayo aliyasema jijini Arusha siku ya Jumanne tarehe 21 Oktoba 2014 alipokuwa akifungua Warsha ya Ngazi ya Juu kuhusu Amani na Usalama iliyoandaliwa na Umoja wa Afrika ambayo itafanyika kwa siku tatu hadi Alhamisi tarehe 23 Oktoba 2014.

Makamu wa Rais alieleza kuwa ugaidi ni changamoto kubwa katika Afrika kwa sababu hakuna hata nchi moja ambayo imesalimika na uovu huo. Alisema kuwa, licha ya nchi za Afrika kulengwa na mashambulizi ya kigaidi pia zinatumika na magaidi kufanya mashambulizi yanayolenga maslahi ya nchi za kigeni, kujificha, kuandaa na kusajili magaidi wapya pamoja na kuwa chanzo cha mapato kwa ajili ya kuendeshea shughuli zao hizo haramu.

Aidha, Dkt. Bilal alibainisha kuwa katika kipindi cha miongo miwili iliyopita Bara la Afrika limeshuhudia likikumbwa na zaidi ya migogoro 20 ambayo imelifanya bara hilo kutambulika na sifa ya kuwa eneo la vita. Ukweli huo unadhihirishwa na idadi kubwa ya vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa ambapo kati ya vikosi 17 duniani, vikosi 9 vipo Barani Afrika. Aidha, asilimia 60 ya agenda za Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa zinajadili namna ya kurejesha na kuimarisha amani Barani Afrika.

Dkt. Bilal alihimiza nchi za Afrika kuunganisha nguvu ili ziweze kutafuta suluhu ya kudumu ya migogoro katika Bara la Afrika kwa kuwa athari zake ni kubwa. Athari hizo ni pamoja na kudumaza uchumi wa nchi na kuharibu miuondombinu ya kijamii ambayo ilijengwa kwa miaka mingi; kukwamisha juhudi za kupunguza umasikini; ukiukwaji wa haki za binadamu pamoja na kuzalisha wakimbizi na wakimbizi wa ndani.

Hata hivyo, Dkt. Bilal alisifu juhudi zinazofanywa na AU na washirika wake ambazo kwa kiasi kikubwa zimesaidia kupunguza migogoro Barani Afrika. Kwa kipindi cha muongo mmoja uliopita, Bara la Afrika limeshuhudia kumalizika kwa vita ya wenyewe kwa wenyewe, usuluhishi wa migogoro ya muda mrefu na migogoro ya baada ya uchaguzi katika nchi za Angola, Liberia, Sierra Leone, Rwanda, Burundi, Cote d’Ivoire na Madagascar.

“Kutokana na kuimarika kwa amani barani Afrika, uchumi wa bara hilo umeendelea kukua kwa kiwango cha kuridhisha. Kwa mujibu wa takwimu zilizopo kati ya nchi kumi duniani ambazo uchumi wake unakua kwa haraka katika kipindi cha muongo mmoja uliopita nchi sita zinatoka barani Afrika.  Aidha, matarajio katika kipindi cha muongo mmoja ujao, nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara uchumi wake utakua kwa kiwango cha asilimia saba” alisema Dkt. Bilal.

Makamu wa Rais aliendelea kueleza kuwa Bara la Afrika bado linakabiliwa na changamoto za kiusalama kama ilivyo katika nchi za Libya; Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo; Sudan; Somalia; Jamhuri ya Afrika ya Kati na Sudan Kusini.

Kwa upande wa Sudan Kusini, alisema kuwa Serikali imekubali ombi la Rais wa nchi hiyo, Mhe. Salvar Kiir la kusaidia usuluhishi wa mgogoro huo. Hivyo, Chama cha Mapinduzi tokea tarehe 12 – 18 Oktoba 2014 kimekuwa kikifanya majadiliano na vyama hasimu nchini Sudan Kusini kutafuta suluhu ya mgogoro huo. Alisema kuwa majadiliano hayo hayataingilia au kuharibu majadiliano yanayoendelea nchini Ethiopia ambayo nayo yanalenga kutafuta ufumbuzi wa mgogoro huo.

Warsha kuhusu amani na uslama Barani Afrika inayoendelea jijini Arusha ni ya tano kufanyika ambapo warsha zilizotangulia zilifanyika katika nchi za Misri na Cote d’Ivoire. Warsha hizo ambazo huwa zinawakutanisha Wajumbe Maalum, Mabalozi, Wataalamu wa masuala ya usalama zinalenga kujadili changamoto za usalama na namna ya kukabiliana nazo barani Afrika. 

-Mwisho-


Wiki ya Umoja wa Mataifa kuadhimisha miaka 69 yazinduliwa

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw.John Haule (katikati) akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu uzinduzi wa maadhimisho ya Wiki ya Umoja wa Mataifa tarehe 21 hadi 25 Oktoba, 2014. Wiki hiyo ambayo huadhimishwa kila mwaka itajumuisha gwaride rasmi na kupandishwa bendera katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es salaam tarehe 24 Oktoba. Sherehe hizo zitahitimishwa na bonanza la michezo mbalimbali litakalo husisha wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa na Wizara ya Mambo ya Nje kwenye viwanja vya Gymkhana tarehe 25 Oktoba. Kauli mbiu ya Maadhimisho ya mwaka huu ni "Agenda ya Maendeleo baada ya 2015 - Asiachwe mtu nyuma (The Post 2015 Development Agenda - leaving No one Behind)". Wakwanza kushoto ni Bwa. Alvaro Rodriguez, Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa hapa nchini, na wakwanza kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa Balozi Celestine Mushy.
Wawakilishi wa Idara na Vitengo kutoka Mambo ya Nje
Bw. Alvaro Rodriguez akizungumza na waandishi wa Habari
Waandishi wa Habari kutoka mashirika mbalimbali ya habari hapa nchini wakisikiliza maelezo kuhusu maadhimisho ya Wiki ya Umoja wa Mataifa.
Kikao kikiendelea


Picha na Reginald philip

Katibu Mkuu akutana na Ujumbe wa Jeshi la Wanamaji la India

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. John Haule (kulia) akizungumza katika kikao na Mkuu wa Msafara wa Jeshi la Wanamaji kutoka India, Bw. Real Admiral R. Hari Kumar pamoja na ujumbe alioambatana nao walipomtembelea Wizarani. Mazungumzo yao yalilenga kukuza, kuendeleza na kuimarisha mahusiano ya Jeshi la Wanamaji kati ya Tanzania na India.
Kulia ni Balozi wa India nchini Tanzania Bw. Debnath Shaw pamoja na ujumbe aliombatana nao Bw. Kumar.
Bwa. Kumar akizungumza 
Afisa  Mambo ya Nje, Bw. Emmanuel Luangisa (kulia) akinukuu mazungumzo.
Kikao kikiendelea
Katibu Mkuu akikabidhiwa zawadi yenye nembo ya Jeshi la Wanamaji la India
Picha ya pamoja

Picha na Reginald Philip.