Wednesday, March 30, 2016

Serikali ya Tanzania na India zasaini mkataba wa makubaliano wa kuwaruhusu wenza wa Watumishi wa Ubalozini kufanya kazi

 Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Dkt. Aziz Mlima akizungumza na Balozi wa India nchini Mhe. Sandeep Arya mara baada ya kuwasili katika ofisi za Wizara kwa lengo la kusaini Mkataba wa Makubaliano utakaowawezesha Wenza wa Watumishi katika Balozi za nchi hizi mbili kufanya kazi.
 Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria, Balozi Baraka Luvanda (kushoto) na Afisa Mambo ya Nje, Bw. Benedict Msuya wakifuatilia mazungumzo na baadae kusimamia zoezi la kusaini mkataba huo.
 Kushoto ni Afisa kutoka ubalozi wa India ambaye aliambatana na Mhe. Arya
 Katibu Mkuu na Mhe. Balozi Arya wakisaini mkataba wa makubaliano baina ya mataifa hayo mawili ambao utaruhusu wenza wa watumishi wa Balozi kutoka Tanzania na India kuruhusiwa kufanya kazi katika nchi hizo.
 Wakibadilishana mkataba mara baada ya kukamilisha zoezi la utiaji saini
Wakipongezana baada ya kufanikisha zoezi la kusaini makubaliano hayo.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje apokea Nakala za Hati za Utambulisho za Balozi Mteule wa Brazil nchini

Naibu Waziri wa Mambo za Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa Mhe. Dkt. Susan Kolimba akipokea Nakala za Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa Brazil hapa nchini, Mhe. Carlos Alfonso Iglesias Puente, zoezi hilo lilifanyika tarehe 30 Machi, 2016 Wizarani Jijini Dar es Salaam. 
Balozi Mteule wa Brazil hapa nchini, Mhe. Carlos Alfonso Iglesias Puente, akizungumza jambo kwa Naibu Waziri Mhe. Susan Kolimba, muda mfupi baada ya kuwasilisha Nakala za Hati zake za Utambulisho.
 Naibu Waziri Mhe. Susan Kolimba, akimweleza jambo Balozi Mteule wa Brazil hapa nchini, Mhe. Carlos Alfonso Iglesias Puente.
 Mazungumzo yakiendelea huku Kaimu Mkuu wa Itifaki, Bw. James Bwana (kulia kwa Naibu Waziri),  Afisa Mambo ya Nje Bw. Lucas Mayenga, Msaidizi wa Naibu Waziri (wa mwisho kulia), pamoja na Msaidizi wa Balozi Mteule (wa kwanza kushoto) kwa pamoja wakifuatilia mazungumzo hayo.
 Naibu Waziri Dkt. Susan Kolimba akiwa katika picha ya pamoja na Balozi Mteule wa Brazil hapa nchini, Mhe. Carlos Alfonso Iglesias Puente.
Picha ya pamoja.
=========================
Picha na Reuben Mchome.

KONSELI MKUU WA TANZANIA JEDDAH AKARIBISHWA RASMI NA MKURUGENZI MKUU WA WIZARA YA MAMBO YA NJE YA SAUDI ARABIA, NAYE AMWALIKA KUTEMBELEA TANZANIA MWEZI JULAI 2016



Pichani Balozi Muhammad Tayeb, Mkurugenzi Mkuu katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Saudi Arabia akimkaribisha Bw. Suleiman Saleh, Konseli Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jeddah, na kufanya nae mazungmzo kuhusu mahusiano baina ya Saudi Arabia na Tanzania.
Kwa mujibu wa Balozi Tayeb, kusainiwa kwa makubaliano hayo kumefungua ukurasa mpya wa mahusiano baina ya Saudi Arabia na Tanzania na hakusita kuonyesha furaha yake kutokana nakuainishwa maeneo mahususi ya mashirikiano  katika sekta za uchumi, uwekezaji na biashara. Kwa upande wake Bw. Saleh alimshukuru Balozi Muhammad Tayeb kwa kumkaribisha Ofisini kwake na alifarijika na upendo alionyesha Balozi huyo kwa Tanzania ambapo  alichukwa fursa hiyo kumualika kutembelea Tanzania kujionea vivutio vya utalii Tanzania Bara na Visiwani ambapo aliukubali mwaliko huo na kuahidi kutembelea Tanzania yeye na familia yake mwezi Julai, 2016.


========================================

Konseli Mkuu wa Ubalozi Mdogo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania uliopo Jeddah, Saudi Arabia, Bw. Suleiman Saleh, Jumanne Machi 29, 2016, amekaribishwa rasmi katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Saudi Arabia alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi Muhammad A. Tayeb, Mkurugenzi Mkuu wa Wizara hiyo.

Balozi Tayeb alimpokea Bw. Saleh Ofisini kwake Jeddah na kuahidi kutoa ushirikiano unaohitajika katika kuimarisha mahusiano baina ya Saudi Arabia na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufuatia kusainiwa hivi karibuni Ikulu, Dar-es-Salaam, makubaliano ya mashirikiano baina ya nchi hizo mbili. Makubaliano hayo ambayo yalisainiwa na  Mhe. Adil Jubeir, Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia na Mhe. Balozi Augustine Mahiga, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, yalishuhudiwa pia na Mhe. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

Tuesday, March 29, 2016

Waziri Mahiga aeleza msimamo wa Serikali juu ya uamuzi wa Bodi ya MCC

 Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Mhe.Balozi  Dkt. Augustine Mahiga(Mb) akiwa katika Mkutano na waandishi wa  habari uliofanyika katika ukumbi wa ofisi ya Wizara ambapo alieleza msimamo wa  Serikali ya Tanzania juu ya kusitishwa kwa fedha za Mpango wa kukabiliana na changamoto za Milenia ambao umekuwa ukitolewa na Shirika la Millenium Challenge Corporation (MCC) la nchini Marekani.
Sehemu ya waandishi wa Habari wakifuatilia Mkutano huo.
Waziri akifafanua jambo kwa waandishi wa habari ambao hawapo pichani. Wengine katika picha ni Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika, Balozi Joseph Sokoine (kushoto) na Bi. Mindi Kasiga, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali. 
=======================================================
Serikali ya Tanzania imesikitishwa na uamuzi wa Serikali ya Marekani wa kutoipatia fedha za awamu ya pili ya Mpango wa ushirikiano wa kushughulikia Changamoto za Milenia (Millenium Challenge Corporation MCC-2) kiasi cha Dola za Marekani milioni 472 kwa ajili ya kukamilisha miradi ya umeme vijijini na kuitaka nchi hiyo kutafakari upya uamuzi huo.


Hayo yalisemwa na Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Dkt. Augustine Mahiga alipozungumza na Waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam kuelezea msimamo wa Serikali kufuatia uamuzi huo.

Mhe. Mahiga alisema kuwa uamuzi huo ambao haukuishirikisha Tanzania kwa namna yoyote umetolewa na Bodi ya MCC ambayo imekutana Jijini Washington DC hivi karibuni.

Katika maelezo yake, Waziri Mahiga alisema kuwa, Awamu ya Kwanza ya mpango huo ilitolewa na Marekani baada ya Tanzania kukidhi vigezo ambavyo ni pamoja na kufuata misingi ya demokrasia, kupambana na rushwa, utawala bora na kuheshimu haki za binadamu. 
Hata hivyo alieleza kushangazwa kwake na uamuzi wa sasa wa nchi hiyo wa kuahirisha kuipatia Tanzania  fedha za awamu ya pili ya mpango huo kwa madai kuwa haikukidhi vigezo hususan kwa kufuta uchaguzi wa Zanzibar na kuanzishwa kwa Sheria ya Makosa ya Mitandao ambayo wamedai inawanyima wananchi uhuru wa kujieleza.

“Tanzania imesikitishwa na uamuzi wa Marekani wa kuinyima fedha za MCC kwa madai kuwa hatujakidhi vigezo ambavyo ni vigezo hivyo hivyo walivitumia kutupatia awamu ya kwanza ya fedha hizo. Ni matumaini yangu kuwa watatafakari upya uamuzi wao” alisema Balozi Mahiga. 

Kuhusu, Zanzibar Balozi Mahiga alifafanua kuwa ni nchi huru ambayo inaendesha mambo yake kwa uhuru hususan masuala ya uchaguzi ambayo si ya muungano. Hivyo uamuzi wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) ya kufuta uchaguzi uliofanyika mwezi Oktoba 2015 baada ya kutokea kasoro huko Pemba, ulikuwa ni uamuzi wa Tume na unatakiwa kuheshimiwa.

Aidha, kuhusu Sheria ya Makosa ya Mitandao ya Mwaka 2015 (Cyber Crime Act), Balozi Mahiga alieleza kuwa nayo kwa kiasi kikubwa ilianzishwa ili kukabiliana na vitendo vya kigaidi na uhalifu mwingine wowote unaofanyika kupitia mitandao. 

“Kwa mantiki hiyo, Tanzania haikupaswa kuadhibiwa kwa kuangalia masuala hayo pekee wakati kwa muda mrefu Tanzania imejijengea sifa ulimwenguni kote ya kufuata misingi ya demokrasia na utawala bora,” alisisitiza Balozi Mahiga.

Akizungumzia uhusiano kati ya Tanzania na Marekani, Waziri Mahiga alisema kuwa unaendelea kama kawaida kwani MCC ni kipengele kimoja tu katika masuala mengine mengi ya ushirikiano kati ya nchi hizi mbili.

“Marekani imekuwa ni mshirika mkubwa wa maendeleo wa Tanzania ambapo kila mwaka huipatia nchi yetu msaada wa kiasi cha Dola za Marekani milioni 700 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo ya elimu na afya. Hivyo MCC ambayo ni mpango mwingine wa msaada kutoka nchi hiyo ni sehemu ya mambo kadhaa tunayoshirikiana na Marekani” alifafanua Dkt. Mahiga.

Akielezea athari zitakazotokana na kukosekana kwa fedha hizo za Awamu ya Pili ya MCC, Mhe. Mahiga alisema kuwa kwa kiasi fulani Tanzania itaathirika hususan katika eneo la usambazaji wa Nishati ya Umeme Vijijini. Hivyo alisisitiza umuhimu wa Marekani kutafakari upya uamuzi wao huo.

“Marekani inazitaka nchi zipambane na kuondokana na umaskini. Umoja wa Mataifa nao umeanzisha Malengo ya Maendeleo Endelevu ambayo yanalenga kupambana na umaskini. Hata hivyo nasikitika kuwa kuondolewa kwa MCC Tanzania hakutaiwezesha kufikia malengo ya milenia wala dhamira njema ya Marekani ya kuzitaka nchi zinazoendelea kuondokana na umaskini. Kwa maana nyingine nasema ni Malengo ya Milenia na MCC dhidi ya Tanzania”, alieleza Dkt. Mahiga.

Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizonufaika na Mpango wa kukabiliana na Changamoto za Milenia (MCC) ambapo katika awamu ya kwanza ya mpango huo, Tanzania ilipatiwa kiasi cha Dola za Marekani Milioni 698. 

Fedha hizo zilikuwa ni kwa ajili ya kufanikisha miradi ya maendeleo katika uboreshaji wa maeneo ya miundombinu ya barabara za Tunduma-Sumbawanga, Tanga-Horohoro na Namtumbo-Songea-Mbinga. 

Pia zilitumika kujenga mfumo wa maji kwa miji ya Dar es Salaam na Morogoro. Vile vile fedha hizo zilitumika kutandaza njia ya kusafirisha umeme chini ya Bahari ya Hindi kati ya Bara na Tanzania Visiwani na pia kujenga barabara zote kuu za Kisiwa cha Pemba na baadhi ya barabra za Unguja kwa kiwango cha lami.

-Mwisho-
 


Balozi wa Tanzania nchini Kenya aomboleza kifo cha Balozi wa DRC nchini humo


Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Mhe. John Haule akitia saini kitabu cha maombolezo ya kifo cha Balozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) nchini Kenya, Mhe. TADUMI ON'OKOKO, kwenye Ubalozi wa DRC Nairobi. Mhe. ON'OKOKO, ambaye pia alikuwa mwenyekiti wa Mabalozi wanaowakilisha nchi zao Kenya, alifariki dunia tarehe 20 Machi 2016 huko Paris, Ufaransa, ambako alikuwa anatibiwa. Anayeshuhudia ni Kaimu Balozi wa DRC, Mhe. Michel Mubare, ambaye alifahamisha kuwa marehemu atazikwa Kinshasa baada ya mipango kukamilika.

Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Mhe. John Haule (Kulia) akimfariji Kaimu Balozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Mhe. Michel Mubare,  baada ya kutia saini kitabu cha maombolezo ya kifo cha aliyekuwa Balozi wa nchi hiyo Kenya, Mhe. Tadumi On'okoko jijini Nairobi.