Tuesday, November 29, 2016

Rais Magufuli amwandalia Rais Lungu dhifa ya Kitaifa Ikulu, Jijini Dar es Salaam


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na mgeni wake Rais wa Zambia Mhe. Edgar Lungu wakielekea sehemu maalumu ilipoandaliwa dhifa ya kitaifa

Waheshimiwa wa Marais Wastaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wakielekea sehemu ilipoandaliwa dhifa kitaifa Ikulu, Jijini Dar es Salaam

Meza kuu wakiwa wamesimama wakati wimbo wataifa ukipigwa

Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli akigonganisha glass na Rais wa Zambia Mhe. Edga Lungu kwenye dhifa ya kitaifa


Rais wa Zambia Mhe. Edgar Lungu akisalimiana na Rais Mstaafu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Alhaji Ali Hassan Mwinyi

Mhe Rais Dkt. John Pombe Magufuli na Rais wa Zambia Mhe. Edgar Lungu awakitoa maelekezo kwa baadhi ya Watendaji wa Serikali mara baada yadhifa. Kulia na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe.Balozi Dkt. Augustine Mahiga

Monday, November 28, 2016

Rais Magufuli ampokea Rais wa Zambia Ikulu, Dar es Salaam

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Rais wa Jamhuri ya Zambia Mhe. Edgar Chagwa Lungu alipowasili Ikulu Jijini Dar es Salaam. Mara baada ya mapokezi wawili hao waliketi kwa mazungumzo maalum yaliyokita katika kuendeleza miradi mbalimbali iliyoanzishwa na nchi hizo mbili ikiwemo reli (TAZARA) na bomba la mafuta (TAZAMA) ili iweze kuleta tija kwa wananchi.

Rais Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na mgeni wake Rais wa Zambia Mhe. Edgar Chagwa Lungu kabla ya kuanza mazungumzo Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Mambo  ya Nje na Ushirikino wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga na Waziri wa Mambo ya Nje wa Zambia, Mhe. Harry Kalaba wakisaini Mkataba wa utaratibu wa kushauriana kidplomasia kati ya Tanzania na Zambia.

Waziri wa Mambo  ya Nje na Ushirikino wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga na Waziri wa Mambo ya Nje wa Zambia, Mhe. Harry Kalaba wakipepongezana mara baada ya kutia saini mkataba.

Waziri wa Mambo  ya Nje na Ushirikino wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga na Waziri wa Mambo ya Nje wa Zambia, Mhe. Harry Kalaba wakionesha mkataba waliosaini kwa hadhira iliyokuwepo ukumbuni

Rais wa Jamhuri ya Zambia Mhe. Edward Chagwa Lungu akizungumza na hadhira iliyokuwepo ukumbini mara baada ya kumaliza mazungumzo na mwenyeji wake Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akifuatilia mazungumzo

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. John Pombe Magufuli akisisitiza jambo alipokuwa akizungumza na hadhira waliokuwepo ukumbini mara baada ya kumaliza mazungumzo na Rais wa Zambia Mhe. Edgar Chagwa Rungu.

Picha ya pamoja

Rais Lungu awasili Tanzania kwa ziara ya Siku tatu

Rais wa Jamhuri ya Zambia, Mhe. Edgar Lungu (kulia) akisalimiana na mwenyeji wake, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli alipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar Es Salaam kwa ziara ya Kiserikali ya siku tatu.

Rais Lungu akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga huku Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akiangalia

Rais Lungu akisalimiana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Aziz Mlima.

Rais Lungu akisalimiana na Balozi wa Tanzania nchini Zambia, Mhe. Grace Mujuma

Rais Lungu akisalimiana na Mkurugenzi wa Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Samuel Shelukindo

Rais Lungu na Mwenyeji wake Rais Magufuli wakiwa wamesimama wakati mizinga ya kumkaribisha Rais Lungu ikipigwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.

Rais Lungu akikagua gwaride lililoandaliwa kwa heshima yake

Viongozi mbalimbali wakiwemo Waheshimiwa Mabalozi wa nchi za Afrika wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini wakishuhudia mapokezi ya Rais Lungu

Rais Lungu na mwenyeji wake wakiangalia vikundi vya utamaduni vinavyotoa burdani uwanjani hapo

Sunday, November 27, 2016

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI



  ZIARA YA KIKAZI NCHINI TANZANIA YA MHE. IDRISS DEBY ITNO, RAIS WA JAMHURI YA CHAD NA MWENYEKITI WA UMOJA WA AFRIKA
TAREHE 27-28 NOVEMBA, 2016

Mheshimiwa Idriss Deby Itno, Rais wa Jamhuri ya Chad na Mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Afrika atakuwa na Ziara ya Kikazi nchini Tanzania tarehe 27-28 Novemba, 2016.

Mheshimiwa Rais Deby atawasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam tarehe 27 Novemba 2016 saa 8:00 mchana na kulakiwa na Mwenyeji wake Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muugano wa Tanzania. Aidha, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Viongozi wengine waandamizi wa Serikali ya Tanzania watakuwepo uwanja wa Ndege katika mapokezi hayo.

Akiwa hapa nchini, Mheshimiwa Rais Deby na Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki watakuwa na mazungumzo rasmi Ikulu, ambapo watapata fursa ya kubadilishana mawazo kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu Ukanda wa Afrika Mashariki na Umoja wa Afrika kwa ujumla.

Mheshimiwa Rais Deby ni Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika kwa Mwaka 2016-2017, kipindi ambacho Umoja huo umeendelea kukabiliana na changamoto mbalimbali barani Afrika, zikiwemo ugaidi, amani na usalama, na changamoto  za maendeleo.

Ujumbe wa Rais wa Chad  unawajumuisha Mke  wa Rais  Mama  Hinda Deby Itno, Mheshimiwa Moussa Faki Mahamat, Waziri wa Mambo ya Nje, Mtangamano wa Afrika, na Ushirikiano wa Kimataifa na viongozi wengine waandamizi wa Serikali ya Chad.

Imetolewa na: KITENGO CHA MAWASILIANO YA SERIKALI, WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI
27 NOVEMBA, 2016

Saturday, November 26, 2016

Makamu wa Rais Mhe. Samia Hassan azindua majengo ya Umoja wa Mataifa (MICT)


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia katika hafla ya uzinduzi wa Taasisi mpya ya kimataifa MICT(Mechanism for International Criminal Tribunals) ambayo imechukua majukumu ya iliyokuwa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ya Rwanda (ICTR). 

 Uzinduzi huo ulifanyika tarehe 25 Novemba, 2016 katika eneo la Lakilaki nje kidogo ya Jiji la Arusha na kuhudhuriwa na Wawakilishi wa mashirika ya kimataifa, Viongozi waandamizi wa Serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania kutoka Taasisi na Mashirika ya Umma, Serikali Kuu na Serikali za Mitaa kwa upande wa Jiji la Arusha  pamoja na sehemu ya wakazi wa Arusha.
Rais wa Taasisi ya MICT (Mechanism for International Criminal Tribunal), Jaji Theodor Meron akihutubia wageni waalikwa katika hafla ya uzinduzi wa majengo ya Kisasa ya MICT.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi, Dkt. Augustine Mahiga (Mb), akiwasalimia wageni waalikwa pamoja na kumkaribisha rasmi Makamu wa Rais Mhe. Mama Samia ili aweze kuhutubia wageni waalikwa. Pamoja na salamu Mhe. Waziri alieleza eneo lililotengwa na Serikali kwaajili ya Taasisi za Kimataifa lina ukubwa wa ekari 430 ambapo ekari 16 zimegaiwa kwa MICT na mpaka sasa zimeshatumika ekari tano tu katika ujenzi wa majengo ambayo yalifanyiwa uzinduzi.
Mhe. Makamu wa Rais akizindua rasmi majengo ya MICT tayari kwa kuanza kutumika. Walioko nyuma kutoka kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Gambo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi, Dkt. Augustine Mahiga na  Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Sheria Bw. Miguel de Serpa Soares .
Mhe. Makamu wa Rais akizungumza wa wakandarasi wa kitanzania ambao walishinda zabuni ya kujenga majengo ya kisasa ya MICT.
Mhe. Mama Samia akitembelea jengo la kuhifadhia nyaraka ambalo litakuwa na huduma tatu ambazo ni pamoja na Maktaba ya sheria; chumba cha kuhifadhia nyaraka kinachoonekana katika picha kinahudumu katika nyuzi joto 24 lilonashauriwa kitaalamu kuhifadhi nyaraka hizo.
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi, Dkt Aziz Mlima akipokea ufafanuzi kutoka kwa Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Celestine Mushy walipotembelea jengo la Mahakama.

Msajili wa MICT, Bw. John Hocking akitoa maelezo kwa Mhe. Makamu wa Rais alipotembelea katika jengo la Mahakama na kupewa ufafanuzi juu ya mpangilio wa kukaa mahakamani hapo wakati kesi zitakapoanza kusikilizwa.
Mhe. Makamu wa Rais akipanda mti katika eneo la majengo ya MICT katika kuhifadhi mazingira.

Mhe. Waziri Mahiga akipanda mti mbele ya jengo la utawala, pembeni yake ni Msaidizi wake Bw. Gerald Mbwafu na Afisa wa MICT.


Mhe. Mama Samia akimkabidhi zawadi Bw. Hocking ikiwa ni pongezi kwa kazi nzuri aliyoifanya kwa kusimamia ujenzi huo. Pia Bw. Hocking amemaliza muda wake wa kuhudumu MICT nchini.

Wazee wa kimila kutoka kabila la Wamasai, wenyeji wanaoishi jirani na Taasisi ya MICT katika vilima vya Lakilaki wakiombea baraka eneo la MICT kabla ya zoezi rasmi la uzinduzi.
Kutoka kulia ni Katibu Mkuu, Balozi Dkt. Aziz Mlima, Balozi wa kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Mhe. Tuvako Manongi na Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Mushy wakifuatilia hotuba ya Mhe. Makamu wa Rais.
Kushoto ni Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Baraka Luvanda akifuatilia hotuba.


Wa pili kulia ni Bw. Gerald Mbwafu, Bi. Blandina Kasagama na Bi. Sekela Mwambegele maafisa wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakifuatilia hafla ya uzinduzi.

Picha ya pamoja ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Rais wa MICT, Mabalozi kutoka Wizarani na viongozi wengine wa MICT pamoja na Mkandarasi wa majengo ya MICT.

Makamu wa Rais akiwa katika picha ya pamoja meza kuu, kutoka kushoto ni John Kocking (Msajili MICT), Theodor Meron (Rais wa MICT), Miguel de Serpa Soares (Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Sheria), kulia ni Mhe. Dkt. Augustine Mahiga ( Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki), Mhe. Mrisho Gambo (Mkuu wa Mkoa wa Arusha), Serge Brammertz (Mwendesha Mashitaka MICT) na Jaji Mohamed Chande Othman (Jaji Mkuu).

Picha ya Pamoja meza kuu na wawakilishi kutoka Serikali ya Tanzania na Umoja wa Mataifa.

Majengo yaliyozinduliwa, kutoka kushoto ni Mahakama, Jengo la Utawala na kulia ni jengo la kuhifadhia nyaraka ambalo ndani yake lina maktaba.
Mti wa asili unaowakilisha amani (Christmas Tree) ambao ulikuwa umekauka  katika eneo la mradi umefanyiwa jitihada za makusudi za kuhudumiwa ili uweze kuota tena.
==========================================================================

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia     Suluhu Hassan amezindua majengo  ya Taasisi mpya ya Kimataifa MICT ambayo inachukua majukumu ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ya Rwanda (ICTR). Uzinduzi huo umefanyika tarehe 25 Novemba, 2016 katika eneo la Lakilaki Jijini Arusha. 

Taasisi hiyo mpya ijulikanayo kama Mfumo wa Kimataifa wa kumalizia Mashauri Masali (international Residual Mechanism for Criminal Tribunal)  ya iliyokuwa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ya Rwanda (ICTR)  imejengwa katika eneo la Lakilaki  nje Kidogo ya Jiji la Arusha.

Pamoja na kuendesha Mashauri Masalia ambayo hayakukamilika baada ya Mahakama ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda kumaliza muda wake,  pia taasisi hiyo itahifadhi nyaraka pamoja na kutoa huduma ya maktaba bure kwa umma hususan katika taaluma ya Sheria ambapo imefanikisha kuanzisha makataba kubwa ya Mfano ya Sheria za Kimataifa katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Mhe. Samia alieleza kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano itaendelea kutoa ushirikiano wa hali na mali kwa Shirika la Umoja wa Mataifa (UN) katika kuhakikisha Taasisi hiyo mpya inafanya kazi zake kwa tija ikiwa pamoja na kusimamia Haki za Binadamu, Utawala wa Sheria pamoja na usawa wa jinsia katika nafasi zote unapewa kipaumbele nchini.

“Aidha napenda nimshukuru Msajili wa Taasisi ya MICT,  Bw. John Hocking ambaye siku zote ameendelea kujitoa kwa hali na mali katika kusimamia ujenzi wa mradi huu na kuhakikisha unakamilika na kuanza kazi kwa wakati, pamoja na wafanyakazi wote wa MICT” alisema Mhe. Samia.

Aidha, Rais wa MICT Jaji Theodor Meron aliishukuru Serikali ya Tanzania hususan Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambao walikuwa waratibu wakuu katika ufuatiliaji na usimamizi wa mradi sambamba na Taasisi nyingine za Umma kama Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mamlaka ya Maji, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Jiji la Arusha kwa ujumla, Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na Shirika la Simu Tanzania (TTCL).

Halikadharika alitoa shukrani za pekee kwa Serikali ya awamu ya nne chini ya Rais Mstaafu  Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete pamoja na Serikali ya awamu ya Tano chini ya Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa ushirikiano waliotoa katika kufanikisha kukamilika kwa mradi.
 
Jaji Theodor pia alieleza majengo ya Taasisi ya MICT yamejengwa kwa kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 8.78 fedha za nchi wanachama za Umoja wa Mataifa na kwamba ardhi kwaajili ya ujenzi ilitolea bure na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania sambamba na huduma nyingine zilizokuwa zikiambana na ujezi huo kama maji, umeme, matengenezo ya barabara katika kiwango cha lami ambayo imeitwa "barabara ya haki", huduma ya mtandao na vifaa vya kujengea ambavyo ni rasilimali ya Tanzania na pia ujenzi huo umetumia mkandarasi mzawa kutoka nchini Tanzania. 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga ameshukuru Shirika la umoja wa Mataifa kwa maamuzi yake mazuri ya kuipa Tanzania heshima ya kuwa mwenyeji wa Taasisi hiyo na akasema Serikali ya Tanzania itahakikisha haki inasimamiwa katika kesi za kimataifa na akakaribisha mashirika mengine ya Kimataifa kuja kujengwa nchini Tanzania. Pia kwa wale wanaofanya tafiti kuhusiana na Taasisi nyingine za kimataifa ni mahali sahihi kwaajili ya kufanikisha tafiti zao.

Mwaka 2010 Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa, lilipitisha Azimio nambari 1966 la kuanzisha Mfumo wa Kimataifa utakaomalizia mashauri ya Masalia kwa iliyokuwa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ya Rwanda (ICTR) yaliyotokea mwaka 1994 na Mauaji ya Halaiki yaliyotokea katika iliyokuwa Yugoslavia ya Zamani (ICTY).  Katika azimio hilo Baraza kuu lilibainisha wazi kwamba Arusha itakuwa makao  makuu ya Tawi hilo jipya la MICT na The Hague kuwa makao makuu ya Tawi Jingine.

Thursday, November 24, 2016

Waziri Mahiga ampokea Mjumbe Maalum kutoka Senegal

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Augustine Mahiga (kulia), akipokea Ujumbe Maalum kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kutoka kwa Rais wa Senegal, Mhe. Macky Sall, kupitia kwa Waziri wake wa Maji, Mhe. Amodou Mansour Faye. Mara baada ya makibidhiano hayo Waziri Mahiga na Waziri Faye walifanya mazungumzo ambayo yalijikita katika kuimarisha na kuendeleza mahusiano mazuri kati ya Tanzania na Senegal.
Mazungumzo yakiendelea.
Waziri Mahiga akiagana na Mjumbe Maalum, Mhe. Faye mara baada ya kumaliza mazungumzo.

Taarifa kwa Vyombo vya Habari

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe.  Dkt. Augustine Mahiga amefanya mazungumzo na waandishi wa  habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari hapa nchini katika Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar Es Salaam. Katika mazungumzo hayo. Mhe. Waziri aliwahabarisha kuhusu ziara ya Rais wa Zambia, Mhe Edgar Lungu anayetarajiwa kuifanya nchini kuanzia tarehe 27 - 29 Novemba 2016.
Waziri Mahiga akiendelea kuzungumza na waandishi wa habari 


Balozi wa Tanzania nchini Zambia, Mhe. Grace Mujuma  akielezea jambo kwa waandishi wa habari waliohudhuria mkutano huo (hawapo pichani), wa kwanza kutoka kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Mindi Kasiga.
Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Samuel Shelukindo naye akielezea faida zitakazo tokana na ziara nzima ya Rais wa Zambia
Sehemu ya waandishi wa habari wakiwa katika kikao na Waziri Mahiga.

1.Rais wa Zambia, Mhe. Edgar Lungu kuzuru Tanzania Novemba 27 - 29, 2016

UTANGULIZI

1.1        Ndugu waandishi, nimewaita leo ili kuwaeleza kuhusu Ziara Rasmi hapa nchini ya Mhe. Edgar Chagwa Lungu, Rais wa Jamhuri ya Zambiainayotarajiwa kufanyika hapa nchini. Najua baadhi yenu mtakuwa mmekwishasikia taarifa za Rais huyokufika nchini hivi karibuni.

1.2        Sasa niwatangazie rasmi kuwa taarifa hiyo ni sahihi na ziara hiyo itafanyika kuanzia tarehe 27 hadi 29 Novemba 2016. Hii ni ziara Rasmi ya kwanza kwa Mhe. Rais Lungu kuifanya nchini tangu alipochaguliwa katika nafasi hiyo ya Urais mwezi Septamba, 2016.

1.3        Ndugu Waandishi, mnafahamu kwamba, mbali na kuwa nchi majirani, mahusiano  kati ya nchi za  Tanzania na Zambia yana historia ndefu, tangu enzi ya waanzilishi wa mataifa haya mawili, yaani Mwalimu Julius Nyerere wa Tanzania na Mzee Kenneth Kaunda wa Zambia.

1.4        Ifahamike kuwa, kutokana na mahusiano haya ya karibu ndipo nchi za Tanzania na Zambia kwa pamoja zilifanya uamuzi wa kihistoria wa kutekeleza mradi mkubwa wa ushirikiano wa ujenzi wa Reli ya TAZARA. Licha ya kwamba mradi huo ni wa kimaendeleo, lakini pia Reli hiyo ya TAZARA ilitoa mchango mkubwa katika ukombozi wa bara la Afrika, wakati ambapo Tanzania na Zambia zikiwa miongoni mwa nchi ziizokuwa mstari wa mbele katika harakati za ukombozi (Frontline States).

1.5        Mradi mwingine mkubwa ambao nchi zetu mbili zimeufanya kwa ushirikiano ni mradi wa Bomba la Mafuta la TAZAMA.

Ndugu waandishi, haya, pamoja na mengineyo mengi ambayo nitayaeleza baadaye, yanaufanya ugeni huu kuwa wa muhimu na wa heshima kubwa sana kwetu.

1.6        Mhe. Rais Lungu anafika nchini kufutia mwaliko rasmi kutoka kwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na akiwa nchini, pamoja na mambo mengine, atafanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake Mheshimiwa Rais Magufuli. Mhe. Rais Lungu ataambatana na Maafisa wengine Waandamizi wa Serikali ya Zambia.

2.0       RATIBA YA MGENI KWA KIFUPI

Ndugu Waandishi, sasa niwaeleze kwa kifupi ratiba ya ziara hiyo.

2.1        Mhe. Rais Lungu anatarajiwa kuwasili nchini siku ya jumapili tarehe 27Novemba 2016saa 10 kamili jioni katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere kwa ndege maalumu ambapo atalakiwa na Viongozi mbalimbali wa Kitaifa wakiongozwa na mwenyeji wake Mhe. Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, ambapo atapigiwa mizinga 21 ya kijeshi kwa heshima yake kumkaribisha nchini.

2.2        Siku inayofuata ya tarehe 28 Novemba 2016 asubuhi, Mhe. Rais Lungu atatembelea Makao Makuu ya Mamlaka ya TAZARA ili kujionea shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na Shirika hilo la ubia baina ya nchi zetu mbili. Baada ya kutoka TAZARA, Mhe. Lungu atazuru pia Shirika la Bomba la Mafuta la TAZAMA, ambapo atatembelea mitambo ya kupampu mafuta, pamoja na matenki ya kuhifadhi mafuta ya TAZAMA vyote vilivyopo eneo la Kigamboni.

2.3        Baada ya ziara hizo za asubuhi, Mhe. Rais Lungu pamoja na ujumbe wake watafanya mazungumzo rasmi na Mhe. Rais Magufuli, pamoja na Viongozi Waandamizi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mazungumzo hayo yatafanyikia Ikulu kuanzia saa 5 kamili? mchana.

2.4        Baada ya mazungumzo rasmi, Mhe. Rais Lungu pamoja na mwenyeji wake Mhe. Rais Magufuli watashuhudia utiaji saini wa Makubaliano na Mikataba mbalimbali minne(4) ya ushirikiano baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzaniakwa upande mmoja na Serikali ya Jamhuri ya Zambia kwa upande mwingine. Kwa kifupi mikataba hiyo inahusu kuimarisha na kukuza zaidi mahusiano mazuri yaliyopo baina ya nchi zetu mbili.

2.5        Jioni ya siku hiyo, Mhe. Rais Lunguatahudhuriadhifa ya kitaifa(State Banquet) itakayoandaliwa  kwa heshima yake na Mhe. Rais Magufuli. Dhifa hiyo itafanyika Ikulu kuanzia saa 12 na nusu jioni. Hilo ndilo litakuwa tukio la mwisho kwa siku ya kwanza hiyo.

2.6        Siku itakayofuata ya tarehe 29 Novemba 2016, Mhe. Rais Lungu atatembelea Bandari ya Dar es Salaam ambapo atajionea shughuli mbalimbali za upokeaji na upitishwaji wa mizigo bandarini hapo. Baada ya tukio hilo, Mhe. Rais Lungu atafanya ziara fupi kwenye Kampuni ya kusafirisha mizigo inayomilikiwa na Zambia inayojulikana kama Zamcargo.

2.7        Baada ya hapo Mhe. Rais Lungu ataelekea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius K. Nyerere ambapo ataagwa rasmi na mwenyeji wake Mhe. Rais Magufuli kurejea nchini Zambia.

3.0       MANUFAA YA ZIARA HIYO

3.1        Ndugu Waandishi, kama nilivyoeleza awali, mahusiano yetu na Zambia ni ya kidugu na yana historia ndefu. Kupitia uhusiano huo, Tanzania na Zambiazimeendelea kufanya kazi kwa kuaminiana na kushirikiana katika nyanja mbalimbali za kitaifa, kikanda na kimataifa. Hivyo, ziara hii ya Mhe. Rais Lungu, itatoa fursa ya kuimarisha zaidi mahusiano hayo kwa manufaa ya Serikali na wananchi wa Tanzania na Zambia.

3.2         Kwa upande wa ushirikiano wa kiuchumi, ziara hiyo inatarajiwa kuzidisha zaidi uhusiano katika maeneo bayana kama ifuatavyo:

a).  Kukuza ushirikiano ili kuongeza ufanisi wa Reli ya TAZARA:
·        Kama nilivyoeleza hapo awali, Reli ya TAZARAni mhimili na kiungo muhimu sana katika ukuzaji wa uchumi wa Tanzania na Zambia, lakini pia na kwa nchi nyingine majirani za ukanda wa kusini na kati mwa Afrika za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Zimbabwe, Malawi n.k. Reli hiyo inatoa huduma ya usafirishaji wa mizigo, rasilimali ghafi pamoja na abiria katika nchi hizo.

·        Hata hivyo, kama ambavyo wengi wenu mtakuwa mnafahamu, ufanisi wa Reli ya TAZARA umekuwa chini ya matarajio ya wadau wa sekta hiyo ya usafiri. Serikali za Tanzania na Zambia kama wamiliki wa Reli hiyo kwa ubia sawa wa 50% kwa 50% zimeendeleakuchukua hatua mbalimbali kuisaidia TAZARA, hususan kwa kushirikiana na marafiki zetu Serikali ya China.

·        Napenda kuwataarifu kuwa, katika ziara hii ya Mhe. Rais Lungu, suala hili la TAZARA litajadiliwa kwa kina baina ya viongozi hao wawili ili Shirika hilo liweze kuongeza ufanisi na kujiendesha kwa tija kibiashara.

b). Kukuza Ushirikiano katika Matumizi ya Bomba la TAZAMA.
·        Ndugu waandishi, bomba la TAZAMA lilijengwa mwaka 1968 kwa lengo la kutoa njia nafuu ya Kusafirisha mafuta ghafi kwenda nchini Zambia na hivyo kuiepusha nchi hiyo na athari za kupanda kwa bei ya mafuta. Hata sasa umuhimu wa bomba hilo bado upo.

·        Nchi zetu mbili zinamiliki bomba hilo kwa ubia ambapo Zambia ina mtaji wa mbili ya tatu na Tanzania inamiliki bomba hilo kwa mtaji wa moja ya tatu. Bomba hilo limekuwa likijiendesha kibiashara kwa faida na limeendelea kuziingizia kipato nchi zetu mbili.

·        Wakati wa ziara hii ya Mhe. Rais Lungu, suala la TAZAMA linatarajiwa pia kujadiliwa, hususan namna ya kulifanya bomba hilo kufanya kazi kwa ufanisi zaidi kwa manufaa ya nchi zetu mbili.

c).  Ushirikiano katika Matumizi ya Bandari ya Dar es Salaam:
·        Ndugu Waandishi, kama mnavyofahamu kuwa nchi ya Zambia haina bahari (land locked country), na kwa muda mrefu imekuwa ikitumia Bandari ya Dar es Salaam kupitisha mizigo yake. Kwa sababu za kiuchumi na za kihistoria, nchi hiyo imeendelea kuwa mdau mkubwa katika matumizi ya bandari hiyo.
·        Tunatarajia pia wakati wa ziara hiyo, Viongozi wetu wawili watapata fursa ya kujadiliana kuhusu suala hilo.

3.3         Ndugu waandishi, yapo masuala mengine ya ushirikiano baina ya nchi zetu mbili yatakayojadiliwa wakati wa ziara hiyo na taarifa kamili itatolewa baada ya kukamilika kwa ziara hiyo.

4.0       HITIMISHO

5.1    Ndugu waandishi, kwa mara nyingine tena tunatarajia kumpokea kiongozi wa kitaifa kutoka nje ya nchi. Huu ni mwendeleze wa utekelezaji mzuri wa Sera ya Mambo ya Nje inayosimamiwa vizuri na Serikali ya Awamu ya Tano ambapo tunanuia kuimarisha mahusiano yetu, hususan ya kiuchumi, na nchi zote majirani na nyinginezo barani Afrika na  kote duniani. 

5.2    Hivyo basi, kupitia kwenu, napenda kuchukua fursa hii kuwaomba Watanzania wote kwa ujumla tujitokeze kwa wingi kumlaki Mhe. Rais Lungu atakapokuwa anawasili kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius K. Nyerere mpaka Hoteli ya Hyatt Regency/Kilimanjaro atakapofikia kwa kupitia Barabara ya Julius K. Nyerere/Pugu.

Asanteni!