Thursday, April 6, 2017

Tanzania na Uganda zakubaliana kushirikiana

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ramadhan Mwinyi ambaye alikuwa mwongozaji wa kikao cha Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kwa ngazi ya Mawaziri kati ya Tanzania na Uganda akitoa neno la ukaribisho kwa wajumbe waliohudhuria kikao hicho.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda, Mhe. Sam Kutesa wakiweka saini Nyaraka yenye maelezo ya masuala yote yaliyokubaliwa katika kikao cha JPC kati ya Tanzania na Uganda. 

Waziri Mahiga na Mgeni wake, Mhe. Sam Kutesa wakionesha nakala za nyaraka za makubaliano mara baada ya kusaini.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda, Mhe. Sam Kutesa wakiweka saini Mkataba utakaotoa fursa kwa Tanzania na Uganda kushirikiana katika huduma za usafiri wa anga.

Prof. Mbarawa na Mhe. Kutesa wakionesha nakala za mikataba mara baada ya kuisaini.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga na Waziri wa Nishati na Madini wa Uganda, Mhe. Mhandisi Irene Muloni wakiweka saini Mkataba ambapo Tanzania na Uganda zitashirikiana kuendeleza mradi wa umeme wa kutumia maji wa MW 14 katika eneo la Kikagati/Murongo. 

Waziri Mahiga na Mhandisi Muloni wakibadilishana nakala za mikataba.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga akisoma hotuba ya kufunga kikao cha JPC kati ya Tanzania na Uganda.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda, Mhe. Sam Kutesa akisoma hotuba kwa wajumbe walioshiriki kikao cha JPC kati ya Tanzania na Uganda


Baadhi ya Viongozi waandamizi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania walioshiriki kikao cha JPC kati ya Tanzania na Uganda. Wa kwanza kulia ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. William Lukuvi na wa pili ni Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Prof. Makame Mbarawa.

Ujumbe wa Tanzania ukifuatilia hotuba za Waheshimiwa Mawaziri wa Mambo ya Nje

Viongozi wa ngazi ya juu wa Serikali ya Uganda wakisikiliza hotuba za Mawaziri.

Ujumbe wa Tanzania ukifuatilia mkutano

Bw. Gerald Mbwafu (kulia) kutoka Wizara ya Mambo ya Nje akisalimiana na Mkurugenzi Msaidizi wa Masuala ya Maji, Bw. Sylvester Matemu kutoka Wizara ya Maaji.

Maafisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje wakionesha nyuso za furaha kuashiria furaha yao baada ya kufanikisha mkutano wa JPC.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

TANZANIA NA UGANDA ZAKUBALIANA KUSHIRIKIANA

Tanzania na Uganda zimefungua sura mpya ya ushirikiano baada ya Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi hizo kusaini nyaraka inayoainisha maeneo mbalimbali ambayo nchi hizo zimekubali kushirikiana kwa pamoja ili kuinua uchumi wa mataifa yao.

Nyaraka hiyo iliyosainiwa leo jijini Arusha imetokana na Kikao cha Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC)  kati ya Tanzania na Uganda kilichofanyika kwa siku tatu kuanzia tarehe 03 Aprili 2017.

 "Makubaliano haya yataongeza chachu ya uhusiano na ushirikiano wetu na Uganda, japokuwa tulichelewa kufanya kikao cha JPC tokea mkataba uliposainiwa mwaka 2007 nchini Uganda". Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga alisema alipokuwa akisoma hotuba ya kufunga.

Kikao cha JPC kilifanyika kwa kuzingatia makundi ya kisekta ambapo katika kila kundi, wajumbe waliainisha maeneo yenye maslahi kwa pande zote ambayo yanajumuisha pamoja na mambo mengine: uendelezaji wa miundombinu; kilimo; viwanda; biashara; uwekezaji; nishati; utalii; utunzaji wa mazingira; uvuvi; ufugaji; afya; elimu; utangazaji; madini na masuala ya kijamii.

Kikao hicho kilitarajiwa kuhitimishwa kwa kusainiwa mikataba sita lakini kutokana na mashauriano ya ndani ya baadhi ya mikataba kutokamilika, mikataba miwili ndio iliweza kusainiwa. Mikataba hiyo ni ushirikiano katika kuendeleza mradi wa Umeme wa kutumia maji wa MW 14 katika eneo la Kikagati/Murongo na huduma za usafiri wa anga.

Mikataba  minne iliyosalia ambayo inahusu ushirikiano katika usafiri wa reli, usafiri wa majini; utangazaji na ulinzi wa raia itasainiwa wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) utakaofanyika hivi karibuni hapa nchini.

Waziri Mahiga alieleza kuwa kusainiwa kwa  mikataba hiyo ni muhimu kwa kuwa itaimarisha zaidi misingi ya mahusiano yetu, hivyo alizihimiza pande zote kukamilisha mashauriano hayo ili mikataba hiyo iweze kusainiwa katika muda uliopangwa.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda, Mhe. Sam Kutesa alisisitiza umuhimu wa Tanzania na Uganda kufanya kazi kwa pamoja ili kuinua uchumi kwa madhumuni ya kuwaondolea umasikini wananchi.

Alisema mradi wa ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Uganda hadi Tanzania ni moja ya miradi itakayosaidia kuboresha maisha ya wananchi, hivyo alisisitiza umuhimu wa kukamilisha taratibu zote zilizosalia ili ujenzi huo uweze kuanza.

Alihitimisha hotuba yake kwa kuzipongeza Tanzania na Uganda kwa kufanikisha uwekaji saini wa mikataba miwili ukiwemo wa kuendeleza mradi wa Umeme wa kutumia maji wa MW 14 katika eneo la Kikagati/Murongo ambao ulikuwa katika majadiliano kwa zaidi ya miaka minane.

 Kikao hicho cha JPC kimefanyika kufuatia maelekezo ya Marais wa nchi hizo waliyoyatoa wakati wa ziara ya Rais wa Uganda nchini mwezi Februari 2017. Viongozi hao waliagiza kikao cha JPC kifanyike kabla ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambao ulipangwa kufanyika jijini Dar Es Salaam tarehe 06 Aprili 2017.

-Mwisho-
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar Es Salaam, 05 Aprili, 2017


Wednesday, April 5, 2017

Rais Magufuli awaapisha Mabalozi wa Tanzania nchini India na Afrika Kusini.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akimuapisha Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Mhe. Sylivester M. Ambokile. Hafla za uapisho huo zimefanyika leo Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais Magufuli akimkabidhi vitendea kazi Mhe. Ambokile.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akimuapisha Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Baraka H. Luvanda . Hafla za uapisho huo zimefanyika leo Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais Magufuli akimkabidhi vitendea kazi Mhe. Luvanda
Sehemu ya viongozi waandamizi wa Serikali na wageni waalikwa waliohudhuria  hafla za uapisho wakiwapongeza viongozi wateule mara baada ya kuapishwa.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufili (mstari wa mbele katikati), Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan (wa pili kushoto), Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi (wa pili kulia) wakiwa katika picha ya pamoja na waheshimiwa Mabalozi walioapishwa na uongozi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Monday, April 3, 2017

Kikao cha JPC kati ya Tanzania na Uganda chafunguliwa jijini Arusha

Ujumbe wa meza kuu, kutoka kulia ni Balozi Innocent Shiyo, Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki; Dkt. Leonard Chamhilo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano; Balozi Ramadhan Mwinyi, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje, Balozi Patrick Mugoya, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Uganda. Mkuu wa Jeshi la Polisi la Uganda.

Bw. Aman Mwatonoka, Mkurugenzi Msaidizi wa Masuala ya Siasa katika Wizara ya Mambo ya Nje ambaye pia ni mwongozaji wa kikao hicho akimkaribisha Naibu Katibu Mkuu, Balozi Mwinyi ili aweze kutoa hotuba ya ufunguzi.

Naibu Katibu Mkuu ambaye ni Mwenyekiti wa kikao hicho, Balozi Ramadhan Mwinyi akitoa hotuba ya ufunguzi.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Uganda, Balozi Patrick Mugoya akihutubia wajumbe wa kikao cha JPC kati ya Tanzania na Uganda.

Balozi Innocent Shiyo, Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda katika Wizara ya Mambo ya Nje akifafanua jambo kuhusu utaratibu wa kuendesha kikao hicho.

Mhe. Grace Mgavano, Balozi wa Tanzania nchini Uganda akijitambulisha kwa wajumbe.

Wajumbe wa kikao wakifuatilia hotuba za ufunguzi.

Ujumbe wa Uganda ukifuatilia mkutano.

Sehemu nyingine ya ujumbe wa Tanzania uliohudhuria mkutano huo.

Picha ya pamoja
 
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

KIKOA CHA JPC KATI YA TANZANIA NA UGANDA CHAFUNGULIWA JIJINI ARUSHA

Tanzania na Uganda zimetakiwa kushirikiana kwa pamoja kutumia rasilimali walizonazo kutatua changamoto zinazowakabili wananchi wa pande zote mbili.

Kauli hiyo imetolewa leo kwa pamoja jijini Arusha na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ramadhan Mwinyi na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Uganda, Balozi Patrick Mugoya walipokuwa wanafungua Kikao cha Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya nchi hizo mbili.

Walieleza kuwa kikao hicho ni cha kwanza kufanyika tokea makubaliano yaliposainiwa mwaka 2007 na kinafanyika kufuatia maelekezo ya Marais wa nchi hizo waliyoyatoa wakati wa ziara ya Rais Yoweri Museveni nchini mwezi Februari 2017.

"Kikao hiki ni fursa kwa wataalamu wetu kujadili na kubuni mfumo bora na endelevu wa Ushirikiano utakaoleta tija kwa pande zote mbili katika kila eneo iwe miuondombinu, biashara, viwanda, uwekezaji, usafiri wa anga na majini, kilimo, elimu, afya, mazingira, utalii, nishati na ufugaji.

Balozi Mwinyi alieleza kuwa licha ya nchi hizo mbili kuwa na mahusiano mazuri tokea miaka ya 60 lakini kiwango cha biashara kati yao ni kidogo mno hivyo aliwashauri wajumbe wa JPC kubuni mikakati itakayonyanyua kiwango cha biashara.

Kwa upande wake, Balozi Mugoya aliwambia wajumbe wa kikao hicho kuwa Tanzania na Uganda sio tu ni nchi majirani, bali ni nchi zenye urafiki mkubwa, hivyo alihimiza urafiki huo utumike kushughulikia changamoto zinazowakabili wananchi wa pande zote. " Tuna changamoto za ukame, uhaba wa maji na malisho kwa wafugaji na wakulima wanaoishi katika mipaka yetu. Hivyo alisisitiza umuhimu wa kikao hicho kutoa mapendekezo ya namna ya kushirikiana kwa kutumia rasilimali zilizopo mipakani na nyinginezo kukabiliana nazo".

Kikao hicho cha JPC kitafungwa rasmi siku ya Jumatano na Mawaziri wa Mambo ya Nje ambapo kabla ya kufungwa kutashuhudiwa uwekaji saini wa makubaliano mbalimbali kati ya Tanzania na Uganda. Makubaliano hayo ni pamoja na Ushirikiano katika kuboresha bandari, usafiri wa majini na huduma ya usafiri wa reli; kuendeleza mradi wa Umeme wa kutumia maji wa MW 14 katika eneo la Kikagati/Murongo; Ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi la Tanzania na lile la Uganda katika masuala ya usalama, Ushirikiano kati ya Wizara ya Elimu, Sayansi naTeknolojia na Wizara ya Elimu ya Uganda, Ushirikiano kati ya Shirika la Utangazaji la Tanzania na la Uganda na Ushirikiano katika huduma za usafiri wa Anga.

-Mwisho-
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar Es Salaam, 03 Aprili, 2017


SADC yalipongeza Baraza la Usalama la UN kwa kuongeza muda kwa Misheni ya Ulinzi DRC


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) kuhusu mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa uliofanyika New York, Marekani na kupitisha Azimio la kuongeza muda kwa vikosi vya usalama vilivyopo DRC. Kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Celestine Mushy.
Baadhi ya waandishi wa habari wakimsikiliza Mhe. Mahiga (hayupo pichani).
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri ya Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (Mb). akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Jijini New York, Marekani.
 =============================================




TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambaye pia ni Mwenyekiti wa  Kamati ya Mawaziri ya Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Mhe. Dkt. Augustine Mahiga  amelipongeza Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC) kwa kuridhia na kupitisha azimio namba 2348 (2017)  la kuongeza muda kwa Misheni ya Ulinzi wa Amani chini ya MONUSCO iliyopo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) hadi tarehe 31 Machi, 2018.

Mhe. Mahiga ametoa pongezi hizo wakati akihutubia Baraza hilo kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa Jijini New York, Marekani hivi karibuni.

Mhe. Mahiga ambaye aliwakilisha nchi 15 za SADC alisema kuwa  anaupongeza Umoja wa Mataifa kwa ujumla chini ya uongozi wa Katibu Mkuu, Bw. Antonio Guterres kwa kufikia uamuzi wa kuongeza muda kwa MONUSCO na jitihada nyingine nyingi za kutafuta suluhu ya kudumu kwa changamoto mbalimbali zinazoikabili  DRC kwa muda mrefu ikiwemo ukosefu wa amani na usalama.

Mhe. Mahiga alisema kuwa, kupitishwa kwa azimio hilo kunatoa matumaini mapya kwa wananchi wa DRC na dunia kwa ujumla kwamba Umoja wa Mataifa una nia ya dhati kuhakikisha amani ya kudumu inapatikana nchini humo.

Aidha, Mhe. Waziri Mahiga alitumia nafasi hiyo kuuomba  Umoja wa Mataifa kutambua mchango mkubwa unaotolewa na  Kikosi Maalum cha  Force Brigade Intervention-FIB kilichoundwa na SADC  ambacho kinashirikiana na MONUSCO katika ulinzi wa amani nchini DRC. 

Alieleza kuwa katika kipindi cha miaka minne tangu kuanzishwa kwa FIB kimeonesha uwezo mkubwa kwa kufanya operesheni ngumu za kukabiliana na vikundi vya waasi na kuvidhibiti, hali iliyopelekea MONUSCO kuaminika zaidi. FIB ina mchango wa vikosi vya ulinzi wa amani kutoka nchi tatu za SADC ambazo ni Tanzania, Afrika Kusini na Malawi.

“Kuanzishwa kwa FIB miaka minne iliyopita ulikuwa ni uamuzi wa pekee kwa Baraza la Usalama na SADC katika masuala ya ulinzi wa amani hususan kwenye maeneo yenye changamoto kubwa za usalama na amani. Hivyo naamini pamoja na kwamba FIB ni Chombo cha muda bado kinahitaji kutambuliwa na kupongezwa” alisema Waziri Mahiga.

Kuhusu changamoto mbalimbali  ambazo MONUSCO inakabiliana nazo ikiwemo matishio mapya ya usalama katika maeneo ya Kivu, mbinu mpya za mashambulizi za waasi, ukatili kwa raia na ukiukwaji wa haki za binadamu Waziri Mahiga alisema masuala haya yanailazimu pia MONUSCO kubadilisha mbinu za operesheni ikiwemo kuongezewa vifaa na bajeti ili kuweza kukabiliana kikamilifu  na changamoto hizo. 

Pia aliliomba Baraza la Usalama, SADC, Umoja wa Afrika, ICGLR na Nchi zinazoongea Kifaransa kushirikiana katika kutafuta suluhu ya kudumu kwa changamoto zinazoikabili DRC kwa sasa.

Vile vile, Mhe. Waziri Mahiga alitumia nafasi hiyo kwa niaba ya SADC kuiomba na kuialika Jumuiya za Kimataifa kuisaidia Tume ya Uchaguzi ya DRC  ili iweze kuandikisha wapiga kura na kuandaa uchaguzi nchi nzima. Pia aliwaomba wanasiasa wa nchini DRC kukabiliana na vurugu za kisiasa zinazoendelea nchini humo kwa sasa na kukwamisha utekelezaji wa Mkataba uliofikiwa mwezi Desemba 2016 chini ya Baraza la Maaskofu (SENCO) la DRC.

Mhe. Mahiga aliongeza kusema kuwa SADC itatuma Misheni Maalum ya Mawaziri nchini DRC katika kipindi cha majuma mawili kuanzia sasa kwa ajili ya kwenda kuzungumza na kushauriana na  wadau mbalimbali wa masuala ya siasa nchini DRC ili kutafuta suluhu.”Sisi , nchi wanachama wa SADC hatupo tayari kuona Mkataba wa Desemba unakwama” alisisitiza Waziri Mahiga.

-Mwisho-

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam, 03 Aprili, 2017.

Sunday, April 2, 2017

Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama yapitisha Bajeti ya Wizara

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Susan Kolimba (wa kwanza kushoto) akiwa na Viongozi wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama meza kuu kabla ya kuanza  kikao. Kamati hiyo imeridhia na kupitisha bajeti ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2017/2018 ambayo baadae itawasilishwa mbele ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kikao cha Kamati kikiendelea

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Ramadhani Mwinyi akifuatilia jambo wakati wa kikao

Naibu Waziri Mhe.Susan Kolimba akizungumza wakati wa Kikao

Saturday, April 1, 2017

Waziri Mkuu wa Ethiopia amaliza ziara nchini

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli (kulia) akiagana na Waziri Mkuu wa Shirikisho la Kidemokrasia la Jamhuri ya Ethiopia, Mhe. Hailemariam Dessalegn mara baada ya kumaliza ziara yake ya siku mbili nchini. Wakati wa ziara hiyo pamoja na mambo mengine alimaliza kwa kutembelea Bandari ya Dar es Salaam na Mhe. Dessalegn ameahidi kuitumia Bandari hiyo kupitisha mizigo ya nchi yake pamoja na kufanya biashara na nchi za Afrika Mashariki.Ziara hiyo ilifanyika kuanzia tarehe 31 Machi hadi 01 Aprili, 2017.
Mhe. Dessalegn akiagana na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Susan Kolimba (Mb) akiagana na Mhe. Dessalegn.
Waziri Mkuu, Mhe. Dessalegn akiagana na Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia, Mhe. Naimi Aziz mara baada ya kumaliza ziara yake hapa nchini
Waziri Mkuu, Mhe. Dessalegn akiagana na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Afrika, Balozi Innocent Shiyo mara baada ya kumaliza ziara yake hapa nchini
Waziri Mkuu Dessalegn akiagana na Afisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bi. Zulekha Tambwe.
 Mhe. Dessalegn akimpungia mkono wa kwaheri Rais Magufuli, viongozi mbalimbali wa Serikali na wananchi (hawapo pichani) waliofika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kwa ajili ya kumuaga  mara baada ya kumaliza rasmi ziara yake nchini.
Rais John Pombe Magufuli (wa kwanza kulia), Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Paul Makonda kwa pamoja wakimpunga mkono wa kwaheri kumuaga Mhe. Dessalegn (hayupo pichani). 

PRESS RELEASE