Thursday, November 9, 2017

Katibu Mkuu afanya mazungumzo na Mhe. Balozi wa China Nchini

 Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Adolf Mkenda akiwa katika mkutano na Balozi wa China Nchini Mhe. Wang Ke alipomtembelea Wizarani, tarehe 09 Novemba,2017.
 Katibu Mkuu Prof. Mkenda ( katikati), kushoto kwake ni Balozi wa China nchini Mhe. Wang Ke, wakiendelea na mazungumzo, wanaofutilia mazungumzo hayo ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia(wa kwanza kulia) Bi. Justa Nyange na anayefuata ni Afisa katika Idara hiyo Bw. Harmesh Lunyumbu.

Katibu Mkuu Prof. Mkenda akipokea zawadi kutoka kwa Balozi wa China Nchini Mhe. Wang Ke, baada ya mkutano

Katibu Mkuu wa Mambo ya Nje akutana kwa mazungumzo na Balozi wa Finland nchini

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Adolf Mkenda akimkaribisha Wizarani Balozi wa Finland nchini, Mhe. Pekka Hukka alipofika kwa ajili ya kujitambulisha kwake kama Katibu Mkuu mpya na kuzungumzia jinsi ya kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Finland. Mazungumzo hayo yalifanyika Wizarani tarehe 09 Novemba,  2017.
Prof. Mkenda akimweleza jambo Balozi Hukka wakati wa mazungumzo yao. Pamoja na mambo mengine wlizungumzia kuimarisha ushirikiano katika masuala ya elimu, biashara na uwekezaji ambapo Prof. Mkenda alitumia fursa hiyo kumshukuru Balozi Hukka kwa msaada unaotolewa na Serikali yake kwa Taasisi ya Uongozi.
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Salvatory Mbilinyi kwa pamoja na Bi. Tunsume Mwangolombe wakifuatilia mazungumzo kati ya Prof. Mkenda na Balozi Hukka (hawapo pichani)
Mazungumzo yakiendelea

Wednesday, November 8, 2017

Katibu Mkuu wa Mambo ya Nje akutana na Mjumbe Maalum kutoka Norway

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Prof. Adolf Mkenda akizungumza na Mjumbe Maalum kutoka Serikali ya Norway kwa Serikali ya Tanzania, Balozi Arild Oyen ambaye alifika Wizarani kwa ajili ya kuwasilisha ujumbe maalum. Pamoja na mambo mengine walizungumzia namna ya kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Norway hususan katika sekta za Nishati, Elimu na Utamaduni. Mazungumzo hayo yalifanyika Wizarani tarehe 08 Novemba, 2017.
Ujumbe wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakifuatilia mazungumzo kati ya Prof. Mkenda na Balozi Oyen (hawapo pichani). Kutoka kushoto ni Bw. Jestas Nyamanga, Mkurugenzi Msaidizi kutoka Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Salvatory Mbilinyi, Kaimu Mkurugenzi Idara ya Ulaya na Amerika na Bi. Ramla Hamis, Afisa Mambo ya  Nje.
Mazungumzo yakiendelea. Wa kwanza kushoto ni Balozi wa Norway nchini, Mhe. Hanne Marie Kaarstad.
Prof. Mkenda na Balozi Oyen wakimsikiliza Balozi Kaarstad mara baada ya kukamilisha mazungumzo yao
Prof. Mkenda akiagana na Balozi Oyen

Katibu Mkuu Prof. Mkenda afanya Mazungumzo na Balozi wa Japan Nchini

 Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Adolf Mkenda akiwa katika mkutano na Balozi wa Japan nchini Mheshimiwa Masaharu Yoshida alipomtembelea Wizarani leo tarehe 08 Novemba,2017. Katika Mkutano huu walizungumzia masuala mbalimbali yanoyohusu uhusiano kati ya Tanzania na Japan hasa katika eneo la uwekezaji.

 Prof.Mkenda akipokea zawadi ya Kalenda ya Mwaka 2018 kutoka kwa Mheshimiwa Balozi Yoshida, kalenda hiyo ni maalum yenye picha  zinazoelezea utamaduni wa Japan.

Katibu Mkuu Prof. Mkenda na Mhe. Balozi Yoshida pamoja na maafisa kutoka Wizarani na Ubalozi wa Japan wakiwa katika picha ya Pamoja baada ya Mkutano.

Waziri Mahiga amkaribisha rasmi Wizarani Katibu Mkuu mpya Prof.Mkenda

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akizungumza na Watumishi wa Wizara (hawapo pichani) wakati wa kikao rasmi cha kumkaribisha Katibu Mkuu mpya wa Wizara Prof. Adolf Mkenda (kulia). Kikao hicho kilifanyika hivi karibuni  katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere. Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi Rasilimali Watu, Bw. Hamid Mbegu.
Sehemu ya Wakurugenzi na Watumishi wa Wizara wakimsikiliza Waziri Mahiga (hayupo pichani)
Sehemu nyingine ya Wakuu wa Idara na Vitengo wakifuatilia kikao
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Adolf Mkenda akiwasalimia Watumishi wa Wizara (hawapo pichani) mara baada ya kukaribishwa rasmi Wizarani.
Watumishi wa Wizara wakimsikiliza Katibu Mkuu (hayupo pichani)
Sehemu nyingine ya Watumishi wa Wizara

Watumishi wengine wa Wizara

Tuesday, November 7, 2017

Waziri Mahiga akutana na Kamishna wa Umoja wa Ulaya

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akiongea na Kamishna wa Umoja wa Ulaya anayeshughulikia Maendeleo na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Neven Mimica alipomtembelea katika ofisi za Wizara Jijini Dar es Salaam tarehe 6 Novemba, 2017. Bw. Mimica alikuwepo nchini kwa ziara ya siku sita (6) ambapo aliwasili nchini tarehe 1 Novemba 2017 na kukamilisha ziara hiyo kwa kukutana na Waziri Mahiga.
Mkuu wa mabalozi wa Umoja wa Ulaya, Mhe. Roeland van de Geer pamoja na afisa wa Ubalozi huo wakifuatilia mazungumzo yaliyokuwa yakiendelea.
Afisa Mambo ya Nje, Bw. Salvatory Mbilinyi na Afisa aliyeambatana na kamishna wakifuatilia mazungumzo.

Picha ya pamoja.
Mazungumzo yakiendelea.

Friday, November 3, 2017

Msichana wa Kitanzania kuiwakilisha nchi Mkutano wa Dunia wa Vijana

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Deusdedit Kaganda akimkabidhi Bendera ya Taifa, Bi Hilda Jacob Mwakatumbula ambaye amechaguliwa na Kamati ya Kimataifa ya Vijana kuiwakilisha Tanzania kwenye Mkutano wa Dunia wa Vijana utakaofanyika Belize, Amerika ya Kati kuanzia tarehe 6 hadi 9 Novemba, 2017. Bi. Mwakatumbula ambaye anachukua Shahada ya Uzamivu katika Chuo Kikuu cha Waseda nchini Japan amepata ufadhili wa kushiriki Mkutano huo kutoka Ofisi ya Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini, Bw. Alvaro Rodriguez (kushoto). Akimkabidhi Bendera hiyo, Bw. Kaganda alimwomba Bi. Mwakatumbula kuwa Balozi mzuri wa Vijana wa Kitanzania kwenye mkutano huo hususan katika kutekeleza Malengo Endelevu ya Maendeleo.
Picha ya pamoja

Thursday, November 2, 2017

Balozi Mbarouk akabidhi Hati za Utambulisho kwa Rais wa Jamhuri ya Kiislam ya Iran


Balozi wa Tanzania katika Jamhuri ya Kiislam ya Iran, Mhe. Mbarouk Nassor Mbarouk, mwenye Makazi yake Umoja wa nchi wa Falme za Kiarabu (U.A.E) akikabidhi Hati za Utambulisho kwa Rais wa Jamhuri ya Kiislam ya Iran, Mhe. Rais Hassan Rouhani. Makabidhiano hayo yalifanyika katika Ikulu ya Rais, Mjini Tehran tarehe 28 Oktoba, 2017.

Mhe. Rais Hassan Rouhani akisoma hati za utambulisho alizokabidhiwa na

Mhe. Balozi Mbarouk, ambapo alitumia fursa hiyo kumkaribisha Mhe. Mbarouk na kuahidi kumpa ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yake.
Mhe. Rais Hassan Rouhani akizungumza na Mhe. Balozi Mbarouk baada ya kukabidhi hati. Katika mazungumzo yao wameahidi kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia na kuongeza maeneo mapya ya ushirikiano kwa lengo la kukuza uchumi wa mataifa yao. 


Wednesday, November 1, 2017

Naibu Waziri Mhe.Dkt Suzan Kolimba afanya mazungumzo na Naibu Mkurugenzi wa Kampuni ya Mawasiliano ya Halotel Wizarani

 Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Suzan Kolimba(Mb) akiwa katika mkutano na Naibu Mkurugenzi wa Kampuni ya simu ya Halotel nchini Bw. Pham Dinh Quan alipomtembelea Wizarani jana tarehe 31 Oktoba,2017, Dar es salaam. 
Katika Mazungumzo yao Bw. Quan alisema kampuni ya halotel hadi sasa imewekeza katika eneo kubwa la Tanzania hasa vijijini, alisema hadi sasa Kampuni hiyo imewekeza asilimia 80 ya eneo la Tanzania na wana mpango wa kuongeza uwekezaji zaidi katika eneo ambalo halijafikiwa. Mhe. Dkt. Kolimba alipongeza kampuni ya Halotel kwa uwekezaji huo mkubwa ambao umesaidia kurahisisha mawasiliano nchini hasa Vijijini.

 

 Mkutano huo ukieendelea.
 Naibu Waziri Mhe.Dkt. Suzan Kolimba (Katikati), Naibu Mkurugenzi wa Halotel Bw. Pham Dinh Quan kushoto kwake na kulia ni  Bw. Emmanuel Luangisa Afisa Mambo ya Nje wakiwa katika picha ya pamoja baada ya mkutano.



Saturday, October 28, 2017

Waziri Mahiga azitaka taasisi kutoa fursa za ajira kwa vijana

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga leo ameongea na vijana kupitia kongamano la Ubalozi Youth Forum lililofanyika katika viwanja vya Leaders Club jijini Dar es Salaam. Waziri Mahiga katika hotuba yake amewataka vijana kuchangamkia fursa zinazotolewa na Taasisi mbalimbali za Kimataifa na za ndani na makampuni binafsi. Waziri Mahiga amezitaja baadhi ya fursa hizo kuwa ni nafasi za ufadhili wa masomo ya elimu ya juu (scholarship) na mafunzo mbalimbali kama vile ujasiriamali, teknolojia, ajira na biashara.

Kongamano hilo lililenga kuwaelimisha vijana kuhusu fursa mbalimbali zinazopatikana kwenye Taasisi za Kimataifa zilizopo nchini na Makampuni binafsi na kuwahamasisha kuchangamkia fursa hizo. Vilevile kongamano hilo lilihudhuriwa na Wanadiplomasia wanaoziwakilisha nchi mbalimbali nchini Tanzania ambapo, vijana walipata fursa ya kuzungumza nao na kujifunza masuala mbalimbali kutoka kwa Wanadiplomasia hao.

Aidha katika Kongamano hilo vijana walipata fursa ya kuonesha bidhaa na huduma mbalimbali walizo zibuni, pia kuonesha bidhaa walizozalisha kutokana na miradi mbalimbali inayofadhili na Mashirika ya kimataifa. Miongoni mwa bidhaa zilizooneshwa ni mazao ya kilimo yaliyofadhiliwa na Umoja wa Mataifa (UN) chini ya mradi wa"ajira stahiki kwa vijana vijijini" (decent rural employment) ambapo hadi sasa jumla ya vijana 480 wamenufaika na mradi huo.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akifuatilia kongamano la Ubalozi Youth Forum
Sehemu ya Wanadiplomasia kutoa nchi mbalimbali Duniani wanaoziwakilisha nchi zao nchini Tanzania wakifuatila Kongamano


Waziri Mhe.Mahiga akihutubia hadhira ya Ubalozi Youth Forum

Waziri Mhe.Mhiga akiangalia moja ya bidhaa iliyobuniwa na kutengenezwa na kijana kwenye maonesho ya kongamano la Ubalozo Youth Forum yaliyofanyika katika viwanja vya  Leaders Club Jijini Dar es Salaam

Friday, October 27, 2017

Program ya Uendelezaji wa Sekta ya Uchukuzi kwa njia ya Barabara kwa Nchi Wanachama wa Jumuiya Utatu wa COMESA-EAC-SADC yazinduliwa.

Waziri wa Ujenzi, uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Prof. Makame Mbalawa akihutubia katika Mkutano wa Mawaziri wa Uchukuzi na Ujenzi wakati wa uzinduzi rasmi wa Program ya Uendelezaji wa Sekta ya Uchukuzi kwa njia ya Barabara kwa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Utatu wa COMESA-EAC-SADC. Mkutano huo ulifanyika katika Hoteli ya Serena Jijini Dar es Salaam tarehe 26 Oktoba 2017.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Balozi Liberat Mfumukeko akihutubia ambapo pamoja na mambo mengine alieleza faida zitakazopatikana kutokana na uzinduzi wa program hiyo na namna Jumuiya ya Afrika Mashariki ilivyojidhatiti kuhakikisha malengo hayo yanafikiwa kwa uhakika.
Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Dkt. Leornard Chamuriho (kulia) pamoja na wajumbe kutoka nchi wanachama wakifuatilia mkutano, wa kwanza kushoto ni Balozi wa Rwanda nchini, Mhe. Eugene Kayihura
Sehemu ya wajumbe wa Tanzania wakifuatilia mkutano, wa pili kulia ni Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Bandari, Mhandisi Deusdedit Kakoko.
Sehemu ya wajumbe kutoka nchi wanachama wakifuatilia mkutano.
Meza kuu wakiongoza Mkutano.
Mkutano ukiendelea.

Thursday, October 26, 2017

Waziri Mahiga afungua Mkutano wa Mawaziri wa nchi wananchama wa Jumuiya ya Utatu wa COMESA-EAC-SADC (TRIPARTITE)

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akifungua Mkutano wa kwanza wa Mawaziri wenye dhamana ya masuala ya Miundombinu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Utatu wa COMESA-EAC-SADC (TRIPARTITE) uliofanyika katika Hotel ya Serena Jijini Dar es Salaam tarehe 26 Oktober 2017.
Viongozi na wajumbe kutoka Nchi Wanachama wakifuatilia Mkutano, wa tatu kutoka kushoto ni Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Prof. Makame Mbalawa na wa nne kutoka kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Aziz Mlima.

Sehemu nyingine ya Wajumbe kutoka nchi Wanachama wakifuatilia Mkutano.
Mkutano ukiendelea.

Picha ya pamoja.
============================================================


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
MHE. WAZIRI MAHIGA AFUNGUA RASMI MKUTANO WA KWANZA WA MAWAZIRI WENYE DHAMANA YA MASUALA YA MIUNDOMBINU WA NCHI WANACHAMA WA JUMUIYA YA UTATU WA COMESA-EAC-SADC (TRIPARTITE) UNAOFANYIKA HAPA DAR ES SALAAM LEO TAREHE 26 OKTOBA 2017

Mkutano wa Kwanza wa Mawaziri wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Utatu wa COMESA-EAC-SADC umefanyika hapa Dar es Salaam, Serena Hoteli leo tarehe 26 Oktoba 2017. Mkutano huo unahusisha jumla ya nchi 26 Wanachama wa Umoja huo. Mkutano huu unafanyika hapa Tanzania kwa kuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki ndiyo Mwenyekiti wa Jumuiya ya Utatu wa COMESA-EAC-SADC.

Mkutano huu umefunguliwa na Mhe. Dkt. Augustine Phillip Mahiga (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo unaongozwa na Mhe. Prof. Makame Mbarawa (Mb), Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
Kufanyika kwa Mkutano wa Mawaziri wenye dhamana ya masuala ya Miundombinu kunatokana na maazimio ya Mkutano wa Pili wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa COMESA, EAC na SADC uliofanyika Johannesburg, Afrika Kusini tarehe 14 Juni, 2011 ambao ulipitisha maeneo matatu ya kutekelezwa kwenye ushirikiano wa Utatu wa COMESA – EAC – SADC. Maeneo hayo ni: 1) Kuunganisha Soko; 2) Kuendeleza Miundombinu ili kuunganisha Nchi Wanachama kwa miundombinu iliyo bora; na 3) Kukuza Viwanda.
Kwa upande wa Sekta za Miundombinu, huu ni Mkutano wa Kwanza wa Mawaziri  wa Nchi Wanachama wa Utatu wa COMESA, EAC na SADC. Mkutano huu katika Ngazi ya Wataalam ulijadili hatua zilizofikiwa na Nchi Wanachama katika uendelezaji wa miundombinu na kupendekeza maamuzi ya kisera kwenye sekta za miundombinu ya uchukuzi (barabara, reli, bandari, anga); teknolojia ya habari na mawasiliano; na nishati.

Kwa ujumla Mkutano wa Mawaziri umepita na kujadili programu kuu zifuatazo:
           i.          Programu ya Uendelezaji wa Sekta za Uchukuzi kwa njia ya Barabara kwa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Utatu wa COMESA-EAC-SADC (Tripartite Transport and Transit Facilitation Programme (TTTFP);

          ii.          Taarifa za utekelezaji wa miradi na programu kuhusiana na Sekta ya Miundombinu ya Uchukuzi (Anga, Barabara, Reli na Bandari); Sekta ya Mawasiliano na Sekta ya Nishati;

         iii.          Maendeleo ya Kanda za Uchukuzi (Corridor Development) za Jumuiya ya Utatu wa COMESA, EAC na SADC, ambapo hatua mbalimbali za Utekelezaji wa Vituo vya Kutoa Huduma kwa Pamoja Mipakani (OSBPs) kwa Nchi Wanachama wa Jumuiya hizo zimejadiliwa;

        iv.          Utekelezaji wa Programu ya Kikanda wa Uendelezaji wa Miundombinu katika Ukanda wa Afrika Mashariki, Ukanda wa Afrika Kusini na Ukanda wa Bahari ya Hindi (Regional Indicative Programme for Eastern Africa, Southern Africa and the Indian Ocean (2014 – 2020); na

         v.          Utekelezaji wa Miradi ya NEPAD Presidential Infrastructure Championship Initiative (PICI);
        vi.          Rasimu ya Mpangokazi wa shughuli za utatu wa COMESA- EAC- SADC hususan uratibu wa mikutano ya miundombinu;
       vii.          Utafutaji raslimali fedha za kuwezesha shughuli za utatu wa COMESA- EAC- SADC; na

     viii.          Uzinduzi rasmi wa Programu ya Uendelezaji wa Sekta za Uchukuzi kwa njia ya Barabara kwa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Utatu wa COMESA-EAC-SADC (Tripartite Transport and Transit Facilitation Programme (TTTFP).

Katika hotuba yake ya ufunguzi, Mhe. Waziri Mahiga, pamoja na kuwakaribisha Mawaziri nchini Tanzania na jijini Dar es Salaam, amesisitiza umuhimu wa kuwa na miradi ya pamoja ya kuendeleza sekta ya miundombinu baina ya Jumuiya za kikanda kama njia madhubuti ya kuwaletea maendeleo ya haraka wananchi. Mhe. Mahiga pia amesisitiza kwamba Tanzania inathamini ushirikiano wa kanda na hivyo itaendelea kushiriki kikamilifu katika juhudi za maendeleo za kikanda ikiwemo zile za Jumuiya ya Utatu (Tripartite) kama njia mojawapo wa utekelezaji wa Sera ya Tanzania ya Viwanda. Mwisho, Mhe. Mahiga amewatakia mkutano mzuri Mawaziri wa Miundombinu akiwaomba kuibua mikakati na mapendekezo madhubuti katika kuendeleza miundombinu katika eneo lote la UTATU.

Aidha, Mawaziri kwa pamoja, wakiongozwa na Mhe. Aggrey Henry Bagiire, Waziri wa Uchukuzi na Ujenzi wa Jamhuri ya Uganda na ambaye atakuwa ni Mwenyekiti wa Mkutano huo kwa nafasi yake kama Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, watazindua rasmi Programu ya Uendelezaji wa Sekta za Uchukuzi kwa njia ya Barabara kwa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Utatu wa COMESA-EAC-SADC (Tripartite Transport and Transit Facilitation Programme (TTTFP).

Uzinduzi huu utafanyika leo tarehe 26 Oktoba, 2017 saa 9.00 Alasiri na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa Serikali na Sekta Binafsi.
I
Imetolewa na,
KITENGO CHA MAWASILIANO YA SERIKALI,
WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI,
TAREHE 26/10/2017