Friday, February 16, 2018

Serikali kutoa viwanja kwa ajili ya Mabalozi kujenga ofisi na makazi Dodoma

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Adolf Mkenda akiongea katika kikao na Waheshimiwa Mabalozi na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa wa hapa nchini kuhusu Mpango Mkuu wa mji wa Serikali mjini Dodoma ambao utakuwa na eneo kwa ajili ya wanadiplomasia.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Mshereheshaji wa kikao, Bi. Mindi Kasiga akitoa utaratibu na ratiba ya kikao hicho.
Prof. Mkenda akiendelea kuongea na wanadiplomasia wa hapa nchini kuhusu Mpango Mkuu wa mji wa Serikali mjini Dodoma.


Waheshimiwa Mabalozi na Wakuu wa Mashirika ya Umma walioshiriki kusikiliza mada kuhusu Mpango Mkuu wa mji wa Dodoma.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Bw. Godwin Kunambi akitoa maelezo kuhusu manispaa yake ilivyojipanga kujenga mji wa Serikali Dodoma.

Mtaalamu kutoka kamati maalum ya kupanga Manispaa ya Dodoma akiwasilisha mada kuhusu mji wa Serikali Dodoma.

Balozi wa Afrika Kusini nchini Tanzania Mhe. Thami Mseleku akiuliza swali kuhusu mpango mkuu wa mji wa Serikali Dodoma.

Balozi wa Mamlaka ya Palestina nchini Tanzania  Mhe. Hazem Shabat akichangia mada kuhusu mpango mkuu wa mji wa Serikali mjini Dodoma.

Balozi wa Malawi nchini Tanzania Mhe. Hawa O. Ndilowe akichangia mada kuhusu mpango mkuu wa mji wa Serikali mjini Dodoma.

Katibu Mkuu (katikati) akijibu maswali ya Waheshimiwa Mabalozi na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa nchini. Wengine katika picha ni Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma, Bw. Godwin Kunambi (kulia) na Kaimu Mkuu wa Mabalozi na Balozi wa Saharawi nchini, Mhe. Ibrahi Buseif.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Serikali kutoa viwanja kwa ajili Mabalozi kujenga ofisi na makazi Dodoma

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Adolf  Mkenda amewahakikishia Waheshimiwa Mabalozi na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa hapa nchini kuwa ahadi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ya kuwapatia viwanja vya ukubwa wa ekari 5 kwa ajili ya ujenzi wa ofisi na makazi ya Balozi mjini Dodoma itatekelezwa kama ilivyoahidiwa.

Rais Magufuli alitoa ahadi hiyo katika sherehe  za  kufungua mwaka wa 2018 ya wanadiplomasia zilizofanyika Ikulu jijini Dar Es Salaam tarehe 09 Februari 2018.

Prof. Mkenda alitoa kauli hiyo kwa Mabalozi na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa wakati wa kuwasilisha mada kuhusu Mpango Mkuu wa Mji wa Serikali mjini Dodoma.

Mada hiyo ilitolewa kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Manispaa ya Dodoma kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) leo Jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa mada hiyo, mji wa Serikali mjini Dodoma utajengwa pembeni ya Barabara ya Dar Es Salaam hadi Dodoma, kilomita 17 kutoka katikati ya mji wa Dodoma na unakadiriwa kugharimu Shilingi za Kitanzania trilioni 10 hadi unakamilika.

Mji huo ambao umesanifiwa kwa asilimia 100 na wataalamu wa Kitanzania umezingatia mahitaji yote muhimu ambayo mji wa kisasa unastahili kuwa nayo. Miongoni mwa mahitaji hayo ni pamoja na miundombinu ya kutosha ikiwemo barabara, maji safi na maji taka, nishati ya umeme, TEHAMA na dampo kwa ajili ya taka ngumu ambalo ujenzi wake umeshakamilika na juhudi zinaendelea za kutafuta mwekezaji kwa ajili ya kubadilisha taka kwa matumizi mengine (recycling).

Aidha, usanifu wa mji huo umezingatia vigezo vya uendelezaji endelevu wa miji duniani ikiwa ni pamoja na utunzaji wa mazingira na urithi wa asili, kuepuka uchafuzi wa hali ya hewa na urahisi wa kufikika.
Wasanifu wa mji huo wakisisitiza kuhusu uendelezaji endelevu wa miji, katika usanifu wao wamezingatia hali ya hewa ya Dodoma ambayo ni ya joto na upepo mkali, hivyo, wametenga maeneo kwa ajili ya upandaji miti itakayopunguza kasi ya upepo na ujenzi wa vyanzo vya maji kwa ajili ya kupoza joto. 

Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma, Bw. Godwin Kunambi alitumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji kwenda kuwekeza katika mji wa Dodoma katika miradi mbalimbali ikiwemo mashule, hospitali, mahoteli, maduka makubwa na miundombinu mingine. “Tumetenga eneo kubwa kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda ambalo limegawanywa katika ukubwa tofauti tofauti kutegemea na mahitaji ya mwekezaji, hivyo wahimizeni wafanyabiashara kutoka katika nchi zenu waje kuwekeza Dodoma”. Bw. Kunambi aliwaambia Mabalozi.

Bw. Kunambi alieleza kuwa Mpango Mkuu wa mji wa Dodoma ulisanifiwa tangu mwaka 1976 na kufanyiwa mapitio mwaka 2010 na sasa wataalamu hao ambao wamepata uzoefu kutoka nchi mbalimbali zikiwemo Nigeria, Malaysia, China na Malawi ili kusanifu mji unaozingatia mahitaji ya sasa.

-Mwisho-
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 16 Februari 2018

Mhe. Rais Magufuli awaapisha Mabalozi wa Tanzania nchini Nigeria na Sweden


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akimwapisha Bw. Muhidin Ally Mboweto kuwa Balozi wa Tanzania nchini Nigeria. Hafla ya uapisho imefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 16 Februari, 2018


Balozi Mboweto akisaini mara baada ya kula kiapo cha kuiwakilisha Tanzania nchini Nigeria
Mhe. Rais Magufuli akimkabidhi vitendea kazi Balozi Mboweto
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mhe. Dkt.John Pombe Joseph Magufuli akimwapisha Dkt. Wilbroad Peter Slaa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Sweden.
Balozi Slaa akisaini kiapo chake
Mhe. Rais Magufuli alimkabidhi Balozi Slaa vitendea kazi
Balozi Mboweto na Balozi Slaa kwa pamoja wakila kiapo cha Maadili ya Viongozi mbele ya Mhe. Rais Magufuli
Mhe. Rais Magufuli kwa pamoja na Balozi Mboweto na Balozi Slaa (walioketi) wakimsikiliza Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Susan Kolimba alipokuwa akitoa nasaha zake kwa Mabalozi hao mara baada ya kuapishwa.
 Wakuu wa Vyombo vya Usalama nchini na wageni wengine waalikwa wakimsikiliza Dkt.Kolimba (hayupo pichani)
Sehemu ya viongozi mbalimbali na wageni waalikwa  wakiwa kwenye hafla ya kuapishwa kwa Balozi Mboweto na Balozi Slaa (hawapo pichani). Kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ramadhan Muombwa Mwinyi


Mhe. Rais Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na Balozi Mboweto mara baada ya kumwapisha
Mhe. Rais akiwa katika picha ya pamoja na Balozi Slaa mara baada ya kumwapisha

 Mhe. Rais Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na Mabalozi walioapishwa na viongozi wengine akiwemo Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Susan Kolimba (wa pili kutoka kushoto), Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi (wa pili kulia) na  Naibu Katibu Mkuu wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ramadhan Muombwa Mwinyi (kushoto)
 Mhe. Rais Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na Mabalozi walioapishwa na viongozi wengine akiwemo Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Susan Kolimba (wa pili kushoto), Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi (wa pili kulia), Naibu Katibu Mkuu wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ramadhan Muombwa Mwinyi (kushoto) na Wakurugenzi na Wakuu wa Vitengo wa Wizara ya Mambo aya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Thursday, February 15, 2018

Waziri Mahiga afanya mazungumzo na Wabunge wa EALA

                         
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Dkt.Augustine Mahiga akizungumza na Wabunge wa EALA (hawapo pichani).
Wabunge wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA)  leo wamekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Dkt.Augustine Mahiga Wizarani mjini Dodoma. Wabunge wa EALA wamewasili mjini Dodoma wakiwa katika ziara ya kutembelea miradi mbalimbali ya Jumuiya inayotekelezwa na nchi wanachama za Jumuiya ya Afrika Masharaiki. 

Katika ziara hii Wabunge wanatembelea miradi inayotekelezwa katika ushoroba wa kati (central corridor) sambamba na kubaini changamoto zinazoikabili miradi hiyo na namna inavyorahisha utoaji huduma kwa wananchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Katika mazungumzo yao na Waziri Mahiga, Wabunge wa EALA wameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa utekelezaji mzuri wa miradi inayotokana na makubaliano ya Jumuiya kama vile ujenzi wa mizani za kisasa sambamba  na kupunguza idadi ya mizani hiyo ili kurahisisha usafirishaji wa bidhaa, hudumu na watu ndani Jumuiya.

Hadi sasa Tanzania kwa upande wa ushoroba wa kati imefanikiwa kupunguza idadi ya vituo vya mizani kutoka  vituo saba hadi vitatu.

Kwa upande wake Waziri Mahiga, amewapongeza Wabunge wa EALA kwa kuona umuhimu wa kutembelea miradi ya Jumuiya inayotekelezwa na nchi Wanachama ambayo inagusa maisha ya wananchi moja kwa moja. Aidha amesema katika ziara hii Wabunge wataweza kubaini changamoto zinazowakabili wananchi, hivyo kuwa katika nafasi nzuri ya kuweza kutatua changamoto hizo wakati wa utekelezaji wa majukumu yao Bungeni.

Mbunge wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki kutoka Tanzania Mhe. Dkt. Ngwaru Maghembe (kushoto) akizungumza na Waandishi wa Habari walipotembelea ofisi za Wizara mjini Dodoma. Kulia ni  Mhe. Wanjiku Muhia  kutoka Kenya ambaye pia ni kiongozi wa msafara wa ziara hiyo
Mhe. Adam Kimbisa Mbunge wa EALA (Tanzania) akizungumza wakati wa Mkutano na Waandishi wa Habari



Mkutano ukiwa unaendelea

Tanzania yashinda Tuzo, Dubai

Mtukufu Shaikh Mansour Bin Zayed Al Nahyan, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais ya Umoja wa Falme za Kiarabu) (UAE) na Balozi wa Tanzania, UAE, Mhe. Mbarouk Nassor Mbarouk (kulia) wakiwa wameshikilia tuzo ya Teknolojia bora inayoibuka Serikalini (Winner of the Best Government Emerging Technologies Award) ambayo Tanzania imeshinda huko Dubai.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

TANZANIA YASHINDA TUZO YA TEKNOLOJIA KATIKA MKUTANO WA DUNIA WA SERIKALI (WORLD GOVERNMENT SUMMIT 2018)
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeshinda Tuzo za Kilele cha Serikali duniani (World Government Summit Awards) katika kundi la Tuzo ya Teknolojia bora inayoibuka Serikalini (Winner of the Best Government Emerging Technologies Award).

Tuzo hiyo ilitolewa na Mtukufu Shaikh Mansour Bin Zayed Al Nahyan, Naibu Waziri Mkuu na Waziri Nchi, Ofisi ya Rais ya Umoja wa Falme za Kiarabu) (UAE) na kupokelewa na Balozi wa Tanzania, UAE, Mhe. Mbarouk Nassor Mbarouk kwa niaba ya Serikali, wakati wa kilele cha Mkutano wa Dunia wa Serikali (World Government Summit) uliohitimishwa jijini Dubai tarehe 13 Februari 2018.

Tuzo hiyo ilitokana na juhudi za Serikali ya Tanzania kupitia Taasisi ya Kilimo ya Mikocheni (Mikocheni Agricultural Research Institute kufanikiwa kulipatia ufumbuzi tatizo la maradhi ya zao la muhogo “Cassava Brown Creek Disease,” na “Cassava Mosaic Disease,” kwa kutumia chombo cha kisasa kinachoitwa “Portable DNA Sequencer”.  Maradhi hayo yanasumbua sana zao la muhogo ambalo ni zao muhimu kwa Tanzania na nchi mbalimbali Afrika na duniani kwa ujumla.

Kwa kutumia teknolojia hii mpya wataalamu wanaweza kugundua magonjwa mbalimbali ya zao la muhogo yanayosababishwa na wadudu, virusi, bacteria na fangasi (pathogens) kwa muda wa siku 2 tu kulinganisha na teknolojia ya zamani ambayo huchukua miezi kadhaa na ina gharama kubwa.

Zao la muhogo ni zao muhimu la chakula na biashara linalotegemewa sio tu na  Tanzania bali na nchi nyingine nyingi duniani.  Inakadiriwa kuwa watu wapatao millioni 800 duniani wanategemea zao la muhogo kwa chakula na biashara. Hivyo, teknolojia hii mpya itanufaisha nchi mbalimbali duniani katika kusaidia na kuendeleza zao hilo.

Nchi nyingine zilizopata Tuzo hiyo ni India na Australia.

Wakati huo huo, Watanzania wenye sifa wanahimizwa kuomba nafasi ya kazi iliyotangzwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya mazingira (UNEP). Nafasi inayotakiwa kujazwa ni ya Chief Biodiversity Unit. Maelezo kuhusu nafasi hiyo yanapatikana katika mawasiliano http://careers.un/bw/jobdetail.aspx?id=88749 na siku ya mwisho ya kuwasilisha maombi ni tarehe 25 Februari 2018.

-Mwisho-
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 15 Februari 2018.

Wednesday, February 14, 2018

Wabunge wa EALA wafanya Ziara Nchi za Afrika Mashariki

Wabunge wa EALA wafanya ziara Nchi za Afrika Mashariki
Wabunge wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) wanafanya ziara ya siku 12 kwa ajili ya kupitia na kuangalia maendeleo na changamoto mbalimbali za Mtangamano pamoja na kutoa elimu kwa umma kuhusu masuala mbalimbali ya Mtangamano wa Jumuiya ya  Afrika Mashariki kupitia vyombo vya habari.
Ziara hiyo ilianza tarehe 12- 23 Februari,2018, katika ziara hiyo waheshimiwa Wabunge wamegawanyika katika makundi mawili, kundi la kwanza linafanya ziara katika ukanda wa kati ( Cetral Corridor) , ziara hii itahusisha Zanzibar na Mikoa ya Dar es salaam, Kilimanjaro, Pwani, Arusha, Dodoma, Shinyanga na Kagera,  kundi la pili watatembelea ukanda wa Kaskazini   ( North Corridor) ziara hiyo itaanzia Kenya, Uganda na kumalizikia Rwanda ambapo ndipo wanapotarajia kukutana kwa kwa ajili ya kikao cha  wiki mbili kwa ajili ya majumuisho ya ziara.
Waheshimiwa Wabunge wanaotemebelea Ukanda wa Kati walianzia safari yao Zanzibar ambapo walifanya ziara katika Bandari ya Zanzibar na pia kufanya mazungumzo na Uongozi wa Taasisi ya Kiswahili Kamisheni. Aidha, wakiwa Dar es salaam walipata fursa ya kutembelea Bandari ya Dar es salaam na kukutana na viongozi wa Bandari pamoja na wadau mbalimbali wanaotumia bandari. Akiongea katika mkutano huo Kaimu Meneja wa Bandari Bw. Feddy Liundi, alisema hadi sasa kuna mafanikio makubwa sana katika Bandari ya Dar es Salaam kwani bandari hiyo inahudumia zaidi ya nchi nane na kati ya hizo Rwanda na Malawi wanaongoza kwa matumizi ya bandari ya Dar es salaam.
Kwa upande wao Waheshiwa walisifia maboresho ya bandari na kusema ndio yamechangia bandari hii kuwa kinara na kivutio kwa wasafirishaji wa mizigo ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Waheshimiwa Wabunge pia walipata nafasi ya kutembelea eneo la mradi wa maboresho ya bandari ya Dar es salaam wa Dar es salaam Maritime Gateaway Project (PMGP) pamoja na kitengo cha Kontena cha TICTS.
Waheshimiwa wabunge walipongeza uongozi wa bandari kwa maboresho makubwa yaliyofanyika na kuahidi kufanyia kazi changamoto zote zilizoainishwa ambazo ni za Kimtangamano. Jumla ya Waheshimiwa Wabunge 21 kutoka nchi sita (6) za Jumuiya Ya Afrika Mashariki wanashiriki katika ziara hii kwa upande wa Ukanda wa kati(Cetral corridol).

========================================================================


 Wabunge wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki ( EALA) wakiwa katika Mkutano na Uongozi wa Bandari ya Dar es salaam, kutoka kushoto ni Mhe.Maryam Ussi (Tanzania), Mhe. Wanjiku Muhia (Kenya) (ambaye pia ni kiongozi wa Msafara katika ziara hii) na wa mwisho kulia ni Kaimu Meneja wa bandariBw. Freddy Liundi, wakiwa katika Mkutano. Mkutano huo ulifanyika katika ukumbi wa mikutano wa Bandari, tarehe 13 Februari,2018.

 Mhe. Josephine Lemoyan (Tanzania) akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) baada ya mkutano, wanaofuatilia ni Mhe. Wanjiku (kushoto), na Mhe. Musamali Paul Mwasa (Uganda)

    Waheshimiwa Wabunge na wadau wengine wakiwa katika Mkutano huo

 Wadau mbalimbali wakifuatilia Mkutano huo

Waheshimiwa Wabunge, wafanyakazi wa bandari pamoja na wadau wengine wakiwa katika picha ya pamoja.

Tuesday, February 13, 2018

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI -Tanzania Mwenyeji wa Mkutano wa Baraza la Wakimbizi Duniani


Rais Mstaafu wa awamu ya nne, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete akiongea na waandishi wa habari kuhusu dhamira ya kuanzishwa kwa Baraza la Wakimbizi Duniani ambalo yeye ni Mwenyekiti Mwenza. Mweingine katika picha ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Augustine Mahiga.



Tanzania Mwenyeji wa Mkutano wa Baraza la Wakimbizi Duniani

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga ametoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa kuisaidia Tanzania kutokana na mchango mkubwa wa kuwahudumia wakimbizi ambao imekuwa ikiutoa kabla na baada ya uhuru, licha ya uchumi mdogo ilio nao. 

Waziri Mahiga ametoa wito huo leo Jijini Dar Es Salaam katika kikao cha Baraza la Wakimbizi Duniani (World Refugees Council-WRF) kinachofanyika kwa siku mbili kuanzia jana kwenye Hoteli ya Hyatt Regecy, Kilimanjaro.

Waziri Mahiga alieleza kuwa Tanzania ilipokea wakimbizi kutoka Poland wakati wa vita ya pili ya dunia na mwaka 1959 ilipokea wakimbizi kutoka nchi ya Rwanda. Aidha, baada ya uhuru, Tanzania imekuwa ikipokea wakimbizi mara kwa mara na wakati wa mauaji ya kimbari nchini Rwanda, Tanzania ilipokea wakimbizi wengi zaidi duniani.

Aliendelea kueleza kuwa athari zinazotokana na kupokea wakimbizi wengi ni nyingi na kubwa hivyo, ni jukumu la Jumuiya ya Kimataifa kuzisaidia nchi zenye wakimbizi wengi, hususan zile zenya uchumi mdogo.

Katika kikao hicho, Waziri Mahiga alitoa ufafanuzi kuhusu msimamo wa Serikali ya Tanzania kujitoa katika mpango wa kutafuta suluhu ya kudumu ya tatizo la wakimbizi duniani (Comprehensive Refugees Response Framework – CRRF). Alisema katika mpango huo wa CRRF, Serikali imesikitishwa na mapendekezo ya mpango huo ya kuitaka Tanzania ikope fedha kutoka Benki ya Dunia kwa ajili ya kuhudumia wakimbizi na kugharamia ukarabati wa miundombinu iliyoharibika. 

Halikadhalika, CRRF inapendekeza kuwepo na utaratibu wa kuwapa uraia, ajira na ardhi wakimbizi wanaoingia nchini ili waweze kuwa huru na kujitegemea.

Alibainisha kuwa Serikali ilishatoa uraia kwa wakimbizi zaidi ya laki moja na nusu. Jumuiya ya kimataifa iliahidi kutoa fedha kwa ajili ya kusaidia makazi na huduma nyingine kwa wakimbizi hao. Hata hivyo, Jumuiya ya Kimataifa haijatekeleza ahadi hiyo, badala yake inaitaka Serikali ichukue mkopo wenye riba kwa ajili ya kuhudumia wakimbizi. 

“Misitu, ardhi, mazingira na miundombimu mingine inaharibika kwa sababu ya wakimbizi, halafu tuchukue mkopo na kulipa deni kwa ajili ya kuhudumia wakimbizi, nadhani sio utaratibu mzuri” Dkt. Mahiga alilalamika.

Dkt. Mahiga alieleza kuwa amewasilisha ujumbe wa Serikali kwenye Baraza hilo ili lifikishe kilio cha Tanzania katika Jumuiya ya Kimataifa kwa matumaini kuwa wao wanasikilizwa zaidi. 

Kwa upande wake, Rais mstaafu wa awamu ya nne, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, alitoa maelezo kuhusu dhamira ya kuanzishwa kwa WRC. Alisema WRC ilianzishwa mwaka 2017 kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Canada na Taasisi isiyo ya kiserikali ya nchi hiyo. Lengo la chombo hicho ni kuangalia sababu zinazopelekea wakimbizi kuongezeka,  matatizo na changamoto zinazowakabili wakimbizi na kutoa maoni ya namna ya kutatua tatizo la wakimbizi duniani.

Baraza hilo linaongozwa na jopo la watu wanne wenye uzoefu wa masuala ya wakimbizi duniani ambao ni Waziri wa Mambo ya Nje wa zamani wa Canada ambaye ni Mwenyekiti, Mhe. Lyord Axworthy, Mwenyekiti Mwenza ni Rais wa zamani wa Tanzania, Mhe. Jakaya Kikwete, Makamu Mwenyekiti ni Mwanadiplomasia wa zamani wa Canada, Mhe. Paul Heinbecker na Mwanaharakati wa haki za binadamu kutoka Pakistan ambaye pia ni Mwenyekiti Mwenza, Mhe. Hina Jilani. 

Baraza lilifanya kikao cha kwanza Geneva, Uswisi mwezi Juni 2017 na baadaye kutembelea nchi za Jordan na Ujerumani. Nchi hizo zimetembelewa kwa sababu Jordan ndio nchi inayopokea wakimbizi wengi kwa sasa duniani na Ujerumani kutokana na kuruhusu kupokea wakimbizi kulisababisha Serikali iliyopo madarakani kupata upinzani mkali katika uchaguzi uliopita.
Kikao cha pili kinafanyika Afrika na Tanzania imechaguliwa kutokana na uzoefu wake katika masuala ya wakimbizi. Aidha, kikao kijacho kitafanyika Bara la Asia katika nchi ya Thailand na kitafuatiwa na kikao kitakachofanyika Bara la Amerika Kusini. 

Katika kikao kinachoendelea nchini, Nchi mbalimbali za Afrika zimealikwa zikiwemo Uganda, Rwanda, Burundi, Kenya ambazo zieleza uzoefu wao kuhusu matatizo na sababu za kutoa wakimbizi.

Baraza hilo linatarajiwa kukamilisha ripoti yake mwaka 2018 na kuiwasilisha kwenye mamlaka husika kwa ajili ya utekelezaji.

-Mwisho-
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 13 Februari 2018




Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Augustine Mahiga akiongea na waandishi wa habari kuhusu msimamo wa Tanzania kujitoa katika Mpango wa kutafuta suluhu ya kudumu ya tatizo la wakimbizi duniani.
Rais Mstaafu wa awamu ya nne, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete akiongea katika kikao cha Baraza la Wakimbizi Duniani kinachofanyika katika Hoteli ya Hyatt Regency, Kilimanjaro.