Monday, April 9, 2018

Waziri Mahiga akutana na Balozi wa Hispania nchini

 Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Augustine Mahiga akifafanua jambo kwenye mazungumzo na Balozi wa Hipania nchini Mhe. Felix Costales Artieda alipomtembelea Wizarani tarehe 09 Aprili,2018, Jijini Dar es Salaam.
Mazungumzo hayo yalijikita katika kuzidi kuimarisha ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Hispania.


 Mhe. Balozi Felix Costales Artieda akieleza jambo kwa Mhe. Waziri Mahiga kwenye mazungumzo hayo.

 Mazungumzo yakiendelea, wanaoshuhudia mazungumzo hayo ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika Bw. Salvatory Mbilinyi(kulia katikati),Katibu wa Waziri Bw. Magabiro Murobi (Kulia mwisho)na kushoto ni Naibu Balozi Bi. Teresa Martin. 
Wakiwa katika Picha ya Pamoja

Friday, April 6, 2018

BALOZI SLAA AWASILISHA HATI ZAKE ZA UTAMBULISHO KWA MFALME WA SWEDEN

Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Mhe. Wilbroad Slaa amewasilisha Hati zake za Utambulisho kwa Mfalme Carl XVI Gustaf wa Sweden. tarehe 06.04.2018
Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Mhe. Wilbroad Slaa akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya maofisa wa ofisi ya Mfalme wa Carl XVI Gustaf wa Sweden na Maofisa wa Ubalozi wa Tanzania nchini sweeden mara baada ya utambulisho


Balozi Mwinyi akutana na Wajumbe wa Kamati ya maandalizi ya Maonyesho ya Bidhaa za Viwanda Vya Tanzania nchini Kenya

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ramadhan Mwinyi akizungumza na wajumbe wa kamati maalum ya maandalizi na Wadhamini wa maonesho ya bidhaa za viwanda vya Tanzania nchini Kenya kwa ajili ya kueleza mikakati mbalimbali itakayowezesha utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi kwa vitendo katika kuelekea Tanzania ya Viwanda. Kikao hicho kilifanyika Ijumaa 6 Aprili  2018.
Baadhi ya wajumbe wa kamati ya maandalizi na wadhamini wa maonesho ya bidhaa za viwanda vya Tanzania nchini Kenya wakisikiliza kwa makini maelekezo ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ramadhani Mwinyi wakati wa kikao baina yao kilichofanyika leo Ijumaa April 6, 2018.
Baadhi ya wadhamini wa maonesho ya bidhaa za viwanda vya Tanzania nchini Kenya wakifuatilia kwa makini maelekezo ya Balozi Mwinyi hayupo pichani
Balozi Ramadhan Mwinyi akiagana na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) Bw. Edwin Rutageruki ambaye pia ni mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya maonesho hayo mara baada ya kumalizika kwa kikao.
Meneja Mkuu wa Kampuni ya Mafuta ya LAKEGAS, Rajesh Chidambarani (katikati) ambaye pia ni mmoja wa wadhamini akibadilisha mawazo na Balozi Mwinyi mara baada ya kumalizika kwa kikao.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Adolf Mkenda (katikati) akibadilisha mawazo na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Balozi Ramadhani Mwinyi na Meneja Mkuu wa Kampuni ya mafuta ya LAKEGAS, Rajesh Chidambarani mara baada ya kumalizika kwa mkutano baina yao tarehe 6 Aprili 2018.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ramadhan Mwinyi (wa tano kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa kamati ya maandalizi na wadhamini wa maonesho ya bidhaa za Viwanda vya Tanzania nchini Kenya tarehe 6 Aprili 2018.








Taarifa kwa Vyombo vya Habari

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
FURSA ZA UFADHILI WA MAFUNZO KWA WATANZANIA
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imepokea fursa za ufadhili wa masomo ya muda mfupi na muda mrefu katika kada mbalimbali kutoka Umoja wa Afrika, Serikali za China, Ujerumani na Jamhuri ya Korea.
Kuhusu ufadhili wa mafunzo ya muda mrefu, Umoja wa Afrika kupitia Mwalimu Nyerere African Union Scholarship Scheme umetoa ufadhili wa mafunzo kwa ngazi ya Shahada ya Uzamili na Uzamivu (PhD) kwenye masuala ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hesabu (STEM). Waombaji wa mafunzo haya ni wanawake pekee wenye umri wa miaka isiyozidi 35 kwa mafunzo ya ngazi ya Shahada ya Uzamili na miaka isiyozidi 40 kwa mafunzo ya ngazi ya Shahada ya Uzamivu (PhD). Maelezo ya ziada kuhusu mafunzo haya yanapatikana kupitia tovuti ya http://www.au.int. au maombi yatumwe kwa OlgaA@african-union.org na nakala kwa mwalimunyerere@africa-union.org. Mwisho wa kutuma maombi ni tarehe 30 Aprili, 2018.  Mafunzo haya yanaratibiwa  na Wizara ya Elimu, Sayansi  na Teknolojia na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma.
Aidha, Baraza la Ufadhili wa Mafunzo la China limetoa nafasi za ufadhili wa mafunzo ya muda mrefu. Maelezo kuhusu mafunzo haya yanapatikana kupitia http://www.esc.edu.cn. Mwisho wa kutuma maombi ni tarehe 30 Aprili, 2018. Mafunzo haya yanaratibiwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Vilevile,  Serikali ya China imetoa fursa ya ufadhili wa mafunzo ya muda mrefu kwa ngazi ya Shahada ya Uzamili katika masuala ya Utawala na Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Nadharia ya Uchumi na Maendeleo ya Taifa. Maelezo ya ziada ya kozi hizi yanapatikana kupitia http://www.isscad.pku.edu.cn. Pia maombi yatumwe kupitia http://www.administration@isscad.pku.edu.cn. Mwisho wa kutuma maombi ni tarehe 30 Mei, 2018. Mafunzo haya yanaratibiwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa pamoja na Ofisi ya Rais, Menejimentii ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Wakati huohuo, Serikali ya China imetoa fursa za ufadhili wa mafunzo kwa wataalam wa kilimo kutoka Tanzania. Mafunzo haya yatafanyika Beijing, China. Mratibu wa mafunzo haya ni Wizara ya Kilimo na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Kwa upande mwingine, Wizara imepokea nafasi za mafunzo ya muda mfupi kutoka Serikali ya Ujerumani katika Kozi ya Stashahada ya Juu ya Usimamizi wa Mazingira kwa Nchi Zinazoendelea (International Postgraduate Course on Environmental Management for Developing Countries). Mafunzo haya yatafanyika Ujerumani kuanzia tarehe 10 Januari, 2019 hadi tarehe 12 Julai, 2019. Mafunzo haya yanaratibiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais, (Mazingira) na Baraza la Mazingira (NEMC).
Pia, Jamhuri ya Korea kupitia Program ya Dkt. Lee Jong-Wook imetoa nafasi mbili za ufadhili wa masomo ya muda mfupi kwa wataalam wa tiba kwa kipindi cha kati ya miezi 2 hadi 12. Mafunzo haya yanaratibiwa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam
06 Aprili, 2018

Waziri Mahiga aongoza kumbukumbu za Wataalam wa Kichina waliokufa wakati wa ujenzi wa Reli ya TAZARA



Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Augustine Mahiga (Mb.), pamoja na Balozi wa China nchini Mhe. Wang Ke  wakiweka mashada ya maua kwenye mnara uliopo kwenye makaburi ya wataalam 70 kutoka China waliokufa wakati wa ujenzi wa Reli ya Tazara, wakati wa maadhimisho ya utamaduni wa Wachina na kuwakumbuka wataalam hao yaliyofanyika kwenye eneo la makaburi walikozikwa wataalam hao lililopo Gongo la mboto, Dar es Salaam. Maadhimisho hayo yalihudhuriwa pia na Waziri wa Katiba na Sheria, Prof. Palamagamba Kabudi na Katibu Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Bw. Joseph Butiku. 
Dkt. Mahiga pamoja na Viongozi mbalimbali kutoka Serikalini wakitoa heshima zao kwa kuinamisha vichwa kama ishara ya kuwakumbuka wataalam hao kutoka China.  


Dkt. Mahiga akiweka Ua katika moja ya kaburi la wataalam hao.Wanaoshuhudia ni Balozi wa China, Mhe. Wang Ke, Prof. Palamagamba Kabudi, Bw. Joseph Butiku na viongozi wengine.
Dkt. Mahiga akihutubia katika hafla hiyo mara baada ya kumaliza zoezi la kuweka maua kwenye makaburi ya wataalam wa kichina waliokufa wakati wa ujenzi wa reli ya Tazara. Katika Hotuba hiyo waziri mahiga aliendelea kuusifu ushirikiano wa Tanzania na China katika sekta mbalimbali, ambapo  Ujenzi wa reli ya Tazara ulipelekea kuanzishwa kwa  viwanda mbalimbali, vikiwemo Kiwanda cha nguo cha Urafiki, Kiwanda cha dhana za kilimo cha Ufi, ambavyo vilipelekea chachu ya maendeleo Tanzania. 
Naye Balozi Wang Ke naye akitoa hotuba yake wakati wa hafla hiyo.
Dkt. Mahiga akizungumza na waandishi wa Habari mara baada ya kumaliza hafla hiyo.
Dkt. Mahiga akiweka saini kwenye kitabu cha kumbukumbu ya vifo vya wataalam hao.








Thursday, April 5, 2018

Waziri Mahiga akutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Shelisheli na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Ugiriki

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Augustine Mahiga (Mb.) akutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Shelisheli Mhe. Balozi Barry J. J. Faure (kushoto), mazungumzo hayo yalifanyika katika ukumbi wa Mkutano wa Wizara tarehe 05 Aprili,2018, Dar es Salaam. Mhe. Faure yuko hapa nchi kwa ziara ya siku mbili (2) ambapo aliwasili tarehe 03 Machi,2018 na anatarajiwa kuondoka tarehe 05 Aprili,2018 

Pamoja na mambo mengine mazungumzo hayo yalijikita katika kukuza zaidi mahusiano kati ya Tanzania na Shelisheli hasa katika maeneo ya vita dhidi ya madawa ya kulevya, usafirishaji haramu wa binadamu na katika sekta ya nishati.
Aidha, katika ziara hiyo Mhe. Faure aliambatana Mwanasheria Mkuu Bw. Frank Ally, na Kamishina Mkuu wa Polisi Bw. Krishnan Labonte wa nchi hiyo.
Ujumbe ulioambatana na Balozi Faure kutoka kulia ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa nchi hiyo Bw. Frank Ally, Kamishina Mkuu wa Polisi wa nchi hiyo Bw. Krishnan Labonte wakifuatilia mazungumzo hayo.
Mkurugenzi wa Idara ya Afrika Mhe. Balozi Grace Mujuma (wa kwanza kushoto), Katibu wa Waziri Bw. Murobi Magabilo (wa kwanza kulia), pamoja na Afisa Mambo ya  Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Isack Isanzu nao wakifuatilia mazungumzo hayo
Dkt. Mahiga akiagana na Balozi Faure mara baada ya kumaliza mazungumzo yao.
Mhe. Mahiga na mgeni wake Balozi Faure, wakiwa katika picha ya pamoja




 Waziri Mahiga akutana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Ugiriki



Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Augustine Mahiga (Mb.) akutana na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Ugiriki Mhe. Terens Quicq (kushoto), mazungumzo hayo yalifanyika katika ukumbi wa Mkutano wa Wizara tarehe 05 Aprili,2018, Dar es Salaam. Mhe. Quicq aliwasili hapa nchini tarehe 04 Aprili,2018 

Pamoja na mambo mengine mazungumzo yalijikita katika kukuza zaidi mahusiano kati ya Tanzania na Ugiriki hasa katika biashara na Uwekezaji katika maeneo ya viwanda vya kuzalisha madawa ya binadamu na wanyama,nishati na utalii.
Ujumbe uliongozana na Mhe. Quicq, kutoka kulia ni Balozi wa Ugiriki nchini Tanzania mwenye makazi yake nchini Kenya, Mhe. Balozi Konstantinos Moatsos(Kulia), Balozi wa Heshima Bw.William K. Ferentinos(katikati) na Bi. Maya Solomou kutoka Ubalozi wakifuatilia mazungumzo hayo.

Mazungumzo yakiendelea
Dkt. Mahiga akiagana na Mhe. Quicq mara baada ya kumaliza mazungumzo yao.
 Wakiwa katika picha ya pamoja baada ya mazungumzo .

Katibu Mkuu afanya mazungumzo na Balozi wa Uingereza nchini

 Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Adolf Mkenda akimkaribisha Balozi wa Uingereza nchini Mhe. Balozi Sara Catherine cooke, alipomtembelea Wizarani kwa ajili ya mazungumzo yaliyofanyika katika ukumbi wa Mkutano wa Wizara tarehe 4 Aprili,2018, Dar es Salaam.

Mazungumzo hayo pamoja na mambo mengine yalijikita kwenye ushiriki wa Tanzania katika Mkutano wa Wakuu wa Serikali na nchi za Umoja wa Madola (CHOGM), Mkutano huo unaotarajiwa kufanyika tarehe 16-20, Jijini London, Uingereza. 

 Prof. Mkenda akifafanua jambo kwa Balozi Sarah Cooke katika mazungumzo hayo.

 Mazungumzo yakiendelea, wanaofuatilia mazungumzo hayo ni Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Celestine Mushy(katikati kulia), anayefuata ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa Bw. Deusdedit Kaganda na wa mwisho kushoto ni Afisa kutoka Ubalozi Bw. Mark Thayre.

Wakiwa katika picha ya pamoja baada ya mazungumzo.

Wednesday, April 4, 2018

Katibu Mkuu akutana na Ujumbe kutoka Ubalozi wa Japan



Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Aldof Mkenda(Kulia) akifafanua jambo kwa Kaimu Balozi wa Japan nchini Bw. Hiroyuki Kubota katika mazungumzo yaliyofanyika katika ukumbi wa Wizara, Dar es Salaam, tarehe 03 Aprili,2018. 

Mazungumzo hayo yalijikita katika kuboresha mahusiano ya Tanzania na nchi ya Japan. Prof. Mkenda alisema Mahusiano ya Tanzania na Japan ni  ya Kihistoria na katika kuendelea kudumisha mahusiano haya na kwa kuzingatia Japan ni kati ya nchi zinazosifika katika Teknolojia mbalimbali za kisasa, aliwakaribisha kuongeza uwekezaji katika eneo hilo. Naye Bw. Kubota aliahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania katika maeneo mbalimbali hasa katika kujenga uwezo wa wataalamu wa Tanzania ili kuweza kushiriki vyema katika uchumi wa Viwanda.
                                     

     Mazungumzo yakiendelea, wanaofuatilia mazungumzo hayo kutoka kushoto ni Maafisa kutoka Ubalozi wa Japan na kulia ni Maafisa kutoka Wizarani.
                                      
Wakiwa katika picha ya pamoja baada ya mazungumzo

Tuesday, April 3, 2018

Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda akutana kwa mazungumzo na Balozi wa China nchini


Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Innocent Shiyo akizungumza na Balozi wa China nchini, Mhe. Wang Ke. Katika mazungumzo yao waligusia umuhimu wa kuimarisha  ushirikiano kati ya Tanzania na China hususan kwenye sekta ya elimu. Mazungumzo hayo yalifanyika Wizarani, Dar es Salaam tarehe 03 Aprili, 2018.
Balozi wa China nchini, Mhe. Wang Ke kwa pamoja na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Msinga iliyopo Moshi Vijijini, Bi. Martina Mroso wakisaini Cheti cha Makabidhiano ya Mchango kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa matundu 16 ya Vyoo na Bwalo la Kulia Chakula katika Shule ya Msingi Msinga. Thamani ya Mchango huo ni shilingi milioni 32.
Mwalimu Mroso akimshukuru Balozi Wang Ke kwa mchango waliotoa kwa ajili ya kuisaidia Shule ya Msingi Msinga iliyopo Moshi Vijijini.
Maafisa kutoka Ubalozi wa China.
Balozi Shiyo na Balozi Wang Ke wakiwa katika picha ya pamoja na Mwalimu Mroso (wa tatu kushoto) pamoja na wajumbe wengine walioshiriki mazungumzo
Mazungumzo yakiendelea

Tanzania na Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi zasaini Mkataba wa Mkopo wa Masharti nafuu.

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa - TAMISEMI, Mhe. Mhandisi Mussa Ibrahim Iyombe (Kushoto), na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi, Mhe. Saif Al Suwaidi, wakisaini Mkataba wa Mkopo wenye Masharti nafuu wa kiasi cha shilingi bilioni34 kwa ajili ya kuboresha barabara ya Uvinza hadi Malagarasi, yenye urefu wa Kilometa 31, kwa kiwango cha lami.

   Mhe. Mhandisi Mussa Ibrahim Iyombe (Kushoto), na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi, Mhe. Saif Al Suwaidi, (Kushoto),wakionesha mkataba huo baada ya kusainiwa.

Mhe. Mhandisi Mussa Ibrahim Iyombe (katikati) na Balozi wa Tanzania nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu, Mhe. Mbarouk Nassor Mbarouk kushoto kwake na wengine ni watumishi wa Wizara, Wizara ya Fedha na watumishi wa Ubalozi wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kusaini Mkataba huo.

Tanzania na Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi zasaini Mkopo wa masharti nafuu


TANZANIA NA MFUKO WA MAENDELEO WA ABU DHABI ZASAINI MKOPO WA MRADI WA UJENZI WA BARABARA YA UVINZA-MALAGARASI YA MKOANI KIGOMA

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi leo tarehe 02 Aprili, 2018 zimesaini mkataba wa mkopo nafuu wa Dola za Kimarekani milioni 15 kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa barabara ya Uvinza-Malagarasi yenye urefu wa kilometa 51.

Hafla fupi ya uwekaji saini wa mkataba huo imefanyika katika makao makuu ya mfuko huo yaliyopo Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) ambapo Mhandisi Mussa Ibrahim Iyombe, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa amesaini kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mhe. Mohamed Saif Al Suwaidi Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi amesaini kwa niaba ya Mfuko huo.

Kusainiwa kwa mkataba huo ni mwendelezo wa ushirikiano baina ya  Tanzania na mfuko huo baada ya kukamilika kwa awamu ya kwanza ya barabara ya Kidahwe-Uvinza (KM 77) ambayo pia ilifadhiliwa na mfuko huo kwa mkopo nafuu wa Dola za Kimarekani milioni 57. Hivyo, kukamilika kwa barabara ya Uvinza –Malagarasi kutaunganisha Daraja la Malagarasi (Kikwete Bridge) ikiwa ni azma ya Serikali ya kuunganisha barabara za Kigoma, Tabora hadi Manyoni (Singida) ambapo pia itaiunganisha nchi jirani za Burundi na Kongo DRC.

Akizungumza baada ya kusaini mkataba huo, Mhandisi Iyombe amesema kuwa, Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuipeleka Tanzania kwenye uchumi wa kati kwa kuimarisha miundombinu mbalimbali ikiwemo barabara ambapo kusainiwa kwa mkataba huo ni ishara mojawapo.
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi kwa upande wake amesema kuwa Mfuko huo uko tayari kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo nchini hususan katika kipindi hiki ambapo Serikali ya Tanzania imeidhihirishia dunia umakini katika kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo kwa kufufua nidhamu ya fedha; kupambana na rushwa pamoja na uwajibikaji kwa manufaa ya watanzania.

Kwa upande wake, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Umoja wa Falme za Kiarabu Mhe. Mbarouk Nassor Mbarouk  amesema kuwa mahusiano baina ya nchi ya Tanzania na UAE yameendelea kukua siku hadi siku, na kwa sababu hiyo wawekezaji; wafanyabiasha na wadau wa maendeleo wa UAE ukiwamo Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi wamezidi kuiamini Tanzania na kuendelea kushirikiana kwa karibu.

Balozi Mbarouk alisema kuwa, UAE ina fursa nyingi sana katika uchumi ambapo Tanzania inaweza kunufaika nazo hususan kwenye upande wa uwekezaji, biashara na utalii. Tanzania inaweza kupata wawekezaji wakubwa kutoka UAE; kupata soko la bidhaa zake hususan mazao ya kilimo na mifugo pamoja na kukuza utalii kupitia familia za kifalme zinazokuja kutalii nchini lakini kwa kuvutia watalii wanaotembelea huku hususan Dubai ili waje pia Tanzania. “Hii yote inawezekana kutokana na mahusiano mazuri yalipo baina ya Tanzania na Umoja wa Falme za Kiarabu yanayoendelea kukua siku hadi siku” …alisema Balozi Mbarouk.

MWISHO,
02 Aprili, 2018
ABU DHABI, UMOJA WA FALME ZA KIARABU