Saturday, December 15, 2018

Waziri Ummy Mwalimu aiwakilisha Tanzania mkutano maalum wa mama na mtoto, India

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu akizungumza kwenye Mkutano Maalum wa 4 wa Mawaziri wa Afya kuhusu Afya ya Mama na Mtoto (Partnership for Maternal, Newborn and Child Health Forum 2018) uliofanyika New Delhi, India kuanzia tarehe 12 hadi 14 Desemba, 2018. 


Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu akisalimiana na Waziri Mkuu wa India, Mhe. Narendra Modi wakati wa ufunguzi wa Mkutano Maalum wa Mawaziri wa Afya uliofanyika katika jiji la New Delhi, India kuanzia tarehe 12 hadi 14 Desemba, 2018.
Picha ya pamoja ya Mawaziri wa Afya pamoja na Waziri Mkuu wa India, Mhe. Narendra Modi wakati wa ufunguzi wa Mkutano huo


Picha ya pamoja ya Mhe.Waziri Ummy Mwalimu na ujumbe wa Tanzania unaoshiriki Mkutano Maalum wa Afya ya Mama na Mtoto jijini New Delhi, India. Wa pili kukia ni Mhe. Baraka Luvanda, Balozi wa Tanzania nchini India


Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee naWatoto, Mhe. Ummy Mwalimu akijadiliana jambo na Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Baraka Luvanda (kushoto} wakati wa Mkutano Maalum wa 4 wa Mawaziri wa Afya kuhusu Afya ya Mama na Mtoto


Mhe. Ummy Mwalimu akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa UNFPA, Marekani, Bibi Natalia Kanem wakati wa Mkutano Maalum wa Mawaziri wa Afya kuhusu Afya ya Mama na Mtoto uliofanyika New Delhi, India
====================================================
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO ASHIRIKI MKUTANO MAALUM WA MAWAZIRI WA AFYA KUHUSU AFYA YA MAMA NA MTOTO ULIOFANYIKA JIJINI NEW DELHI, INDIA KUANZIA TAREHE 12-14 DISEMBA, 2018.

Tanzania imeshiriki katika Mkutano Maalum unaojadili Afya ya Mama na Mtoto unaojulikana kama "4th Partnership for Maternal,Newborn and Child Health 2018" uliofanyika katika jiji la New Delhi, India kuanzia tarehe 12 hadi 14 Desemba,2018. 

Katika Mkutano huu,Tanzania imewakilishwa na Mhe.Ummy Mwalimu,Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Mkutano huu ulifunguliwa na Mhe.Shri Narendra Modi, Waziri Mkuu wa India tarehe 12 Desemba, 2018. Mkutano huu unawakutanisha pamoja Mawaziri wa Afya kutoka nchi mbalimbali duniani kwa lengo la kujadili changamoto zilizopo katika eneo la Afya ya Mama na Mtoto na kuweka mikakati ya pamoja ya kuzitatua changamoto hizo ili kuboresha upatikanaji wa huduma za Afya ya Mama na Mtoto.

Katika hotuba yake ya ufunguzi, Waziri Mkuu wa India alieleza mafanikio yaliyopatikana katika kupunguza vifo vya mama mjamzito na watoto wachanga kufuatia mikakati mizuri iliyowekwa na Serikali ya India na kuzitaka nchi washiriki kuweka mipango thabiti itakayotekelezeka katika kupunguza vifo vya mama na mtoto.

Kwa upande wake, Mhe.Ummy Mwalimu alieleza hatua mbalimbali zilizochukuliwa katika kupunguza vifo vya mama na motto nchini Tanzania ikiwemo kuboresha utoaji wa huduma za afya katika ngazi za chini kwa kuboresha vituo vya Afya na kuajiri watumishi wapya kwenye maeneo yenye upungufu. Pia, ameeleza hatua nyingine zinazochuliwa na serikali ni kumlinda mwanamke kutokana na unyanyasaji wa jinsia ambapo madawati ya jinsia yamezinduliwa katika majeshi ya polisi na magereza ili kuhakikisha mwanamke analindwa wakati wote. 

Kadhalika, Mhe.Ummy ameueleza mkutano huo mikatikati iliyopo nchini ya kuhakikisha uboreshaji na utoaji wa huduma za Afya ya Mama na Mtoto unakuwa endelevu, ambapo aliweka bayana mipango hiyo ni pamoja na Kuongeza bajeti ya fedha katika sekta ya Afya, kuimarisha huduma za afya ya Mama na Mtoto kuanzia ngazi ya jamii. 

Mipango mingine ni kuimarisha huduma kwa kuboresha vituo vya afya na kuajiri watumishi wanaohitajika, kutoa elimu ya uzazi wa mpango kwa walengwa pamoja na kutoa huduma stahiki ili kupunguza na kumlinda motto kutokana na maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.

Suala jingine la msingi zaidi ni kuilinda jamii kwa kutoa elimu ya kutosha kuhusu magonjwa ya saratani hususani saratani ya mlango wa kizazi ambayo sasa ni tatizo kubwa kwa akina mama duniani kote.

-Mwisho-



































Wednesday, December 12, 2018

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI



TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Viongozi kutoka nchini Cuba na Umoja wa Mataifa wanafanya ziara za kikazi nchini Tanzania zenye lengo la kuimarisha uhusiano na ushirikiano baina ya Tanzania na mamlaka hizo.

Naibu Waziri wa Kilimo wa Cuba, Mhe. Jose Miguel Rodriguez de Armas na ujumbe wake waliwasili nchini tarehe 12 Desemba 2018 na watakuwepo hadi tarehe 19 Desemba 2018.

Ziara ya Mhe. Naibu Waziri wa Cuba na ujumbe wake hailengi tu kukuza na kuimarisha ushirikiano wa kihistoria kati ya Cuba na Tanzania, bali  inalenga pia kufanya majadiliano na wadau husika, ya namna ya kuondoa changamoto zinazokikabili kiwanda cha Labiofam ili kiweze kufanya kazi kwa ufanisi.  

Wakati wa ziara hiyo, Mhe. Naibu Waziri anatarajiwa kufanya mazungumzo na viongozi wa juu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Wizara ya Kilimo na Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC).

Kiwanda cha Labiofam kimejengwa Kibaha mkoani Pwani kwa msaada wa Serikali ya Cuba kwa ajili ya kutengeneza viuadudu vya kuua viluwiluwi wa mbu wanaosababisha ugonjwa wa malaria.

  Kwa upande wa Umoja wa Mataifa, ujumbe wa Umoja huo ukiongozwa na Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya Misheni za Ulinzi na Amani, Bw. Jean- Pierre Lacroix na Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa MONUSCO utafanya ziara nchini tarehe 13 na 14 Desemba 2018.

Ziara hiyo ni sehemu ya kuadhimisha mwaka mmoja tokea shambulizi lililofanywa na waasi wa Allied Democratic Forces dhidi ya kombania ya Tanzania katika maeneo ya Simulike, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Askari 14 wa Tanzania walipoteza maisha katika shambulizi hilo.

Ujumbe huo unatarajiwa kufanya mazungumzo na viongozi wa Serikali na vyombo vya ulinzi na usalama akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga kuhusu kuboresha ushiriki wa Tanzania katika vikosi vya kulinda amani.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dodoma
 12 Desemba 2018


Tuesday, December 11, 2018

Maonesho ya Jua Kali/Nguvu Kazi yamalizika kwa mafanikio kwa Tanzania


Seneta wa Kaunti ya Uasin Gishu, Mhe. Profesa Magrate Kamar akifunga Maonesho ya 19 ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Jua Kali/Nguvu Kazi jana yaliyofanyika kwa muda wa siku kumi katika Kaunti ya Uasin Gishu mjini Endoret Kenya. Kwenye hotuba yake Prof. Kamar aliwataka wajasiriamali kuongeza mawasiliano miongoni mwao ili kukuza soko la bidhaa zao ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ambazo zimekuwa na viwango bora

 Naibu Katibu wa Wizara ya Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto wa Zanzibar,  Bi. Mau Makame Rajab akitoa neno la shukrani katika sherehe ya kufunga  maonesho ya 19 ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Jua Kali/Nguvu Kazi jana zilizofanyika katika Kaunti ya Uasin Gishu mjini Eldoret, Kenya.
Afisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Hassan Mnondwa akipokea cheti cha pongezi jana kwa mchango wake wa kufanikisha kufanyika kwa maonesho ya 19 ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Jua Kali/Nguvu Kazi yaliyofanyika katika kaunti ya Uasin Gishu, Eldoret nchini Kenya

Afisa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi na Ajira, Bi. Sara Daudi akipokea cheti cha pongezi jana  kwa mchango wake wa kufanikisha kufanyika kwa maonesho ya 19 ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Jua Kali/Nguvu Kazi yaliyofanyika katika kaunti ya Uasin Gishu, Eldoret.

Siku ya Tanzania ilivyosherehekewa sambamba na maonesho ya Jua Kali/Nguvu kazi

Gavana wa Kaunti ya Uasin Gishu, Jackson K. Mandgo alipokuwa akizungumza na wajasirimali katika sherehe ya siku ya Tanzania viwanja vya michezo Kaunti ya Uasin Gishu mjini Eldoret katika maonesho ya Jua Kali/Nguvu Kazi yanayoendelea mjini hapo. Kushoto ni Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Mhe. Dkt. Pindi Chana.

Gavana wa Kaunti ya Uasin Gishu, Mhe. Jackson K. Mandgo akiweka saini kitabu cha wageni mara baada ya kufika  kwenye banda la  Tanzania lililopo kwenye viwanja vya michezo vya Kaunti ya Uasin Gishu mjini Eldoret katika maonesho ya Jua Kali/Nguvu Kazi. Mhe.Mandgo alikuwa mgeni rasmi katika sherehe ya siku ya Tanzania katika maonesho hayo zilizofanyika tarehe 9 Desemba 2018. Kulia ni Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Mhe. Dkt. Pindi Chana na kushoto ni Seneta wa Kaunti ya Uasin Gishu, Mhe. Profesa Margrate Kamar.

Gavana wa Kaunti ya Uasin Gishu, Mhe. Mandgo akipanda mti ikiwa ni kumbukumbu ya maadhimisho ya miaka 57 ya Uhuru wa Tanzania Bara zilizoadhimishwa leo tarehe 09 Desemba 2018. Wanaoshuhudia tukio hilo ni pamoja na  Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Mhe. Dkt. Pindi Chana
Gavana wa Kaunti ya Uasin Gishu, Mhe. Jackson K. Mandgo akinunua nguo alipotembelea Banda la Wajasiriamali wa Tanzania baada ya kufurahia bidhaa mbalimbali zikiwemo nguo. Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Mhe. Dkt. Pindi Chana aliambatana na Gavana huyo kutembelea mabanda ya wajasiriamali kutoka Tanzania.



Gavana wa Kaunti ya Uasin Gishu, Mhe. Jackson K. Mandgo akivishwa vazi la kabila la Wamaasai kutoka Tanzania na kukabidhiwa mkuki na Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Mhe.Dkt. Pindi Chana wakati wa sherehe ya siku ya Tanzania zilizofanyika sambamba na maonesho ya Jua Kali/Nguvu Kazi
===============================================

Gavana wa Kaunti ya Uasin Gishu nchini Kenya, Mhe. Jackson K. Mandgo amezishauri Serikali za Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuweka bidhaa za wajasiriamali katika maduka makubwa (super market) ili wananchi kuzinunua na kuacha tabia ya kuthamini bidhaa za kutoka nje.

Gavana Mandgo aliyasema hayo wakati wa kusherehekea siku ya Tanzania iliyofanyika sambamba na maonesho ya 19 ya Afrika Mashariki ya Jua kali/Nguvu Kazi yanayoendelea katika Viwanja vya michezo vya Kaunti ya Uasin Gishu mjini Eldoret Kenya ambapo alikuwa mgeni rasmi kwenye siku ya Tanzania. Mhe. Mandgo alisema kwamba bidhaa za wajasirimali kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zinakidhi vigezo vya kuuzwa katika maduka hayo kutokana na kuwa na  ubora wake.

Katika maonesho ya Jua Kali/Nguvu Kazi kila nchi husherehekea siku yake kwa kutangaza bidhaa na utamaduni wake. Tanzania ilitumia fursa hiyo kusherehekea miaka 57 ya Uhuru wa Tanzania Bara iliyoadhimishwa nchini kote tarehe 9 Desemba 2018.

Gavana Mandgo alisema kwamba wajasiriamali wanauwezo mkubwa wa kutengeneza  bidhaa bora ambazo kwa bahati mbaya hazipatikani katika maduka makubwa (super makert) hivyo alitoa wito kuwa wakati umefika sasa kwa bidhaa hizo kuuzwa katika maduka hayo.

Aidha alizishauri nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kuvitumia Vituo vya Elimu za Ufundi kama VETA hapa nchini, kutoa taaluma zaidi kwa wajasiriamali kwa lengo la kuzalisha bidhaa zenye ubora na viwango vya kimataifa.

Alisema kwamba  Serikali ya Kenya hususan Kaunti ya Uasin Gishu ya  Eldoret itapeleka Mswada katika Baraza lake kwa kufanyia marekebisho ya sheria ya kutoa vyeti kwa wajasiriamali ambao watatahiniwa kwa  ubora wa bidhaa ambazo wanazalisha badala ya kufanya mitihani ya kuandika.

Pia alizitaka ofisi zote za Serikali ya Kaunti ya Uasin Gishu, kutumia samani zinazotengenezwa na wajasiriamali kutokana  na kuwa  ni madhubuti na zenye ubora kuliko zilivyotengenezwa kutoka  nje ya Afrika Mashariki.

Gavana Mandgo ameipongeza Tanzania  kwa kusherehekea miaka 57 ya Uhuru wa Tanzania Bara.


Tanzania yazidi kung'ara Maonesho ya Jua Kali/Nguvu Kazi nchini Kenya


Waziri wa Biashara na Viwanda wa Kaunti ya Siaya Kenya Mhe. Jaokon O. Odinga (katikati) akizungumza na Balozi wa Tanzania nchini Kenya Balozi Dkt. Pindi Chana (kulia)  alipotembelea banda la Tanzania katika Maonesho ya 19 ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Jua Kali/Nguvu Kazi yanayoendelea katika Kaunti ya Uasin Gishu mjini Eldoret nchini Kenya, pembeni ni Mkurugenzi  Kitengo cha Diaspora Balozi Anisa Mbega wa Wizara ya Mambo ya Nje na  Ushirikiano wa Afrika Mashariki. 

Balozi wa Uganda nchini Kenya, Mhe. Phibby Otaala (kushoto) akibadilishana mawazo na Afisa Biashara wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Hassan Mnondwa (aliyesimama) juu ya ubora wa bidhaa za Tanzania zinazozasilishwa  na wajasiriamali  na kuuzwa katika maonesho ya Jua kali/Nguvu Kazi alipotembelea banda la Tanzania. Anayeweka saini kitabu cha wageni ni  Mhe. Namugwanya Benny Bugembe (MP) Waziri wa Nchi anayesimamia Mamlaka ya Jiji la Kampala Uganda.
Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Mhe. Dkt. Pindi Chana wa pili kutoka kushoto, Balozi wa Uganda nchini Kenya Mhe. Phibby Otaala wa pili kutoka kulia wakishikana mikono pamoja na viongozi wengine wa Uganda. Kutoka kushoto ni Waziri wa Biashara  na Viwanda wa Kaunti ya Uasin Gishu Dkt. Emily Kongos na kulia ni Mhe. Namugwanya Benny Bugembe (MP) Waziri wa Nchi anayesimamia Mamlaka ya Jiji la Kampala Uganda wakishikana mikono kuonesha ishara ya mshikamano wa viongizi wanawake wa Afrika Mashariki.

Juu na Chini ni Wananchi wa Kaunti ya Uasin Gishu wakitembelea kwa wingi katika mabanda ya Tanzania   wakifurahia na kununua bidhaa zinazozalishwa na Wajasiriamali na kuoneshwa katika maonesho ya Jua Kali/Nguvu Kazi yanayoendelea  mjini Eldoret.
Maonesho ya 19 ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Jua Kali/Nguvu Kazi yanayoendelea  kufanyika katika Kaunti ya Uasin Gishu mjini Eldoret Kenya ni ya kwanza kufanyika nje ya miji mikuu ya Nchi Wanachama za Jumuiya ya Afrika Mashariki.


Friday, December 7, 2018

Watanzania wanogesha maonyesho ya 19 ya Jua Kali/ Nguvu Kazi


Juu na Chini ni Wajasiriamali wa Tanzania wakionesha bidhaa zao katika maonesho ya 19 ya Afrika Mashariki ya Jua Kali/Nguvu Kazi yanayofanyika katika Kaunti ya Uasin Gishu jijini Eldoret nchini Kenya. Kiasi cha Wajasirimali  wa Tanzania 250 waliwasili  mjini humo kwa ajili ya kushiriki maonesho  hayo.



Wananchi mbalimbali waliojitokeza kwenye maonyesho hayo wakionekana wakifurahia bidhaa za wajasiriamali zilizozalishwa na Watanzania wakati walipoyatembelea mabanda ya Tanzania katika maonesho ya 19 ya Jua Kali/Nguvu Kazi yanayoendelea jijini la Eldoret nchini Kenya.

Thursday, December 6, 2018

Japan yaadhimisha Siku ya Taifa

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe. Joseph Kakunda (Mb.) akihutubia kwenye maadhimisho ya siku ya Taifa la Japani ambapo katika hotuba yake ameipongeza Japan kwa kuendeleza ushirikiano na Tanzania katika sekta mbalimbali zinazo changia maendeleo ya nchi kama vile ujenzi wa miundombinu, Elimu na Afya.  Aidha, Mhe. Kakunda ameihakikishia Japan kuwa Tanzania itaendelea kudumisha na kuimarisha ushirikiano pamoja na kuendeleza urafiki wa kidiplomasia kati ya Mataifa hayo mawili. Hafla hiyo imeudhuriwa na Mabalozi mbalimbali na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa yaliyopo nchini Tanzania. Maadhimisho hayo yamefanyika katika makazi ya Balozi Masaki, jijini Dar es Salaam 
Balozi wa Japan nchni naye akitoa hotuba kwenye maadhimisho ya siku ya Japan.
Balozi wa Japani akiwa katika picha ya pamoja na wageni waalikwa walio hudhuria maadhimisho hayo.




Tuesday, December 4, 2018

Waziri Mahiga atembelea kiwanja kitakachojengwa Ofisi za Wizara kilichopo Ihumwa Dodoma

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga (kushoto) akisalimiana na Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Bw. Godwin Kunambi alipofika eneo la kiwanja cha Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki lililopo Eneo la Mji wa Serikali la Ihumwa jijini Dodoma kwa ajili ya kuangalia maandalizi ya mwisho kabla ya kuanza  ujenzi wa Ofisi za Wizara unaotarajiwa kuanza hivi karibuni. Katikati ni Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu,  Bibi Maimuna Tarishi. 
Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Bw. Kunambi kwa pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bibi Dorothy Mwanyika (mwenye miwani myeusi) wakimwonesha Mhe. Waziri Mahiga ramani inayoonesha kilipo kiwanja cha Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. 

Mhe. Waziri akimsikiliza Bibi Tarishi alipokuwa akimweleza jambo kuhusu ramani hiyo 
Mhe. Waziri Mahiga akiwaeleza jambo Katibu Mkuu,Ofisi ya Waziri Mkuu, Bibi Tarishi,  Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bibi Mwanyika na Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Bw. Kunambi  alipofika eneo la kiwanja kilichotengwa kwa ajili ya kujenga Ofisi za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kilichopo Ihumwa. 
Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Bw. Kunambi akimwonesha  Mhe. Waziri Mahiga ukubwa wa eneo la kiwanja cha Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

 

Mhe. Mahiga akimsikiliza Mkurugenzi wa Kitengo cha Ununuzi na Ugavi cha Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Manyama Mapesi akimweleza kuhusu eneo hilo la kiwanja cha Wizara kilichopo Ihumwa. Wengine ni Watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki waliofika kwenye kiwanja hicho.