Friday, April 12, 2019

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje akutana kwa mazungumzo na Mtaalam wa Uchumi kutoka Ujerumani


Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro akizungumza wakati wa kikao na Prof. Helmut Asche (kulia) ambaye ni Mtaalam wa Uchumi hususan masuala yanayohusiana na Ubia wa Kiuchumi kati ya Ulaya na Afrika (EPA) kutoka Ujerumani. Kikao hicho kilifanyika hivi karibuni jijini Dodoma.
Prof. Asche kutoka Ujerumani akizungumza kwenye kikao kati yake na Naibu Waziri, Mhe. Ndumbaro. Kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe akimsikiliza Prof. Asche. 
Katibu Mkuu, Dkt. Mnyepe akichangia hoja wakati wa kikao hicho
Prof. Asche akifafanua jambo kuhusu EPA wakati wa kikao kati yake na Mhe. Dkt. Ndumbaro huku wajumbe wengine wakifuatilia. Kulia ni  Bw. Jestas Nyamanga, Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. 
Dkt. Mnyepe (kulia) akiwa na Dkt. Edwin Mhede (katikati), Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara wakifuatilia kikao. 
Kikao kikiendelea
Mhe. Dkt. Ndumbaro akiteta jambo na Prof. Asche mara baada ya mazungumzo kati yao
Mhe. Dkt. Ndumbaro akiwa na Prof. Asche na wajumbe wengine wakati wa chakula cha jioni kilichoandaliwa kwa heshima ya Prof. Asche.


Thursday, April 11, 2019

Vivutio vya Utalii kutangazwa Malaysia, Ufilipino, Thailand na Indonesia

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Vivutio vya Utalii kutangazwa Malaysia, Ufilipino, Thailand na Indonesia

Dodoma, 11 Aprili 2019

Makampuni 20 ya Mawakala wa Utalii na Tiketi za ndege (Tour Operators & Travel Agents) pamoja na Waandishi wa Habari kutoka katika nchi za Malaysia, Indonesia, Ufilipino na Thailand walifanya ziara ya mafunzo ya kutembelea vivutio vya utalii nchini  kuanzia tarehe 1 – 7 Aprili 2019.

Mafunzo hayo yaliyoratibiwa na Ubalozi wa Tanzania nchini Malaysia kwa kushirikiana na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) yalijumuisha washiriki 20 ambapo Malaysia ilitoa washiriki 5, Thailand washiriki 6, Philippines Washiriki 4 na Indonesia washiriki 5.

Washiriki hao walitembelea maeneo mbalimbali yakiwemo Hifadhi ya Mamlaka ya Ngorongoro, Mbuga ya Serengeti, duka Maarufu la kuuza madini ya Tanzanite, duka maarufu la zawadi la Arusha Cultural Heritage, sehemu ya historia ya masalia ya Binadamu wa Kale la Olduvai (Oldupai) Gorge na Kijiji cha Wamasai ili kujifunza uhalisia wa maisha yao. Wakiwa kwenye maeneo hayo, wageni walifanikiwa kuona wanyama maarufu watano- big five (Simba, Nyati, Faru, Chui na Tembo) na kushuhudia makundi ya Wanyama aina ya Nyumbu, Pundamilia, na Swala ambao hufanya ziara ya mzunguko maarufu kama Great Migration.

Wageni kabla ya kuagwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii, Jaji Mstaafu Thomas Mihayo pamoja na Bibi. Devotha Mdachi, Mkurugenzi Mwendeshaji wa Bodi ya Utalii waliahidi kuitangaza Tanzania kama eneo jipya la utalii kwa nchi zao.

Wakati huo huo, Balozi wa Tanzania nchini Malaysia, Mhe. Dkt. Ramadhani Dau amepokea nafasi 160 za ufadhili wa masomo ya elimu ya juu (scholarships) kwenye taaluma mbalimbali zenye thamani ya Dola za Marekani milioni 1.9 sawa na Shilingi bilioni 4 za Tanzania. Ufadhili huo umetolewa na Chuo Kikuu cha Selangor (University of Selangor) ambacho pia kinajulikana kama UNISEL kilichopo katika Mkoa wa Selangor, Malaysia, unahusisha masomo ya Bachelors of Civil Engineering, Bachelors of Electrical Engineering, Bachelors of Mechanical Engineering, Bachelors of Occupational Health and Safety, Bachelors of Medical Laboratory, Bachelors of Industrial Biotechnology, Bachelors of Computer Science na Bachelors of Information Technology. Hivi karibuni Watanzania watafahamishwa utaratibu wa kuomba masomo hayo.


Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,

Rais na Makamu Mkuu wa Chuo cha Kikuu cha UNISEL, Prof. Dkt. Mohammad Redzuan Bin Othaman akimkabidhi barua yenye kuainisha ufadhili wa masomo ya elimu ya juu kwa Watanzania kwa Balozi wa Tanzania nchini Malaysia, Mhe. Dkt. Ramadhani Dau.
Dkt. Dau akiangalia miundombinu ya Chuo Kikuu cha UNISEL
Moja ya Vyumba vya madarasa

Dkt. Dau akipata maelezo kuhusu uendeshaji wa chuo hicho.
Wageni kutoka Malaysia, Indonesia, Thailand na Ufilipino walipowasili Tanzania kwa ajili ya ziara ya mafunzo kwenye vivutio vya utalii.
Wageni kutoka Malaysia, Indonesia, Thailand na Ufilipino wakipata chakula.
Balloon lililowabeba wageni kuwazungusha katika mbuga ya Serengeti.


Wednesday, April 10, 2019

Waziri Kabudi akutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Ufaransa nchini

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa Prof. Palamagamba John Kabudi, akimkaribisha Balozi wa Ufaransa nchini, Mheshimiwa Frédéric Clavier alipomtembelea ofisini kwake  jijini Dodoma tarehe 10 Aprili 2019.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirkiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa Prof. Palamagamba John Kabudi, akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo baina yake na Balozi wa Ufaransa nchini Mheshimiwa Frédéric Clavier. Katika mazungumzo hayo Tanzania na Ufaransa wamekubaliana kushirikiana katika kilimo cha zabibu, uzalishaji na uuzaji wa mvinyo katika nchi mbalimbali duniani na usafiri wa anga.
Mazungumzo yakiendelea.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa Palamagamba John Kabudi akiagana na Balozi wa Ufaransa nchini Mheshimiwa Frédéric Clavier baada ya mazungumzo baina yao.


Prof. Kabudi azungumza na Uongozi wa Airtel jijini Dodoma.


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb.) amekutana na kufanya mazungumzo na Uongozi wa kampuni ya Simu ya Airtel, mazungumzo hayo yamefanyika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki jijini Dodoma Tarehe 10 Aprili,2019.
Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi akiwa katika picha ya pamoja na Uongozi wa Kampuni ya Simu za Mkononi Airtel nchini, wapili kutoka kushoto ni Mwanasheria wa Bharti Airtel Bw. Mukesh Bhavnani, wa kwanza kulia Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Tanzania Bw. Sunil Colaso na wakwanza kilia ni Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Airtel Tanzania Bi. Beatrice Singano.


========================================


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb.) leo tarehe 10 Aprili,2019 Jijini Dodoma amekutana na kufanya mazungumzo na Uongozi wa Kampuni ya Simu za Mkononi Airtel ukiongozwa na Bw. Mukesh Bhavnani, Mwanasheria wa Bharti Airtel, Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Tanzania Bw. Sunil Colaso na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Airtel Tanzania Bi. Beatrice Singano.

Katika mazungumzo hayo, Uongozi wa Airtel umemuhakikishia Mheshimiwa Kabudi kuwa Kampuni ya Bharti Airtel itaendelea kuwa Mbia mzuri na Serikali na kwamba wataendelea kupanua wigo wa huduma zao katika maeneo yote nchini na kuhakikisha hudua hizo zinakuwa za viwango na nafuu kwa watumiaji. Na kwamba mpango wao wa uwekezaji na kupanua wigo wa huduma zao hususan maeneo ya vijijini utakuwa moja ya chachu ya maendeleo ya kiuchumi nchini.

Kwa upande wake, Mheshimiwa Kabudi pamoja na kuwashukuru kwa kumtembelea ameihakikishia Bharti Airtel kuwa Serikali iko tayari kuendelea na ubia walionao na iko tayari kuendelea kushauriana na kushirikiana namna bora ya kuimarisha ubia huo ili kuhakikisha huduma zinazotolewa zinakuwa na viwango na zinafika katika maeneo mengi nchini kwa gharama nafuu.

Katibu Mkuu wa Mambo ya Nje akutana kwa mazungumzo na Balozi wa Ufaransa nchini

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano  wa Afrika Mashariki, Dkt.  Faraji Kasidi Mnyepe  alikutana   na kufanya mazungumzo na Balozi wa Ufaransa nchini, Mheshimiwa Frédéric Clavier. Mazungumzo yao yalifanyika hivi karibuni katika Ofisi za Wizara jijini Dodoma. 

Mazungumzo yakiendelea

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano  wa Afrika Mashariki, Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe, akiagana na Balozi wa Ufaransa nchini, Mheshimiwa Frédéric Clavier, mara baada ya mazungumzo kati yao.

Prof. Kabudi akutana kwa mazungumzo na Balozi wa Belarus nchini


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa Prof. Palamagamba John Kabudi, tarehe 9 Aprili, 2019, alikutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Belarus nchini Tanzania mwenye makazi yake Nairobi, Kenya, Mheshimiwa Dmitry Kuptel. Balozi Kuptel yupo nchini kwa ziara ya siku nne kwa lengo la kuimarisha ushirikiano baina ya Tanzania na Belarus.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa Prof. Palamagamba John Kabudi, akimuonesha  Balozi Dmitry Kuptel ulipo mkoa wa Dodoma  wakati alipokuwa akimuelezea Balozi huyo kuhusu uamuzi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa kuhamia Dodoma.

Ujumbe wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashiriki ambao unaohusisha Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Bw. Emmanuel Buhohela (wa kwanza kulia),  Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria, Bibi Caroline Chipeta (kushoto kwa Waziri) na Afisa Mambo ya Nje, Bw. Mohamed Kamal (katikati)  wakimsikiliza Mhe. Waziri Kabudi wakati wa  mazungumzo yake na  Balozi wa Belarus (hayupo pichani)
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa Prof. Palamagamba John Kabudi, akiwa katika picha ya pamoja na ujumbe  wa Tanzania na Belarus ulioshiriki katika mazungumzo hayo.

Tuesday, April 9, 2019

Prof. Kabudi ahimiza wawekezaji kutoka nchi za Nordic kuja kuwekeza Tanzania

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa Prof.  Palamagamba John Kabudi (Mb.), leo tarehe 9 Aprili, 2019 akiwa jijini Dodoma amefungua rasmi Kongamano la kwanza la Uwekezaji pamoja na Mkutano wa mwaka wa Diaspora wa Tanzania linalofanyika nchini Sweden. Ufunguzi wa kongamano hilo ulirushwa moja kwa moja na  Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC1). Kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe.

 Waziri  wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa Prof. Palamagamba John Kabudi, akiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Kasidi Faraji Mnyepe, wakifuatilia kongamano hilo lililorushwa moja kwa moja na TBC 1 huku wao wakiwa Dodoma.

Kongamano likiendelea.

Monday, April 8, 2019

Tanzania na Romania zakubaliana kuimarisha ushirikiano



Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa Palamagamba John Kabudi(Mb.), akiwa katika mazungumzo na Mjumbe Maalum wa Rais wa Romania katika Masuala ya Umoja wa Mataifa (UN),  Balozi Daniela Gitman. 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John  Kabudi, akimwonesha Balozi Daniela Gitman (katikati) ulipo mkoa wa Dodoma katika ramani ya Tanzania
Mjumbe Maalum wa Rais Klaus Iohannis wa Romania katika Umoja wa Mataifa (UN)  Balozi Daniella Gitman (kushoto) akimkabidhi Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb.) ujumbe maalum wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, 


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mheshimiwa Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiwa katika picha ya pamoja na ujumbe kutoka Romania. Wa pili kulia ni Kaimu Mkurugenzi Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo  Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Mona Mahecha.

Friday, April 5, 2019

Waziri Kabudi aongoza kumbukumbu za Wataalam wa Kichina waliokufa wakati wa ujenzi wa Reli ya TAZARA

 Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb.),  akiweka shada la Ua kwenye mnara uliopo kwenye makaburi ya wataalam 70 kutoka China waliokufa wakati wa ujenzi wa Reli ya Tazara, wakati wa maadhimisho ya utamaduni wa Wachina na kuwakumbuka wataalam hao yaliyofanyika kwenye eneo la makaburi walikozikwa wataalam hao lililopo Gongo la mboto, Dar es Salaam. Maadhimisho hayo yalihudhuriwa pia na Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari, Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Mhe. Dkt. Hassan Abbas na Kurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bw. Caesar C. Waitara na viongozi mbalimbali wa serikali
 Prof. Palamagamba Kabudi pamoja na Viongozi mbalimbali kutoka Serikalini wakitoa heshima zao kwa kuinamisha vichwa kama ishara ya kuwakumbuka wataalam hao kutoka China. 
 
 Prof. Palamagamba pamoja na Mhe. Wang Ke wakiweka maua katika moja ya kaburi la wataalam hao.
 Bw. Caesar Waitara akiweka Ua katika moja ya kaburi la wataalam hao.
 Prof. Palamagamba John Kabudi(Mb.), akihutubia katika hafla hiyo mara baada ya kumaliza zoezi la kuweka maua kwenye makaburi ya wataalam wa kichina waliokufa wakati wa ujenzi wa reli ya Tazara. Katika Hotuba hiyo waziri Kabudi aliendelea kuusifu ushirikiano wa Tanzania na China katika sekta mbalimbali ambapo  Ujenzi wa reli ya Tazara ulipelekea kuanzishwa kwa  viwanda mbalimbali.
Aidha,  alieleza kuwa kutoka na Ushirikiano ulipo Tanzania inatarajia kufungua ubalozi mdogo katika mji wa Guangzhou pamoja na kuanzisha Safari ya Ndege za Shirika la Tanzania (ATCL) kuelekea moja kwa moja Guanghzou ambapo utapelekea kuongeza watalii kutoka China kuja kutembelea vivutio vilivyopo nchini Tanzania.
Balozi Wang Ke naye akitoa hotuba yake wakati wa hafla hiyo.

 Sehemu ya wageni waalikwa wakisikiliza kwa makini hotuba zilizo kuwa zikiendelea kutolewa na Prof. Palamagamba John Kabudi na Balozi Wang Ke (hawapo pichani) 
 Prof. Palamagamba John Kabudi akiweka saini kwenye kitabu cha kumbukumbu ya vifo vya wataalam hao.

 Prof. Palamagamba John Kabudi akizungumza na waandishi wa Habari mara baada ya kumaliza hafla hiyo.
Prof. Palamagamba John Kabudi pamoja na Balozi Wang Ke wakiwa katika picha ya pamoja na wageni engine waliohudhuria tulip hilo.

Thursday, April 4, 2019

Nafasi ya kazi katika Jumuiya ya Madola


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

NAFASI YA AJIRA KATIKA JUMUIYA YA MADOLA, LONDON, UINGEREZA.

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, inawahamasisha Watanzania wenye sifa kuomba nafasi ya ajira katika Jumuiya ya Madola, London, Uingereza.

Nafasi hiyo ni Afisa Rasilimali Watu Msaidizi atakayefanya kazi katika kitengo cha Rasilimali Watu na Usimamizi wa Miundombinu. Taarifa zote muhimu kuhusu fursa hiyo ya ajira zinapatikana kwa kupitia tovuti http://thecommonwealth.org.jobs.

Kwa kuzingatia sera ya Jumuiya ya Madola ya usawa wa kijinsia, Sekretarieti ya taasisi hiyo inawahimiza wanawake wengi zaidi wenye vigezo kuomba nafasi hizo. Mchakato wa kumpitisha mtaradhia wa nafasi hiyo utazingatia uwiano wa kikanda hususan kwa nafasi za maafisa waandamizi.

Mwisho wa kutuma maombi kwa nafasi hizo ni Ijumaa tarehe 12 Aprili, 2019.

 Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dodoma
4 Aprili, 2019.

Wednesday, April 3, 2019

Jaji Mstaafu Mark Bomani awataka Watanzania Kuchangia fursa katika Sekta ya Madini

 Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba John Kabudi (Mb.) akimsikiliza kwa makini mgeni wake Jaji Mstaafu Mark Bomani alipomtembelea ofisini kwake jijini Dar es salaam.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Profesa Palamagamba John Kabudi (kushoto) akiwa na mgeni wake Jaji Mstaafu Mark Bomani alipomtembelea ofisini kwake jijini Dar es salaam.

==========================
Mwanasheria mkuu wa kwanza Tanzania Jaji Mstaafu Mark Bomani, amewataka watanzania kuchangamkia fursa ya mabadiliko ya sheria katika sekta za maliasili na madini yaliyofanyika hivi karibuni,kutokana na sheria hizo kuweka mazingira ya usawa (win - win situation)tofauti na sheria zilizokuwepo awali kutoa kipaumbele kwa wawekezaji kutoka Nje ya nchi.

Jji Mstaafu Mark Bomani ameyasema hayo alipomtembelea ofisini kwake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba John Kabudi (Mb.) kwa lengo la kubadilishana mawazo kuhusu sekta ya madini nchini na kuongeza kuwa Tanzania ina utajiri mkubwa wa madini unaotosha kuendesha Nchi  ukiachilia mbali maliasili nyingine zilizopo tatizo ni kuwa madini hayo hayakulinufaisha Taifa.

Mabadiliko ya sheria waliyoyafanya yatasaidia sana,sasa ni jukumu letu sisi Watanzania kuichangamkia fursa hiyo na tusisubiri kulalamika kama ilivyo kawaida yetu,tfanye kazi kwa bidii maana utajiri huu wa madini tuutumie na kujiletea maendeleo binafsi na yanchi kwa ujumla kwa kuwa sasa sheria hizi mpya zimeweka uwanja sawa”

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Profesa Palamagamba Kabudi mbali na kumshukuru Jaji Mstaafu Mark Bomani kumtembelea ofisini kwake ameongeza kuwa mabadiliko yaliyofanyika katika sheria za madini yametokana kwa kiasi kikubwa na ripoti ya tume iliyoundwa kuchunguza sekta ya madini ikiongozwa na Jaji Mstaafu Mark Bomani.

“Haya yoote tuliyoyabaini na kuyaeleza kama upungufu yamo kwenye ripoti ya Bomani ingawa kuna mengine tuliyoyaongeza kama vile mrahaba ulio chini,kutolipa kodi na mengine mengi na kwakuwa Rais wa Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli ameutangaza mwaka 2019 kuwa mwaka wa uwekezaji,Mzee Bomani amekuja ili tubadilishane mawazo tuone namna ya kuuboresha mwaka huu wa uwekezaji”

Ameongeza kuwa wamezungumzia namna ya kuweka mikakati ya kuwavutia wawekezaji wenye tija kuja nchini kuwekeza ili Taifa liweze kunufaika na madini kupitia kodi,ajira kwa vijana na kwamba ujio wa Jaji Mstaafu Mark Bomani ofisini kwake umemjengea ari na nia ya kuonana na viongozi wengine waliolitumikia Taifa kwa tija ili aweze kupata maoni yao ya namna ya kuendesha shughuli za serikali katika wizara aliyopangiwa kazi na Rais Dkt John Pombe Magufuli.


Ujumbe wa Libya wakutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje Prof. Palamagamba Kabudi

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof Palamagamba John Kabudi akiwa katika mazungumzo na Kiongozi wa Ujumbe kutoka Libya Mhe. Jamal El Barak


=======================================

Tanzania na Serikali ya Umoja ya Libya, zimekubaliana kuingia katika mazungumzo ya kina yenye lengo la kupitia miradi yote na uwekezaji,  iliyokuwa ikifanywa na Serikali ya Libya hapa nchini kabla ya machafuko nchini humo na pia kuangalia maeneo mapya ya uwekezaji ambayo Libya imeonesha nia ya kutaka kuwekeza chini ya Kamati ya pamoja baina ya nchi hizo mbili.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Profesa Palamagamba John Kabudi ameyasema hayo jijini Dar es salaam wakati wa mazungumzo na Kiongozi wa Ujumbe kutoka Libya na kuongeza kuwa baada ya hali ya Libya kutengemaa na Amani kuongezeka wamekubaliana kuingia katika uwekezaji.

“Nimemueleza mgeni wangu kuwa mwaka huu wa 2019 Tanzania tumeutangaza kuwa ni mwaka wa uwekezaji na yeye ameonesha nia ya nchi yake na makampuni ya Libya kutaka kuja kuwekeza hapa nchini,tumejadili pia jinsi ya kufufua kamati ya pamoja kati ya Libya na Tanzania kwakuwa mkutano wa mwisho ulifanyika mwaka 2000 baada ya Kamati hiyo kukutana sasa tutajadili miradi mbalimbali ambayo Libya imewekeza,mitaji iliyoiwekeza lakini pia tutaangalia maeneo mapya wanayopendekeza kuwekeza”

Aidha Profesa Palamagamba John Kabudi amefafanua kuwa lengo jipya katika sheria za uwekezaji Tazania ni kuhakikishia Nchi inakuwa na mfumo wa sheria na uwekezaji ambao kila upande unapata tofauti na mfumo wa zamani ambao wawekezaji walikuwa wakinufaika na nchi inanyonywa.

Kwa upande wake Kiongozi wa Ujumbe kutoka Libya Mhe. Jamal El Barak amesema wamekuja dhumuni la ujumbe wao kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli ni kumjulisha kuwa Serikali ya Umoja wa Libya iko tayari kufufua na kuendeleza mahusiano ya kidiplomasia baina ya nchi hizo baada ya hali ya Amani kutengemaa nchini Libya kutokana na mahusiano ya Tanzania na Libya kuwa ya kihistoria.

Mbali na hayo Mhe Jamal El Barak ameongeza kuwa Libya iko tayari kushirikiana na Tanzania katika sekta mbalimbali za uwekezaji kwa kuwa wanatambaua mazingira ya uwekezaji Tanzania ni mazuri hasa baada ya kuhakikishiwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki kuwa mazingira ya uwekezaji yameboreshwa.

Si mara yetu ya kwanza kuwekeza hapa nchini,kabala ya machafuko nchini mwetu tulikuwa tumewekeza katika sekta mbalimbali na sasa tutaangalia maeneo mapya ya uwekezaji”