Friday, September 6, 2019

TANZANIA NA UGANDA ZAKUBALIANA KUIMARISHA BIASHARA ILI KUKUZA UCHUMI


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akitoa hotuba wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Kwanza la Biashara kati ya Tanzania na Uganda uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam tarehe 6 Septemba 2019. Ufunguzi huo ulihudhuriwa pia na Rais wa Uganda, Mhe. Yoweri Kaguta Museveni, Mawaziri, Wafanyabiashara kutoka Tanzania na Uganda na wadau mbalimbali
Rais wa Uganda, Mhe. Yoweri Kaguta Museveni nae akihutubia Kongamano hilo litakalofanyika tarehe 6 na 7 Septemba 2019.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi akizungumza wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Kwanza la Biashara kati ya Tanzania na Uganda
Marais wakiwa meza kuu pamoja na Mawaziri kutoka Tanzania na Uganda akiwemo Waziri wa Elimu wa Uganda ambaye pia ni Mke wa Rais Museveni, Mhe. Mama Janeth Museveni (kushoto)
Mawaziri wa Tanzania wakiwa Ukumbini kabla ya ufunguzi rasmi kuanza 
Wadau mbalimbali wakiwemo Mabalozi walioshiriki ufunguzi wa Kongamano la Biashara kati ya Tanzania na Uganda
Wadau wengine wakiwa ukumbini kabla ya ufunguzi wa kongamano la biashara kuanza
Marais pamoja na Mawaziri wakiwa wamesisimama kwa heshima wakati nyimbo za mataifa yao zikipigwa kabla ya kuanza ufunguzi rasmi wa kongamano la kwanza la biashara kati ya Tanzania na Uganda
Picha inayoonesha washiriki wa kongamano hilo
Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akibadilishana  Hati ya Makubaliano  kuhusu ushirikiano kati ya Tanzania na Uganda kwenye masuala ya Kilimo na Waziri wa Uganda, Mhe. Vincent Mwahiche mara baada ya kusaini. Wanaoshuhudia ni Mhe. Rais Magufuli na Mhe. Rais Museveni pamoja na baadhi ya Mawaziri kutoka Tanzania na Uganda
Mhe. Prof. Kabudi kwa pamoja na waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda, Mhe. Sam Kutesa wakionesha Hati mbalimbali za Makubaliano mbalimbali walizosaini ikiwemo Hati ya Makubaliano ya ushirikiano katika masuala ya Uhamiaji, Magereza na Tume ya Pamoja ya Ushirikiano

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe (katikati) akibadilishana mawazo na Mkurugenzi Mkazi wa Taasisi ya Trademark East Afrika, Bw. John Ulanga (kushoto) na mdau mwingine kabla ya kuanza kwa Kongamano la Biashara kati ya Tanzania na Uganda
Dkt. Mnyepe akiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Uganda, Balozi Patrick Mugoya pamoja na Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bibi Caroline Chipeta wakimsikiliza Mratibu wa Program (MC) ya ufunguzi wa Kongamano la Biashara kati ya Tanzania na Uganda
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ramadhan Muombwa Mwinyi (kushoto) akimsikiliza mdau kutoka sekta binafsi, Bw. Mustapha Hassanal ambaye alishiriki Kongamano la Biashara kati ya Tanzania na Uganda.
=================================================================================

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

TANZANIA NA UGANDA ZAKUBALIANA KUIMARISHA SEKTA YA BIASHARA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli amesema Serikali ya Tanzania na Uganda zimedhamiria kuimarisha sekta ya biashara kwa kushughulikia changamoto zote zilinazoikabili sekta hiyo.

Kauli hiyo imetolewa na Mhe. Rais Magufuli leo tarehe 6 Septemba 2019 wakati wa ufunguzi rasmi wa Kongamano la Kwanza la Biashara kati ya Tanzania na Uganda lililofanyika kwenye Kituo cha Mikutano cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

Mhe. Rais Magufuli amesema kwamba wakati sasa umefika wa kutumia makongamano na mahusiano ya kihistoria, kidiplomasia na kindugu yaliyopo kati ya Tanzania na Uganda ili kusukuma mbele agenda ya maendeleo ya kiuchumi kwa maslahi ya nchi hizo mbili. Aliongeza kwamba nchi hizi mbili zina rasilimali za kutosha kujiletea maendeleo ikiwemo utalii, madini, mifugo, uvuvi, kilimo na gesi na mafuta.

Akionesha kusikitishwa na kiwango kidogo cha ufanyaji biashara kati ya Tanzanai na Uganda, Mhe. Rais Magufuli alieleza kuwa kwa miaka mingi kiwango hicho bado kipo chini sana ukilinganisha na nchi nyingine zinazoshirikiana kibiashara na Tanzania. Alisema hadi sasa ni Kampuni 22 pekee za Uganda zimewekeza nchini huku tani 167,000 pekee za mizigo zikipita Tanzania kwa mwaka 2017/2018 tofauti na tani milioni 7.1 za bidhaa zilizoingizwa nchini humo.


Akielezea sababu zilizoshusha kiwango cha biashara kati ya nchi hizi mbili, Mhe. Rais Magufuli alisema kuwa ni pamoja na urasimu kutoka kwa watendaji wa Serikali hizi mbili, kuwepo kwa vikwazo vya kodi na visivyo vya kodi; miundombinu hafifu ya usafiri na usafirishaji na ufanisi mdogo wa Mamlaka ya Bandari Tanzania.

Hata hivyo, Mhe. Rais Magufuli alifafanua kuwa, Serikali ya Tanzania iliitambua changamoto hiyo mapema na kuanza kuchukua jitihada za makusudi za kukabiliana nayo ili kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara kati ya Tanzania na Uganda. Alisema jitihada hizo ni pamoja na kuboresha miundombinu ya usafiri na usafirshaji kwa kuanza ukarabati wa reli ya kati na ununuzi wa vichwa vya treni; upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam kwa gharama ya takribani Shilingi Trilioni moja na ujenzi wa Reli ya Kiwango cha Kimataifa kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza.

Aidha, Mhe. Dkt. Magufuli aliongeza kuwa, Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Uganda zimefufua vivuko kwa ajili ya kusafirisha mizigo kutokea Bandari ya Mwanza kupitia Bandari ya Portbell nchini Uganda pamoja na kufufua shirika la ndege la Tanzania na Uganda ambapo Ndege za Shirika la Tanzania zilianza safari nchini Uganda mwezi Agosti 2018 huku ndege za Shirika la Uganda zikizindua safari zake nchini mwezi Agosti 2019.

Jitihada zingine ni kudhibitiwa kwa vitendo vya uhalifu kwenye Bandari pamoja na kuimarishwa kwa vituo vya kutoa huduma za pamoja mipakani na kuendelea kubuni mipango mahsusi ya kitaifa yenye lengo la kuboresha biashara na uwekezaji.

“Nawakaribisha sana Uganda tufanye biashara yenye tija kwani kimsingi tumechelewa. Hivyo ni imani yangu kuwa Mkutano huu utakuwa mwanzo wa biashara kubwa kwa watu wetu” alisisitiza Mhe. Rais Magufuli.

Mhe. Rais alitumia fursa hiyo kutoa rai kwa wafanyabiashara na wawekezaji wa pande zote kuheshimu sharia na kanuni zilizowekwa na nchi husika na zile za Jumuiya ya Afrika Mashariki ili kujenga uchumi wa nchi hizi mbili. Vilevile, alitoa wito kwa washiriki wa Kongamano hilo kuchangamkia fursa za kibiashara zilizopo kati ya nchi hizi mbili na kutumia kongamano hilo kuainisha changamoto zote za kibiashara na kutoa mapendekezo ya namna ya kuzitatua.

Akizungumzia Mradi wa Bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani, Tanga ambao unarajiwa kutengeneza zaidi ya ajira 20,000, Mhe. Rais Magufuli alitoa rai kwa Serikali ya Uganda kuongeza kasi ya kukamilisha masuala yaliyosalia ili mradi huo uanze mapema.

Kwa upande wake, Rais wa Uganda, Mhe. Yoweri Kaguta Museveni aliwataka watendaji wa Serikali zote kutambua umuhimu wa sekta ya biashara na mchango wake katika maendeleo ya nchi zao badala ya kuendelea kuweka vikwazo na urasimu.

Aidha, Mhe. Rais Museveni alimshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuupa kipaumbele Mradi wa Bomba la Kusafirisha Mafuta Ghafi kutoka nchini kwake hadi Tanzania na kuahidi kutekeleza yale yote waliyokubaliana ili mradi huo uanze kutekelezwa haraka iwezekanavyo.

Awali akizungumza kwenye Kongamano hilo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi alisema kuwa, Tanzania na Uganda zimefanya mkutano wa tatu wa Tume ya pamoja ya Ushirikiano ambapo masuala ya kuimarisha ushirikiano katika sekta mbalimbali yalijadiliwa. Alisema kuwa, Mkutano huo pamoja na mambo mengine pia  uliteua Maafisa kutoka pande hizo mbili kwa ajili ya kusimamia utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania, Bw. Salum Shamte ambaye alizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara na sekta binafsi nchini alisema kuwa, ana imani kubwa kuwa Kongamano hilo la biashara litakuwa mwanzo mzuri wa kukuza biashara kati ya Tanzania na Uganda, kwani litatoa nafasi kwa wafanyabiashara na wawekezaji wa Uganda na Tanzania kuelewa kwa undani fursa zilizopo kati ya nchi hizi mbili. Pia alisisitiza umuhimu wa kampuni za Uganda kufanya biashara kwa ubia na kampuni za Tanzania na vivyo hivyo kwa kwa Tanzania ili kurahisisha biashara miongoni mwao.

Wakati wa Kongamano hilo ambalo limewashirikisha zaidi ya wafanyabiashara na wawekezaji 1,000 kutoka Tanzania na Uganda, Mhe. Rais Magufuli na Mhe. Rais Museveni walishuhudia kusainiwa kwa Hati za Makubaliano ya ushirikiano katika masuala ya Uhamiaji, Magerereza, Kilimo na Tume ya Pamoja ya Ushirikiano.


Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam.
6 Septemba 2019

WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI, PROF. PALAMAGAMBA JOHN KABUDI AFUNGUA RASMI MKUTANO WA TATU WA TUME YA USHIRIKIANO KATI YA TANZANIA NA UGANDA

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi akitoa hotuba wakati wa ufunguzi rasmi wa Mkutano wa Tatu wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Uganda  uliofanyika  kwa ngazi ya Mawaziri kwenye Ukumbi wa Mikutano katika Jengo la Mamlaka ya Bandari Tanzania jijini Dar es Salaam tarehe 5 Septemba 2019. Wengine katika picha ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda, Mhe. Sam Kutesa (katikati),  Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe (kushoto) na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Uganda, Balozi Patrick Mugoya (kulia).
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda, Mhe. Sam Kutesa nae akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Tatu wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Uganda.
Mhe. Prof. Kabudi akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano wa tume ya pamoja ya ushirikiano
Sehemu ya Mawaziri wakifuatilia hotuba za Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania na Uganda (hawapo pichani)
Sehemu ya Mawaziri kutoka Uganda walioshiriki Mkutano wa Tatu wa Tume ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Uganda
Makatibu Wakuu kutoka Wizara mbalimbali za Tanzania wakiwa kwenye mkutano wa tatu wa tume ya pamoja ya ushirikiano
Makatibu Wakuu kutoka Wizara mbalimbali za Uganda nao wakiwa kwneye mkutano wa tatu wa tume ya ushirikiano
Balozi wa Tanzania nchini Uganda, Mhe. Dkt. Aziz Mlima akiwa pamoja na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Wilbroad Kayombo kwenye Mkutano wa Tume ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Uganda 
Sehemu ya ujumbe wa Uganda ulioshiriki Mkutano wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Uganda


Sehemu ya ujumbe wa Tanzania nao ukiwa kwenye Mkutano wa Tatu wa Tume ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Uganda
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe akizungumza wakati wa mkutano uliofanyika kwa ngazi ya Makatibu Wakuu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Uganda, Balozi Patrick Mugoya nae akizungumza wakati wa mkutano uliofanyika kwa ngazi ya Makatibu Wakuu
Mkutano ukiendelea
Ujumbe wa Uganda

Ujumbe wa Tanzania


Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bibi Caroline Chipeta (kulia) akijadiliana jambo na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Afrika, Bw. Wilbroad Kayombo pamoja na Afisa Mambo ya Nje, Bi. Blandina Kasagama wakati wa Mkutano wa Tatu wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Uganda

Mhe. Prof. Kabudi akiagana na Mhe. Sam Kutesa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda mara baada ya kumalizika kwa mkutano wa tatu wa tume ya pamoja ya ushirikiano kati ya Tanzania na Uganda

Thursday, September 5, 2019

MWAKILISHI MKAZI WA UNDP AKABIDHI NAKALA ZA HATI ZA UTAMBULISHO

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi akisalimiana na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Bi. Christine Musisi katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki alipofika Wizarani kukabidhi nakala ya hati za utambulisho.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi akiwa katika mazungumzo na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Bi. Christine Musisi. Mazungumzo hayo yamefanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki jijini Dar es Salaam wakati Bi. Musisi alipofika Wizarani hapo kukabidhi nakala ya hati za utambulisho kwa Waziri.

Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Bi. Christine Musisi akifurahia jambo wakati wa mazungumzo na Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi(hayupo pichani) wakati alipofika katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki jijini Dar es Salaam,kukabidhi nakala ya hati za utambulisho kwa Waziri.

 Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi akimsikiliza Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Bi. Christine Musisi (hayupo pichani)
Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi akiwa katika mazungumzo na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Bi. Christine Musisi. 

Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi akipokea nakala za hati za utambulisho kutoka kwa mwakilishi mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Bi. Christine Musisi.

Wednesday, September 4, 2019

WAZIRI WA MAMBO YA NJE PROF. PALAMAGAMBA JOHN KABUDI AWAAGA WANAFUNZI WANAOKWENDA ISRAEL KUSHIRIKI MAFUNZO YA KILIMO


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi akizungumza wakati wa hafla fupi ya kuwaaga wanafunzi 44 kati ya 100 waliochaguliwa kwenda nchini Israel kushiriki program ya mafunzo ya kilimo kwa kipindi cha miezi tisa kuanzia mwezi Septemba 2019. Hafla hiyo imefanyika kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam tarehe 4 Septemba 2019. Wengine katika picha kutoka kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati, Bw. Ayoub Mndeme na Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Bw. Emmanuel Buhohela.
Prof. Kabudi akizungumza na wanafunzi hao 
Wanafunzi hao wakimsikiliza Prof. Kabudi (hayupo pichani)
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirkiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe naye akiwaasa wanafunzi hao kuzingatia maadili na kuwa wazalendo wanapokuwa kwenye mafunzo nchini Israel
Dkt. Mnyepe akizungumza
Mhe. Prof. Kabudi akimkabidhi tiketi na hati ya kusafiri, Bi. Janeth Barnaba ambaye ni mmoja wa wanafunzi wanaokwenda kushiriki mafunzo ya kilimo nchini Israel
Mwanafunzi mwingine akipokea tiketi na hati yake ya kusafiria tayari kuelekea nchini Israel tarehe 5 Septemba 2019 kwa ajili ya kuanza program ya mafunzo ya kilimo
Prof. Kabudi akiendelea na zoezi la kuwakabidhi wanafunzi hao tiketi na hati zao za kusafiria kama inavyoonekana pichani
Zoezi la kukabidha tiketi na hati za kusafiria likiandelea
Wanafunzi wakishuhuda mwenzao akikabidhiwa hati yake ya kusafiria na tiketi ya ndege
Prof. Kabudi akikabidhi hati za kusafiria na tiketi za ndege kwa wanafunzi wanaokwenda Israel kushiriki program ya mafunzo ya kilimo kwa vitendo
mwanafunzi akifurahia kukabidhiwa hati ya kusafiria na tiketi ya ndege vitakavyomwezesha kwenda Israel kushiriki mafunzo ya kilimo
Prof. Kabudi akimkabidhi hati ya kusafiria na tiketi ya ndege mwanafunzi atakayeshiriki program ya mafunzo ya kilimo nchini Israel
Wanafunzi wakiwa wameshikilia hati zao za kusafiria na tiketi za ndege zitakazowawezesha kusafiri kwenda Israel kushiriki program ya mafunzo ya kilimo
Mhe. Prof. Kabudi akiwaasa wanafunzi hao mara baada ya kuwakabidhi tiketi zao na hati za kusafiria zitakazowawezesha kwenda Isarel kuanza mafunzo ya kilimo kwa vitendo. Prof. Kabudi aliwataka wanafunzi hao kuwa waadilifu, wasikivu, wachapakazi, wazalendo na warejee nyumbani wakiwa na ujuzi na maarifa kwa manufaa ya Taifa.
===============================================================

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Serikali ya Tanzania inaungana na Serikali ya Afrika Kusini kulaani vikali vitendo vya ubaguzi na mashambulizi vinavyofanywa na raia wachache wa nchi hiyo dhidi ya raia wa nchi zingine za Afrika na kuziasa nchi zingine kutolipa kisasi kutokana na vitendo hivyo.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi wakati wa hafla fupi ya kuwaaga wanafunzi 100 kutoka Tanzania wanaokwenda Israel kushiriki mafunzo ya kilimo iliyofanyika leo tarehe 4 Septemba 2019 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

Mhe. Prof. Kabudi amesema kuwa, vitendo vinavyofanywa na raia wachache wa Afrika Kusini vya kuwashambulia raia kutoka nchi zingine za Afrika na kuharibu mali zao vinasikitisha na kuivunjia heshima nchi hiyo. Hata hivyo, alisema kuwa Serikali ya Tanzania inaunga mkono kauli ya Rais wa Afrika Kusini, Mhe. Cyril Ramaphosa aliyoitoa hivi karibuni ya kukemea na kulaani vikali vitendo vinavyofanywa na raia hao wachache.

Aidha, ameongeza kuwa, vitendo hivyo  ambavyo vinatokana na raia hao wengi kukosa ajira, ardhi na pia kutopenda kujishughulisha havihalalishi watu wengine wakiwemo watanzania kulipa kisasi kwa namna yoyote ile.

“Ni jambo la kusikitisha lakini Serikali ya Afrika Kusini inalisimamia kikamilifu na sisi tupo tayari kushirikiana nao ili kulitafutia ufumbuzi wa kudumu.Nawasihi Watanzania wenzangu tusilipize kisasi na tutaendelea kuwalinda raia wa Afrika Kusini waliopo Tanzania kwani tunaamini kuwa Afrika ni moja na waafrika ni ndugu zetu” alisema Prof. Kabudi.

Kadhalika, Prof. Kabudi alieleza kuwa hadi sasa hakuna taarifa kuhusu Mtanzania kuuawa, kujeruhiwa au kuharibiwa mali kutokana na vurugu hizo. Pia alisema kuwa Wizara itaendelea kutoa taarifa za uhakika kadri zinavyopatikana kutoka kwenye vyanzo vya uhakika ukiwemo Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini.

Wakati huohuo, Mhe. Prof. Kabudi amewaaga wanafunzi 44 kati ya 100 waliochaguliwa kwenda nchini Israel kushiriki mafunzo ya kilimo kwa vitendo kwa kipindi cha miezi tisa kuanzia mwezi Septemba 2019. Wanafunzi hao ambao wengi wamehitimu katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Taasisi ya Kilimo ya Uyole ya Mbeya na Ukiriguru ya Mwanza wanakwenda kushiriki mafunzo hayo ya vitendo kwenye sekta mbalimbali za kilimo ikiwemo uzalishaji na teknolojia. Kati ya Wanafunzi hao, 16 wameondoka nchini tarehe 4 Septemba, 2019, kuelekea Israel, 44 wataondoka nchini tarehe 5 Septemba 2019 na idadi iliyosalia itaondoka tarehe 10 Septemba 2019.

Katika hotuba yake, Mhe. Prof. Kabudi amewataka wanafunzi hao vijana kuzingatia mafunzo hayo ili kuja kutoa mchango wao kwenye mapinduzi ya kilimo ambayo yatachochea mapinduzi ya viwanda nchini. Aidha aliwaasa kuwa waadilifu, kufanyakazi kwa bidii, kushikamana na kujiepusha na vitendo viovu.

“Mnaenda Israel kutafuta ujuzi, uzoefu na ubunifu katika maeneo ya uzalishaji mazao. Hivyo tunaamini kuwa mna nafasi kubwa ya kuja kuibadilisha Tanzania katika eneo la kilimo na mtaleta mapinduzi ya kilimo kwani vijana mpo wengi nchini, mna ari na ni nguvu kazi ya Taifa” alisisitiza Prof. Kabudi.

Akiielezea Israel, Mhe.Prof. Kabudi amesema kuwa nchi hiyo ni nusu jangwa kama ilivyo baadhi ya mikoa hapa nchini. Hata hivyo Israel inaongoza kwa kuuza mazao ya mbogamboga na matunda kwenye nchi za Ulaya kutokana na watu wa nchi hiyo kutumia maarifa katika kugeuza ukame kuwa fursa. Hivyo aliwataka wanafunzi hao kuhakikisha wanapata maarifa na kujifunza mbinu bora na teknolojia za kisasa ili kuja kuendeleza kilimo kikiwemo kile cha umwagiliaji kwenye mikoa kama Singida, Manyara, Shinyanga na Dodoma.

Wanafunzi hao mia moja (100) wamechaguliwa kati ya wanafunzi 1,440 waliotuma maombi ya kwenda kushiriki program ya mafunzo ya kilimo nchini Israel ambayo hufanyika kwa kipindi cha miezi tisa. Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki iliratibu zoezi la upatikanaji wa wanafunzi hao kwa maelekezo ya Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoyatoa mwezi Novemba 2018 alipofanya mazungumzo na Balozi wa Israel nchini, Mhe. Noah Gal Gendler.


Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam.
4 Septemba 2019

Tuesday, September 3, 2019

MKUTANO WA TATU WA TUME YA USHIRIKIANO KATI YA TANZANIA NA UGANDA KUFANYIKA DAR ES SALAAM


Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Wilbroad Kayombo akizungumza wakati wa Mkutano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Uganda uliofanyika kwa ngazi ya wataalam jijini Dar es Salaam tarehe 3 Septemba 2019. Mkutano huo wa wataalam utafuatiwa na mkutano wa Makatibu Wakuu tarehe 4 Septemba 2019 na kuhitimishwa na Mkutano wa Mawaziri tarehe 5 Septemba 2019.  Kutoka kushoto walioketi ni Balozi wa Tanzania nchini Uganda, Mhe. Dkt. Azizi Mlima na Balozi wa Uganda nchini, Mhe. Richard Kabonero
Sehemu ya ujumbe wa Uganda wakiwa kwenye mkutano wa tume ya pamoja ya ushirikiano kati ya Tanzania na Uganda uliofanyika kwa ngazi ya wataalam
Kiongozi wa ujumbe wa Uganda kwenye mkutano wa ngazi ya wataalam akizungumza wakati wa Mkutano huo 
Sehemu ya wataalam kutoka sekta mbalimbali za Tanzania ikiwemo Nishati, miundombinu, elimu, afya, biashara na uwekezaji
Mkutano ukiendelea
=====================================================
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

MKUTANO WA TUME YA PAMOJA YA USHIRIKIANO KATI YA TANZANIA NA UGANDA

Mkutano wa Tatu wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Uganda umeanza leo tarehe 3 Septemba 2019 jijini Dar es Salaam kwa ngazi  ya wataalamu.

Mkutano huo  ambao pamoja na mambo mengine utajadili masuala mbalimbali ya ushirikiano baina ya nchi hizi mbili, utafuatiwa na ngazi ya Makatibu Wakuu tarehe 4 Septemba 2019 na Mawaziri tarehe 5 Septemba 2019.

Lengo la Mkutano wa Tatu wa Tume ya Ushirikiano ni kujadili na kutathmini hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa masuala mbalimbali yaliyokubalika kwenye Mkutano wa Pili uliofanyika jijini Kampala, Uganda mwezi Agosti 2018 pamoja na kutathmini utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa kwenye mkutano wa Mawaziri kuhusu masuala ya Mipaka kati ya Tanzania na Uganda uliofanyika mkoani Kagera mwezi Julai 2017.

Kadhalika, mkutano huu wa Tatu utatoa fursa kwa nchi hizi mbili kujadiliana na kukubaliana kuhusu agenda mbalimbali za ushirikiano. Miongoni mwa maeneo hayo ya ushirikiano ni pamoja na: Siasa na Diplomasia, Ulinzi na Usalama, Maendeleo ya Miundombinu, Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Utalii, Kilimo na Uvuvi, Maji na Mazingira, Afya, Elimu na Mafunzo na Habari na Utamaduni.

Mkutano wa Tatu wa Tume ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Uganda pia utashuhudia Kongamano la Kwanza la Biashara na Uwekezaji kati ya nchi hizi litakalofanyika tarehe 6 Septemba 2019. Kongamano hili litahusisha maonesho ya bidhaa na huduma mbalimbali kutoka Tanzania na Uganda.

Tangu kuanzishwa kwa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Uganda tayari nchi hizi zimefanya vikao viwili vya pamoja. Kikao cha mwisho kilifanyika jijini Kampala, Uganda mwezi Agosti 2018. Vikao vya tume ya pamoja ya ushirikiano huwashirikisha viongozi na wataalam kutoka sekta mbalimbali za nchi hizi mbili.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam.
3 Septemba 2019