Friday, October 18, 2019

KUAPISHWA RASMI KWA MFALME MPYA WA JAPAN

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

KUAPISHWA RASMI KWA MFALME MPYA WA JAPAN   

Dodoma, 19 Oktoba 2019
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt. (Mst) George Mkuchika (Mb.) atahudhuria sherehe za kuapishwa na kutambulishwa kwenye Jumuiya ya Kimataifa kwa Mfalme Naruhito wa Japan zitakazofanyika jijini Tokyo tarehe 22 Oktoba 2019.

Mhe. Mkuchika anamwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ambaye aliakwa katika sherehe hizo na Waziri Mkuu wa Japan, Mhe. Shinzo Abe.

Kwa mujibu wa katiba na sheria za Kifalme za Japan, Mfalme Naruhito amerithi kiti cha Baba yake, Mfalme Akihito ambaye alitangaza kujiuzulu rasmi nafasi yake tarehe 30 Aprili 2019 kutokana na umri wake kuwa mkubwa sanjari na kusumbuliwa na matatizo ya kiafya. Mfalme Naruhito alichukua madaraka hayo tarehe 1 Mei 2019.

Mhe. Mkuchika na ujumbe wake wanatarajia kuondoka nchini tarehe 19 Oktoba 2019 na kurejea tarehe 24 Oktoba 2019.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,

Thursday, October 17, 2019

TANZANIA KUWA MWENYEJI WA MKUTANO WA 18 WA MAWAZIRI WA MAMBO YA NJE WA NCHI ZA AFRIKA NA NORDIC KUANZIA TAREHE 7-8 NOVEMBA 2019




17 Oktoba, 2019

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

TANZANIA KUWA MWENYEJI WA MKUTANO WA 18 WA MAWAZIRI WA MAMBO YA NJE WA NCHI ZA AFRIKA NA NORDIC KUANZIA TAREHE 7-8 NOVEMBA 2019

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi za Afrika na Nordic (Norway, Denmark, Finland, Sweden na Iceland) unaotarajiwa kufanyika tarehe 08 Novemba 2019 kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.Hii ni mara ya kwanza kwa mkutano huu kufanyika hapa nchini tangu kuanzishwa kwake mwaka 2000.
Mkutano huu unatarajiwa kuhudhuriwa na washiriki takribani 250 ambao kati yao thelathini na nne (34) ni Mawaziri wa Mambo ya Nje akiwemo Mhe. Prof. Palamagamba J.A.M. Kabudi (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Kadhalika, Mabalozi wa nchi shiriki za Afrika katika nchi za Nordic, Mabalozi wa nchi za Nordic hapa nchini, watendaji kutoka Wizara za Mambo ya Nje za nchi shiriki, wawakilishi wa taasisi za biashara na uwekezaji na Wafanyabiashara za hapa nchini wanatarajiwa kushiriki katika mkutano huu.
Lengo la kuanzishwa kwa mkutano huu, ambao kwa mara ya kwanza ulifanyika mwaka 2000, ilikuwa ni kutoa nafasi kwa nchi za Nordic na nchi chache za Afrika marafiki zao wa karibu, kujadiliana kuhusu masuala mbalimbali ya ushirikiano kati ya pande hizo mbili, kuainisha vipaumbele katika ushirikiano huo na kuweka mikakati ya pamoja ya kutekeleza vipaumbele hivyo. Nchi za Afrika na Nordic zimekuwa zikipokezana uenyeji wa mikutano hii kila mwaka. Mwaka 2017, mkutano huu ulifanyika Abuja, Nigeria na mwaka 2018 ulifanyika Copenhagen, Denmark na mwaka huu, utafanyika Tanzania.
Kwa mwaka huu, mkutano huu utajadili namna ya kuimarisha mahusiano yenye tija kwa maendeleo ya nchi washiriki hususan namna ya kukuza ushirikiano kwenye sekta ya biashara na uwekezaji kwa maendeleo endelevu. Aidha, ushirikiano kwenye masuala ya ulinzi na usalama unatarajiwa kupewa kipaumbele kwenye mkutano huu ikizingatiwa kuwa utekelezaji wa shughuli za maendeleo unategemea uwepo wa amani na usalama. 
Tanzania ni nchi ya kipaumbele kwa nchi za Nordic. Ushirikiano kati ya Tanzania na nchi za Nordic ulianza hata kabla ya uhuru wa Tanganyika ambapo wamisionari kutoka nchi hizo walikuja kufanya kazi hapa nchini kwenye sekta za afya na elimu. Katika sekta ya elimu, nchi hizo zilianzisha Kituo cha Kilimo cha Uyole na Kituo cha Elimu cha Kibaha kupitia Mradi wa Nordic-Tanganyika Project. Ushirikiano wa karibu kati ya Tanzania na nchi za Nordic ulichangiwa kwa kiwango kikubwa na falsafa zilizokuwa zinafanana kuhusu maendeleo ya watu, ukombozi wa Afrika, urafiki miongoni mwa viongozi wetu na nafasi ya kimkakati ya Tanzania katika Bara la Afrika. 
Hadi sasa, Tanzania ni nchi pekee iliyopokea msaada mkubwa kifedha kutoka katika nchi za Nordic. Kuanzia mwaka 2013 hadi 2019, Tanzania imepokea takribani shilingi za kitanzania bilioni 900 kutoka kwa nchi za Nordic. Nchi hizo zimekuwa zikisaidia sekta mbalimbali hapa nchini ikiwemo: elimu; afya; miundombinu; nishati; TEHAMA; utafiti; ukusanyaji wa kodi; bajeti; misitu; usawa wa jinsia; hali ya hewa; na ukuzaji wa sekta ya biashara. Kufuatia ushirikiano huu wa kihistoria kati ya Tanzania na nchi za Nordic, nchi hizo ziliiomba Serikali ya Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano wa mwaka huu na Serikali kuridhia kwa minajili ya kuendelea kuboresha ushirikiano kati ya pande hizi mbili kwa manufaa ya pande zote.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam.

Job Announcement at the United Nations Environment Programme

PRESS RELEASE

Job Announcement at the
United Nations Environment Programme
  • Dodoma, 17th October 2019. 

The Ministry of Foreign Affairs and East African Cooperation has received vacancy notification from the United Nations Environment Programme (UNEP) inviting qualified Tanzanians to apply for the post of Chief Scientist available at the Science Division.

Application details can be found on the https://www.unenvironment.org/work-with-us

Closing date for application is 24th October 2019.

Issued by;
Government Communication Unit,
Ministry of Foreign Affairs and East African Cooperation,

Wednesday, October 16, 2019

Balozi Kairuki awasilisha Hati za Utambulisho kwa Rais wa Vietnam

Balozi wa Tanzania nchini China ambaye anawakilisha pia Jamhuri ya Watu wa Vietnam, Mhe. Mbelwa Kairuki akiwasilisha Hati za Utambulisho kwa Rais wa Jamhuri ya Watu wa Vietnam, Mhe. Nguyen Phu Trong katika Ikulu ya Vietnam leo jijini Hannoi
Balozi wa Tanzania nchini China ambaye anawakilisha pia Jamhuri ya Watu wa Vietnam, Mhe. Mbelwa Kairuki akiwa katika picha ya pamoja na Rais wa Jamhuri ya Watu wa Vietnam, Mhe. Nguyen Phu Trong katika Ikulu ya Vietnam leo jijini Hannoi.

Tuesday, October 15, 2019

PROF KABUDI KATIKA KONGAMANO LA MIAKA 20 BILA NYERERE - UDSM

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb), akitoa hotuba yake wakati akifungua kongamano la miaka 20 bila Baba wa Taifa, Hayati Mwl. Julias Nyerere katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Katika Kongamano hilo, Waziri Kabudi amemuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.  
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Bashiru Ally (kushoto) Spika wa Bunge Mstaafu, Anne Makinda pamoja na viongozi wengine wa Serikali na wastaafu wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb), katika kongamano la miaka 20 bila Baba wa Taifa, Hayati Mwl. Julias Nyerere katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam


Baadhi ya washiriki wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb), katika kongamano la miaka 20 bila Baba wa Taifa, Hayati Mwl. Julias Nyerere katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam

Monday, October 14, 2019

Wanafunzi Uganda Wafanya Mdahalo kuhusu Mwalimu Nyerere

Balozi wa Tanzania nchini Uganda, Mhe. Dkt. Aziz P. Mlima (katikati), Mwambata Jeshi, Brig. Gen. Stephen Mkumbo na Afisa anayesimamia masuala ya Utawala Ubalozini wakiwa katika hafla ya Kumbukizi ya Miaka 20 ya Siku ya Mwalimu Nyerere iliyofanyika kwenye Ubalozi wa Tanzania nchini Uganda tarehe 13 Oktoba 2019. Hafla hiyo ilifanyika kwa kufanya mdahalo kuhusu maisha ya Mwalimu Nyerere ambapo wanafunzi mbalimbali kutoka Tanzania wanaosoma elimu ya juu nchini Uganda walishiriki mdahalo huo.
Wanafunzi walioshiriki wakifuatilia kwa makini hoja zilizokuwa zinawasilishwa katika mdahalo huo kuhusu maisha ya Mwalimu Nyerere.
Sanjari na Mdahalo huo, uongozi mpya wa wanafunzi wa Tanzania wanaosoma vyuo vikuu nchini Uganda walitumia hafla hiyo kuapishwa rasmi kushika madaraka waliyochaguliwa.
Balozi Mlima akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wa wanafunzi wa Tanzania wanaosoma nchini Uganda.
Uongozi wa wanafunzi wa Tanzania wanaosoma nchini Uganda wakiwa katika picha ya pamoja.




Sunday, October 13, 2019

WIZARA YA MAMBO YA NJE YAKABIDHIWA JENGO JIPYA NA CHINA

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) na Balozi wa China hapa Nchini, Balozi Wang Ke,wakikata utepe kuashiria ufunguzi rasmi wa Jengo jipya  la Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Masharii lililojengwa kwa ufadhili wa Serikali ya Jamhuri ya Watu China na kukabidhiwa Serikaali ya Tanzania. Tukio hilo limefanyika jijini Dar es Salaam. 

Naibu katibu Mkuu, Mizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Ramadhani Mwinyi na Balozi wa China hapa Nchini, Balozi Wang Ke wakisaini mkataba wa makabidhiano ya jengo jipya la Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Anayeshuhudia ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb).

Balozi wa China Nchini, Balozi Wang Ke akishikana mkono na Naibu katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Ramadhani Mwinyi mara baada ya kubadilishana nyaraka walizosaini za kukabidhiana Jengo jipya la Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki lililojengwa kwa msaada wa Jamhuri ya Watu wa China Jijini Dar es Salaam.

Balozi wa China hapa Nchini, Balozi Wang Ke akisoma hotuba yake wakati wa makabidhiano ya jengo jipya  la Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki yaliyofanyika jijini Dar es salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb), akisoma hotuba yake wakati wa makabidhiano ya jengo jipya la Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki yaliyofanyika jijini Dar es salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb), Balozi wa China nchini nchini Tanzania Wang Ke na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje mara baada ya kukabidhiana jengo jipya la wizara hiyo.


Jengo jipya la Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki lililopo jijini Dar Es Salaam  lililojengwa kwa msaada wa Jamhuri ya Watu wa China kwa jailli ya matumizi ya Ofisi za Wizara hiyo.

Mkutano wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wanaoshughulikia masuala ya Afrika Mashariki wamalizika Jijini Arusha.

12 Oktoba 2019, Arusha.
Mkutano wa 30 wa Baraza la kisekta la Mawaziri wanaoshughulikia masuala ya Afrika Mashariki na Mipango umemalizika tarehe 12 Oktoba 2019 kwenye Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jijini Arusha - Tanzania. Mkutano huu wa siku sita (06) umefanyika katika Ngazi zifuatazo:
  1. Mkutano katika Ngazi ya Maafisa Waandamizi tarehe 7 na 8 Oktoba, 2019;
  2. Mkutano katika Ngazi ya Makatibu Wakuu tarehe 9 na 10 Oktoba 2019 na
  3. Mkutano katika Ngazi ya Mawaziri tarehe 11 na 12 Oktoba 2019.
Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huu umeongozwa na Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Damas D. Ndumbaro (Mb) akisaidiana na Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Innocent L. Bashungwa (Mb); Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Balozi Dkt. Augustine P. Mahiga (Mb); Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaju (Mb); Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mary Mwanjelwa pamoja na viongozi wengine waandamizi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano  Tanzania.

Mkutano huu umetoa maamuzi na maelekezo mbalimbali ya kisera na kimkakati kwa Nchi Wanachama pamoja na Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kuhusu Utekelezaji wa maamuzi na maelekezo ya mikutano ya Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki iliyopita pamoja na mkutano wa 10 hadi 28 wa Baraza la kisekta la Mawaziri wanaoshughulikia masuala ya Afrika Mashariki na Mipango; Utekelezaji wa Soko la pamoja la Afrika Mashariki; Utekeleaji wa maagizo katika taarifa ya mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (2000 – 2017); Vipaumbele vya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa mwaka 2020/21; Maelekezo kuhusiana na mikutano ya Wakuu wa taasisi za masuala ya Uhamiaji na Kazi za Jumuiya, na maagizo ya hadidu za rejea za maandalizi ya mkakati wa mpango wa sita wa maendeleo ya Afrika Mashariki (2021/22).

Aidha, mkutano huu ulitoa mapendekezo katika taarifa ya hali ya ulipaji wa michango ya Nchi Wanachama katika Jumuiya; Taarifa ya uhamasishaji katika masuala ya rasilimali za jumuiya ya Afrika Mashariki na mikakati ya ushirikiano; Taarifa ya Tume ya Ukaguzi ya Jumuiya kwa mwaka 2017/18; Taarifa ya maendeleo ya makubaliano ya maeneo huru ya biashara katika utatu wa COMESA-EAC-SADC;Taarifa ya maendeleo ya makubaliano kuhusu eneo huru la kibiashara barani Afrika (AFCFTA); Taarifa ya maendeleo ya masuala ya kisiasa, na Kalenda ya majukumu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kipindi cha mwezi Julai hadi Desemba 2019.

Vilevile, wajumbe wa mkutano wamejadili kuhusiana na maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 20 tangu kuanzishwa kwa jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 2000, baada ya kuvunjika kwa jumuiya ya awali iliyoundwa mwaka 1967 na kuvunjika mwaka 1977.

Mkutano wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wanaoshughulikia masuala ya Afrika Mashariki umemalizika tarehe 12 Oktoba 2019 Jijini Arusha, Tanzania.
Pichani ni viongozi wa ujumbe kutoka Nchi Wanachama katika ngazi ya Mawaziri wakisaini maamuzi na mapendekezo waliyoyatoa katika mkutano wa 30 wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wanaoshughulikia masuala ya Afrika Mashariki na Mipango.
Kutoka kulia ni Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Damas D. Ndumbaro (Mb); Waziri anayeshughulikia masuala ya Jumuiya ya Afrika Mshariki, Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa kutoka Rwanda, Mhe. Balozi Olivier J.P Nduhungiuhe; Katibu Mkuu Wizara ya Afrika Mashariki na Maendeleo ya Kikanda kutoka Kenya, Mhe. Ken M. Obura; Waziri Ofisi ya Rais anayeshughulikia masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kutoka Burundi, Mhe. Isabelle Ndahayo; Waziri wa Masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kutoka Uganda, Mhe. Rt. Dkt. Kirunda Kivejinja; pamoja na Waziri wa Biashara, Viwanda na masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kutoka Sudan Kusini, Mhe. Paul Mayom Akec kutoka.

Mawaziri wa Serikali ya Tanzania walioshiriki katika mkutano wa 30 wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wanaoshughulikia masuala ya Afrika Mashariki na Mipango wakiwa katika kikao cha ndani cha maandalizi pamoja na maafisa wengine waandamizi kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (hawapo pichani).

Pichani; Kutoka kushoto ni Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Damas D. Ndumbaro, Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Innocent L. Bashungwa (Mb); Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Balozi Dkt. Augustine P. Mahiga (Mb); Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mary Mwanjelwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaju (Mb). 

Mkurugenzi wa Idara ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Stephen P. Mbundi akijadili jambo pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya MiundombinuMhandisi Steven D. M. Mlote (kulia) na Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughulikia sekta za uzalishaji na jamii, Mhe. Christophe Bazivamo (kushoto). 

Saturday, October 12, 2019

Watalii kutoka Israel wawasili nchini kwa ziara ya siku nane.

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Utalii Tanzania, Bi. Devotha Mdachi akiwakaribisha watalii kutoka nchini Israel mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro kwa ndege ya shirika la El Al Israel, leo tarehe 12 Oktoba 2019.
Watalii wapatao 920 wameendelea kuwasili nchini katika makundi tofauti ambapo Watalii wanaowasili kupitia uwanja wa Kimataifa wa Kilimanjaro wanatarajiwa kufika 720 na Watalii 200 kwa wale waliokwishawasili kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, Zanzibar. 

Sehemu ya Watalii kutoka nchini Israel wakipata huduma mara baada ya kuwasili ndani ya Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro.
Wakiwa nchini watalii hao watatembelea hifadhi ya Serengeti, Ngorongoro, Tarangire, Manyara pamoja na Zanzibar ili kuweza kujionea vivutio mbalimbali na kujifunza mambo mbalimbali ya mila na utamaduni wa kitanzania.

Sehemu nyingine ya Watalii kutoka nchini Israel wakipata huduma mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro.
Kikundi cha ngoma cha Wamasai kikitumbuiza katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro ikiwa ni ishara ya kuwalaki wageni hao.



Friday, October 11, 2019

Madereva wa taxi kutoka Uingereza wapanda Mlima Kilimanjaro

11 Oktoba 2019, Dodoma

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Madereva wa taxi kutoka Uingereza wapanda Mlima Kilimanjaro

Timu ya madereva taxi watano kutoka Uingereza ilifanya ziara nchini kuanzia tarehe 28 Septemba hadi 10 Oktoba 2019. Ziara hiyo iliratibiwa na Wizara kupitia Ubalozi wetu London kwa kushirikiana na TTB. Timu hiyo ilikuja nchini kwa ajili ya kupanda mlima Kilimanjaro ikiwa ni zoezi la hisani ili kuchangisha fedha kwa ajili ya maveterani wa kijeshi (military veterans) huko Uingereza. 

Katika kutambua uamuzi mzuri wa timu hiyo kuuchagua mlima Kilimanjaro kwa zoezi hilo la hisani na kwa malengo ya kunufaika na ujio wao katika kutangaza vivutio vyetu vya utalii nchini Uingereza, Wizara ya Mambo ya Nje kwa kushirikiana na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) iliwaandalia timu hiyo ziara ya kutembelea vivutio vya utalii mbalimbali hapa nchini zikiwemo mbuga za wanyama za Serengeti, Ngorongoro na Tarangire.

Vilevile, Timu hiyo ya madereva taxi baada ya kumaliza kutembelea vivutio vilivyotajwa hapo juu walitangazwa kuwa mabalozi wa hiari wa utalii (tourism goodwill ambassadors) wa Tanzania kwa lengo la kutangaza vivutio vya utalii vya hapa nchini wawapo katika shughuli zao huko Uingereza. Hafla ya kuwatangaza ilifanyika Hotel ya Mount Meru Arusha. Baada ya kutangazwa kuwa mabalozi wa hiari, walisaini Hati ya Makubaliano (MoU) kati ya timu hiyo na TTB tayari kwa kutekeleza majukumu yao.

Tukio hilo lilihudhuliwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya maliasili na Utalii Dkt. Aloyce Nzuki, akimuwakilisha Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangallah (Mb), Waziri wa Maliasili na Utalii na Mkuu wa mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Gambo. Aidha, Mgeni Rasmi katika shughuli hiyo alikuwa Balozi wa Uingereza hapa nchini, Mhe. Sarah Cooke.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Mrisho Gambo akitoa neno katika hafla ya uwekaji saini wa Hati ya Makubaliano (MoU) kati ya Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) na Timu ya Madereva wa taxi watano kutoka Uingereza. Makubaliano hayo yalihusu timu ya madereva wa Uingereza kuwa Mabalozi wa hiari wa kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania nchini Uingereza.
Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Mhe. Sarah Cooke akizungumza katika hafla hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa TTB, Dkt. Devota Mdachi na Kiongozi wa Madereva wa Taxi wakiweka saini MoU. 

Hati ya Makubaliano baada ya kusainiwa ikioneshwa kwa wajumbe walioshiriki hafla ya uwekaji saini.
Madereva wa Taxi, baadhi yao wakiwa na wenza wao baada ya hafla ya uwekezaji saini MoU
Timu ya Madereva kutoka Uingereza ikipanda mlima Kilimanjaro kwa lengo la kuchangisha fedha kwa ajili ya maveterani wa kijeshi (military veterans) huko Uingereza.
Timu ya Madereva wa Taxi kutoka Uingereza ikiwa katika kilele cha Mlima Kilimanjaro (Uhuru Peak).



Thursday, October 10, 2019

                                         TAARIFA KWA UMMA

UJIO WA WATALII ZAIDI YA 1000 KUTOKA ISRAEL

Tanzania inatarajia kupokea watalii zaidi ya 1000 kutoka nchini Israel ambao wanakuja nchini kwa ajili ya kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii mwezi huu wa Oktoba.

Kundi la kwanza lililokuwa na zaidi ya watalii 200 liliwasili nchini kuanzia tarehe 05 Oktoba na kundi la pili lenye zaidi ya watalii 520 linatarajiwa kuwasili nchini tarehe 12 na kundi la tatu lenye watalii zaidi ya 200 litawasili nchini tarehe 13 Oktoba kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA). Watalii wengine zaidi wanatarajiwa kuwasili nchini mwezi huu baada ya Makampuni ya Uwakala wa Utalii kukamilisha taratibu za safari zao.

Watalii hao wanatarajiwa kutembelea Visiwa vya Zanzibar, Hifadhi za Taifa za Serengeti, Tarangire na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro. Ujio wa watalii hao unatokana na jitihada za kuitangaza nchi zinazofanywa na Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kupitia Ubalozi wa Tanzania nchini Israel kwa kushirikiana na wadau wa utalii  wa ndani na nje ya nchi.

Tanzania imejipanga kuwapokea na kuwatembeza watalii hao katika vivutio vya utalii vilivyoko nchini. Serikali inawakaribisha watalii hao kutembelea vivutio hivyo vya utalii ambavyo nchi imebarikiwa kuwa navyo ili wakawe mabalozi wazuri wa kuitangaza Tanzania nchini kwao na kwingine watakakokwenda.

Imetolewa na:

Dkt. Faraji K. Mnyepe
Katibu Mkuu
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
DODOMA

PROF. KABUDI AHUDHURIA MAADHIMISHO YA SIKU YA HISPANIA HAPA NCHINI

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akihutubia wakati wa maadhimisho ya siku ya Uhispania yaliyofanyika Jijini Dar Es Salaam kwenye Makazi ya Balozi wa Uhispania hapa Nchini. Kulia kwa Prof. Palamagamba John Kabudi ni Balozi wa Hispania hapa Nchini Mhe. Fransisca Maria Pedro's Carretero.

Balozi wa Hispania hapa Nchini Mhe. Fransisca Maria Pedro's Carretero akihutubia wakati wa maadhimisho ya siku ya Uhispania yaliyofanyika Jijini Dar Es Salaam kwenye Makazi ya Balozi huyo hapa Nchini.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akigongeana glasi ishara ya kutakiana kheri na Balozi wa Hispania hapa Nchini Mhe. Fransisca Maria Pedro's Carretero,wakati wa maadhimisho ya siku ya Uhispania yaliyofanyika Jijini Dar Es Salaam kwenye Makazi ya Balozi wa Uhispania hapa Nchini.

Baadhi ya waalikwa walihohudhuria maadhimisho ya siku ya Uhispania yaliyofanyika Jijini Dar Es Salaam kwenye Makazi ya Balozi wa Uhispania hapa Nchini.

Mkutano wa 30 wa Baraza la Mawaziri la kisekta linaloshughulikia masuala ya Afrika Mashariki na Mipango waendelea jijini Arusha katika ngazi ya Makatibu Wakuu

Mkutano wa 30 wa Baraza la Mawaziri la kisekta linaloshughulikia masuala ya Afrika Mashariki na Mipango waendelea jijini Arusha katika ngazi ya Makatibu Wakuu. Mkutano katika ngazi hiyo ulikuwa wa siku mbili na umemalizika leo.
Pamoja na mambo mengine, mkutano umejadili masuala mbalimbali ya utekelezaji ya jumuiya ya Afrika Mashariki na kutoa mapendekezo katika mkutano wa ngazi ya Mawaziri utakaofanyika tarehe 11 na 12 Oktoba 2019.
Pichani; wa pili kutoka kushoto ni Mwenyekiti wa mkutano ngazi ya Makatibu Wakuu kutoka Rwanda, Balozi Richard Masozera akiongoza mkutano huo, wa pili kutoka kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Miundombinu, Mhandisi Steven D. M. Mlote, kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughulikia sekta za uzalishaji na jamii, Mhe. Christophe Bazivamo na kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi katika Wizara inayoshughulikia masuala ya jumuiya ya Afrika Mashariki kutoka Kenya, Bw. Rafael Kanoth.

Kiongozi wa ujumbe wa Tanzania katika mkutano wa ngazi ya Makatibu Wakuu ambaye pia ni Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Laurean Ndumbaro (kushoto) akisaini taarifa ya mapendekezo mbalimbali katika mkutano huo kwaajili ya kuwasilisha taarifa hiyo katika mkutano wa ngazi ya Mawaziri. Pembeni yake ni Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, Prof. Sifuni Mchome akishuhudia zoezi la utiaji saini.

Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Amina Shaaban pamoja na Dkt. Ndumbaro na Prof. Mchome wakifuatilia majadiliano katika mkutano huo.

Kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Siasa, Ulinzi na Usalama, Balozi Stephen P. Mbundi pamoja na wajumbe wengine wa mkutano wakifuatilia majadiliano katika mkutano huo.

Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt. Evaristo Longopa (kushoto) pamoja na sehemu nyingine ya ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo wakifuatilia majadiliano.


Sehemu nyingine ya wajumbe wa Tanzania wakifuatilia majadiliano katika mkutano.

Viongozi wa ujumbe wa mkutano katika ngazi ya Makatibu Wakuu kutoka nchi wanachama wakikamilisha zoezi la utiaji saini wa taarifa ya mapendekezo ya mkutano huo.

Wednesday, October 9, 2019

UBALOZI WA TANZANIA NCHINI INDIA WAANZA MAJUKUMU YA UENYEKITI WA KUNDI LA MABALOZI KUTOKA NCHI ZA SADC WALIOPO NCHINI HUMO

Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Baraka Luvanda akipokea Makabrasha kutoka kwa Balozi wa Namibia nchini India, Mhe. Gabriel P. Sinimbo ikiwa ni ishara ya kukabidhiwa uenyekiti wa Kundi la Mabalozi wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC ) waliopo India. Tanzania ilipokea uenyekiti wa Jumuiya hiyo kutoka kwa Namibia mwezi Agosti 2019 wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Balozi Luvanda (katikati) akizungumza mara baada ya kupokea uenyekiti wa kundi la Mabalozi kutoka Nchi za SADC waliopo India. Katika picha ni Balozi Sinimbo (kulia) kutoka Namibia na Balozi E.A Ferreira (kushoto) kutoka Msumbiji.
Mkutano ukiendelea
Mhe. Balozi Luvanda akiwa katika picha ya pamoja na na Mabalozi kutoka nchi za SADC waliopo India pamoja na Maafisa wa Ubalozi mara baada ya kikao cha Mabalozi hao kilichofanyika kwenye Jengo la Ubalozi jijini New Delhi.
Mhe. Balozi Luvanda akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Zambia nchini India, Mhe. Judith K. Kapijimpanga ambaye kabla ya kuiwakilisha Zambia nchini India alihudumu katika nafasi hiyo nchini Tanzania.
Maafisa wa Ubalozi wa Tanzania, New Delhi, Dkt. Kheri Goloka (kushoto) na Bi. Natihaika Msuya (katikati) wakiwa katika picha ya pamoja na Mwenyekiti wa kundi la Mabalozi wa nchi za SADC nchini India aliyemaliza muda wake Balozi wa Namibia  Mhe. Gabriel P. Sinimbo.