Tuesday, February 16, 2021

BALOZI BRIGEDIA JENERALI IBUGE; USHAWISHI WA TANZANIA BADO NI IMARA KIKANDA NA KIMATAIFA

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Brigedia Jenerali Wilbert A. Ibuge amaeleza kuwa nguvu ya ushawishi wa Tanzania katika majukwaa ya kikanda na kimataifa bado upo imara, licha ya Tanzania kutoa mchango mkubwa katika ukombozi wa Bara la Afrika na uanzishwaji wa Jumuiya za Kikanda kama vile Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) hadi hivi sasa Tanzania bado ni kinara katika kutetea na kuadai maslahi ya Bara la Afrika.

Balozi Brigedia Jenerali Ibuge, amebainisha haya alipokuwa akizungumza na wadau kutoka Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC) ambao waliitemebelea Makao Makuu ya Wizara jijini Dodoma kwa lengo la kujifunza kuhusu majukumu ya Wizara, hasa katika kutetea maslahi ya Nchi nje ya mipaka ya Tanzania. Katibu Mkuu aliendelea kubainisha kuwa Wizara katika utekelezaji wa sera ya mambo ya nje pamoja na mambo mengine inahakikisha kuwa inatoa kipaumbele kwenye kulinda maslahi ya Nchi ikiwewo ulinzi na usalama.


NDC kwa upande wao wameipongeza Wizara kwa kazi nzuri inayofanywa na Ofisi zake za Ubalozi sehemu mbalimbali duniani katika kutangaza fursa zilizopo nchini kwenye maeneo yao ya uwakilishi madhalani utalii, biashara ya madini na mazao ya kilimo, pia kuvutia wawekezaji kuja kuwekeza nchini.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Brigedia Jenerali Wilbert A. Ibuge (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wadau na uongozi wa NDC na Watendaji wa Wizara.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Brigedia Jenerali Wilbert A. Ibuge akisisitiza jambo wakati alipokuwa akizungumza na wadau kutoka Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC) walipofanya ziara ya mafunzo Wizarani.

 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Brigedia Jenerali Wilbert A. Ibuge akipokea kalenda kutoka kwa Mkuu wa Chuo cha NDC Brigedia Jenerali Ibrahim Michael Muhona baada ya kumaliza kutoa mhadhara
Sehemu ya Wadau kutoka NDC wakifuatilia mhadhara uliokuwa ukitolewa na viongozi wa Wizara
Mkurugenzi wa Siasa,Ulinzi na Usalama Balozi Stephen P. Mbundi akifafanua jambo kwa wadau kutoka NDC wakati walipofanya ziara ya mafunzo Wizarani

TANZANIA MBIONI KUSAINI MKATABA WA ENEO HURU LA BIASHARA YA UTATU COMESA-EAC-SADC


Tanzania imeshiriki katika Mkutano wa Pili wa Dharura wa Baraza la Mawaziri la Utatu uliofanyika kwa njia ya video. Katika mkutano huo moja ya agenda ilikuwa nchi Wanachama kutoa taarifa kuhusu hatua iliyofikiwa katika kusaini na kuridhia mkataba wa kuanzishwa kwa Eneo Huru la Biashara ya Utatu ya COMESA-EAC-SADC. Katika mkutano huo Tanzania kupitia Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Dkt. Leonard Chamuriho imeeleza kuwa ipo katika hatua za kusaini na kuridhia mkataba huo. 

Mkutano huo ulioitishwa kwa dharura pia ulilenga kupitia na kujadili rasimu ya mwongozo wa utatu wa usimamizi na ufuatiliaji wa uvukaji salama wa watu na bidhaa mipakani katika kipindi hiki cha Ugonjwa wa Virusi vya Korona (UVIKO-19). Jumuiya za COMESA, EAC na SADC baada ya kugundua kuwa nchi mbalimbali ziliaandaa miongozo ya kudhibiti maambukizi ya UVIKO-19 bila kuathiri uchumi na biashara iliamua kuratibu maandalizi ya miongozo ya kikanda ili kuondokana na changamoto za biashara baina ya nchi wanachama. Nchi wanachama zimekubaliana kuwa mkutano uitishwe tena baada ya wiki mbili ili kujadili agaenda hii na kufikia maamuzi ya pamoja.

Katika mkutano huo kwa upande wa Tanzania ulihudhuriwa na Waziri wa Afya Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. William Ole Nasha, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe.Geofrey Pinda Watendaji na Maafisa mbalimbali wa Serikali


Kutoka kulia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. William Ole Nasha, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Dkt. Leonard Chamuriho, Waziri wa Afya Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe.Geofrey Pinda wakifuatilia Mkutano wa Pili wa Dharura wa Baraza la Mawaziri la Utatu uliokuwa ukiendelea kwa njia ya video


Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Brigedia Jenerali Wilbert A. Ibuge akifuatilia Mkutano wa Pili wa Dharura wa Baraza la Mawaziri la Utatu uliokuwa ukiendelea kwa njia ya video
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Dkt. Leonard Chamuriho akichangia jambo katika Mkutano wa Pili wa Dharura wa Baraza la Mawaziri la Utatu uliofanyika kwa njia ya video

Badhi ya Watumishi wa Serikali waliohudhuria Mkutano wa Pili wa Dharura wa Baraza la Mawaziri la Utatu uliokuwa ukiendelea kwa njia ya video wakifualia mjadala uliokuwa ukiendelea
Kutoka kulia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. William Ole Nasha, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Dkt. Leonard Chamuriho, Waziri wa Afya Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe.Geofrey Pinda wakifuatilia Mkutano wa Pili wa Dharura wa Baraza la Mawaziri la Utatu uliokuwa ukiendelea kwa njia ya video

Mkutano ukiendelea

 

Saturday, February 13, 2021

BALOZI IBUGE: SIJARIDHISHWA NA MAENDELEO YA UJENZI WA MAJENGO CHUO CHA DIPLOMASI

 Na Mwandishi wetu,

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge ameonesha kutoridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa majengo ya mihadhara katika chuo cha Diplomasia na kumuagiza Mkandarasi anayetekeleza mradi huo kuzingatia thamani ya fedha, muda wa mkataba na ubora.

Balozi Ibuge ametoa maagizo kwa Mkandarasi huyo ambaye ni Kampuni ya Casco Construction pamoja na mshauri muelekezi Ask architects wakati alipotembelea mradi huo katika chuo cha Diplomasia leo jijini Dar es Salaam kusema kuwa endapo Mkandarasi hata fanya hivyo atakuwa amekiuka masharti ya mkataba na mkataba wake utasitishwa mara moja.

“Huu mradi ni mradi wenye maslahi ya Taifa majadiliano yaishe leo mkataba ulishaisha tangu mwezi Disemba 2020, hizi ni hela za walipa kodi…..nataka nione thamani halisi ya fedha [Value for Money] ya walipa kodi katika mradi huu, siatakubali kupoteza fedha za walipa kodi,” Amesema Balozi Ibuge

Katibu Mkuu ameuagizo pia uongozi wa chuo hicho kuhakikisha kuwa unasimamia ujenzi wa majengo hayo kwa karibu zaidi na umakini ili kuiwezesha serikali kupata thamani halisi ya fedha katika mradi huo wenye maslahi mapana ya Taifa.

Awalia akiongea na wahadhiri pamoja na wafanyakazi katika chuo hicho Balozi Ibuge amewataka wote kwa pamoja kuhakikisha kuwa wanatekeleza diplomasia ya uchumi kutokana na mabadiliko ya dunia.

“Najua mmeanzisha mitaala inayogusia masuala ya diplomasia ya uchumi hadi mmeanza kuanzia baadhi ya matawi katika baadhi ya mikoa hili ni jambo jema, lakini uwezo wa nyinyi kuleta [link] ya utekelezaji wa diplomasia ya uchumi ambao ndiyo Wizara yetu inasimamia…unapohusisha na nchi nyingine ni lazima utafiti wenu pamoja na kuboresha wigo wa utekelezaji wa diplomasia ya uchumi,”

Balozi Ibuge ameongeza kuwa diplomasia ya uchumia inaambatana na siasa pamoja na diplomasia ya utamaduni wetu hasa kwenye lugha ya kiswahili hiyo ndiyo sehemu ya mahusiano yetu na wengine.

“Urathi wa ukombozi kusini mwa Afrika anayehusika ni Tanzania sasa Chuo cha Diplomasia ambapo ndipo mawazo mazuri ya namna bora ya sisi kuhakikisha tunaiendeleza na kuishindania na kuhakikisha hakuna mwingine wa kushindana na sisi, njia pekee ni kupitia kwenu nyinyi na tafiti zenu,” Amesema Balozi Ibuge

Kwa upande wake Mkandarasi anayetekeleza mradi huo Mhandisi Cosmas Salufu kutoka kamupuni ya ujenzi ya Casco, pamoja na mshauri elekezi mhandisi Ally Simbano kutoka kampuni Ask Architects kwa pamoja wameahidi kutekeleza maagizo ya Katibu Mkuu na kuhakikisha kuwa thanami halisi ya fedha inapatikana katika mradi huo.

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge (aliyesimama) akiongea na wahadhiri pamoja na wafanyakazi wa chuo cha Diplomasia leo Jijini Dar es Salaam wakati alipofanya ziara chuoni hapo 


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akiongea na uongozi wa chuo cha Diplomasia leo Jijini Dar es Salaam  


Afisa Miliki wa Chuo cha Diplomasia, Mhandisi Athumani Mashaka akimueleza jambo Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge wakati akitembelea mradi wa ujenzi wa majengo chuoni hapo


Mhandisi Cosmas Salufu pamoja na Mshauri Elekezi Mhandisi Ally  wakimsikiliza Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge wakati wa ziara ya ukaguzi wa majengo




Friday, February 12, 2021

MKUTANO WA SADC TROIKA WASOGEZA MBELE MKUTANO WA WAKUU WA NCHI

 Na Mwandishi wetu,

Mkutano wa Wakuu wa nchi na Serikali za Utatu wa Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC- TROIKA) uliopangwa kufanyika mwezi Machi 2021 umesogezwa mbele hadi mwezi Mei au Juni 2021 kutokana na changamoto za (Covid 19).

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. William Ole Nasha (Mb) amesema kuwa mkutano huo umekutana kwa lengo la kupitia na kuridhia mapendekezo ya Mawaziri wa afya wa SADC uliofanyika mwishoni wa mwezi Februari 2021.  

“Awali mawaziri wa Afya wa SADC walipendekeza kuwa mkutano wa Baraza la Mawaziri ufanyike kwa njia ya mtandao pamoja na ule wa Wakuu wa Nchi uliokuwa umepangwa pia kufanyika mwezi Machi usogezwe mbele hadi mwezi Mei au Juni 2021 kutegemeana na hali ya maambukizi ya ugonjwa wa COVID 19 itakavyokuwa na kuongeza kuwa mikutano mingine yote itafanyika kwa njia ya mtandao (Video Conference) hadi hapo hali ya maambukizi itakapokuwa imetengemaa,” Amesema Mhe. Ole Nasha

Mkutano wa (SADC TROIKA) umetanguliwa na Mkutano wa Makatibu Wakuu ambapo, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge ameeleza kutokana na hali halisi ya kujitokeza kwa kirusi cha Covid 19 kilichojitokeza kusini mwa Jangwa la Afrika imekuwa vigumu kufanyika kwa mkutano huo wa ana kwa ana na badala yake imeamuliwa mkutano huo usogezwe mbele hadi mwezi Mei au Juni 2021.

“Mwezi Januari 2021 Mawaziri wa Afya wa SADC walikutana na kufanya mkutano kwa njia ya mtandao na kufikia maazimio kuwa mkutano wa Wakuu wa nchi na Serikali uhairishwe hadi mwezi Mei au Juni kutegemeana na hali ya COVID 19 itakapokuwa imetengemaa……. ambapo pamoja na mambo mengine, mkutano wa Baraza la Mawaziri umeridhia kusogezwa mbele kwa mkutano huo,” Amesema Balozi Ibuge

Utatu wa SADC TROIKA kwa sasa unaundwa na nchi za Msumbiji, Tanzania na Malawi.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. William Ole Nasha (Mb) akiwa amesimama wakati wimbo wa Taifa wa Msumbiji ulipokuwa ukipigwa wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Utatu wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC TROIKA) uliofanyika kwa njia ya mtandao  


Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. William Ole Nasha (Mb) akiandika jambo wakati wa mkutano cha SADC TROIKA) uliofanyika kwa njia ya mtandao


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akichangia mada katika mkutano wa Makatibu Wakuu wa SADC TROIKA 


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akifuatilia mkutano wa Makatibu Wakuu wa SADC TROIKA 



Thursday, February 11, 2021

BIASHARA KATI YA TANZANIA, SAUDI ARABIA YAZIDI KUIMARIKA

 Na Mwandishi wetu,

Urari wa kibiashara kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Saudia Arabia umezidi kukuwa ambapo mpaka sasa miradi 14 ya uwekezaji kutoka nchini humo imesajiliwa katika kituo cha taifa cha uwekezaji (TIC)huku kampuni nane za Kitanzania zikipata kibali cha kuuza minofu ya samaki nchini humo.

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge ameyasema hayo katika mazungumzo yake na  Balozi wa Saudi Arabia hapa nchini, Mhe. Mohamed Bin Mansour Al Maliki anayemaliza muda wake wa uwakilishi hapa nchini.

“Kwa hakika kipindi hiki mahusiano ya Saudi Arabia na Tanzania yameimarika vizuri kwa manufaa ya pande zote mbili, ambapo katika sekta ya uwekezaji kumekuwa na miradi 14 iliyoandikishwa katika Kituo cha Taifa cha Uwekezaji (TIC) ambapo uwiano wa biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Saudi Arabia unazidi kuongezeka na kuimarika,” Amesema Balozi Ibuge

Balozi Ibuge ameongeza kuwa zipo fursa nyingi za uwekezaji ambazo kupitia juhudi za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki pamoja na wadau wa sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya kilimo, kampuni kubwa kampuni kubwa ya Serikali ya Saudi Arabia ipo katika hatua za mwisho za kuja kuwekeza katika sekta za mifugo na kilimo hapa nchini.

Balozi Ibuge ameeleza kuwa kwa upande wa Tanzania “kampuni nane zimepata kibali cha kuuza minofu ya samaki katika soko la Saudi Arabia ikiwa ni moja kati ya juhudi ambazo zimekuwa zikifanywa na Balozi Al Maliki kwa kushirikiana na Serikali katika kuimarisha mahusiano ya nchi zote mbili,”.

Kwa upande wake Balozi, anayemaliza muda wake wa uwakilishi hapa nchini Mhe. Al Maliki ambaye amekuwa hapa nchini kwa kipindi cha miaka minne amesema anajisikia fahari na bahati kupata fursa ya kuiwakilisha nchi yake hapa Tanzania na kwamba katika kipindi chake chote  amepata ushirikiano mkubwa.

“Kwa kweli wakati wote wa uwakilishi wangu, nimekuwa nikipata ushirikiano wa kutosha wakati wa kutekeleza majukumu yangu jambo hili limenifurahisha sana……........na nitakuwa balozi mwema kwa Tanzania,” Amesema Balozi Al Maliki

Balozi Al Maliki amewasihi watanzania kuendelea na utamaduni wao unaowafanya kuheshimika duniani kote hususani katika suala la umoja, amani na mshikamano bila ya kujali itikadi za kisiasa na dini.

Tanzania na Saudi Arabia zimekuwa na ushirikiano wa muda mrefu katika sekta ya kilimo, elimu, afya, biashara na uwekezaji, maji, utalii, kwa lengo la kuhakikisha utekelezaji wa diplomasia ya uchumi unafikiwa kwa wakati.

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akiongea na Balozi wa Saudi Arabia hapa nchini, Mhe. Mohamed Bin Mansour Al Maliki wakati balozi huyo alipokuwa anamuaga katika ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam


Balozi wa Saudi Arabia hapa nchini, Mhe. Mohamed Bin Mansour Al Maliki akimueleza jambo Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge katika ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akimkabidhi zawadi ya picha ya Mlima Kilimanjaro Balozi wa Saudi Arabia hapa nchini, Mhe. Mohamed Bin Mansour Al Maliki katika ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam


Balozi wa Saudi Arabia hapa nchini, Mhe. Mohamed Bin Mansour Al Maliki akimkabidhi zawadi Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge katika ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam




 









Wednesday, February 10, 2021

MHE. OLE NASHA ASHIRIKI MKUTANO WA BUNGE LA NNE LA AFRIKA MASHARIKI

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. William Tate Ole Nasha (Mb) ashiriki katika Mkutano wa Pili, Kikao cha Nne, Bunge la Nne la Afrika Mashariki uliofanyika kwa njia ya mtandao. 

Kikao hicho kimefunguliwa na Spika wa Bunge hilo Mhe. Martin Ngoga na baadaye kuendelea kuliongoza Bunge katika utekelezaji wa majukumu yake ya siku. Shughuli ziliyofanywa na Bunge hilo na kufuatiliwa na Mhe. Ole Nasha ilikuwa ni kusomwa kwa mara ya kwanza Muswada wa Afrika Mashariki kuhusu Mifugo wa mwaka 2021, uwasilishwaji wa taarifa ya Kamati ya Kilimo, Utalii na Maliasili ambayo inaangazia tathmini ya utekelezaji wa shughuli za Kamisheni ya Bonde la Ziwa Viktoria na uwasilishwaji wa Hoja ya Azimio la Bunge la kulishawishi Baraza la Mawaziri la Afrika Mashariki kuhusu uharakishwaji wa kuanzisha mfuko wa dharura wa kukabiliana na magonjwa ya mlipuko katika Jumuiya. 

Bunge la Afrika Mashariki linaendelea na vikao vyake kwa njia ya mtandao ambavyo vitafanyika kwa kipindi cha wiki tatu kuanzia tarehe  28 Januari hadi 17 Februari 2021. 

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. William Tate Ole Nasha akifuatilia Kikao cha Bunge la Afrika Mashariki kilichokuwa kikiendelea kwa njia ya video 

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. William Tate Ole Nasha akifuatilia Kikao cha Bunge la Afrika Mashariki kilichokuwa kikiendelea kwa njia ya video

TANZANIA YACHAGULIWA KUNUFAIKA NA MRADI WA ZAIDI YA SHILINGI BILIONI 8 WA INTRA – ACP

 


Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji ambaye pia anaiwakilisha Tanzania katika Umoja wa Ulaya Mhe. Jestas Nyamanga akifafanua kuhusu upatikanaji wa soko la migebuka na dagaa wa Kigoma katika soko la Umoja wa Ulaya jijini Dar es Salaam


BALOZI IBUGE AWATAKA MABALOZI KUKUZA DIPLOMASIA YA UCHUMI

 Na Mwandishi wetu,

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge amewataka mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali duniani kuongeza jitihada za kuhakikisha Diplomasia ya Uchumi inaleta tija iliyokusudiwa.

Balozi Ibuge ametoa kauli hiyo wakati alipokutana na kufanya mazungumzo kwa nyakati tofauti na Balozi wa Tanzania nchini Zimbambwe, Mhe. Prof. Emmanuel Mbennah pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Marekani Mhe. Wilson Masilingi katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.

Balozi Ibuge katika mazungumzo yake na Balozi wa Tanzania nchini Zimbambwe Prof. Mbennah amemtaka kuhakikisha kuwa anafanya kazi kwa weledi katika kuimarisha uhusiano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Zimbabwe pamoja na kukuza diplomasia ya uchumi kwa kuzingatia maelekezo ya Serikali. 

“Balozi nakusihi kuendelea kufanya kazi kwa bidii na weledi ili kufanikisha azma na malengo ya Serikali katika kuhakikisha tunaimarisha uhusiano wetu wa kidiplomasia na Zimbabwe lakini pia kukuza diplomasia ya Uchumi kati yetu na Zimbabwe,” Amesema Balozi Ibuge.

Kwa upande wake, Balozi Prof. Mbennah amemhakikishia Katibu Mkuu kuwa uhusiano wa Jamhuri ya Muungano na Tanzania na Zimbabwe ni mzuri na imara.

Katika tukio jingine, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Tanzania nchini Marekani Mhe. Wilson Masilingi ambapo pamoja na mambo mengine wamejadili umuhimu wa kuhakikisha kuwa Tanzania inanufaika ipasavyo na uhusiano mzuri wa kidiplomasia ilionao na Marekani. 

Katika kuhakikisha hilo, Balozi Ibuge alimsisitiza Balozi Masilingi kuendelea kufanya kazi kwa bidii katika kutekeleza Diplomasia ya Uchumi kwa manufaa ya Taifa.  

Nae balozi Masilingi amemhakikishia Katibu Mkuu kuwa Ubalozi wa Tanzania nchini Marekani unaendelea kutekeleza diplomasia ya uchumi kwa kasi inayotakiwa.

Balozi wa Tanzania nchini Zimbambwe Mhe. Prof. Emmanuel Mbennah akimuelezea jambo Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge wakati wa mazungumzo yaliyofanyika katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akiongea na Balozi wa Tanzania nchini Zimbambwe Mhe. Prof. Emmanuel Mbennah 


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge katika picha ya pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Zimbambwe Mhe. Prof. Emmanuel Mbennah 


Balozi wa Tanzania nchini Marekani Mhe. Wilson Masilingi akimuelezea jambo Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge wakati wa mazungumzo yaliyofanyika katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam 


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akimsikiliza Balozi wa Tanzania nchini Marekani Mhe. Wilson Masilingi mazungumzo yaliyofanyika katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam. Kulia ni Msaidizi wa Katibu Mkuu Bi. Eva Ng’itu 


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akiongea na Balozi wa Tanzania nchini Marekani Mhe. Wilson Masilingi


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge katika picha ya pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Marekani Mhe. Wilson Masilingi