Monday, June 7, 2021

BARAZA LA KISEKTA LA MAWAZIRI WANAOSHUGHULIKIA MIPANGO KATIKA EAC KUKUTANA ARUSHA

Mkutano wa 31 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta linaloshughulikia masuala ya Afrika Mashariki na Mipango katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (SCMEACP) unafanyika jijini Arusha kuanzia tarehe 7 hadi 11 Juni 2021.


Mkutano huo ambao umeanza kwa Ngazi ya Wataalam leo tarehe 7 hadi 9 Juni 2021 utafuatiwa na Mkutano wa Makatibu Wakuu utakaofanyika tarehe 10 Juni 2021 na kuhitimishwa na Mkutano wa Mawaziri utakaofanyika tarehe 11 Juni 2021.


Akifungua Mkutano wa Ngazi ya Wataalam, Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughilikia Sekta za Uzalishaji na Jamii, Mhe. Christophe Bazivamo amezipongeza Nchi Wanachama kwa kufufua viwanda vidogo na kutumia bidhaa za ndani hususan katika kipindi hiki cha janga la ugonjwa wa Corona ambalo limeathiri kwa kiasi kikubwa shughuli za uzalishaji na ufanyaji biashara katika nchi nyingi duniani zikiwemo zile za EAC.


Ameongeza kusema kuwa, ugonjwa wa Corona umetoa funzo kubwa kwa Nchi Wanachama wa EAC kwamba zinaweza kufanya biashara miongoni mwao na kujitosheleza kwa mahitaji mbalimbali ya msingi kwa maendeleo ya wananchi wa nchi hizo ikiwa ni utekelezaji wa Itifaki mojawapo muhimu ya Jumuiya ya Soko la Pamoja.


Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mkutano huo wa Ngazi ya Wataalam, Bi. Alice Yalla kutoka Jamhuri ya Kenya amesisitiza wajumbe kujadili kwa umakini agenda mbalimbali zilizopo mbele yao na kutoa mapendekezo yenye tija, ikizingatiwa kuwa Sekta ya Mipango ni moja ya Sekta muhimu katika Jumuiya ambayo pamoja na mambo mengine pia hushughulika na tathmini ya mipango na masuala yote yanayotekelezwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki.


Mkutano wa Wataalam pia utapitia agenda mbalimbali muhimu ambazo zitawasilishwa kwenye Mkutano ngazi ya Makatibu Wakuu utakaofanyika tarehe 9 na 10 Juni 2021 kwa majadiliano na hatimaye agenda hizo zitawasilishwa kwenye Mkutano ngazi ya  Mawaziri unaotarajiwa kufanyika jijini hapa tarehe 11 Juni 2021.


Miongoni mwa agenda hizo ni pamoja na Taarifa ya Utekelezaji wa maazimio yaliyofikiwa kwenye vikao vilivyopita; Taarifa kuhusu hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa Itifaki ya Soko la Pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki; Kupitia maelekezo ya Baraza la Mawaziri kuhusu  Rasimu ya Maboresho ya Utaratibu wa Mafao katika Jumuiya ya Afrika Mashariki; Taarifa kuhusu ombi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo la kujiunga na EAC; Taarifa kuhusu hatua iliyofikiwa ya utatu wa Jumuiya za EAC-COMESA-SADC katika Eneo Huru la Biashara Barani Afrika; Taarifa ya Uchangiaji wa Bajeti ya EAC kutoka Nchi Wanachama; na Taarifa ya majadiliano kuhusu Eneo Huru la Biashara Barani Afrika.


Ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa Ngazi ya Wataalam unaongozwa na Mkurugenzi wa Idara ya Siasa, Ulinzi na Usalama katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Stephen Mbundi. Kadhalika Mkutano huo umehudhuriwa na Wajumbe kutoka nchi zote wanachama ambazo ni Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda na Sudan Kusini.

Mkurugenzi wa Idara ya Siasa, Ulinzi na Usalama katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Stephen Mbundi akiongoza ujumbe wa Tanzania kwenye mkutano wa majadiliano kwa ngazi ya wataalam uliofanyika jijini Arusha tarehe 7 Juni 2021 kwa ajili ya kuandaa Mkutano wa 31 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta linaloshughulikia masuala ya Afrika Masahriki na Mipango katika Jumuiya ya Afrika Mashariki unaotarajiwa kufanyika Arusha tarehe 11 Juni 2021. Mkutano kwa ngazi ya wataalam unafanyika kuanzia tarehe 7 hadi 9 Juni 2021 na utafuatiwa na Mkutano wa Makatibu Wakuu tarehe 10 Juni 2021. Kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Biashara, Uwekezaji  na Sekta za Uzalishaji katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Benard Haule.
Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughulikia Sekta ya Uzalishaji na Jamii, Mhe. Christophe Bazivamo akifungua rasmi Mkutano wa Ngazi ya Wataalam uliofanyika jijini Arusha kwa ajili ya kuandaa Mkutano wa 31 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta linaloshughulikia masuala ya Afrika Masahriki na Mipango katika Jumuiya ya Afrika Mashariki unaotarajiwa kufanyika  tarehe 11 Juni 2021

Mkurugenzi katika Wizara ya Afrika Mashariki na Maendeleo ya Kikanda ya Kenya na Mwenyekiti wa Mkutano wa Ngazi ya Wataalam,  Bi. Alice Yalla akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano huo uliofanyika jijini Arusha ikiwa ni maandalizi ya Mkutano wa 31 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta linaloshughulikia masuala ya Afrika Masahriki na Mipango katika Jumuiya ya Afrika Mashariki unaotarajiwa kufanyika tarehe 11 Juni 2021.

Ujumbe wa Kenya ukiwa kwenye mkutano wa ngazi ya wataalam

Sehemu ya ujumbe wa Tanzania ukishiriki Mkutano wa ngazi ya wataalam
Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bibi Agnela Nyoni akifuatilia ufunguzi wa mkutano wa wataalam uliofanyika Arusha kwa ajili ya kuandaa Mkutano wa 31 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta linaloshughulikia masuala ya Afrika Masahriki na Mipango katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) unaotarajiwa kufanyika tarehe 11 Juni 2021.
Ujumbe wa Uganda ukiwa kwenye mkutano wa ngazi ya wataalam
Balozi Mteule na Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki  Bibi Caroline Chipeta akifuatilia mkutano wa ngazi ya wataalam uliofanyika Arusha ikiwa ni maandalizi ya Mkutano wa 31 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta linaloshughulikia masuala ya Afrika Masahriki na Mipango katika Jumuiya ya Afrika Mashariki unaotarajiwa kufanyika tarehe 11 Juni 2021.
Ujumbe kutoka Taasisi mbalimbali za Jumuiya ya Afrika Mashariki nao ukishiriki mkutano wa ngazi ya wataalam
Mkutano ukiendelea
Mjumbe kutoka Rwanda akiwa kwenye mkutano wa wataalam
Mjumbe wa Burundi naye akifuatilia mkutano
Sehemu ya ujumbe wa Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ukishiriki mkutano wa wataalam
Mkutano ukiendelea
Mjumbe kutoka Tanzania akishiriki mkutano wa ngazi ya wataalam
Mkutano ukiendelea


BALOZI MULAMULA AKUTANA NA KUFANYA MAZUNGUMZO NA MKURUGENZI MTENDAJI WA BENKI YA DUNIA KANDA YA AFRIKA

 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia Kanda ya Afrika kundi la kwanza Dkt. Taufila Nyamadzabo ofisini kwake jijini Dodoma. Dkt alifika Ofisini kwa Mhe. Waziri kujitambulisha na kujadiliana namna ya kuimarisha mahusiano kati ya Tanzania na Benki hiyo.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia Kanda ya Afrika kundi la kwanza Dkt. Taufila Nyamadzabo ofisini alipomtembelea kwake jijini Dodoma.

 Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia Kanda ya Afrika kundi la kwanza Dkt. Taufila Nyamadzabo ofisini kwake jijini Dodoma.

Mazungumzo kati ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia Kanda ya Afrika kundi la kwanza Dkt. Taufila Nyamadzabo aliyemtembelea ofisini kwake jijini Dodoma yakiendelea.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia Kanda ya Afrika kundi la kwanza Dkt. Taufila Nyamadzabo ofisini kwake jijini Dodoma.

Waziri Mulamula amesema mazungumzo yake na Dkt. Taufila ambaye pia alikuwa anajitambulisha yamelenga kujadili masuala mbalimbali ya ushirikiano kati ya Benki ya Dunia na Tanzania ili kuimarisha mahusiano hayo na hivyo kunufaika na miradi ya maendeleo.

Akiongelea uhusiano baina ya Tanzania na Benki ya Dunia Mhe. Balozi Mulamula amesema Tanzania imejipanga kuhakikisha mahusiano kati ya Tanzania na Benki hiyo yanaimarika na kuendeleza uwezo wa Watanzania wanaosimamia miradi ya maendeleo inayofadhiliwa na Benki ya Dunia ikiwa ni pamoja na kuendeleza sekta binafsi na kuifanya kuwa imara.

“leo hapa tumejadiliana juu ya mahusiano yetu, kuangalia namna ya kuyaboresha ili kunufaika na miradi  ya maendeleo inayofadhiliwa na Benki hiyo, kuwajengea uwezo watu wetu wanaosimamia utekelezaji wa miradi hiyo na uimarishaji wa Sekta binafsi ili kuwa imara na hivyo kufikia maendeleo ya kweli,” alisema Balozi Mulamula

Akiongelea kuhusu mipango ya Serikali ya kuimarisha Sekta Binafsi Mhe Waziri Mulamula amemuhakikishia Dkt. Taufilo nia na mtizamo wa Serikali wa kuweka mazingira mazuri ya kufanya biashara na kuwekeza nchini ikiwa ni pamoja na kushirikiana na sekta binafsi hasa ikizingatiwa kuwa Benki ya Dunia inachukulia sekta binafsi kama chachu ya maendeleo na hivyo kuwa na miradi ya kusaidia ukuzaji wa Sekta binafsi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji huyowa Benki ya Dunia Kanda ya Afrika kundi la kwanza Dkt. Taufila Nyamadzabo amesema miongoi mwa mambo waliyojadili leo ni pamoja na umuhimu wa kuhusisha sekta binafsi na kuiendeleza.

Amesema miongoni mwa vipaumbele vya Benki ya Dunia kwa sasa ni kuimarisha Sekta binafsi na kuifanya kuwa imara hasa katika maeneo ya biashara na uwekezaji pamoja na kuimarisha miundombinu ya usafirishaji, na ukuzaji wa teknolojia ya habari na mawasiliano ili kuiwezesha duniani kuendelea kufanya shughuli zake hasa katika kipindi hiki cha changamoto ya ugonjwa wa Covid 19.

Amesema wamekubaliana kuendelea kushirikiana na kuimarisha mahusiano kati ya Tanzania na Benki hiyo na hivyo kuiwezesha Tanzania kunufaika na miradi ya maendeleo inayosimamiwa na benki hiyo.

 


Saturday, June 5, 2021

TUME YA PAMOJA TANZANIA NA MSUMBIJI ZAJADILI MASUALA YA ULINZI, USALAMA NA AMANI

Tume ya pamoja ya Ulinzi na Usalama ya Tanzania na Msumbiji imekutana kujadili  masuala ya ulinzi na usalama kati ya Mataifa hayo.

Akiufungua Mkutano huo wa tatu wa Tume ya pamoja ya ulinzi na usalama kati ya Tanzania na Msumbiji Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula, amesema mkutano huo ni wa muhimu kwakuwa unatoa fursa ya kuangalia namna ya kukabiliana na matukio yanayotishia ulinzi na usalama yamejitokeza kusini mwa Tanzania na kaskazini mwa Msumbiji ili kwa pamoja kupata suluhisho la kudumu.

“Mkutano wa leo pia utatoa fursa ya kuangalia masuala ya Ulinzi na Usalama, masuala ya mtambuka ambayo ni pamoja na umaskini na utawala bora katika nchi zetu mbili, kikao hiki ni muhimu sana kwani kitarudisha imani kwa wananchi na kuonesha kuwa hatujalala hadi hali itengamae kule Msumbiji,” Amesema Balozi Mulamula

Balozi Mulamula ameongeza kuwa, anaamini kupitia majadiliano yaliyoanza kuanzia tarehe 3 Juni kwa ngazi ya Wataalamu / Makatibu Wakuu hadi leo terehe 5 Juni mkutano wa ngazi ya Mawaziri utapitia mapendekezo ya vikao vya awali kuweza kuchukua maamuzi katika maeneo masuala ya ulinzi, usalama na usalama wa jamiii.

Ujumbe wa Msumbiji umeongozwa na Waziri wa Ulinzi wa Msumbiji Mhe Jaime Augusto Neto na kuainisha masuala jumuishi kuhusu ulinzi na usalama na kwamba ni Imani yake kuwa kikao hicho kitatoka na maazimio ya utekelezaji ili kuwa na mtangamano imara.

Katika tukio jingine Umoja wa Ulaya umesema unaunga mkono hatua za muendelezo na mabadiliko ya sera za kijamii na maendeleo yanayofanywa Nchini,chini ya uongozi wa Rais  wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan na kwamba unapongeza hatua hizo.

Akizungumza kwa niaba ya mabalozi wa Jumuiya ya Ulaya hapa Nchini katika kikao kazi walichokiandaa Jijini Dar es Salaam,Balozi wa Umoja huo Mhe Manfredo Fanti ameongeza kuwa matamko ya Rais Samia kuhusu ushirikiano kati ya Tanzania na Jumuiya za Kimataifa,sekta binafsi,uhuru wa kujieleza,haki za binadamu na utawala bora yanatia moyo.

“Matamko na maelekezo ya Mhe. Rais Samia kuhusu ushirikiano kati ya Tanzania na Jumuiya za Kimataifa,sekta binafsi,uhuru wa kujieleza,haki za binadamu na utawala bora yanatia moyo na kutuhamasisha kuwashawishi wawekezaji na wafanyabiashara kuja kuwekeza Tanzania,” Amesema Balozi Fanti. 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula amesema mkutano huo ulikuwa ni wa muhimu kwa kuwa unaweka misingi ya kuaminiana na kuimarisha mahusiano kati ya Tanzania na Umoja huo ili kuweka mazingira bora ya Mabalozi hao kuhamasisha wawekezaji na wafanyabiashara kutoka katika Mataifa yao kuja kuwekeza hapa nchini.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) akipitia moja ya nyaraka kabla ya kuanza kwa mkutano wa tatu wa Tume ya Pamoja ya Ulinzi na Usalama kati ya Tanzania na Msumbiji uliofanyika Dar es Salaam. Kulia ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Elias Kwandikwa 


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) akiteta jambo na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Elias Kwandikwa kabla ya kuanza kwa mkutano wa tatu wa Tume ya Pamoja ya Ulinzi na Usalama kati ya Tanzania na Msumbiji uliofanyika Dar es Salaam


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akifungua mkutano wa tatu wa Tume ya Pamoja ya Ulinzi na Usalama kati ya Tanzania na Msumbiji uliofanyika jijini Dar es Salaam  


Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Elias Kwandikwa akiwasilisha mada katika mkutano wa tatu wa Tume ya Pamoja ya Ulinzi na Usalama kati ya Tanzania na Msumbiji uliofanyika Dar es Salaam  


Waziri wa Ulinzi wa Msumbiji, Mhe. Jaime Augusto Neto akiwasilisha mada katika mkutano wa tatu wa Tume ya Pamoja ya Ulinzi na Usalama kati ya Tanzania na Msumbiji  


Wajumbe wa mkutano wa tatu wa Tume ya Pamoja ya Ulinzi na Usalama kati ya Tanzania na Msumbiji wakifuatilia mkutano


Wajumbe wakiwa katika picha ya pamoja  


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) akiwa katika kikao kazi na mabalozi wa Umoja wa Ulaya wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini. Kikao hicho kimefanyika Dar es Salaam ambapo Umoja wa Ulaya umeeleza kuridhishwa na hatua zinazochukuliwa na Serikali ya Tanzania katika kuimarisha mahusiano na Jumuiya za Kimataifa.


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) akiwa katika kikao kazi na mabalozi wa Umoja wa Ulaya wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini. Kikao hicho kimefanyika Dar es Salaam ambapo Umoja wa Ulaya umeeleza kuridhishwa na hatua zinazochukuliwa na Serikali ya Tanzania katika kuimarisha mahusiano na Jumuiya za Kimataifa.



Friday, June 4, 2021

BALOZI MULAMULA ATEMBELEA VYOMBO VYA HABARI VYA IPP

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) ametembelea vyombo vya habari vya Kampuni ya IPP Ltd na kuvipongeza kwa kufanya kazi vizuri.

Balozi Mulamula ametembelea ‘The Guardian Ltd’ inayozalisha magazeti ya The Guardian na Nipashe, Radio One, Capital radio, East Africa radio, ITV, Capital TV pamoja na East Africa TV.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) akisalimiana na Mkurugenzi Mtendaji wa ITV na Radio One, Joyce Mhavile wakati alipowasili kwa ajili ya kutembelea vyombo vya habari vya IPP


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) akipokelewa na uongozi wa The Guardian Ltd wakati alipokuwa natembelea kampuni hiyo leo Jijini Dar es Salaam


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akisalimiana na Mhariri Mkuu wa Gazeti la Nipashe, bb. Beatrice Bandawe 


Mhariri Mkuu wa Gazeti la Nipashe, Bb. Beatrice Banda akimfafanulia jambo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula wakati Balozi Mulamula alipotembelea Ofisi za The Guardin Ltd 


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akielea jambo wakati alipokuwa katika studio za East Africa radio jijini Dar es Salaam


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akielea jambo wakati alipokuwa katika studio za East Africa radio jijini Dar es Salaam


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akitambulishwa baadhi ya vipindi vya Capital radio  


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akielezewa jinsi habari na vipindi mbalimbali vinavyotayarishwa katika studio za ITV. Mkurugenzi Mtendaji wa ITV na Radio One, Joyce Mhavile


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiwa studio za ITV 




Thursday, June 3, 2021

BALOZI MBAROUK AKUTANA NA KUFANYA MAZUNGUMZO NA MWAKILISHI WA KAMPUNI YA SHELL

Mheshimiwa Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb), Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki leo tarehe 3 Juni 2021 amekutana na kufanya mazungumzo na Bw. Ahmed Salim anayeratibu Mahusiano kati ya Kampuni ya Shell na Serikali. Bw. Salim ameeleza ameeleza lengo la ziara yake Wizarani ni kuelezea dhamira ya Kampuni ya Shell ya kuwekeza katika Sekta ya Gesi (LNG) Nchini. 

Balozi Mbarouk licha ya kupongeza uamuzi wa Kampuni ya Shell ya kuwekeza nchini amemweleza Bw. Salim kuwa Wizara na Serikali ipo tayari kutoa ushirikiano kwa kampuni hiyo katika shughuli zao uwekezaji. Pia amweleza kuhusu dhamira ya Serikali ya kuendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na ufanyaji biashara nchini. 

Bw. Salim ameeleza kuwa Kampuni ya Shell inatarajia kufanya uwekezaji wenye thamini ya fedha za kitanzania zaidi shilingi bilioni 30.
Mheshimiwa Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb), Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akimkaribisha Bw. Ahmed Salim anayeratibu Mahusiano kati ya Kampuni ya Shell na Serikali alipowasili Wizarani jijini Dodoma.
Mheshimiwa Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb), Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akimweleza jambo Bw. Ahmed Salim anayeratibu Mahusiano kati ya Kampuni ya Shell wakati wa mazungumzo yaliyofanyika katika jijini Dodoma

Mheshimiwa Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb), Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akimsikiliza Bw. Ahmed Salim anayeratibu Mahusiano kati ya Kampuni ya Shell na Serikali alipowasili Wizarani jijini Dodoma
Mazungumzo yakiendelea

BALOZI MULAMULA AKUTANA NA KUFANYA MAZUNGUMZO NA BALOZI WA CHINA NCHINI NA NAIBU KATIBU MKUU WA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI

Mheshimiwa Balazo Liberata Rutageruka Mulamula (Mb) Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki leo tarehe 3 Juni 2021 kwa nyakati tofauti amekutana na kufanya mazungumzo na Mhe. WANG Ke Balozi wa China nchini Tanzania na Mhandisi Steven Mlote, Naibu Katibu Mkuu wa Sekretariet ya Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Mipango, Miundombinu, Fedha na Utawala. 

Balozi WANG amemtembelea Balozi Mulamula kwa lengo la kumuaga baada ya kumaliza muda wake wa utumishi hapa nchini. Balozi WANG ameeleza furaha na kuridhishwa kwake na namna Wizara na Serikali kwa ujumla ilivyompa ushirikiano kwa kipindi chote alichokuwa nchini akitekeleza majukumu yake. Aidha, ameonyesha furaha yake juu ya namna mahusiano kati ya Tanzania na China yanavyoendelea kushamiri na hivyo kuchagiza maendeleo kwa Nchi zote mbili. 

Balozi Mulamula kwa upande wake amempongeza na kumshukuru Balozi WANG kwa utumishi na mchango wake alioutoa katika kudumisha na kukuza mahusiano kati ya Tanzania na China. Sambamba na pongezi hizo Balozi Mulamula amemtakia kheri Balozi WANG katika maisha yake na utumishi. Vilevile Balozi Mulamula amemwakikishia Balozi WANG kuwa Tanzania itaendelea kudumisha na kukuza mahusiano mazuri yaliyopo kati ya Tanzania na China yaliyodumu kwa nyakati zote. 

Katika hatua nyingine Mheshimiwa Balozi Mulamula na Mheshimiwa Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb), Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa pamoja wamekutana na kufanya mazungumzo na Mhandisi Steven Mlote, Naibu Katibu Mkuu Sekretariet ya Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Mipango, Miundombinu, Fedha na Utawala. Mhandisi Mlote amefika Wizarani kwa lengo la kujitambulisha kwa Waziri Mulamula na Naibu Waziri Mbarouk na kuwapongeza kwa kuteuliwa kushika nyadhifa hizo. 

Balozi Mulamula na Balozi Mbarouk wamemweleza Mhandisi Mlote kuwa Wizara na Serikali kwa ujumla itaendelea kutoa ushirikiano kwa Sekretariet ya Jumuiya ya Afrika Mashariki katika shughuli zao za kuiletea maendeleo Jumuiya. Aidha, wameipongeza Sekretariet kwa kazi nzuri ya kutekeleza miradi ya kimkakati kama vile ujenzi barabara, miradi ya umeme na maji ambayo inaleta mchango mkubwa katika kukuza uchumi kwa Nchi wanachama. 
Mheshimiwa Balazo Liberata Rutageruka Mulamula (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo na Mhandisi Steven Mlote, Naibu Katibu Mkuu Sekretariet ya Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Mipango, Miundombinu, Fedha na Utawala yaliyofanyika katika Ofisi za Wizara jijini Dodoma
Mheshimiwa Balazo Liberata Rutageruka Mulamula (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akimsikiliza Mhandisi Steven Mlote, Naibu Katibu Mkuu Sekretariet ya Jumuiya ya Afrika Mashariki

Mazungumzo yakiendelea


Mheshimiwa Balazo Liberata Rutageruka Mulamula (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb), Naibu Waziri (kulia) na Mhandisi Steven Mlote,Naibu Katibu Mkuu Sekretariet ya Jumuiya ya Afrika Mashariki wakiwa katika picha pamoja baada ya mazungumzo yaliyofanyika katika Ofisi za Wizara jijini Dodoma.

Wednesday, June 2, 2021

BALOZI SOKOINE AKUTANA NA KUFANYA MAZUNGUMZO NA BALOZI WA RWANDA NCHINI

Balozi Joseph Edward Sokoine, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki leo tarehe 2 Juni, 2021 amekutana na kufanya mazungumzo na Mhe. Meja Generali Charles Karamba, Balozi wa Rwanda nchini Tanzania. 

Balozi Karamba amefika Ofisini kwa Katibu Mkuu kwa lengo la kujitambulisha kwake, na kumpongeza kwa kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Balozi Sokoine kwa upande wake amemwahidi Balozi Karamba ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yake ili kuimarisha zaidi uhusiano kati ya Tanzania na Rwanda. 

Aidha, Balozi Karamba ameeleza kuridhishwa kwake na namna Bandari ya Dar-es- Salaam inavyoshughulikia kwa haraka upitishaji wa bidhaa na mizigo ya Rwanda inayopitia katika Bandari hiyo, jambo ambalo linachochea ukuaji wa biashara kati ya Tanzania na Rwanda.

Mheshimiwa Meja Generali Charles Karamba Balozi wa Rwanda nchini Tanzania akisaini kitabu cha wageni alipowasili katika Ofisi za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki jijini Dodoma.

Mazungumzo yakiendelea.

Balozi Joseph Edward Sokoine Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akiwa katika picha ya pamoja na Mheshimiwa Meja Generali Charles Karamba Balozi wa Rwanda nchini Tanzania.
Balozi Joseph Edward Sokoine Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akielezea jambo wakati wa mazungumzo na Mheshimiwa Meja Generali Charles Karamba Balozi wa Rwanda nchini Tanzania.
Mheshimiwa Meja Generali Charles Karamba Balozi wa Rwanda nchini Tanzania akielezea jambo wakati wa mazungumzo na Balozi Joseph Edward Sokoine Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Wakati huohuo Waheshimiwa Mabalozi Wastaafu waliowahi kuiwakilisha Nchi sehemu mbalimbali duniani wamekutana na kufanya mazungumzo Watendaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa lengo la kubadilishana uzoefu katika musuala Diplomasia na Mahusiano ya Kimataifa.  
Mheshimiwa Balozi Begum Taji akifuatilia mazungumzo yaliyokuwa yakiendelea.
Mheshimiwa Balozi Christopher C. Liundi akizungumza wakati wa kikao kati ya Mabalozi Wastaafu na Watendaji wa Wizara.
Sehemu ya Watendaji wa Wizara wakifuatilia kikao
Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi Rasilimali Watu Bw. Alex B.D.J Mfungo akielezea jambo wakati wa kikao kati ya Mabalozi Wastaafu na Watendaji wa Wizara


 

Tuesday, June 1, 2021

BALOZI MULAMULA AWASILISHA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI BUNGENI JIJINI DODOMA

Mheshimiwa Balozi Liberata Rutageruka Mulamula (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki leo amewasilisha bungeni makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2021/2022 katika Mkutano wa Bajeti unaoendelea jijini Dodoma. 

Akiwasilisha bungeni hotuba hiyo Balozi Mulamula ameeleza kuwa ili Wizara iweze kutekeleza kikamilifu majukumu yake kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022, analiomba Bunge Tukufu liidhinishe jumla ya shilingi 192,265,438,000. Kati ya fedha hizo shilingi 178,765,438,000 ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na shilingi 13,500,000,000 ni kwa ajili ya Bajeti ya Maendeleo.

Aidha Balozi Mulamula ameyataja majukumu ambayo Wizara imeyapa kipaumbele kuyatekeleza katika Mwaka wa Fedha 2021/2022, kama ifuatavyo;

  • Kuendelea kutekeleza diplomasia ya uchumi ikiwa ni pamoja na kuwezesha balozi zetu kuwa kiungo muhimu cha kukuza uwekezaji, upatikanaji wa masoko ya bidhaa na huduma zinazozalishwa nchini na kuvutia watalii; 
  • Kuendelea kuboresha na kuimarisha uhusiano na nchi nyingine, jumuiya za kikanda na mashirika ya kimataifa;
  • Kuendelea kuweka mazingira wezeshi, kuratibu na kuhamasisha ushiriki wa Watanzania wanaoishi nje ili kushiriki kikamilifu katika kuchangia maendeleo ya nchi;
  • Kuendelea kulinda na kutetea misingi ya Taifa letu ndani na nje ya nchi;
  • Kuendelea kushawishi na kuhamasisha matumizi ya lugha ya Kiswahili kwa nchi moja moja, jumuiya za kikanda na kimataifa;
  • Kuendelea kushiriki katika juhudi za kulinda na kuimarisha amani duniani na maendeleo kupitia Umoja wa Mataifa;
  • Kuendelea kujenga na kukarabati majengo kwa ajili ya balozi zetu ili kupunguza gharama na kuleta mapato kwa Serikali;
  • Kuendelea kufungua ofisi za Balozi na Konseli Kuu mpya katika nchi za kimkakati;
  • Kuendelea kushiriki kikamilifu katika kuimarisha utangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC);
  • Kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Wizara, masuala ya uhusiano wa kimataifa na utangamano wa kikanda; 
  • Kuendelea kusimamia utekelezaji wa majukumu ya Taasisi zilizopo chini ya Wizara; na
  • Kuendelea kusimamia rasilimali watu na fedha Makao Makuu ya Wizara na Balozini.
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limeidhinisha bajeti ya Wizara, jumla ya shilingi 192,265,438,000 kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022. 
Mheshimiwa Balozi Liberata Rutageruka Mulamula (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akiwasilisha Bungeni Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara kwa mwaka wa Fedha 2021/2022.

Mheshimiwa Balozi Liberata Rutageruka Mulamula (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk  (Mb) Naibu Waziri (wa kwanza kushoto mstari wa mbele) na Balozi Joseph Edward Sokoine, Katibu Mkuu (Watatu kutoka kushoto mstari wa mbele) wakiwa katika picha ya pamoja na Watendaji wa Wizara baada ya uwasilishwaji wa Hotuba ya Bajeti. 

Mheshimiwa Balozi Liberata Rutageruka Mulamula (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akiwasilisha Bungeni Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara kwa mwaka wa Fedha 2021/2022.

Sehemu ya Watendaji wa Wizara na Wageni Waalikwa wakiwa tayari kufuatilia uwasilishwaji wa Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa mwaka wa Fedha 2021/2022.
Mheshimiwa Balozi Liberata Rutageruka Mulamula (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akiwa katika picha ya pamoja Wageni waliofika bungeni jijini Dodoma kufuatilia uwasilishwaji wa Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa mwaka wa Fedha 2021/2022.
Mheshimiwa Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb) Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akijibu maswali Bungeni baada ya uwasilishwaji wa Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara kwa mwaka wa Fedha 2021/2022

Balozi Joseph Edward Sokoine, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akitambulishwa Bungeni, kabla ya uwasilishwaji wa Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022.

Mheshimiwa Balozi Liberata Rutageruka Mulamula (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Mheshimiwa Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk Naibu Waziri wakifuatilia mjadala uliokuwa ukiendelea Bungeni