Thursday, September 23, 2021

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE MHE. BALOZI MBAROUK ATEMBELEA MAKAO MAKUU YA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI JIJINI ARUSHA

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk ameipongeza Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuendelea kuratibu na kuendesha shughuli mbalimbali za mtangamano kwa manufaa ya Nchi Wanachama wa Jumuiya hiyo.

 

Mhe. Balozi Mbarouk ametoa pongezi hizo leo tarehe 23 Septemba 2021 jijini Arusha wakati wa mazungumzo yaliyofanyika kati yake na Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, Mhandisi Steven Mlote ikiwa ni ziara yake ya kwanza aliyoifanya kwenye Makao Makuu ya Jumuiya hiyo kwa lengo la kujitambulisha tangu kuteuliwa kwake kwenye wadhifa huo.

 

Wakati wa mazungumzo hayo, Mhe. Balozi Mbarouk alimweleza Mhandisi Mlote kwamba, amefarijika kutembelea Ofisi hizo na kujionea shughuli mbalimbali za uendeshaji zinazofanyika na kusisitiza kuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki itaendelea kuwa Jumuiya muhimu kwa nchi zote sita wanachama kwa kuwa ni kiunganishi kikubwa katika kuziletea maendeleo endelevu ya kiuchumi, kisiasa na kijamii nchi hizo.

 

Aidha alisisitiza kuwa, Tanzania itaendelea kutekeleza majukumu mbalimbali kama yalivyoainishwa kwenye Mkataba ulioanzisha Jumuiya hiyo ikiwa ni pamoja na kutoa michango yake ya mwaka ajili ya kuwezesha uendeshaji wa Jumuiya hiyo.

 

Kwa upande wake, Mhandisi Mlote ambaye alimwakilisha Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, alimshukuru Mhe. Mbarouk kwa kutenga muda na kutembelea Ofisi hizo na alitumia fursa hiyo kumweleza mfumo mzima wa uendeshaji wa Jumuiya kupitia Sekretarieti.

 

Mbali na kufanya mazungumzo na Naibu Katibu Mkuu, Mhe. Naibu Waziri pia alipata fursa ya kuzungumza na Spika wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA), Mhe. Ngoga Karoli Martin pamoja na Rais wa Mahakama ya Afrika Mashariki, Jaji Nestor Kayobera ambapo kwenye mazungumzo yao viongozi hao walijadili masuala mbalimbali yanayohusu mchango wa Bunge na Mahakama hiyo kwenye Mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

 

Kadhalika, wakati wa ziara hiyo, Mhe. Balozi Mbarouk alimtembelea Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. John Mongella ambapo viongozi hao walijadili masuala mbalimbali ya ushirikiano kati ya Mkoa huo na Wizara hususan yale yanayohusu kuimarisha diplomasia ya uchumi kupitia sekta ya utalii ambayo imeshamiri kwenye mkoa huo.

 

Wakati huohuo, Mhe. Mbarouk amekitembelea Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC) ambacho ni moja ya Taasisi iliyo chini ya Wizara na kuitaka Menejimenti ya Kituo hicho kuendelea kuboresha utoaji huduma za kituo hicho lii kuendana ushindani uliopo kwenye sekta ya huduma ya utalii wa mikutano.

 

Aidha, Mhe. Naibu Waziri aliwahimiza AICC kukamilisha mchakato wa kuanza ujenzi wa Kituo kipya cha Mikutano cha Kimataifa cha Mlima Kilimanjaro (MKICC) ambacho kitakuwa na uwezo wa kuhudumia mikutano mikubwa zaidi katika ukanda wa Afrika Mashariki.


Vilevile alipata fursa ya kutembelea baadhi ya miradi ya uwekezaji inayomilikiwa na AICC ikiwemo Kumbi, Hospitali, Kiwanja kitakapojengwa kituo cha MKICC na nyumba za makazi zaidi ya 600 zilizopo maeneo ya Kijenge, Soweto na Barabara ya Range kwenye Jiji la Arusha.


Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk, akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili kwenye Ofisi za Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhandisi Steven Mlote (kushoto) kwa ajili ya kuanza ziara yake kwenye Ofisi za Makao Makuu ya Jumuiya hiyo zilizopo jijini Arusha. Ziara hiyo ambayo ililenga kujitambulisha na kujionea shughuli za utendaji za Sekretarieti imefanyika tarehe 23 Septemba 2021.

Mhe. Naibu Waziri akizungumza na Mhandisi Mlote ambaye alimpokea kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Jumuiyay wakati wa ziara yake ya kujitambulisha aliyoifanya kwenye Ofisi za Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki jijini Arusha tarehe 23 Septemba 2021.

Mhandisi Mlote akimkabidhi Mhe. Balozi Mbarouk  zawadi ya machapisho mbalimbali kuhusu Jumuiya ya Afrika Mashariki

Mhe. Balozi Mborouk na Mhandisi Mlote wakiwa katika picha ya pamoja na wajumbe walioambatana nao wakati wa mazungumzo yaliyofanyika kati yao

Mhe. Balozi Mbarouk akizungumza na Rais wa Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhe. Jaji...alipomtembelea ofisini kwake wakati wa ziara yake kwenye Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki jijini Arusha tarehe 23 Septemba 2021. Kushoto ni Msajili wa Mahakama hiyo.

Mhe. Balozi Mbarouk akiwa katika picha ya pamoja na Mhe. Jaji Kayobera

Mhe. Balozi Mbarouk akiwa katika picha ya pamoja na Rais wa Mahakama ya Afrika Mashariki, Mhe. Jaji Kayobera, Mhandisi Mlote (kulia) na Msajili wa Mahakama hiyo (kushoto)

Mhe. Balozi Mbarouk akiwa katika picha ya pamoja na Spika wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhe.Ngoga Karoli Martin (kulia)  mara baada ya kumaliza mazungumzo yao

Mhe. Balozi Mbarouk akisikiliza maelezo kuhusu utendaji kazi wa Kituo cha Jumuiya ya Afrika Mashariki cha Kuratibu mwenendo wa magari ya  mizigo hususan katika kipindi hiki cha ugonjwa wa UVIKO-19

Mhe. Balozi Mbarouk akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili kwenye Ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. John Mongella. Mhe. Mbarouk alimtembelea Mkuu huyo wa Mkoa wakati wa ziara yake ya kikazi kwenye Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki

Mhe. Balozi Mbarouk akiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Mongella

Mhe. Balozi Mbarouk akizungumza na Menejimenti ya Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC) alipokitembelea kwa ajili ya kujionea shughuli mbalimbali zinanatekelezwa na Kituo hicho ambacho ni moja ya Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo hicho, Bw. Savo Mung'ong'o.

Kikao kikiendelea na baadhi ya wajumbe wa Menejimenti ya AICC

Mhe. Balozi Mbarouk akiwa katika picha ya pamoja naWajumbe wa Menejimenti ya AICC

Mhe. Balozi Mbarouk akipata maelezo kuhusu Ukumbi wa Simba uliopo AICC. 

Mhe. Balozi Mbarouk akipata maelezo alipotembelea nyumba za kupangisha ikiwa ni baadhi ya miradi ya uwekezaji inayomilikiwa na AICC

 

Wednesday, September 22, 2021

UKRAINE KUFUNGUA KITUO CHA KUSHUGHULIKIA VISA NCHINI TANZANIA

Ukraine imeeleza kuwa Oktoba, 2021 inatarajia kufungua kituo chake cha kushughulikia VISA kwa Watanzania wanaosafiri kwenda nchini humo kwa shughuli mbalimbali. Hatua hii inalenga kuwaondolea usumbufu Watanzania wanaosafiriki kwenda nchini humo ambapo kwa sasa wanalazimika kwenda jijini Nairobi, Kenya kushugulikia VISA za safari zao. 

Haya yameelezwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk ambaye mapema leo alifanya mazunguzo kwa njia ya Mtandao na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine Mhe. Dmytro Senik.

Balozi Mbarouk ameongeza kuwa katika mazumgumzo hayo pia wamejadili namna ya kushirikiana katika maeneo ya Biashara na Uwekezaji, Kilimo, Elimu na Viwanda. Katika eneo la kilimo Naibu Waziri Senik ameleza kuwa Ukuraine ipo tayari kushirikiana na Tanzania katika kilimo cha ngano ili kuongeza uzalishaji na ubora wa zao hilo. Vilevile Waziri Senik ameeleza utayari wa Ukraine kusaini makubaliano ya ushirikiano katika sekta ya ya elimu na Tanzania. 

Aidha, Naibu Waziri Senik ameeleza kuwa siku za usoni anatarajia kufanya ziara nchini Tanzania ambapo ataambatana na ujumbe wa wafanyabiashara na wawekezaji wa nchini Ukraine kwa lengo la kuangalia fursa mbalimbali za uwekezaji na biashara. 

Julai 2021, Tanzania na Ukraine zimetimiza miaka 29 ya mahusiano ya kidiplomasia ambapo zimeendelea kushirikiana katika sekta mbalimbali ikiwemo biashara na elimu. Mathalani idadi ya watalii wanaotembelea nchini kutoka Ukraine imeongezeka kutoka 1352 mwaka 2014 hadi 7260 kwa mwaka 2020.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk akiwa katika mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine Mhe. Dmytro Senik (hayuko pichani) yaliyofanyika leo Septemba 22, 2021. 
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine Mhe. Dmytro Senik wakiwa katika mazungumzo.

  Mazungumzo yakiendelea

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk akifuatilia mazungumzo.

Saturday, September 18, 2021

MABALOZI WAASWA KUTEKELEZA DIPLOMASIA YA UCHUMI

Na Mwandishi Wetu, Dar

Serikali imewaelekeza mabalozi walioteuliwa hivi karibuni kuhakikisha kuwa wanatekeleza na kusimamia diplomasia ya uchumi kwa maslahi mapana ya Taifa.

Maelekezo hayo yametolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) katika hafla ya kufunga mafunzo maalumu ya wiki mbili yaliyokuwa yanatolewa kwa mabalozi hao katika Chuo cha Diplomasia Jijini Dar es Salaam.

“Leo nimefunga mafunzo ya wiki mbili kwa mabalozi wetu walioteuliwa hivi karibuni, na imekuwa ni utaratbu wa Wizara kuwanoa kabla ya kwenda katika vituo vyao vya kazi. Mafunzo haya huwajengea uwezo mabalozi kupata ufahamu zaidi pamoja na kujua majukumu yao katika kuendeleza diplomasia ya uchumi, kuhamasisha wawekezaji, utalii na maeneo mengine mengi,” Amesema Balozi Mulamula.

Pamoja na mambo mengine, Balozi Mulamula amewasisitiza mabalozi umuhimu wa kufahamu na kutekeleza Diplomasia ya Siasa iliyopo ndani ya Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi CCM (2020-2025) ili kuweza kuwasaidia kujua dira a nchi.

Pia Balozi Mulamula aliwataka mabalozi kuhakikisha kuwa wanaendeleza lugha ya Kiswahili katika mataifa wanayoenda kuiwakilisha Tanzania kwani kwa kufanya hivyo kutasaidia sana kukuza na kuendeleza lugha ya Kiswahili.

“Kubwa zaidi nimewaagiza kuhakikisha kuwa wanaendeleza lugha ya Kiswahili, kwa sasa lugha ya Kiswahili imekuwa ni bidhaa muhimu sana……..kiswahili ni muhimu sana na sasa Kiswahili kinazungumzwa na zaidi ya watu milioni 500 duniani,” Amesema Balozi Mulamula.

Aidha, Waziri Mulamula amewataka mabalozi kuhakikisha pamoja na mambo mengine, wanatekeleza majukumu yao vyema na kujenga taswira nzuri ya Serikali.

Awali akiongea na mabalozi, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab aliwapongeza kwa uteuzi na kuwashauri kuendelea kujituma katika kazi na kuleta mabadiliko ambayo Serikali imeyapanga hasa katika diplomasia ya uchumi.

Balozi Fatma amewaasa mabalozi waliomaliza mafunzo yao kuhakikisha kuwa wanatekeleza diplomasia ya uchumi pamoja na diplomasia ya siasa kwa weledi ili kuleta manufaa ya Taifa.

Tarehe 27 Julai, 2021 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan aliwaapisha mabalozi 13 Ikulu jijini Dar es salaam.

Mkuu wa Chuo cha Diplomasia Balozi Abdulrahman Kaniki (aliyesimama) akiongea na mabalozi waliomaliza mafunzo maalumu chuoni hapo jijini Dar es Salaam


Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab akiongea na mabalozi waliomaliza mafunzo maalum katika Chuo cha Diplomasia Jijini Dar es Salaam


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) akiongea na mabalozi waliomaliza mafunzo maalum katika Chuo cha Diplomasia Jijini Dar es Salaam


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab katika picha ya pamoja na mabalozi walimaliza mafunzo maalum katika Chuo cha Diplomasia Jijini Dar es Salaam


 

Friday, September 17, 2021

NUU YATAKIWA KUTUMIA TEKNOLOJIA KUKUZA DILOMASIA YA UCHUMI

 Na Mwandishi Wetu, Dar

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Stergomena Tax ameishauri Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) kutumia teknolojia vizuri katika kukuza na kuendeleza diplomasia ya uchumi pamoja na masuala ya ulinzi na usalama

Dk. Stergomena Tax ametoa ushauri huo wakati alipokuwa akifunga mafunzo maalumu ya siku tano ya Wajumbe wa Kamati ya NUU yaliyoandaliwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki leo Jijini Dar es Salaam.

Pamoja na mambo mengine, mafunzo hayo yamelenga kuwaongezea ujuzi wabunge ambao ni wajumbe wa kamati hio katika masuala ya diplomasia ya uchumi, maslai ya taifa, mawasiliano ya kidemokrasia, uchumi wa bluu, ushirikiano wa Kimataifa na usalama wa nyaraka za kibalozi.

"Huwezi ukatenganisha diplomasia na ulinzi na usalama hususani katika dunia ya sasa ambayo ni dunia ya teknolojia, inayokuwa kwa kasi, diplomasia inatengemea ulinzi na usalama, diplomasia inaongoza maslahi ya Taifa haya ni mambo ambayo hayawezi kutenganishwa," amesema na kuongeza kuwa;

"Teknolojia hii ni muhimu sana katika kuendeleza uchumi na masuala ya diplomasia, ulinzi na usalama kama ikitumika vyema, ila ni vyema tukazitambua pande zote mbili wakati tunatumia teknolojia hii tunalo jukumu ya kutuletea manufaa lakini pia tunalo jukumu la kuwa walinzi wa rasilimali za Taifa letu,"

Awali akimkaribisha Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mwenyekiti wa Kamati ya NUU Bw. Mussa Zungu amewasihi watanzania kubadilika na kujikita kujenga uchumi imara.

“Uchumi imara unahitaji diplomasia katika kusimamia maslahi mapana ya Taifa……………hatuwezi kupigwa kama tutakuwa na  watu imara wanaopigania maslahi ya taifa letu, lazima sisi kama kamati inayo ‘cross-cut’ masuala mengi tusimamie maslahi ya taifa letu” Amesema Mhe. Zungu

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine amesema Wizara itaendelea kuboresha mafunzo mbalimbali kwa kamati ya NUU kwa lengo la kuwajengea uwezo na ujuzi katika kutekeleza majukumu yao kadri dunia inavyo kwenda.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) Bw. Mussa Zungu (Mb) akitoa hotuba kwa wajumbe wa kamati anayoiongoza Jijini Dar es Salaam


Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Stergomena Tax akihutubia Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) katika hafla ya kufunga mafunzo maalumu kwa kamati hiyo Jijini Dar es Salaam 


Wajumbe wa Kamati ya NUU wakimsikiliza Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Stergomena Tax (hayupo pichani) alipokuwa akihutubia 


Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Stergomena Tax akimsikiliza Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine  


Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Stergomena Tax akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Katai ya NUU mara baada ya kumaliza mafunzo maalumu yaliyoandaliwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Jijini Dar es Salaam

Wednesday, September 15, 2021

WAKAZI WA MARA WANUFAIKA NA MAADHIMISHO YA "SIKU YA MARA"

Septemba 15 kila mwaka Tanzania na Kenya hufanya maadhimisho ya Siku ya Mara (Mara Day), ambayo pia huusisha maonesho ya bidhaa mbalimbali sambamba na utoaji elimu inayolenga kuhimiza umuhimu wa kuhifadhi mazingira ya Bonde la Mto Mara. 

Sherehe za maadhimisho haya ambayo hufanyika kwa zamu baina ya Tanzania na Kenya, mwaka huu 2021, Maadhimisho ya 10 ya Siku ya Mara yanafanyika katika Wilaya ya Tarime, mkoani Mara. Kama ilivyo ada ya maadhimisho haya kuendeshwa kwa ushirikiano baina ya pande mbili (Tanzania na Kenya) mwaka huu pia kumekuwa na ushiriki wa pande zote mbili. 

Madhimisho ya Kumi ya Siku ya Mara mwaka huu 2021 yanaongozwa na Kauli Mbiu isemayo “Tuhifadhi Mto Mara kwa Utalii na Uchumi Endelevu” 

Akizungungumza kwenye maadhimisho hayo Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso ametoa wito kwa Mkuu wa Mkoa, Wakuu wa Wilaya, Wenyeviti wa Halmashauri pamoja na Wenyeviti wa Vijiji kuhakikisha wanashughulikia kwa mtazamo chanya suala la utunzaji wa mazingira na vyanzo vya maji katika maeneo yetu.

“Suala la kuhifadhi ya mazingira ya Bonde la Mto Mara ikiwa ni pamoja na vyanzo vya maji limekua likitiliwa mkazo na Serikali ili kuhakikisha kuwa maji yaliyopo yanahifadhiwa na kutunzwa kwa mujibu wa sheria. Wito wangu kwenu ni kwamba tuendeleze ushirikiano katika uhifadhi wa mazingira ili pawepo na vyanzo vya maji vya uhakika, vyenye maji ya kutosha na yenye ubora wakati wote kwa ajili ya maendeleo” alisema Mhe. Aweso

Akizungumza kwenye ufunguzi wa maadhimisho hayo Mkuu wa Wilaya ya Tarime ambaye pia ni Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Lt. Col. Michael Mangwela Mtenjela amebainisha baadhi ya mafanikio yaliyofikiwa tokea kuanza kwa Maadhimisho haya mwaka 2012 kuwa ni pamoja na; ongezeko la upandaji miti, ongezeko la watalii, kuongezeka kwa ushirikiano baina ya jamii za pande zote mbili zinazozunguka Bonde la Mto Mara na uwekwaji wa mawe ya kuonesha mipaka (bikoni) katika eneo la Bonde. 

“Mwaka huu Idadi ya miti na vigingi imeongezeka ikilinganishwa na mwaka 2020 ambapo miti 2600 ilipandwa pamoja na vigingi 20 katika Wilaya ya Butiama. Ongezeko hili linatokana na juhudi za makusudi zinazochukuliwa na Mkoa wa Mara katika kuhifadhi ikolojia ya Bonde la Mto Mara na Mkoa mzima wa Mara” alieleza Mheshimiwa Lt.Col. Mtenjela.

Kwa upande wake Balozi wa Tanzania nchini Kenya Mhe. Dkt. John Simbachawene ameeleza kuwa Mara Day ni jukwaa linatoa fursa nzuri ya utetezi na ushirikiano kati ya watendaji wa serikali, asasi za kiraia, sekta binafsi, washirika wa maendeleo na mashirika yasiyo ya kiserikali katika mashirikiano ya kuimarisha usimamizi na maendeleo ya rasilimali za maji katika Bonde la Mto Mara. 

Katika kuadhimisha Siku ya Mto Mara mwaka 2021, sambamba na shughuli zingine zilizokuwa zikiendelea Mkoa wa Mara umepanda miti 13,000 na kuweka vigingi 70 katika vijiji vya Mrito na Kerende vilivyopo wilayani ya Tarime.

Akizungumza katika hafla ya ufunguzi wa madhimisho hayo Bi. Bhoke Mwita amkazi wa Tarime ameelezea kuridhishwa kwake na mafanikio aliyoyaona tokea kuanzishwa kwa maadhimisho ya Siku ya Mara. Ambapo ameeleza kuwa hapo awali pamoja na kunufaika na Mto Mara hawakutambua umuhimu wa kutunza mazingira yanayo uzunguka hivyo kusababisha uharibifu wa Ikolojia ya Bonde, tofauti na ilivyo sasa ambapo kupitia Maadhimisho haya wamejifunza na kuhamasika kutunza mazingira ya Bonde la Mto Mara. 

Tunazishukuru sana Serikali zetu ya Tanzania na Kenya kwa kuridhia kufanyika kwa Maadhimisho haya, licha kupata fursa ya kushiriki maonesho tunapata elimu kubwa kuhusu umuhimu wa kulinda Bonde la Mto Mara, sasa tumefikia mahali ambapo sisi wenyewe tunakuwa mlinzi dhidi ya kila mmoja kuzuia uharibifu katika mazingira ya Bonde la Mto. Kwa mafanikio tuanayoendelea kuyaona na kunufaika nayo hatuna budi kuendelea kuhifadhi mazingira kwa ajili ya mandeleo yetu wenyewe. Alisema Bi. Bhoke Mwita

Mto Mara ambao ni eneo muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi pamoja na baioanuai zilizopo unaanzia katika chemchem ya Enapuyapui iliyopo kwenye misitu ya Milima ya Mau nchini Kenya, ambapo maji ya Mto huo hutiririka kupitia pori la akiba la Hifadhi ya Taifa ya Maasai-Mara kwa upande wa Kenya na hatimaye katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (SENAPA) kwa upande wa Tanzania, kabla ya kumwaga maji yake katika Ziwa Victoria. Mto huu unapita katika Wilaya nne kwa upande wa Tanzania ambazo ni Serengeti, Tarime, Rorya na Butiama.

Maadhimisho haya yanatokana na Mkutano wa 10 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Bonde la Ziwa Victoria lililoamua kuwe na Maadhimisho ya Siku ya Mara kila mwaka ifikapo tarehe 15 Septemba katika Mkutano uliofanyika Mei 4,2021 jijini Kigali, Rwanda ili kuhamasisha na kutoa elimu kwa wadau juu ya utunzaji wa mazingira na rasilimali maji katika Bonde la Mto Mara.
Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) akisalimiana na Bw. Eliabi Chodota Kaimu Mkurugenzi wa Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Kijamii katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, wakati alipowasili katika viwaja vya Chuo cha Uwalimu cha Tarime kwenye Maadhimisho ya 10 ya Siku ya Mara
Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) akisaini kitabu cha wageni kwenye Maadhimisho ya 10 ya Siku ya Mara yaliyofanyika Wilayani Tarime, Musoma
Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (wapili kulia) akiwa ameambatana na viongozi na watendaji mbalimbali wa Serikali wakati akielekea kuona bidhaa mbalimbali za wafanyabiashara walioshiriki maonesho ya Maadhimisho ya Siku ya Mara
Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) akisisitiza jambo wakati akizungumza na Wananchi wa Tarime (hawapo pichani) kwenye kilele cha Maadhimisho ya 10 ya Siku ya Mara


Balozi wa Tanzania nchini Kenya Mhe. Dkt. John Simbachawene akizungumza na wananchi waliojitokeza kushiriki kilele cha Maadhimisho ya 10 ya Siku ya Mara yaliyofanyika katika viwaja vya Chuo cha Uwalimu cha Tarime, Musoma.
Balozi wa Tanzania nchini Kenya Mhe. Dkt. John Simbachawene (wakwanza kulia) akifuatilia Maadhimisho ya 10 ya Siku ya Mara yaliyokuwa yakiendelea katika viwaja vya Chuo cha Uwalimu cha Tarime, Musoma
Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) akifuatilia maelezo kuhusu huduma mbalimbali za Mamlaka ya Kodi Tanzania (TRA) alipotembelea banda la Mamlaka hiyo kwenye kilele cha Maadhimisho ya 10 ya Siku ya Mara
Mkuu wa Wilaya ya Tarime Mhe. Lt. Col. Michael Mangwela Mtenjela akizungumza na wananchi waliojitokeza kwenye ufunguzi wa Maadhimisho ya 10 ya Siku ya Mara yaliyofanyika katika viwaja vya Chuo cha Uwalimu cha Tarime, Musoma. 
Kaimu Mkurugenzi wa Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Kijamii Bw. Eliabi Chodota (wakwanza) katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akifuatilia matukio mbalimbali yaliyokuwa yakiendela kwenye kilele cha Maadhimisho ya 10 ya Siku ya Mara yaliyofanyika katika viwanja vya Chuo cha Uwalimu cha Tarime, Musoma

Meza Kuu wakifuatilia matukio mbalimbali yaliyokuwa yakiendela kwenye Maadhimisho ya 10 ya Siku ya Mara yaliyofanyika katika viwanja vya Chuo cha Uwalimu cha Tarime, Musoma

Waziri mwenye Dhamana ya Usimamizi wa Rasilimali Maji Mhe. Job Kiyiapi kutoka Kenya akizungumza na wananchi (hawapo pichani) waliojitokeza kushiriki kilele cha Maadhimisho ya 10 ya Siku ya Mara yaliyofanyika katika viwaja vya Chuo cha Uwalimu cha Tarime, Musoma.
Meza Kuu wakijumuika kuchea na kikundi cha kwaya kilichokuwa kikitoa burudani kwenye Maadhimisho ya 10 ya Siku ya Mara yaliyofanyika katika viwanja vya Chuo cha Uwalimu cha Tarime, Musoma