Monday, April 4, 2022

MKUTANO MAALUM WA 47 WA BARAZA LA MAWAZIRI LA EAC NGAZI YA WATAALAM UMEFUNGULIWA JIJINI ARUSHA

Mkutano Maalum wa 47 wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki unafanyika jijini Arusha kuanzia tarehe 4 hadi 6 Aprili 2022.

Mkutano huu unafanyika katika mpangilio ufuatao; tarehe 4 Aprili 2022 Mkutano Ngazi ya Wataalam, tarehe 5 Aprili 2022 Mkutano Ngazi ya Makatibu Wakuu na tarehe 6 Aprili 2022 Mkutano Ngazi ya Mawaziri.

Pamoja na mambo mengine Mkutano Ngazi ya Wataalamu unaandaa taarifa ya masuala ya Fedha na Utawala itakayowasilishwa kwenye mkutano wa Makatibu Wakuu na baadae kwenye mkutano wa Mawaziri.


Kaimu Mkurugenzi Idara ya Sera na Mipango katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bw. Justin Kisoka (kushoto) akichangia hoja katika Mkutano  Maalum wa 47 wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Ngazi ya Wataalam unaofanyika leo tarehe 4 Aprili 2022 jijini Arusha, Tanzania.
Kulia ni Mkurugenzi Idara ya Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii, Bw. Eliabi Chodota akifatilia mkutano huo.


Mkutano ukiendelea, kulia ni ujumbe wa Tanzania ukifuatilia majadiliano katika mkutano huo.

Meza kuu ikiongoza Mkutano.

Mkurugenzi Kitengo cha Sheria katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Caroline Chipeta akifatilia majadiliano katika mkutano.

Sehemu nyingine ya ujumbe wa Tanzania

Ujumbe kutoka taasisi za Jumuiya ya Afrika Mashariki ukifuatilia majadiliano.

 

WAZIRI FORD ARIDHISHWA NA UTOAJI HUDUMA ‘ENGENDERHEALTH’

Na Mwandishi wetu, Dar

Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika, Amerika ya Kusini na Visiwa vya Karibian Mhe. Vicky Ford ameonesha kuridhishwa na utoaji wa huduma katika kituo cha afya EngenderHealth Tanzania kilichopo Yombo Jijini Dar es Salaam.

Mhe. Ford ameoneshwa kuridhishwa na utoaji wa huduma jumuishi kwa familia, mama, watoto, vijana na watu wenye ulemavu wakati alipofanya ziara katika kituo cha EngenderHealth Tanzania ambacho kinafadhiliwa na Serikali ya Uingereza.

“Nimeridhika na utoaji wa huduma katika kituo hiki hasa baada ya kuongea na akina mama, vijana na watu wenye ulemavu kwa nyakati tofauti maelezo yao kwangu yanaonesha huduma ni nzuri na zinaridhisha,” amesema Waziri Ford

Pia nimeona mazingira ya kituo hiki pamoja na kuongea madaktari, wauguzi na watoa huduma kwa kweli wamenifariji kazi yao ni nzuri na nawaomba waendelee kufanya kazi kwa bidi bila kuchoka, ameongeza Waziri Ford

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkaazi wa EngenderHealth Tanzania, Dkt. Moke Magoma ameishukuru Serikali ya Uingereza kwa ufadhili wa baadhi huduma katika kituo hicho na kuahidi kuwa wataendelea kufanya kazi kwa bidi na weledi katika kuwahudumia watanzania wanaotumia kituo hicho.

“Mheshimiwa Waziri kwa niaba ya wafanyakazi wa kituo hiki tunakushukuru sana kwa ufadhili wa huduma za wahanga wa unyanyasaji na Watoto na watu wenye ulemavu huduma hii imekuwa na msaada mkubwa sana katika jamii, tunakuahidi kufanya kazi kwa bidi na weledi,” amesema Dkt. Magoma

Baadhi ya akina mama waliokuwa katika kituo hicho kwa ajili ya matibabu na huduma mbalimbali wameomba kuongezewa watumishi ili kupunguza msongamano wa wagonjwa Pamoja na kujengewa kituo nmumuishi ambacho kitaweza kusaidia upatikanaji wa huduma zote katika eneo moja.

Kituo cha EngenderHealth Tanzania kanafadhiliwa na Serikali ya Uingereza katika huduma za mama, mtoto, vijana na wenye ulemavu hasa wahanga wa unyanyasaji wa kijinsia, unyanyasaji wa watoto. 

Huduma nyingine zinazotolewa kituoni hapo ni pamoja na huduma jumuishi kwa familia, mama, Watoto, vijana na wenye ulemavu.

Waziri Ford yupo nchini kwa ziara ya kikazi ya siku tatu nchini kuanzia tarehe 3 - 5 Aprili 2022.    

Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika, Amerika ya Kusini na Visiwa vya Karibian Mhe. Vicky Ford akisalimiana na uongozi wa kituo cha Afya cha EngenderHealth mara baada ya kuwasili kituoni hapo Yombo Vituka Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika, Amerika ya Kusini na Visiwa vya Karibian Mhe. Vicky Ford akiongea na akina mama waliokuwa katika kituo cha afya cha EngenderHealth  Yombo Vituka wakati wakisubiria huduma za afya  





Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika, Amerika ya Kusini na Visiwa vya Karibian Mhe. Vicky Ford akiongea na mmoja wa wauguzi katika kituo cha afya cha EngenderHealth  Yombo Vituka 

Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika, Amerika ya Kusini na Visiwa vya Karibian Mhe. Vicky Ford akiongea na mmoja wa wauguzi katika kituo cha afya cha EngenderHealth  Yombo Vituka 

Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika, Amerika ya Kusini na Visiwa vya Karibian Mhe. Vicky Ford akiwa katika kituo cha huduma ya macho, masikio na utengamao kwa mtoto  katika kituo cha afya cha EngenderHealth  Yombo Vituka 


Mhe. Zungu akutana na Rais Mwenza wa Bunge la Pamoja la EU na OACPS

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Bunge la Umoja wa Ulaya yamekubaliana kuimarisha ushirikiano miongoni mwao na miongoni mwa wabunge wao. Hayo yameafikiwa tarehe 02 Aprili 2022 kwenye makao makuu ya Bunge la Umoja wa Ulaya nchini Ufaransa, wakati wa mazungumzo baina ya Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mussa Azzan Zungu na  Rais mwenza wa Bunge la Pamoja la Umoja wa Ulaya na Jumuiya ya Nchi za Afrika, Caribbean na Pasifiki (OACPS), Mhe. Prof. Carlos Zorrinho). 

Mazungumzo hayo yaliyofanyika pembezoni mwa Mkutano wa 41 wa Bunge  la OACPS na EU  ambapo Mhe. Zungu anaongoza ujumbe wa Tanzania, viongozi hao walikubaliana pia kupitia Mabunge yao kuhakikisha kuwa uhusiano mzuri uliopo baina ya Tanzania na Umoja wa Ulaya na baina ya Bunge la Tanzania na Bunge la Umoja  wa Ulaya unaimarishwa zaidi.

Aidha, Mhe. Zungu alitumia fursa hiyo kumwalika Mhe. Zorrinho pamoja na  baadhi ya Wabunge wa Bunge la EU kuitembelea Tanzania na kujionea wenyewe hatua mbalimbali zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suhuhu Hassan katika kusukuma maendeleo ya Tanzania. Rais huyo mwenza wa Bunge la Pamoja la Ulaya na ACP alipokea mwaliko huo kwa furaha  na kuahidi kufanya ziara hiyo nchini siku zijazo akiambatana na baadhi wa Wabunge wa Bunge la Umoja wa Ulaya. Alieleza kuwa Tanzania ni moja ya nchi za kipaumbele kwa Umoja wa Ulaya na Bunge hilo linafurahishwa na hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Tanzania kusimamia ajenda za maendeleo na ustawi wa jamii, hususan katika kuboresha mazingira ya uwekezaji na kuimarisha demokrasia na haki za binadamu.

Mhe. Zungu alimwomba mwenyeji wake huyo kuwahamasisha wawekezaji wa Ulaya waendelee kuja kuwekeza nchini kwenye masuala ya uchimbaji wa gesi na maeneo mengine, kwani Tanzania imebarikiwa kuwa na fursa nyingi za uwekezaji.

Viongozi hao walihitimisha mazungumzo yao kwa kusisitiza umuhimu wa kuongeza ushawishi wa mabunge yao kutoa miongozo itakayoimarisha ushirikiano baina ya Umoja wa Ulaya na nchi za Afrika, Carribean na Pacific pamoja na masuala yanayohusu kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuimarisha amani eneo la ukanda wa maziwa makuu hususan nchini Msumbiji. Professa Zorrinho alieleza kuwa EU ina imani kubwa zaidi na Tanznaia katika masuala ya usuluhishi wa migogoro na kukuza amani duniani.

Katika mazungumzo hayo, Mhe. Zungu aliambatana na Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji na kwenye Umoja wa Ulaya, Mhe. Jestas Abuok Nyamanga na maafisa wengine waandamizi wa Ubalozi na Bunge.

Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mussa Assan Zungu  (kushoto) akisalimiana na Mhe. Professa Carlos Zorrinho, Rais mwenza wa Bunge la Pamoja la OACPS na EU (kulia) wakati wa kikao chao kilichofanyika katika ofisi za Bunge la EU zilizopo Strasbourg,Ufaransa. Tukio hilo lilifanyika tarehe 02 Aprili,2022 wakati wa Mkutano wa Bunge la Pamoja la OACPS na EU unaoendelea Strassbourg.


 Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Mussa Assan Zungu (aliyesimama) akichangia katika moja ya kikao cha Bunge la Pamoja la OACPS na EU kilichofanyika katika ofisi za Bunge la EU zilizopo Strasbourg, Ufaransa. Tukio hilo lilifanyika tarehe 02 Aprili, 2022. Mhe.Zungu analiwakilisha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika vikao hivyo.


Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mussa Assan Zungu  (katikati kulia) akiwa katika kikao chake na Mhe. Professa Carlos Zorrinho, Rais mwenza (co-President) wa Bunge la Pamoja la OACPS na EU (wa pili kushoto) wakati wa kikao chao kilichofanyika katika ofisi za Bunge la EU zilizopo Strasbourg,Ufaransa. Tukio hilo lilifanyika tarehe 02 Aprili, 2022 wakati wa Mkutano wa Bunge la Pamoja la OACPS na EU unaoendelea Strasbourg. Kulia mwa Mhe. Zungu ni Mhe. Jestas Nyamanga, Balozi wa Ubalozi wa Jamhuri wa Muungano nchini Ubelgiji na kwenye Umoja wa Ulaya (kulia) na maofisa wengine kutoka Bunge la Tanzania na Bunge la EU.


Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mussa Assan Zungu,  (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Mhe. Balozi Dkt George Pinto Chikoti, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya OACPS (kulia) na Mhe Balozi Jestas Abuok Nyamnaga (kushoto) nje ya ukumbi kunakofanyika Mkutano wa 60 wa Bunge la OACPS unaofanyika katika ofisi za Bunge la EU jijini Strasbourg, Ufaransa. Tukio hilo lilifanyika tarehe 29 Machi, 2022. Mhe. Zungu analiwakilisha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika vikao hivyo.

Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Mussa Assan Zungu  (aliyesimama kulia) akibadilishana mawazo na mmoja wa Wabunge wa Bunge la Umoja wa Ulaya wakati wa Mkutano wa 41 wa Bunge la Pamoja la OACPS na EU uliofanyika katika ofisi za Bunge la EU zilizopo Strasbourg,Ufaransa. Tukio hilo lilifanyika tarehe 02 Aprili, 2022. Mhe. Zungu analiwakilisha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika vikao hivyo.

NCHI WANACHAMA WA SADC ZAPONGEZWA KWA KUJITOLEA KULINDA AMANI YA KANDA

Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ambaye pia ni Waziri wa Uhusiano wa Kimataifa na Ushirikiano wa Afrika Kusini, Mhe. Dkt. Naledi Pandor amezipongeza Nchi Wanachama wa SADC zikiwemo zile zinazochangia vikosi nchini Msumbiji kwa kuendelea kujitolea kwenye masuala ya ulinzi wa amani kwa maslahi mapana ya wananchi wa Msumbiji na kanda ya SADC kwa ujumla.

Mhe. Pandor ametoa pongezi hizo wakati akifungua rasmi Mkutano wa Dharura wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika uliofanyika jijini Pretoria, Afrika Kusini tarehe 03 Aprili 2022.

Amesema Mkutano huo ni mwendelezo wa majadiliano yanayofanywa na Nchi Wanachama wa SADC kuhusu namna ya kuisadia Msumbiji katika kupambana na vitendo vya ugaidi na ukatili vilivyoripotiwa kwenye maeneo ya Kaskazini mwa Jimbo la Cabo Delgado.

“Nia ya dhati na msaada unaoendelea kutolewa kwa Msumbiji na Nchi Wanachama ni wa kupongezwa. Hii ni ishara kwamba sote tuna nia moja ya kupambana na ugaidi ambao unatishia jitihada zinazofanywa na jumuiya katika kukuza mtangamano wa SADC na maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Hata hivyo niwahakikishie kuwa jitihada hizi si za bure zimezaa matunda” alisema Dkt. Pandor.

Kadhalika ameipongeza Misheni ya SADC nchini Msumbiji (SAMIM) kwa kazi nzuri wanayofanya ya kurejesha hali ya amani na utulivu na kuwawezesha wananchi wa Msumbiji hususan wale wanaoishi Kaskazini mwa nchi hiyo kwenye Jimbo la Cabo Delgado kuendelea na shughuli zao za maendeleo pasipo kuhofia vitendo vya ugaidi. 

"Tumekutana hapa kwa niaba ya wakuu wetu wa Nchi na Serikali, kupokea na kujadili ripoti na mapendekezo kuhusu mwenendo wa Misheni ya SADC nchini Msumbiji. Niwajulishe tu Ripoti inatia moyo kwani mambo mengi mazuri yamefanyika tangu SAMIM ianze kazi nchini Msumbiji na hali ya usalama nchini humo hususan maeneo ya kaskazini mwa Jimbo la Cabo Delgado inaendelea kuimarika na wananchi wameanzaa kurejea katika shughuli zao za kawaida”, alisema Mhe. Pandor.

Pia alieleza umuhimu wa kufunguliwa kwa Kituo cha Kikanda cha Kupambana na Ugaidi ambacho kilizinduliwa rasmi tarehe 28 Februari 2022 jijini Dar Es Salaamkwamba ni hatua muhimu katika kuimarisha usalama kwenye kanda ya SADC.

“Tumefurahishwa na uzinduzi wa Kituo cha Kikanda cha Kupambana na ugaidi nchini Tanzania tarehe 28 Februari 2022. Hii ni hatua muhimu katika kuimarisha mfumo wa usalama wa kanda yetu ambao utafanya kazi kwa kushirikiana na Kituo cha Kanda cha Tahadhari za Mapema” alieleza Dkt. Pandor.

Vilevile alitumia nafasi hiyo kuushukuru Umoja wa Ulaya kwa kuendelea kuchangia kwenye maeneo mbalimbali ya Misheni hiyo na kutoa wito kwa washirika wengine wa maendeleo kuendelea kusaidia na kuunga mkono jitihada za SADC za kurejesha amani na usalama nchini Msumbiji na maeneo mengine.

Awali akimkaribisha Dkt. Pandor kuzungumza, Katibu Mtendaji wa SADC, Bw. Elias Magosi alisema kuwa Sekretarieti ya SADC itaendelea kushirikiana na Nchi Wanachama wa SADC ili kuhakikisha lengo lilowekwa la kukomesha kabisa vitendo vya kigaidi nchini Msumbiji linatimia. Pia naye alizipongeza nchi wanachama na Misheni ya SADC iliyopo Msumbiji kwa kuendelea kujitolea kwa dhati na kueleza kuwa hali ya amani na utulivu imerejea kwa kiasi kikubwa nchini Msumbiji hususan kwenye maeneo ya kaskazini mwa Jimbo la Cabo Delgado.

Nchi Wanachama kumi (10) za Misheni ya SADC nchini Msumbiji ni Tanzania, Angola, Malawi, Lesotho, Namibia, Afrika Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Botswana, Zimbabwe na Zambia. 

Ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano huo uliongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe. Ujumbe huo unamjumuisha Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenerali Venance Mabeyo, Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Mhe. Meja Jenerali Mstaafu Gaudence Milanzi na Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Agnes Kayola.

Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ambaye pia ni Waziri wa Uhusiano wa Kimataifa na Ushirikiano wa Afrika Kusini, Mhe. Dkt. Naledi Pandor (wa pili kulia meza kuu) akifungua  rasmi Mkutano wa Dharura wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika uliofanyika jijini Pretoria, Afrika Kusini tarehe 03 Aprili 2022. Wa pili kushoto ni Katibu Mtendaji wa SADC, Bw. Elias Magosi.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ambaye pia anaongoza ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa Dharura wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC,  Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe (wa kwanza kulia) akiwa na wajumbe alioongozana nao kutoka Tanzania.
Sehemu ya ujumbe wa Tanzania ulioshiriki Mkutano huo. Kushoto ni Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenerali Venance Mabeyo na kulia ni Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Mhe. Meja Jenerali (Mst.) Gaudence Milanzi.

Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ambaye pia ni Waziri wa Uhusiano wa Kimataifa na Ushirikiano wa Afrika Kusini, Mhe. Dkt. Naledi Pandor (wa pili kulia) akifuatilia itifaki za ufunguzi  rasmi wa Mkutano wa Dharura wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika uliofanyika jijini Pretoria, Afrika Kusini
tarehe 03 Aprili 2022
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ambaye pia ni kiongozi wa ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa Dharura wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC,  Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe (wa kwanza kulia) akiwa na wajumbe wa Tanzania na wajumbe wa nchi nyingine za SADC wakishiriki taratibu za ufunguzi rasmi wa mkutano huo uliofanyika  jijini Pretoria, Afrika Kusini.
Sehemu ya ujumbe wa Malawi ulioshiriki Mkutano huo


Sehemu ya ujumbe wa Lesotho wakati wa ufunguzi wa mkutano






Sunday, April 3, 2022

BALOZI MULAMULA AKUTANA NA WAZIRI WA UINGEREZA JIJINI DODOMA

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (katikati) akimkaribisha Waziri wa Uingereza anayeshughulikia Afrika, Amerika ya Kusini na Visiwa vya Karibian Mhe. Vicky Ford (kulia) walipokutana kwa ajili ya chakula cha jioni jijini Dodoma wa kwanza kushoto ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Fatma Rajab.  

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (wa pili kushoto) akizungumza na  Waziri wa Uingereza anayeshughulikia Afrika, Amerika ya Kusini na Visiwa vya Karibian Mhe. Vicky Ford (wa kwanza kulia) walipokutana kwa ajili ya chakula cha jioni jijini Dodoma wa kwanza kushoto ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Fatma Rajab.

Waziri wa Uingereza anayeshughulikia Afrika, Amerika ya Kusini na Visiwa vya Karibian Mhe. Vicky Ford (wa kwanza kulia) akizungumza wakati alipokutana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula jijini Dodoma


Mazungumzo kati ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (kulia) na Waziri wa Uingereza anayeshughulikia Afrika, Amerika ya Kusini na Visiwa vya Karibian Mhe. Vicky Ford (kushoto) yakiendelea walipokutana na  jijini Dodoma.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akionesha zawadi y apicha ya michoro ya Tingatinga ambayo alimpatia zawadi Waziri wa Uingereza anayeshughulikia Afrika, Amerika ya Kusini na Visiwa vya Karibian Mhe. Vicky Ford walipokutana jijini Dodoma.


Waziri wa Uingereza anayeshughulikia Afrika, Amerika ya Kusini na Visiwa vya Karibian Mhe. Vicky Ford akionesha zawadi ya picha ya michoro ya tingatinga ambayo alipewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula walipokutana kwa jijini Dodoma.


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (kushoto) akitoa maelezo kuhusiana na michoro ya picha ya tingatinga ambayo alimpatia Waziri wa Uingereza anayeshughulikia Afrika, Amerika ya Kusini na Visiwa vya Karibian Mhe. Vicky Ford walipokutana jijini Dodoma


Balozi Liberata Mulamula (wa pili kushoto) katika picha ya pamoja na Waziri wa Uingereza anayeshughulikia Afrika, Amerika ya Kusini na Visiwa vya Karibian Mhe. Vicky Ford ambaye alifika jijini Dodoma kwa ziara ya kikazi nchini tarehe 03 Aprili 2022.



Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Uingereza anayeshughulikia Afrika, Amerika ya Kusini na Visiwa vya Karibian Mhe. Vicky Ford ambaye yuko nchini kwa ziara ya siku tatu kuanzai tarehe 3-5 Aprili 2022.

Katika mazungumzo yao viongozi hao wamekubaliana kuendelea kushirikiana na kuimarisha uhusiano mzuri ulioko baina ya Tanzania na Uingereza.

Balozi Mulamula amemshukuru Mhe. Ford kwa uamuzi wa kuja kuitembelea Tanzania na kujionea utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambayo inafadhiliwa na Uingereza na kumualika kuja tena nchini wakati mwingine.

Naye Mhe. Ford ameelezea kufurahishwa ridhishwa na utekelezaji wa miradi hiyo jambo ambalo amesema inatia moyo kuona fedha zinazotolewa na nchi hiyo zinafanya kazi iliyokusudiwa na hivyo kusaidia harakati za kubadili maisha ya Watanzania.

Waziri Ford aliwasili nchini kupitia uwanja wa Ndege wa Kimataifa ya Kilimanjaro ambako alitembelea miradi ya maendeleo katika mji wa Moshi na baadaye jijini Dodoma ambako alikwenda Ikulu ya Chamwino na kukutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan .

Tarehe 04 Aprili 2022, Mhe. Ford atatembelea miradi ya kituo cha afya EngenderHealth Tanzania kilichopo Yombo, kituo cha kuzuia biashara ya binadamu na ulinzi wa watoto vya Jijini Dar es Salaam na kuzindua mradi wa maendeleo wa elimu bunifu nchini unaoitwa Shule Bora utakaofanyika Kibaha mkoani Pwani.

Jioni ya tarehe 04 Aprili 2022 Mhe. Ford atakuwa na mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuelezea ziara yake nchini na anatarajiwa kuondoka nchini tarehe 05, Aprili 2022

WAZIRI UINGEREZA ANAYESHUGHULIKIA MASUALA YA AFRIKA AWASILI DODOMA KWA ZIARA YA KIKAZI

 

Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika, Amerika Kusini na Visiwa vya Karibian Mhe. Vicky Ford akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Anthony Mtaka baada ya kuwasili jijini Dodoma akiwa katika ziara ya kikazi ya siku tatu nchini kuanzia tarehe 3 - 5 Aprili 2022.

 

Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika, Amerika Kusini na Visiwa vya Karibian Mhe. Vicky Ford akisalimiana na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje  na Ushirikiano wa Afrika Masshariki Balozi Fatma Rajab baada ya kuwasili jijini Dodoma akiwa katika ziara ya kikazi ya siku tatu nchini kuanzia tarehe 3 - 5 Aprili 2022.

Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika, Amerika Kusini na Visiwa vya Karibian Mhe. Vicky Ford akizungumza na wenyeji wake katika uwanja wa ndege wa Dodoma  baada ya kuwasili jijini Dodoma akiwa katika ziara ya kikazi ya siku tatu nchini kuanzia tarehe 3 - 5 Aprili 2022.


Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika, Amerika Kusini na Visiwa vya Karibian Mhe. Vicky Ford akisaini kitabu cha wageni katika uwanja wa ndege wa Dodoma  baada ya kuwasili jijini Dodoma akiwa katika ziara ya kikazi ya siku tatu nchini kuanzia tarehe 3 - 5 Aprili 2022.


Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika, Amerika Kusini na Visiwa vya Karibian Mhe. Vicky Ford (katikati) akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Anthony Mtaka (kushoto) kulia ni Balozi wa Uingereza nchini Mhe. David Concor akifuatilia mazungumzo hayo.


 
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Anthony Mtaka (kushoto) akizungumza na Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika, Amerika Kusini na Visiwa vya Karibian Mhe. Vicky Ford (katikati) huku Balozi wa Uingereza nchini Mhe. David Concor (kulia) akifuatilia mazungumzo hayo
 
 
Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika, Amerika Kusini na Visiwa vya Karibian Mhe. Vicky Ford amewasili jijini Dodoma akiwa katika ziara ya kikazi ya siku tatu nchini kuanzia tarehe 3 - 5 Aprili 2022.

Waziri huyo amepokelewa katika uwanja wa ndege wa  Dodoma na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Anthony Mtaka na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Fatma Rajab. 

Baada ya kuwasili jijini Dodoma Waziri Ford alielekea Ikulu ya Chamwino ambako alikutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanznsia Mhe.  Samia Suluhu Hassan na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushrikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula.

Katika ziara yake nchini Mhe. Ford pamoja na mambo mengine,  anatarajiwa kuzindua mpango mpya wa Elimu bunifu nchini ambao unafadhiliwa na serikali ya Uingereza. 

katika ziara yake nchni Waziri Ford ataungana na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf  Mkenda na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Innocent Bashungwa kuzindua mpango huo mpya wa maendeleo wa elimu bunifu nchini unaoitwa Shule Bora utakaofanyika Kibaha mkoani Pwani tarehe 04 Aprili 2022.

Mpango wa Shule Bora utaongeza upatikanaji wa elimu kwa watoto zaidi ya milioni nne (4) nchini, umelenga kuboresha viwango vya elimu kwa watoto wenye ulemavu, watoto wanaotoka maeneo yenye upungufu wa rasilimali na wasichana.

Kati ya mwaka 2015-2020 Uingereza kupitia ufadhili katika sekta ya elimu imesaidia zaidi ya watoto milioni 15.6 duniani kote kupata elimu, ikiwa ni pamoja na wasichana milioni 8.1.
 
Waziri Ford pia atakuwa na mikutano na ziara mbalimbali jijini Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya kazi mbalimbali zinazofanywa nchini katika kuimarisha uhusiano kati ya Uingereza na Tanzania kupitia nyanja za biashara, mabadiliko ya tabianchi na kupambana na uhalifu mkubwa na uliopangwa.


 

MKUTANO WA DHARURA WA KAMATI YA MAWAZIRI WA SADC KUFANYIKA PRETORIA, AFRIKA KUSINI

Mkutano wa Dharura wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Extra-Ordinary Ministerial Committee of the Organ) ambao utahusisha pia Jamhuri ya Msumbiji na Nchi Zinazochangia Vikosi katika Misheni ya SADC iliyopo Msumbiji (SAMIM) utafanyika Pretoria, Afrika Kusini tarehe 03 Aprili 2022.

Mkutano huo ambao umetanguliwa na Mkutano wa Kamati ya Kudumu ya Makatibu Wakuu (Senior Officials meeting), unalenga pamoja na mambo mengine Kupokea na Kujadili Ripoti ya Maendeleo ya Misheni ya SADC nchini Msumbiji (SAMIM) pamoja na Mapendekezo mbalimbali kutoka kwa Makatibu Wakuu.

Itakumbukwa kuwa, wakati wa Mkutano wa dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC ulichofanyika jijini Maputo, Msumbiji mwezi Juni 2021, uliridhia kupelekwa kwa Misheni ya SAMIM (SADC Mission in Mozambique) nchini Msumbiji kwa ajili ya kuisaidia nchi hiyo kupamabana na ugaidi na vitendo vya unyanyasaji kwa wanawake na watoto vilivyokuwa vinaendelea kwenye baadhi ya Wilaya zilizopo kwenye Jimbo la Cabo Delgado.

Misheni hiyo ambayo ilianza kazi rasmi mwezi Julai 2021, inajumuisha Nchi Wanachama kumi (10) za SADC ambazo ni Tanzania, Angola, Malawi, Lesotho, Namibia, Afrika Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Botswana, Zimbabwe na Zambia.

Lengo kuu la misheni hiyo ni kukomesha matishio ya ugaidi,  kuimarisha hali ya ulinzi na  usalama, kurejesha utawala wa sheria kwenye maeneo yaliyoathirika kwenye Jimbo la Cabo Delgado na kuisadia Msumbiji kwa kushirikiana na Mashirika yanayotoa misaada ya kibinadamu ili kuyawezesha kutoa misaada kwenye maeneo yaliyoathirika na vitendo vya kigaidi ikiwemo kuwasaidia watu walioyakimbia makazi yao.

Ujumbe wa Tanzania kwenye mkutano huo utaongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe. Viongozi wengine kutoka Tanzania watakaoshiriki Mkutano huo ni pamoja na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenerali Venance Mabeyo, Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Mhe. Meja Jenerali (Mst) Gaudence Milanzi na Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Agnes Kayola.

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Venance Mabeyo akitoa taarifa fupi kwa Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ambaye pia ni Kiongozi wa Ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa Dharura wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Ministerial Committee of the Organ-MCO) ambao utahusisha pia Jamhuri ya Msumbiji na Nchi Zinazochangia Vikosi katika Misheni ya SADC iliyopo Msumbiji (SAMIM) unaofanyika Pretoria, Afrika Kusini tarehe 03 Aprili 2022.

Sehemu ya ujumbe wa Tanzania wakati wa kikao kati yao na kiongozi wa ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa Kamati ya Mawaziri wa SADC unaofanyika Pretoria, Afrika Kusini tarehe 03 Aprili 2022. Kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Agnes Kayola.

Kiongozi wa Ujumbe wa Tanzania, Dkt. Mnyepe (wa tatu kulia walioketi) akiwa na Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Mhe. Gaudence Milanzi (wa pili kulia walioketi) na wajumbe wengine wakimsikiliza Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Venance Mabeyo wakati akitoa taarifa kuhusu maandalizi ya Mkutano wa Dharura wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ambao utahusisha pia Jamhuri ya Msumbiji na Nchi Zinazochangia Vikosi katika Misheni ya SADC iliyopo Msumbiji (SAMIM) unaofanyika Pretoria, Afrika Kusini tarehe 03 Aprili 2022. 

Wajumbe wengine wa Tanzania wanaoshiriki Mkutano.

Friday, April 1, 2022

DIASPORA KUTOKA CANADA, TANROADS WAJADILI TEKNOLOJIA UJENZI WA BARABARA

Na Mwandishi wetu, Dar

Diapora kutoka nchini Canada, ambaye pia ni mwekezaji aliyeonesha nia ya kuwekeza katika miundombinu ya barabara nchini Bw. Joseph Katallah amekutana na uongozi wa Wakala wa Barabara Nchini (Tanroads) na kujadiliana nao kuhusu matumizi ya teknolojia mpya ya ujenzi wa barabara.

Bw. Katallah anashirikiana na Kampuni ya Geopolymer Solutions LLC ya Marekani inayomilikiwa na Bw. Rodney Zubrod ambayo imebuni teknolojia mpya ya ujenzi wa barabara  za lami na madaraja.

Akiongea katika kikao kilichofanyika leo Jijini Dar es Salaam, baina ya Geopolymer Solutions LLC na Tanroads Bw. Katallah amesema kuwa teknolojia hiyo hutumia mabaki ya uchafu wa migodini na viwandani hususan viwandani vinavyotengeneza alumina na vioo ni nzuri na hulinda mazingira.

“Tunashukuru kupata nafasi hii kuweza kupata nafasi ya kushirikiana na Tanroads katika majadiliano ya awali, mwitikio ni mkubwa na tunaendelea na majadiliano na tunaamini teknolojia hii itasaidia kupunguza gharama pamoja na kutunza mazingira,” amesema Bw. Katalla 

Kwa upande wa Kaimu Mtendaji Mkuu – Tanroads Mhandisi Nkolante Ntije amesema wamekuwa na kikao kizuri na wamesikiliza uwasilishaji wa Geopolymer Solutions LLC na kuona kuna uwezekano kutumia ‘material’ hiyo na kuiwezesha serikali kupata barabara nzuri na zilizojengwa kwa gharama nafuu.

“Serikali ina taratibu zake za kufanya utafiti kwa teknolojia yoyote mpya kabla ya kuanza kuitumia na baada ya utafiti na kujiridhisha kuwa teknolojia hiyo ni nzuri tunaamini tutakuwa tumepata jambo nzuri ambalo nchi yetu inaweza kuitumia teknolojia hiyo na kupunguza gharama katika ujenzi wa barabara kwa sababu miundombinu katika nchi yetu inahitajika sana,” amesema Mhandisi Ntije.

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kupitia idara ya Diaspora imeendelea kuwahamasisha Diaspora wengine wenye malengo ya kuwekeza katika sekta mbalimbali nchini na inawahakikishia ushirikiano katika hatua za kurasimisha uwekezaji.

Kaimu Mtendaji Mkuu – Tanroads Mhandisi Nkolante Ntije akiongea wakati wa kikao baina ya Geopolymer Solutions LLC na Tanroads Jijini Dar es Salaam na 

Kaimu Mkurugenzi Idara ya Diaspora katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Tagie Daisy Mwakawago akifafanua jambo wakati wa kikao kilichofanyika Jijini Dar es Salaam

Mwekezaji  kutoka nchini Canada, Bw. Joseph Katallah (katikati) akielezea juu ya teknolojia mpya ya Geopolymer na matumizi yake, kulia ni Rais na mmiliki wa Kampuni ya Geopolymer Solutions LLC ya nchini Marekani, Bw. Rodney Zubrod, kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Idara ya Diaspora katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Tagie Daisy Mwakawago

Rais na mmiliki wa Kampuni ya Geopolymer Solutions LLC ya nchini Marekani, Bw. Rodney Zubrod akiwasilisha matumizi ya teknolojia mpya ya Geopolymer kwa washiriki (hawapo pichani)

Rais na mmiliki wa Kampuni ya Geopolymer Solutions LLC ya nchini Marekani, Bw. Rodney Zubrod akiwasilisha matumizi ya teknolojia mpya ya Geopolymer

Kikao baina ya Kampuni ya Geopolymer Solutions LLC na Tanroads kikiendelea 


Watalii wengi zaidi kutoka Urusi Kutembelea Tanzania

Tanzania inatarajiwa kupokea watalii wengi zaidi siku za hivi karibuni kutoka nchini Urusi, kutokana na nchi hiyo kuwekewa vikwazo na Umoja wa Ulaya na Marekani. Hayo yamebainishwa katika mazungumzo yaliyofanyika baina ya Balozi wa Tanzania nchini humo, Mhe. Fredrick I. Kibuta na Mbunge kutoka Bunge la Shirikisho la Urusi, Mhe. Ammosov Petr Revaldovich ambaye ni mwakilishi wa Jimbo la Skha-Yakutia lililopo Kaskazini mwa Urusi.

“kutokana na vikwazo vilivyowekwa na Umoja wa Ulaya na Marekani dhidi ya Urusi, Watalii wengi raia wa Urusi wanatarajiwa kuja Afrika ikiwemo Tanzania na kwamba Tanzania iandae mazingira wezeshi ikiwemo kuzingatia suala la usalama wa watalii”, Mhe. Revaldovich alieleza.

Mhe. Revaldovich alisisitiza umuhimu wa Tanzania na Urusi kukuza uhusiano katika nyanja mbalimbali ikiwemo kuanzisha uhusiano wa kimiji (Sister City). Alitolea mfano wa Jimbo la Skha-Yakutia linaweza kuanzisha uhusiano na mkoa wa Arusha au Kilimanjaro ambayo ni mikoa ya Utalii kama ilivyo kwa jimbo hilo. Kiongozi huyo aliwakaribisha watalii raia wa Tanzania kutembelea jimbo lake la Sakha-Yakutia ambalo kwa miaka minne iliyopita imekuwa likipokea watalii wengi kutoka barani Afrika na nchi nyingine duniani. Watalii wanapenda kutembelea jimbo hilo kwa ajili ya kuogelea kwenye maji yenye nyuzi joto hasi sitini na moja (-61 nyuzi joto).

Kwa upande wake, Mhe. Kibuta aliihakikishia Urusi kuwa Tanzania ipo tayari kupokea watalii kutoka nchi hiyo na kwamba hali ya hewa ni nzuri na usalama kwa watalii upo. Aliongeza kuwa, licha ya kuwepo kwa miundombinu ya kuridhisha ya utalii nchini, Serikali inaendelea kuwekeza na kuboresha kwenye miundombinu hiyo. 

Balozi wa Tanzania nchini Urusi, Mhe. Fredrick I. Kibuta (kulia) na Mbunge kutoka Bunge la Shirikisho la Urusi, Mhe. Ammosov Petr Revaldovich ambaye ni mwakilishi wa Jimbo la Skha-Yakutia lililopo Kaskazini mwa Urusi wakikabidhiana kitabu kuhusu mbinu za kuzalisha asali.