Saturday, July 23, 2022

WAZIRI MULAMULA AKUTANA NA MKURUGENZI MTENDAJI WA UNON

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula amekutana kwa mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa Nairobi (UNON), Bi. Zainab Hawa Bangura katika Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki tarehe 23 Julai 2022 jijini Arusha. 

Viongozi hao wamejadili juu ya kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Ofisi ya Umoja wa Mataifa Nairobi katika masuala ya upatikanaji wa fursa za ajira, kuwajengea uwezo wananchi katika maeneo mbalimbali ya utendaji, kukuza lugha ya kiswahili kupitia kitengo cha lugha cha ofisi hiyo na ushirikiano katika masuala ya biashara na ugavi.

Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda kutika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi Ellen Maduhu akifuatilia mazungumzo kati ya Mhe. Mulamula na Bi. Bangura (hawapo pichani). 

Maafisa walioambatana na viongozi hao wakifuatilia mazungumzo.

Sehemu nyingine ya maafisa wakifuatilia mazungumzo.

Mazungumzo yakiendelea.

Mhe. Balozi Liberata Mulamula pamoja na Bi. Bangura wakiwa katika picha ya pamoja na ujumbe walioambatana nao katika mazungumzo yao.

Mhe. Balozi Liberata Mulamula pamoja na Bi. Bangura wakiagana baada ya mazungumzo.



 

RAIS NDAYISHIMYE AKABIDHIWA UENYEKITI WA EAC

Rais wa Jamhuri ya Burundi, Mhe. Jen. Evariste Ndayishimye amekabidhiwa nafasi ya Uenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Mwenyekiti aliyemaliza muda wake Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Uhuru Kenyatta wakati wa Mkutano wa 22 wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki uliomalizika tarehe 22 Julai 2022.

 

Akikabidhi nafasi hiyo Mhe. Kenyatta aliwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya jumuiya hiyo wakati wa uongozi wake ambapo alieleza kwamba Jumuiya imefanikiwa kukamilisha mchakato wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kuwa mwanachama, Kuondolewa kwa vikwazo vya kibiashara 13 kati ya 22 vilivyokuwepo awali, kutafuta ufumbuzi wa pamoja katika changamoto za Covid–19 na kuanzisha mchakato utakaowezesha nchi wanachama kupata chanjo ya Covax.

 

Masuala mengine ya utekelezaji ni; Kuhakikisha Burundi inafanikiwa kushiriki katika Shirikisho la Afrika Mashariki, kusimamia ushiriki wa asasi za kiraia na ushiriki wa sekta binafsi katika utekelezaji wa majukumu ya kikanda.

 

Naye Rais wa Burundi, Mhe. Jen. Ndayishimye baada ya kupokea majukumu hayo ya nafasi ya Mwenyekiti, alimshukuru Mhe. Kenyatta kwa uongozi bora na kwa mafanikio yaliyopatikana katika uongozi wake.

 

Aidha, akazishukuru nchi wanachama wa Jumuiya hiyo kwa kuiamini Burundi kuongoza, na akaeleza uelekeo wa utekelezaji wa majukumu katika kipindi chake cha uongozi utazingatia masuala yafuatayo; Kukuza mtangamano wa Afrika Mashariki na kuimarisha ujirani mwema; kuharakisha mkakati wa viwanda katika Jumuiya; Kuzingatia ombi la Jamhuri ya Shirikisho la Somalia kujiunga na Jumuiya hiyo na Usimamizi wa agenda ya amani na usalama ili kuondoa migogoro.

Masuala mengine yatakayosimamiwa ni pamoja na; Kuimarisha mfumo wa mageuzi ya kitaasisi, Kuendelea kusisitiza umuhimu wa maridhiano ya kitaifa ili kuweza kuyafikia maridhiano ya kisiasa katika ngazi ya jumuiya, Ushirikishwaji wa Wanawake na Vijana; na Wake za viongozi kushirikishwa katika utekelezaji wa malengo ya jumuiya.

 

Naye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia katika mkutano huo alimuaga Mhe. Kenyatta kwakuwa anaelekea kipindi cha mwisho cha uongozi wake nchini Kenya  kuitakia nchi hiyo uchaguzi mkuu mwema unaotarajiwa kufanyika mwezi Agosti 2022.

 

Pamoja na mambo mengine mkutano huo umemchagua Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Uhuru Kenyatta kuwa msimamizi wa mazungumzo ya amani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC); umefanya uapisho wa majaji wa Mahakama ya Afrika Mashariki ambao ni; Mhe. Jaji Leonard Gacuko kutoka Burundi na Mhe. Jaji Cheborion Barishaki kutoka Uganda.

 

Pia mkutano huo ulikabidhi zawadi kwa wanafunzi wa sekondari walioshinda katika nafasi mbalimbali kwenye mashindano ya uandishi wa insha kwa lugha ya Kiswahili, kiingereza na kifaransa. Walishiriki hao ni wale ambao walishiriki mashindano hayo kuanzia mwaka 2019 hadi 2021 lakini hawakukabidhiwa zawadi kufuatia kutoitishwa kwa mikutano ya Wakuu wa Nchi ya ana kwa ana kutokana na changamoto ya maambukizi yaCovid-19.

===========================================


Rais wa Jamhuri ya Kenya na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki aliyemaliza muda wake wa uongozi, Mhe. Uhuru Kenyatta akikabidhi vitendea kazi kwa Mwenyekiti mpya wa Jumuiya hiyo Rais wa Jamhuri ya Burundi, Mhe. Evariste Ndayishimye. Makabidhiano hayo yamefanyika wakati wa Mkutano wa 22 wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika tarehe 22 Julai jijini Arusha.

Rais wa Jamhuri ya Kenya na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki aliyemaliza muda wake wa uongozi, Mhe. Uhuru Kenyatta akimpongeza Mwenyekiti mpya wa Jumuiya hiyo Rais wa Jamhuri ya Burundi, Mhe. Evariste Ndayishimye kwa kuaminiwa kushika nafasi hiyo. Anayeshuhudia ni Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dkt. Peter Mathuki.


Rais wa Jamhuri ya Burundi na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhe. Evariste Ndayishimye akiongoza Mkutano wa 22 wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki baada ya kukamilika kwa makabidhiano ya nafasi hiyo ya Mwenyekiti.

Friday, July 22, 2022

BARABARA YA KIKANDA YA ARUSHA BYPASS CHACHU YA MAENDELEO YA KIUCHUMI KWA NCHI ZA EAC

Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wamesisitiza umuhimu wa kujenga miundombinu bora na ya kisasa ili kuweza kuyafikia malengo ya pamoja ya maendeleo ya kiuchumi katika jumuiya.

 

Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika mashariki aliyemaliza muda wake, Mhe. Uhuru Kenyatta wakati wa hafla ya ufunguzi wa barabara ya kikanda ya Arusha Bypass uliofanyika leo tarehe 22 Julai jijini Arusha na kuhudhuriwa na nchi zote wanachana pamoja na mgeni mwalikwa Serikali ya Shirikisho la Somalia.

 

Pia akafafanua kuwa barabara hiyo pamoja na mambo mengine itasaidia kupunguza msongamano wa magari, itaongeza mawasiliano na muingiliano wa kijamii, itakuza biashara, itarahisisha usafiri wa mizigo na kupunguza umasikini kwa nchi wanachama na kujiletea heshima duniani.

 

Naye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyeji wa mkutano huo, Mhe. Samia Suluhu Hassan katika hotuba yake ameeleza kuwa barabara iliyozinduliwa ina urefu wa kilomita 42.4 na imegharimu kiasi cha shilingi Billioni 197.4 na kwamba imejengwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Kenya.

 

Vilevile, ameishukuru Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA) na Washirika wa Maendeleo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki “East Africa Trademark” kwa kuendelea kutoa uwezeshaji wa kifedha kukamilisha kwa awamu ya kwanza ya mradi huo na kukubali kuendelea kuwezesha awamu ya pili ya mradi wa barabara inayoanzia Arusha, Horiri, Taveta, Voi yenye urefu wa kilomita 117.

 

Kadhalika, Mhe. Rais Samia ametoa rai kwa wananchi kutumia fursa za miundombinu katika kukuza sekta za utalii, biashara, uwekezaji, usafirishaji wa mizigo na akawataka wananchi kutunza miundombinu iliyopo kuiwezesha serikali kuendelea na ujenzi wa miundombinu katika maeneo mengine kama vile uimarishaji wa miundombinu ya reli, bandari na usafiri wa anga.

 

Maboresho hayo ya miundombinu yatawezesha kuiunganisha Afrika Mashariki na nchi nyingine za Afrika na kulitumia vema soko la eneo huru la biashara la Afrika.

========================================


Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki wakikata utepe kuashiria ufunguzi wa barabara ya EAC Arusha Bypass uliofanyika eneo la Kisongo nje kidogo ya jiji la Arusha tarehe 22 Julai 2022.

Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki wakiwa wamesimama wakati ulipopigwa wimbo wa Taifa na wa Jumuiya ya Afrika Mashariki baada ya kuwasili kwenye hafla ya uzinduzi wa barabara ya EAC Arusha Bypass.

Rais wa Jamhuri ya Muungano, Mhe. Samia Suluhu Hassan (mwenye mask nyeupe) akiwasili eneo la Kisongo nje kidogo ya mji wa Arusha kwenye hafla ya ufunguzi wa barabara ya EAC Arusha Bypass. Kulia kwake ni Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dkt. Peter Mathuki akimuongoza Mhe. Rais Samia jukwaani.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula akiwasili katika eneo la Kisongo nje kidogo ya mji wa Arusha kushiriki hafla ya ufunguzi wa Barabara ya EAC Arusha Bypass.

WAKUU WA NCHI ZA EAC WASISITIZA UMUHIMU WA SOKO LA PAMOJA KATIKA KUKUZA UCHUMI WA KIKANDA

 Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wamesisitiza umuhimu wa soko la pamoja katika kukuza uchumi wakati waliposhiriki Mkutano Maalum wa Ngazi ya Juu wa Soko la Pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki.

 

Mkutano huo maalum wa ngazi ya Wakuu wa Nchi uliofanyika tarehe 21 Julai 2022 na mkutano maalum wa ngazi ya Mawaziri uliofanyika tarehe 20 Julai 2022 jijini Arusha ni sehemu ya mikutano ya awali kuelekea Mkutano wa 22 wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki utakaofanyika tarehe 22 Julai 2022.

 

Katika mkutano huo Wakuu wa Nchi walijadili na kuyawekea msisitizo masuala mbalimbali ya hali ya halisi ya utekelezaji wa Itifaki ya Soko la Pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki sambamba na kuainisha changamoto zinazohitaji ufumbuzi wa pamoja katika kuyafikia malengo ya jumuiya hiyo.

 

Akichangia mada wakati wa mkutano huo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ambaye pia ni mwenyeji wa mkutano huo, amesisitiza juu ya kukuza uzalishaji pamoja na  kuongeza thamani ya mazao na bidhaa  zinazozalishwa ndani ya jumuiya ili kuweza kuingia katika ushindani wa kibiashara kimataifa.

 

Aidha, aliongeza kufafanua kuwa katika kuyafikia malengo ya pamoja ni muhimu kwa nchi wanachama kuwekeza katika amani na utawala bora ili nchi ziweze kuongeza nguvu katika usimamizi wa rasilimali na uzalishaji badala ya kuwekeza katika migogoro.

 

Naye Mwenyekiti wa mkutano huo na Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Uhuru Kenyatta amesisitiza umuhimu wa kuwa na mawasiliano kupitia ujenzi wa miundombinu ambao ndio msingi mkuu wa kuyafikia malengo ya soko la pamoja.

 

Vilevile akaeleza kwa sasa nchi wanachama zimeunganishwa kupitia ujenzi wa miundombinu ya kisasa na akatolea mfano ujenzi wa reli ya kisasa unaofanywa na Tanzania ambao utaziunganisha nchi wanachama na kwamba kwa upande mwingine Tanzania na Kenya zinaunganishwa kupitia ujenzi wa miundombinu uliofanywa mipakani katika eneo la Namanga na Taveta.

 

Maeneo mengine yaliyojadiliwa ni pamoja na fursa za kiuchumi zilizoongezeka kufuatia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kujiunga na jumuiya hiyo, umuhimu wa usimamizi wa rasilimali kama vile madini na umuhimu wa ushiriki wa sekta binafsi katika kuyafikia malengo yaliyowekwa.

 

Kadhalika, mkutano huo ulijadili mafanikio yaliyofikiwa na jumuiya hiyo ikiwemo, uhuru wa kufanya biashara, mtangamano wa kijamii na fursa za kuvuka mipaka kupitia Hati ya kusafiria ya kielektroni ya Afrika Mashariki na kuondoleana visa miongozi mwa nchi wanachama.

 

Mkutano huo umehudhuriwa na Nchi zote saba wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambao ni pamoja mwenyekiti wa mkutano huo Jamhuri ya Kenya; Mwenyeji wa mkutano huo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Jamhuri ya Uganda; Jamhuri ya Burundi, Jamhuri ya Rwanda, Jamhuri ya Sudan Kusini, na Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo. Pia ulihudhuriwa na Jamhuri ya Shirikisho la Somalia ambaye alikuwa mgeni mwalikwa katika mkutano huo.


==========================================================



Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula akiwatambulisha viongozi mbalimbali wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Uhuru Kenyatta baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Arusha tarehe 21 Julai 2022.
Mhe. Kenyatta yupo nchini kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa 22 wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki utakaofanyika tarehe 22 Julai 2022.

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine aliposhiriki Mkutano Maalum wa Ngazi ya Juu wa Soko la Pamoja la Afrika Mashariki uliofanyika tarehe 21 Julai 2022 jijini Arusha.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dkt. Peter Mathuki akimkaribisha Waziri anayeshughulikia masuala ya Rais wa Jamhuri ya Sudan Kusini, Mhe. Barnaba Marial Benjamin mara baada ya kuwasili katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha kushiriki Mkutano Maalum wa Ngazi ya Juu wa Soko la Pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika tarehe 21 Julai 2022 jijini Arusha.
Mhe. Benjamin anamwakilisha Rais wa Jamhuri ya Sudan Kusini, Mhe. Salva Kiir katika mkutano huo pamoja na Mkutano wa 22 wa Wakuu wa Nchi wa EAC .



Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mwigulu Nchemba akifafanua kwa wananchi juu ya umuhimu wa soko la pamoja na fursa zake kwa taifa na wanachi wa Tanzania kwa ujumla kupitia kituo cha Luninga cha TBC1 .

Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji akifafanua juu ya fursa za biashara na uwekezaji zinazopatikana katika Soko la Pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa wananchi kupitia kituo cha Luninga cha TBC1.

Sehemu ya wajumbe wa mkutano huo wakifatilia majadiliano ya Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika.
Wapili kushoto ni Mkurugenzi Idara ya Siasa, Ulinzi na Usalama katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Stephen Mbundi akifuatilia Mkutano Maalum wa Ngazi ya Juu wa Soko la Pamoja la Afrika Mashariki uliofanyika tarehe 21 Julai 2022 jijini Arusha.

Thursday, July 21, 2022

VACANCY ANNOUNCEMENT


 

KATIBU MKUU BALOZI SOKOINE AKUTANA NA MABALOZI PUNDE BAADA YA KUAPISHWA


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine (katikati) Mhe. Balozi Dkt. Suleiman Haji Suleiman (kulia) na Mhe. Luteni Jenerali Mathew Edward Mkingule Balozi wa Tanzania nchini Zambia (kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja 

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine tarehe 20/07/2022 alikutana na kufanya mazungumzo na Mhe. Balozi Dkt. Suleiman Haji Suleiman na Mhe. Luteni Jenerali Mathew Edward Mkingule Balozi wa Tanzania nchini Zambia katika ofisi za Wizara jijini Dodoma.

Balozi Sokoine katika mazungumzo hayo yaliyofanyika muda mfupi baada ya viongozi hao kuapa kutumikia nyadhifa hizo katika hafla iliyofanyika Ikulu jijini Dodoma alisisitiza kuwa pamoja na kukuza uhusiano wa kidiplomasia ni muhimu pia kuendelea kuongeza jitihada katika kutekeleza sera ya diplomasia ya uchumi kwenye vituo vyao vya uwakilishi. 

Aidha Katibu Mkuu Balozi Joseph Sokoine amewapongeza Waheshimiwa Mabalozi kwa kuteuliwa katika nafasi hizo na amewatakia kheri katika utekelezaji wa majukumu yao. 
Mazungumzo yakiendelea

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine (kulia) Mhe. Balozi Dkt. Suleiman Haji Suleiman (kushoto) na Mhe. Luteni Jenerali Mathew Edward Mkingule Balozi wa Tanzania nchini Zambia (katikati) wakiwa kwenye mazungumzo yaliyofanyika katika ofisi za Wizara jijini Dodoma

BALOZI MUSHY ATAFUTA FURSA NCHINI AUSTRIA


Balozi wa Tanzania nchini Austria, Mhe. Celestine J. Mushy  (katikati) akutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo la Austria (Austrian Development Agency - ADA), Mhe. Balozi Friedrich Stift (kushoto) na Mkurugenzi wa  Idara ya Programme na Miradi ya Kimataifa, Bw. Heinz Habertheuer.  Viongozi hao walizungumzia masuala ya namna ya kuisaidia na kuiingiza Tanzania  kwenye  kundi la nchi zinazopewa kipaumbele kwa miradi inayofadhiliwa na Shirika hilo.   Vilevile, Mkurugenzi alieleza kuwa wanakamilisha mpango wa kuongezea mtaji wa Kampuni ya BioTan Group Ltd ya mwekezaji wa Austria inayozalisha na kubangua Korosho bila matumizi ya  kemikali (organic cashewnut).






 


Wednesday, July 20, 2022

MKUTANO WA KAMATI YA MAWAZIRI WANAOSHUGHULIKIA URATIBU NA UDHIBITI WA MAAFA WAFANYIKA MALAWI

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Sera, Bunge na Uratibu, Mhe. George Simbachawene (Mb.), ameongoza ujumbe wa wa Tanzania kwenye Mkutano wa Kamati ya Mawaziri wanaoshughulika na Uratibu na Udhibiti wa Maafa kwa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika tarehe 19 Julai, 2022, Lilongwe, Malawi.


Mkutano huu pamoja na masuala mengine, ulijadili agenda kuhusu Uendeshaji wa Kituo cha Operesheni za Dharura na huduma za Kibinadamu cha SADC na kuhimiza Nchi Wanachama kukamilisha michakato ya ajira za kushikiza ili Kituo hicho kiweze kupata watumishi wa kutosha ili kukiwezesha kutekeleza majukumu yake kikamilifu.

Akichangia hoja katika agenda hii, Mhe. Simbachawene aliipongeza Sekretarieti ya SADC kwa jitihada mbalimbali zinazotekelezwa na pia alishauri kuwa Sekretarieti ya SADC iangalie njia mbalimbali za kushirikiana na wadau wa maendeleo katika kuimarisha utendaji kazi wa Kituo hicho.

Mkutano huu wa Mawaziri ulitanguliwa na Kikao cha Makatibu Wakuu wa Kamati ya Mawaziri wanaoshughulikia masuala ya Uratibu na Uthibiti wa Maafa, kilichofanyika tarehe 17 Julai 2022. Meja Jenerali Michael  Mumanga, Mkurugenzi wa Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu - Idara ya Maafa, aliongoza ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Kikao hicho. Pamoja nae aliambatana na Afisa Mwandamizi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Maafa, Afisa Mwandamizi kutoka Kurugenzi ya Hali ya Hewa na Afisa Mambo ya Nje kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. 



Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Sera, Bunge na Uratibu, Mhe. George Simbachawene (wa pili kushoto), ameongoza ujumbe wa wa Tanzania kwenye Mkutano wa Kamati ya Mawaziri wanaoshughulika na Uratibu na Udhibiti wa Maafa kwa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika tarehe 19 Julai, 2022, Lilongwe, Malawi. Pichani Mhe. Simbachawene akiwa katik apicha ya pamoja na Wajumbe kutoka Nchi za SADC walioshiriki mkutano huo.

Picha ya pamoja

 

WAZIRI MULAMULA AONGOZA UJUMBE WA TANZANIA MKUTANO WA 24 WA KAMATI YA MAWAZIRI WA SADC

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Liberata Mulamula ameongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa 24 wa Kawaida wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Ushirikiano katika masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (MCO) uliofanyika jijini Pretoria, Afrika Kusini kuanzia tarehe 16 hadi 19 Julai, 2022. 

 

Mkutano huo ambao ulitanguliwa na Mkutano wa Makatibu Wakuu pamoja na mambo mengine umepokea na kujadili agenda mbalimbali zilizowasilishwa kwao ikiwemo Mapitio ya Utekelezaji wa Maamuzi ya Mkutano wa 23 wa MCO na Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC; Hali ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Kanda; na Tathmini ya Hali ya Ulinzi na Usalama katika Kanda.

 

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano huo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye pia ni Waziri wa Uhusiano wa Kimataifa na Ushirikiano wa Afrika Kusini, Mhe. Dkt. Naledi Pandor amesema hali ya usalama katika kanda kwa ujumla inaridhisha na kwamba Nchi Wanachama wa SADC ziendelee kujitolea katika masuala ya ulinzi na usalama kwa maslahi mapana ya wananchi wa nchi hizo.

 

Kadhalika amesisitiza nchi wanachama kuendelea kupambana na ugaidi na vitendo vyote vya kigaidi katika Kanda huku akipongeza  Misheni ya SADC nchini Msumbiji (SAMIM) kwa kazi nzuri wanayoendelea kuifanya nchini humo ambapo wamefanikiwa kurejesha hali ya amani na usalama katika Jimbo la Cabo Delgado. 

 

Kuhusu utekelezaji wa maazimio yatokanayo na Mkutano wa 23 wa Kamati hiyo ya Mawaziri, Mhe. Dkt. Pandor amezipongeza Nchi Wanachama  na Sekretarieti ya SADC kwa kutekeleza maazimio hayo kwa takriban asilimia 81. 

 

“Utekelezaji huu bila shaka unadhihirisha dhamira ya dhati iliyopo miongoni mwetu ya kuhakikisha tunafikia lengo la kuimarisha amani na utulivu katika kanda”, alisema Mhe. Pandor.

 

Akizungumzia masuala ya demokrasia katika nchi wanachama, Mhe. Pandor amesisitiza nchi wanachama kuendelea kuendesha chaguzi zake kwa kufuata miongozo ya kidemokrasia ya SADC na ile ya nchi husika ili chaguzi hizo zikamilike kwa amani na utulivu.

 

“Katika kujenga amani na utulivu katika kanda, SADC itaendelea kuzingatia misingi ya demokrasia ili kuzuia migogogoro kwa maslahi mapana ya wananchi katika kanda. Kwa kuzingatia misingi hiyo SADC kama kanda itaendelea kuendesha chaguzi kwa kufuata misingi ya demokrasia, uwazi, amani na ukweli. Serikali za Angola na Lesotho zitakuwa na uchaguzi mkuu mwezi Agosti na Oktoba mwaka huu mtawalia. Tunawatakia wanachama wenzetu uchaguzi wa amani” alisisitiza Mhe. Pandor.



Awali akizungumza, Katibu Mtendaji wa SADC, Bw. Elias Magosi amesema kuwa Sekretarieti ya SADC itaendelea kushirikiana na Nchi Wanachama hususan katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zilizopo katika kanda zikiwemo za kiusalama, kijamii na kiuchumi.

 

Pia alimpongeza Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri anayemaliza muda wake Mhe. Pandor kwa kazi nzuri aliyofanya katika kipindi chote na kumkaribisha Mwenyekiti mpya ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Namibia na kumwahidi ushirikiano.

 

Mbali na Mhe. Balozi Mulamula, Ujumbe wa Tanzania ulimjumuisha pia Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stergomena Tax, Mwakilishi wa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Mnadhimu Mkuu wa Jeshi, Lt. Jenerali Salum Othman, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Kuzuia na  Kupambana na Rushwa,  Kamishna wa Polisi Salum  Hamduni, Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Mhe. Meja Jenerali Mstaafu Gaudence Milanzi, Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Agnes Kayola.Kupambana na Rushwa,  Kamishna wa Polisi Salum  Hamduni na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kasiga.

 

Waziri wa Mambo ya Nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula akiongoza ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa 24 wa Kawaida wa Kamati ya Mawazirii wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-MCO) uliofanyika Pretoria, Afrika Kusini tarehe 19 Julai 2022. Mkutano huo umemjumuisha pia Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stergomena Tax, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na  Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma M. Rajab, Mwakilishi wa Mkuu wa Majeshi na Mnadhimu Mkuu wa Jeshi, Mhe. Lt. Jenerali Salum Othman na Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Mhe. Meja Jenerali Mstaafu Gaudence Milanzi

 Mhe. Balozi Mulamula na Mhe. Dkt. Tax wakiwa wamesimama kwa heshima kutekeelza itifaki za ufunguzi wa mkutano ikiwemo kupigwa wimbo wa Taifa la Afrika Kusini na ule wa SADC
Mhe. Dkt. Tax akiwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma M. Rajab wakatib wa Mkutano wa 24 wa Kamati ya Mawaziri wa SADC
 

Mwakilishi wa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Mnadhimu Mkuu wa Jeshi, Mhe. Lt. Jenerali Salum Othman (kulia) akiwa na Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Mhe. Meja Jenerali Mstaafu Gaudence Milanzi kwenye Mkutano wa 24 wa Kamati ya Mawaziri wa SADC

Mkutano ukiendelea