Tuesday, October 25, 2022

TANZANIA YAIKUMBUSHA JUMUIYA YA KIMATAIFA KUISADIA AFRIKA KUKABILIANA NA MABADILIKO YA TABIANCHI

Tanzania imeikumbusha Jumuiya ya Kimataifa kutekeleza ahadi  yake ya  kuzisaidia kiuchumi nchi za Afrika ili kuziwezesha kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazotokana na mabadiliko ya Tabianchini kama makubaliano ya  Mkataba wa Paris  yanavyoelekeza.


Wito huo umetolewa na  Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro wakati akihutubia maadhimisho ya miaka 77 ya Umoja yaliyofanyika jijini Dar es Salaam leo tarehe 24 Oktoba 2022.



Amesema  Mkataba huo unaitaka Jumuiya ya Kimataifa  kuzisaidia nchi za Afrika katika maeneo mbalimbali ikiwemo kujenga uwezo, kubadilishana  teknolojia na kuhakikisha nchi hizo  kiuchumi ili kuziwezesha kujitegemea katika kukabiliana na athari zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi.



“Wiki mbili zijazo kuanzia leo, Mkutano wa 27 wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi utafanyika Sharm El Sheikh, Misri. Ni kwa muktadha huo tunahitaji kuikumbusha Jumuiya ya Kimataifa kwamba pamoja na mchango mdogo wa Afrika katika ongezeko la joto duniani, bado Afrika ni Bara linaloathirika zaidi na mabadiliko hayo kutokana na uwezo mdogo wa kukabiliana na changamoto hizo. Hivyo, tunaikumbusha Jumuiya ya Kimataifa kutimiza ahadi kulingana na maelekezo katika  Mkataba wa Paris,’’ amesema Mhe. Dkt. Ndumbaro.



Aidha,  Mhe. Dkt. Ndumbaro amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na Jumuiya ya Kimataifa katika kutekeleza program mbalimbali za maendeleo nchini ikiwa ni pamoja na Malengo ya Maendeleo Endelevu kwa manufaa ya wananchi.



Mhe. Dkt. Ndumbaro amesema, Tanzania inapoungana na ulimwengu mzima kuadhimisha miaka 77 ya Umoja wa Mataifa ni kielelezo kinachowakumbusha wadau wote nchini kujiimarisha katika ushirikiano ili kuiwezesha Tanzania kutekeleza pamoja na mambo mengine Mpango wake wa Maendeleo wa Miaka Mitano; Malengo ya Maendeleo Endelevu na Mpango wa Tatu wa Umoja wa Mataifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano.



Amesema kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu inayosema “Maendeleo Yanayozingatia Ujumuishwaji wa Makundi yote” imebeba ujumbe mzito unaomkumbusha kila mmoja kuungana na kutafuta suluhu kwa changamoto mbalimbali zinazoikabili dunia pasipo kumwacha mtu yoyote nyuma.



Pia amesema Tanzania ipo kwenye hatua za mapitio ya utekelezwaji  wa Malengo ya Maendeleo Endelevu na kuwataka wadau mbalimbali kushirikiana nayo ili kufanikisha mapitio hayo.


Vilevile, wakati wa maadhimisho hayo,  Mhe. Dkt. Ndumbaro ameuomba Umoja wa Mataifa kuitambua Lugha ya Kiswahili kama Lugha rasmi ya Umoja huo.



“Tunapoadhimisha miaka 77 ya Umoja wa Mataifa, Tanzania inaikumbusha dunia kuwa wakati umefika sasa wa kuridhia Kiswahili kuwa miongoni mwa Lugha rasmi za Umoja huo” alisema Dkt. Ndumbaro.



Kwa upande wake, Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Kimataifa nchini, Bw. Zlatan Milisic ameipongeza Tanzania kwa kuendelea kuhifadhi wakimbizi na kwamba Umoja wa Mataifa na Taasisi zake utaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuwaletea wananchi maendeleo.



Amesema Umoja huo unachangia katika miradi mbalimbali ya  kuwainua kiuchumi wanawake na vijana walio katika mazingira magumu ikiwemo kuchangia katika uunzishwaji wa madawati ya jinsia yaliyo chini ya Jeshi la Polisi ambapo kwa mwaka huu madawati 400 yameanzishwa nchini kote.



Wakati wa maadhimisho hayo, Mhe. Dkt. Ndumbaro alipata fursa ya kuzindua Tovuti ya Kwanza ya Umoja wa Mataifa inayochapisha maudhui yake kwa Lugha ya Kiswahili.



Maadhimisho hayo ya aina yake yamehudhuriwa na Viongozi na wadau mbalimbali wakiwemo Mhe. Tabia Mwita, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Zanzibar, Mhe. Lela Muhammed Mussa, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Zanzibar, Mabalozi na Wakuu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa yaliyopo nchini.

Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro akihutubia wakati wa maadhimisho ya Miaka 77 ya Umoja wa Mataifa. aadhimisho hayo ambayo yalibeba kaulimbiu isemayo "Maendeleo yanayozingatia Ujumuishwaji wa Makundi Yote" yamefanyika kwenye Viwanja vya Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam hivi karibuni
Mhe. Dkt. Ndumbaro akiwa na Viongozi wengine walioshiriki maadhimisho ya miaka 77 ya Umoja wa Mataifa. Wa kwanza kulia ni Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Robert Kahendaguza na wa tatu kulia ni Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini, Mhe. Bw. Zlatan Millisic
Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini, Mhe. Zlatan Milisic akizungumza wakati wa maadhimisho ya miaka 77 ya Umoja wa Mataifa
Mhe. Dkt. Ndumbaro akifuatilia Wimbo wa Taifa wakati wa maadhimisho ya miaka 77 ya Umoja wa Mataifa
Mhe. Dkt. Ndumbaro akikagua gwaride la heshima liloandaliwa maalum kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 77 ya Umoja wa Mataifa
Mhe. Dkt. Ndumbaro akishuhudiwa tukio maalum la upandishaji wa Bendera ya Umoja wa Mataifa kama ishara ya kuadhimisha miaka 77 ya Umoja huo

Mkurugenzi Msaidizi katika Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa ambaye pia alikuwa Mshereheshaji wa maadhimisho ya miaka 77 ya Umoja wa Mataifa , Bi. Ellen Maduhu akitoa mwongozo wa maadhimisho hayo kwa washiriki
Wanafunzi kutoka Shule ya Sekondari ya Kibasila ya jijini Dar es Salaam wakitoa burudani na elimu kuhusu historia ya Umoja wa Mataifa kupitia sanaa ya uimbaji
Mhe. Dkt. Ndumbaro akizindua rasmi Tovuti ya Umoja wa Mataifa inayochapisha maudhui yake kwa Lugha ya Kiswahili
Picha ya pamoja




 

TANZANIA YAJIDHATITI KUSHIRIKIANA NA WADAU KUKUZA UCHUMI



 

Monday, October 24, 2022

RAIS TSHISEKEDI AMALIZA ZIARA YA KITAIFA NCHINI

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Mhe. Felix Tshisekedi amemaliza ziara ya Kitaifa ya siku mbili aliyoifanya nchini tarehe 23 na 24 Oktoba, 2022. 

Rais. Tshisekedi ameagwa na mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam. 

Mapema kabla ya kuondoka, Mhe. Rais Tshisekedi ametembelea mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) Jijini Dar es Salaam na kujionea hatua mradi huo ulipofikia. 

Rais Tshisekedi alipotembelea mradi wa ujenzi wa SGR, aliambatana na Waziri wa Maambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax pamoja na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Prof. Makame Mbarawa.

Juni 14, 2019 Rais Tshisekedi kwa mara ya kwanza alifanya ziara ya siku mbili nchini Tanzania.

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Mhe. Felix Tshisekedi akimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania - (TRC), Bw. Masanja Kadogosa wakati Rais Tshisekedi alipofanya ziara katika mradi wa ujenzi wa SGR Jijini Dar es Salaam. Mhe. Tshisekedi ameambatana na Waziri wa Maambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax pamoja na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Prof. Makame Mbarawa. 


Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Mhe. Felix Tshisekedi akimuuliza jambo Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania - (TRC), Bw. Masanja Kadogosa wakati Rais Tshisekedi alipofanya ziara katika mradi wa ujenzi wa SGR Jijini Dar es Salaam

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na Mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Kongo, Mhe. Felix Tshisekedi wakiwa katika jukwaa la salamu za heshima za kijeshi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es salaam kabla ya Rais Tshisekedi kuondoka nchini baada ya kumaliza ziara yake

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Mhe. Felix Tshisekedi akiagana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es salaam baada ya kumaliza ziara yake nchini

Rais wa Jamhuri ya KIdemokrasia ya Kongo, Mhe. Felix Tshisekedi akimuaga Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es salaam baada ya kumaliza ziara yake nchini

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan pamoja na viongozi waandamizi wa serikali wakimuaga Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Mhe. Félix Tshisekedi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam baada ya kuhitimisha ziara yake nchini





Sunday, October 23, 2022

TANZANIA, DRC ZAKUBALIANA KUIMARISHA BIASHARA NA UCHUMI

Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Samia Suluhu Hassan inaedelea kuudhirihishia ulimwengu kuwa imedhamiria kushirikiana na wadau wote, zikiwemo nchi jirani ili kuleta manufaa ya kiuchumi na kijamii kwa pande zote.

Ziara ya Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) nchini, Mhe. Felix Tshisekedi ambayo ni mwendelezo wa ziara kadhaa za viongozi wa kitaifa na mashirika ya kimataifa nchini ni kielelezo cha wazi cha kutambua nguvu ya ushirikiano katika kukuza uchumi wa nchi na dunia kwa ujumla.

Rais Samia na mgeni wake, Rais Tshiseked katika mazungumzo yao yaliyofanyika Ikulu Jijini Dar Es Salaam tarehe 23 Oktoba 2022, waliafikiana nchi zao ziongeze nguvu kuimarisha ushirikiano katika sekta za kiuchumi, miundombinu, biashara, usafirishaji, uwekezaji, ulinzi, usalama na mawasiliano.

Rais Samia aliwaambia waandishi wa habari kuwa wamekubaliana kuondoa vikwazo vyote visivyo vya kibishara ili kukuza biashara na kwamba mawaziri wa biashara wa pande zote mbili wameagizwa  kulifanyia kazi suala hilo haraka iwezekanavyo. 

"Ikumbukwe DRC ni mwanachama mpya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na katika mikakati ya kuendeleleza miundombinu ya Jumuiya hiyo, kuna mpango wa kujenga ushoroba wa kati utakaounganisha Tanzania na DRC ili kukuza biashara na mtangamano baina ya nchi wanachama', alisema Rais Samia.

Kwa upande wake, Rais Tshisekedi alisisitiza umuhimu wa kuimarisha usalama kwa sababu bila ya amani na usalama hakuna miradi itakayoweza kutekelezwa

“Sisi kwetu DRC usalama ni muhimu sana na ndiyo maana mimi kama Rais nimeweka mkazo wa kujenga na kuimarisha uhusiano wa kindugu na majirani zetu,” alisema Rais Tshisekedi.

Rais Samia na mgeni wake walishuhudia uwekaji saini wa Mkataba wa Teknolojia ya Habari na Posta uliosainiwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye na Waziri wa Mambo ya Nje wa DRC, Mhe. Christophe Lutundula.

Uwekaji saini wa mkataba huo umekuja muda mfupi baada ya nchi hizo pia kusaini Hati ya Makubaliano ya kushirikiana katika masuala ya ulinzi na usalama wakati wa Mkutano wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya nchi hizo uliofanyika Jijini Dar Es Salaam mwezi Septemba 2022. Ikumbukwe pia Rais Samia alifanya ziara ya kitaifa nchini DRC mwezi Agosti 2022 mara baada ya kushiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika nchini humo ambapo Rais Tshesiked alikabidhiwa uenyekiti wa Jumuiya hiyo.

Ziara hii ya Rais wa DRC na nyingine zilizofanywa na viongozi wa ngazi tofauti baina ya nchi hizi mbili pamoja na uamuzi wa Tanzania wa kufungua Ofisi ya Konseli Kuu katika mji wa Lubumbashi vinatajwa kuwa vitaimarisha uhusiano na kukuza biashara baina ya mataifa hayo mawili yenye utajiri mkubwa wa maliasili.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na waandishi wa Habari (hawapo pichani) Ikulu Jijini Dar es Salaam

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Mhe. Felix Tshisekedi akizungumza na waandishi wa Habari (hawapo pichani) Ikulu Jijini Dar es Salaam

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Mhe. Felix Tshisekedi wakishuhudia utiaji saini wa Mkataba wa Teknolojia ya Habari na Posta uliosainiwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye na Waziri wa Mambo ya Nje wa DRC, Mhe. Christophe Lutundula Ikulu Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Stergomena Tax akifuatilia Mkutano wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Mhe. Felix Tshisekedi na waandishi wa Habari uliofanyika Jijini Dar es Salaam




RAIS WA JAMHURI YA KIDEMOKRASIA YA KONGO MHE. FELIX TSHISEKEDI AWASILI NCHINI

 

Rais wa Jamhuri ya Muunganbo wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akimpokea mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Mhe. Felix Tshisekedi baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam kwa ziara ya Kitaifa ya siku mbili tarehe 23 na 24 Oktoba, 2022 

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Mhe. Felix Tshisekedi akiteta jambo na Rais wa Jamhuri ya Muunganbo wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan baada ya kuwasili nchini kwa ziara ya kitaifa ya siku mbili  

Rais wa Jamhuri ya Muunganbo wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akimtambulisha Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Mhe. Felix Tshisekedi kwa Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa na Mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Kongo (DRC) Mhe. Felix Tshisekedi wakiwa katika jukwaa la salamu za heshima za kijeshi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es salaam

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa na Mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Kongo (DRC) Mhe. Felix Tshisekedi wakiwa katika jukwaa la salamu za heshima za kijeshi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es salaam

Rais wa Jamhuri ya Kongo (DRC) Mhe. Felix Antonio Tshisekedi akikagua paredi maalumu aliyoandaliwa na Jeshi la Wananchi (JWTZ) mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam













TANZANIA YAJIVUNIA USHIRIKIANO IMARA NA UMOJA WA MATAIFA

Tanzania imesema inajivunia ushirikiano kati yake na Umoja wa Mataifa (UN) na kuahidi kuendeleza ushirikiano huo katika kuendeleza programu mbalimbali za maendeleo endelevu.

Ahadi hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb.), alipokuwa akizungumza na waandishi wa Habari kuhusu maadhimisho ya miaka 77 ya Umoja wa Mataifa Duniani katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam ambapo maadhimisho hayo huadhimishwa kila mwaka tarehe 24 Oktoba.

“Tanzania inanufaika na uanachama wake kwenye Umoja wa Mataifa katika maendeleo. Kwa mfano, kupitia Mpango wa Malengo ya Milenia na Malengo ya Maendeleo Endelevu. Umoja wa Mataifa unaendelea kusaidia nchi wanachama kutekeleza malengo hayo ili kukuza amani, utawala wa sheria, haki za binadamu na maendeleo kwenye sekta mbalimbali. Tanzania imekuwa mnufaika wa mikakati hiyo na  mwezi Mei, 2022, Umoja wa Mataifa ulizindua mpango wake mpya wa ushirikiano unaojulikana kwa jina la United Nations Sustainable Development Cooperation Framework baina ya Tanzania na Umoja huo, unaolenga kuleta maendeleo kwenye maeneo mbalimbali nchini,” alisema Balozi Mbarouk.

Pamoja na mambo mengine, Balozi Mbarouk aliongeza kuwa Ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini inasaidia kuhamasisha wadau mbalimbali kama vile taasisi za Serikali, asasi za kiraia, wanataaluma na kadhalika kupitia programu zake ili kuleta maendeleo ya Watanzania kama vile kuboresha huduma za afya, kutokomeza umaskini, njaa, kuhuisha sekta ya elimu, kupambana na mabadiliko ya tabianchi, na kukuza sayansi na teknolojia.

“Manufaa mengine ni ajira kwa Watanzania kwenye taasisi mbalimbali za Umoja wa Mataifa pamoja na misheni za kulinda amani za Umoja huo, suala linalonufaisha maisha ya Mtanzania mmoja mmoja lakini pia Taifa kwa ujumla,” Aliongeza Balozi Mbarouk.

Kwa upande wake, Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Tanzania, Bw. Zlatan MiliÅ¡ić amesema Umoja wa Mataifa umelenga kusaidia watu, ustawi, dunia na mazingira ili kuwawezesha wananchi kufikia vipaumbele vya maendeleo ya taifa na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs). 

“Tunaishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano wake kwa kuweka mazingira wezeshi kwa mashirika ya Umoja wa Mataifa. Umoja wa Mataifa unaahidi kuendelea kufanya kazi na Serikali ya Tanzania ikiwa ni pamoja na kuunga mkono jitihada za maendeleo za Serikali ili kuiwezesha kufikia vipaumbele vyake vya maendeleo na SDGs,” amesema Bw. MiliÅ¡ić. 

Mgeni rasmi katika maadhimisho ya miaka 77 ya Umoja wa Mataifa Duniani anatarajia kuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro (Mb.)

Maadhimisho rasmi ya Siku ya Umoja wa Mataifa yatafanyika rasmi tarehe 24 Oktoba 2022 katika viwanja vya Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam. Kauli mbiu ya madhimisho ya mwaka huu ni “Maendeleo yanayozingatia ujumuishwaji wa makundi yote”.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk akizungumza na waandishi wa Habari (Hawapo pichani) kuhusu maadhimisho ya miaka 77 ya Umoja wa Mataifa Duniani katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Tanzania, Bw. Zlatan MiliÅ¡ić. 

Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Tanzania, Bw. Zlatan MiliÅ¡ić akizungumza na waandishi wa Habari (Hawapo pichani) kuhusu maadhimisho ya miaka 77 ya Umoja wa Mataifa Duniani katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk pamoja na Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Tanzania, Bw. Zlatan MiliÅ¡ić wakizungumza na waandishi wa Habari kuhusu maadhimisho ya miaka 77 ya Umoja wa Mataifa Duniani katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam



Saturday, October 22, 2022

TANZANIA NA URENO ZASAINI HATI KUIMARISHA USHIRIKIANO

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Ureno zimesaini Hati ya Makubaliano ya kuanzisha Majadiliano ya Kisiasa baina yao ili kuimarisha ushirikino kwa kuanzisha rasmi majadiliano ya kukuza ushirikiano huo.

Hati hiyo, imesainiwa  tarehe 21 Oktoba 2022 jijini Lisbon kati ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ureno, Mhe. João Gomes Cravinho.


Akizungumza wakati wa mazungumzo rasmi kati yao, Mhe. Dkt. Tax amesema anaishukuru Serikali ya Ureno na Serikali yake kwa hatua hii muhimu katika ushirikiano wa kidiplomasia na kwamba kusainiwa kwa hati hiyo kunalenga kuupeleka ushirikiano huo katika hatua nyingine ya juu ambapo nchi hizi mbili zitaongeza zaidi ushirikiano katika maeneo mbalimbali yenye maslahi kwao  ikiwemo biashara, uwekezaji, utalii, uchumi wa buluu, usafirishaji na elimu.


Vilevile amesema kwamba hii ni ishara kwamba nchi hizi mbili zina nia ya ya dhati ya kushirikiana kwenye masuala mbalimbali ya manufaa kwa pande zote mbili.


“Ziara yangu nchini Ureno imekuwa ni ya manufaa makubwa kwani kwa mara ya kwanza katika historia ya ushirikiano baina ya Tanzania na nchi hii tumesaini Hati ya Makubaliano ya kuanzisha majadiliano ya kisiasa baina yetu. Hii ni hatua ya juu katika ushirikiano wa kidiplomasia kwani sasa masuala mengi ya ushirikiano kati yetu ikiwemo biashara, uwekezaji, utalii, yataimarika  na kwenda viwango vingine vya juu kwa manufaa ya pande zote mbili”, alisema Dkt. Tax.


Ameongeza kusema kuwa, wamekubaliana na Waziri mwenzake kuweka mikakati thabiti ya pamoja ya ufuatiliaji wa utekelezaji wa maeneo mbalimbali  ya ushirikiano waliyokubaliana ambapo pia  Mhe. Dkt. Tax amewataka Watanzania kutumia hatua ya kusainiwa kwa mkataba huo kama chachu ya kuanza kuchangamkia  fursa mbalimbali zilizopo Ureno ikiwemo biashara kwa bidhaa za kahawa, chai, samaki, viungo vya chakula na mbao.


Pia,  wakati wa mazungumzo yao, Tanzania imesisitiza umuhimu wa nchi hiyo kushirikiana nayo katika medani za kimataifa hususan kuendelea kupaza sauti ili nchi za Ulaya ziendelee kuisadia Tanzania  na nchi za Afrika katika kukabiliana na changamoto zinazotokana na  mabadiliko ya Tabianchi.


Kwa upande wake,  Mhe. João  Gomes Cravinho amemshukuru Mhe. Dkt. Tax kwa kukubali mwaliko wake na kutembelea nchini humo na kwamba Ureno inathamini mchango wa Tanzania kupitia ushirikiano uliopo kati yao ikiwa ni pamoja na ushirikiano katika medani za Kimataifa.


Amesema ana imani kuwa kusainiwa kwa Hati hiyo muhimu ni mwanzo mpya wa ushirikiano huo ambapo nchi hizi mbili sasa zitazingatia na kujitoa zaidi katika kuhakikisha ushirikiano uliopo unaimarika zaidi.


“Hatua ya kusainiwa kwa Hati hii ni ya kihistoria.. Kilichobaki sasa ni kuhakikisha yale tuliyokubaliana leo na kupitia hati hiyo yanatekelezwa” alisema Mhe. Gomez.


Akizungumzia maeneo ambayo nchi hiyo imepiga hatua na ipo tayari kushirikiana na Tanzania kuwa ni pamoja na eneo la Nishati Mbadala. Alisema nchi hiyo hadi sasa imefikia asilimia 62 ya matumizi ya Nishati hiyo na kwamba malengo yao ni kufikia asilimia 80 ifikapo mwaka 2026.


Wakati wa mazungumzo yao viongozi hao pia walikubaliana kuimarisha ushirikiano katika masuala ya biashara, elimu, utalii, sanaa na michezo pamoja na kukuza Lugha ya Kiswahili kwa upande wa Ureno na Kireno kwa upande wa Tanzania.


Ziara ya Mhe. Waziri Tax nchini Ureno ni matokeo ya majadiliano kati ya Rais  wa Ureno, Mhe. Rebelo De Sousa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Isdor Mpango walipokutana mwezi Juni 2022 pembezoni mwa Mkutano wa Pili wa Umoja wa Mataifa kuhusu Bahari ambapo walizungumza kuhusu umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya nchi hizi mbili.


Mhe. Dkt. Tax amehitimisha ziara yake ya siku mbili aliyoifanya nchini humo kuanzia tarehe 20 hadi 22 Oktoba 2022 kwa mwaliko wa Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Mhe. João Gomes Cravinho. Itakumbukwa kuwa, Mhe. Waziri Tax alianza ziara yake nchini Poland kuanzia tarehe 17 hadi 19 Oktoba 2022 kabla ya kutembelea Ureno.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax kwa pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ureno, Mhe.Mhe. João Gomes Cravinho wakisaini Hati ya Makubaliano ya Kuanzisha Majailiano ya Kisiasa kati ya Tanzania na Ureno. Hati hiyo imesainiwa hivi karibuni jijini Lisbon wakati wa ziara ya kikazi ya Mhe. Dkt. Tax aliyoifanya nchini humo kuanzia tarehe 20 hadi 22 Oktoba 2022. Pamoja na mambo mengine kusainiwa kwa Hati hiyo kunatoa fursa kwa nchi hizi mbili kuanza majadiliano rasmi ya ushirikiano kwenye maeneo mbalimbali ya manufaa kwa pande mbli kama vile biashara, uwekezaji, elimu na uchumi wa bluu.

Waheshimiwa Mawaziri wakibadilisha Hati hiyo muhimu mara baada ya kusaini
Mhe. Dkt. Tax na Mhe. Gomes wakionesha Hati hiyo mara baada ya kusaini
Mhe. Dkt. Tax na Mhe. Gomes wakiwa katika mazungumza rasmi kuhusu namna ya kuimarisha na kuboresha ushirikiano kati ya Tanzania na Ureno
Sehemu ya Ujumbe kutoka Serikali ya Ureno wakishiriki mazungumzo rasmi ya Mawaziri
Sehemu ya Ujumbe wa Tanzania wakishiriki mazungumzo rasmi kati ya Mhe. Dkt. Tax na Mhe. Gomes (hawapo pichani). Wa kwanza kulia ni Balozi wa Tanzania nchini Ureno mwenye makazi nchini Ufaransa, Mhe. Samwel Shelukindo akifuatiwa na Brigedia Generali Mbaraka Mkeremy kutoka Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa pamoja na Bw. Charles Mbando, Katibu wa Waziri
Mhe. Dkt. Tax (katikati) akimsikiliza Mhe. Gomes (hayupo pichani) wakati wa  mazungumzo rasmi  kati yao. Kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambi ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Swahiba Mndeme na kushoto ni Mhe. Balozi Shelukindo.
Maafisa kutoaka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakinukuu mazungumzo kati ya Mhe. Dkt. Tax na Mhe. Gomes. Kushoto ni Bi. Liliani Kimaro na Bi. Sekela Mwambegele.

Mhe. Gomes akimkabidhi zawadi Mhe. Dkt. Tax mara baada ya kukamilisha mazungumzo rasmi

Mhe. Dkt. Tax naye akimpatia zawadi Mhe. Gomes. Zawadi hiyo ni bidhaa za Tanzania ikiwemo Korosho, Kahawa, Asali, Batiki na Viungo vya Chakula
Mhe. Gomes akimtambulisha Mhe. Dkt. Tax kwa wasaidizi wake

Ujumbe wa Tanzania
Maafisa wanaosimamia masuala ya Sheria kutoka Tanzania na Ureno wakiandaa Hati ya Makubaliano kabla ya kusainiwa. Kushoto ni Bw. Ibrahim Mmbaga, kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Mkuu wa Itifaki wa Ureno akisoma Hati ya Makubaliano kwa Mawaziri  kabla ya kusainiwa 

Mhe. Dkt. Tax na mwenyeji wake Mhe. Gomes wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kukamilisha mazungumzo kati yao
Mhe. Dkt. Tax akiagana na Mhe. Gomes mara baada ya kukamilisha mazungumzo na kusainiwa kwa Hati ya Makubaliano

Picha ya pamoja 

 

Friday, October 21, 2022

TANZANIA YANADI FURSA ZA UWEKEZAJI NCHINI URENO

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax amesema Serikali ya Tanzania inaendelea kuboresha mazingira ya Uwekezaji na ufanyaji biashara nchini ikiwa ni pamoja na kuzifanyia maboresho baadhi ya sheria za usimamizi wa biashara ili kuongeza ufanisi kwa sekta binafsi katika uzalishaji.

 

Mhe. Dkt. Stergomena ametoa kauli hiyo  jijini Lisbon wakati akifungua rasmi Jukwaa la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania  na Ureno lililoloandaliwa kwa ushirikiano kati ya Ubalozi wa Tanzania nchini Ureno na Taasisi ya Biashara na Uwekezaji ya Ureno na  kuishirikisha Jumuiya yaWafanyabiashara wa Ureno.

 

Mhe. Dkt. Tax amesema dhamira kuu ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji na ufanyaji biashara hususan kwa kuishirikisha ipasavyo sekta binafsi. Amesema tayari Serikali imefanya majadiliano ya mara kwa mara na sekta biafsi ili kutatua changamoto zinazoikabili sekta hiyo.

 

Amesema katika kuboresha mazingira ya uwekezaji na ufanyaji biashara nchini masuala mbalimbali yanaboreshwa zikiwemo huduma, sheria, miundombinu pamoja na kuishirikisha kikamilifu sekta binafsi ambayo ni muhimu katika kuchangia uchumi wa nchini.

 

“Tupo hapa leo ili kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Ureno hususan katika masuala ya biashara na uwekezaji. Tanzania inaendelea kuhamasisha uwekezaji kutoka ndani na nje ya nchi kwa kuboresha mazingira ya uwekezaji. Katika maboresho hayo ni pamoja na Serikali kushirikiana kwa karibu na  sekta binafsi ili kuiwezesha sekta hii kuwa na ufanisi na kuchangia uchumi ipasavyo” amesema Dkt. Tax.

 

Amesema Serikali inaendelea kuboresha miundombinu kama barabara, bandari, reli, viwanja vya ndege na upatikanaji wa maji na umeme ili kuwawezesha wawekezaji kutopata changamoto zozote pale wanapokuja nchini kuwekeza.

 

 “Serikali imefanya jitihada za makusudi za kuhakikisha miundombinu yote ya msingi kama maji, umeme, barabara, reli, usafiri wa anga na mawasiliano ya simu vinapatikana kwa ngazi tofauti tofauti. Kupitia maboresho haya ni imani yetu  wawekezeji watapata ujasiri wa kuwekeza Tanzania na si mahali pengine popote”, amesisitiza Dkt. Tax.

 

Amesema masuala mengine yanayohamasisha uwekezaji, biashara na utalii nchini ni pamoja na ushiriki wa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Filamu ya kutangaza Utalii nchini ya The Royal Tour, Sera ya Mambo ya Nje yenye msisitizo katika Diplomasia ya Uchumi ambayo imekuwa chachu katika kuwajengea ujasiri wawekezaji nchini pamoja na ushiriki wa Tanzania kwenye majukwaa mbalimbali ya kimataifa ya biashara na uwekezaji kama Maonesho ya Biashara ya Dubai ya mwaka 2020. Vyote hivi  vimeipaisha zaidi Tanzania duniani na kuchangia ongezeko la watalii na wawekezaji nchini.

 

Dkt. Tax alitumia fursa hiyo pia kuwakaribisha wawekezaji na wananchi wa Ureno kwa ujumla kutembelea Tanzania ili kujionea vivutio mbalimbali vya utalii huku akiwahamasisha kuangalia Filamu ya Utalii ya Royal Tour ambayo ameilezea kuwa ni ya aina yake kwani mhusika mkuu katika Filamu hiyo ni Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 

Kwa upande wake, Waziri anayeshughulikia Biashara na Uwekezaji wa Ureno, Mhe. Bernardo Ivo Cruz amepongeza ziara ya Mhe. Dkt. Tax nchini humo akisema imekuja wakati mwafaka ambao wakati dunia ikiendelea kushuhudia changamoto mbalimbali za kiuchumi, Tanzania na Ureno zinaangalia  namna ya kushirikiana katika biashara na uwekezaji ili kujikwamua kiuchumi.

 

“Tanzania ni mshirika wetu muhimu katika biashara na uwekezaji na tupo tayari kuimarisha ushirikiano huu. Nakupongeza Mhe. Waziri kwa kufanya ziara katika kipindi hiki na tunaahidi kushirikiana na Tanzania katika maeneo mbalimbali ya uwekezaji ikiwemo Kilimobiashara, Uchumi wa Bluu, Miundombinu na Sekta zingine za uwekezaji” alisema Mhe. Cruz.

Pia aliongeza kusema nchi yake inao Mpango wa miaka sita wa ushirikiano katika biashara na uwekezaji kuanzia mwaka 2021-2027 ambapo Tanzania ni miongoni mwa nchi zitakazonufaika na mpango huo.

 

Akiwasilisha mada kuhusu Fursa za Uwekezaji zilizopo nchini kwa washiriki wa Jukwaa hilo, Mkurugenzi wa Biashara na Uwekezaji kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Bw. Revocatus Rasheli amewahamasisha wawekezaji na wafanyabiasha kutoka Ureno kuchangamkia fursa mbalimbali za biashara na uwekezaji nchini huku akisema tayari anayo mkononi miradi 100 chini ya Sekta ya Umma na miradi 36 chini ya Sekta Binafsi ambayo ipo tayari na kwamba ni kiasi cha wawekezaji hao kuchagua na kuwekeza.

Aliongeza kusema Tanzania katika kuhamasisha uwekezaji imetenga ardhi yenye ukubwa wa Hekta milioni 1.6 kwa ajili ya uwekezaji wa kilimo ambapo tayari Hekta 6,000 zipo Mkoani Morogoro kwa ajili ya uwekezaji wa kilimo.

 

Pia alitumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji hao kuwekeza kwenye sekta ya utalii ikiwa ni pamoja na kujenga Hoteli, Nyumba za Makazi na  Kumbi za Mikutano.

 

“Serikali ya Tanzani ainazo fursa nyingi za uwekezaji. Nawakaribisha kuwekeza kwenye kilimo, uvuvi, madini, miundombinu lakini pia ujenzi wa hoteli, nyumba za makazi na kumbi za mikutano hususan katika miji mikuu ikiwemo Dar es Salaana na Makao Makuu ya Nchi yetu Dodoma ambako mahitaji ni makubwa zaidi” alisisitiza Bw. Rasheli.

 

Kadhalika, Mkurugenzi huyo amesema Ureno ni mdau muhimu katika ushirikiano na Tanzania na kwamba ipo haja ya kuongeza  biashara kati ya nchi hizi mbili ambapo  amesema hadi sasa Ureno imesajili miradi 13 nchini yenye thamani ya Dola za Marekani Milioni Tisa ambayo imetoa fursa za ajira 325 kwa watanzania.

 

“Ziara hii ni muhimu sana kwetu Tanzania na Ureno, ni imani yetu kuwa ziara hii itaongeza wawekezaji na wafanyabiashara kutoka Ureno kuja nchini ili kwa pamoja nchi hizi zinufaike kupitia ushirikiano mzuri uliopo” alisisitiza Bw. Rasheli.

 

Naye Mkurugenzi wa Utafiti na Mipango wa Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanziabar (ZIPA) Bw. Emmanuel Mashimba amesema Serikali ya Zanzibar inaendelea kuweka mazingira wezeshi katika kuvutia wawekezaji na wafanyabiashara na kwamba Ureno ni miongoni mwa nchi muhimu ambazo Zanzibar ipo tayari kushirikiana nazo katika sekta za uchumi wa bluu, utalii na miundombinu.

 

Mhe. Dkt. Tax yupo nchini Portugal kwa ziara ya kikazi ya siku mbili kuanzia tarehe 20 hadi 22 Oktoba, 2022. Akiwa nchini humo, Mhe. Dkt. Tax pamoja na mambo mengine atakutana kwa mazungumzo rasmi na mwenyeji wake Waziri wa Mambo ya Nje, Mhe. Joao Gomez Cravinho pamoja na kusaini Hati ya Makubaliano ya kuanzisha Majadiliano ya Kisiasa kati ya Tanzania na Ureno.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akiwa kwenye mazungumzo rasmi na Waziri wa Nchi wa Ureno anayeshughlikia masuala ya Biashara na Uwekezaji, Mhe. Bernardo Ivo Cruz mara baada ya kuwasili kwenye Makao Makuu ya Ofisi za Taasisi ya Biashara na Uwekezaji za nchi hiyo zilizopo jijini Lisbon. Akiwa katika taasisi hiyo, pamoja na mambo mengine Mhe. Dkt. Tax alifungua rasmi Jukwaa la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Ureno ambalo liliishirikisha Jumuiya ya Wawekezaji kutoka nchini humo. Mhe. Waziri Tax na yupo nchini Ureno kwa ziara ya kikazi ya siku mbili kuanzia tarehe 20n hadi 22 Oktoba 2022

Mhe. Dkt. Tax akifungua rasmi Jukwaa la Uwekezaji kati ya Tanzania na Ureno lililofanyika Lisbon. Pamoja na mambo mengine Mhe. Dkt Tax alitumia nafasi hiyo kuwakaribisha wawekezaji na wafanyabiashara wa Ureno kuwekeza nchini
Waziri wa Nchi wa Ureno anayeshughulikia masuala ya Biashara na Uwekezaji, Mhe. Bernardo Ivo Cruz naye akizungumza wakati wa Jukwaa la Biashara kati ya Tanzania na Ureno

Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Baiashara na Uwekezaji ya Ureno, Bw.Kuis Castro Henriques naye akiwakaribisha kwenye Ofisi za Taasisi yake washiriki wa Jukwaa la Uwekezaji kati ya Tanzania na Ureno
Mkurugenzi wa Uwekezaji na Biashara kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Bw. Revocatus Rasheli akinadi fursa mbalimbali za biashara na uwekezaji zilizopo nchini kwa washiriki wa Jukwaa
la Uwekezaji kati ya Tanzania na ureno lililofanyika Lisbon
Balozi wa Tanzania nchini Ureno mwenye makazi yake nchini Ufaransa, Mhe. Samwel Shelukindo (kulia) akishiriki Jukwaa la Uwekezaji kati ya Tanzania na Ureno. 

Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Swahiba Mndeme (wa pili kulia) akiwa na Brigedia Generali Mbaraka Mkeremy wakifuatilia Jukwaa la Uwekezaji kati ya Tanzania na Ureno

Washiriki wa Jukwaa la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania  na Ureno wakifuatilia mada zilizowasilishwa kwao

Washiriki wengine wakifuatilia matukio

Washiriki wengine kutoka Tanzania wakifuatilia mada wakati wa Jukwaa la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Ureno lililofanyika Lisbon
Mhe. Dkt. Tax akimpatia zawadi kutoka Tanzania Mhe. Cruz. Zawadi hiyo ni mchanganyiko wa bidhaa za Tanzania kama vile Kahawa, Korosho, Batiki, Asali na Viungo vya Chakula

Mhe. Dkt. Tax akiagana na Mhe. Cruz mara baada ya ufunguzi wa Jukwaa la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Ureno

Picha ya pamoja