Monday, December 12, 2022

UBUNIFU, UBORA WA BIDHAA ZA WAJASIRIAMALI WATIA FORA MAONESHO YA JUAKALI

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Riziki Pembe Juma ameeleza kuridhishwa na namna Wajasiriamali wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wanavyoongeza viwango vya ubora na ubunifu katika huduma na bidhaa wanazozalisha. 

Waziri Riziki Pembe Juma ameeleza hayo alipozungumza kwenye sherehe za ufunguzi wa maonesho ya 22 ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Wajasiriamali Wadogo na Wakati maarufu kama Juakali, zilizofanyika tarehe 11 Disemba 2022 katika viwanja vya Uhuru vya Kololo jijini Kampala, Uganda. 

Amesema hatua iliyofikiwa na Wajasiriamali hao ni dalili nzuri ya kufikiwa kwa lengo la kuyafanya maonesho hayo y’a Juakali kuwa jukwaa la fursa ya kukuza masoko, kubadilishana uzoefu na teknolojia. 

Ameongeza kuwa hali hiyo inatokana na ukweli kuwa wajasiriamali hao bado wanahitaji kuendelea kujifunza zaidi, kubadilishana uzoefu na teknolojia baina yao katika Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

“Sote tumeshuhudia bidhaa mbalimbali zinazouzwa katika baadhi ya mabanda yaliyopo katika maonesho haya ambayo yamejumuisha nchi zote wanachama, bidhaa zina ubora na ubunifu wa hali ya juu. Ongezeko hili la ubunifu na ubora wa bidhaa za wajasiriamali hawa kila mwaka, ni dalili njema kuwa wana Afrika Mashariki katika siku za usoni tutakuwa na bidhaa zinazotosheleza mahitaji yetu kwa ubora na wingi hali ambayo itasaidia kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje” alisema Mhe. Waziri Riziki

Mhe. Waziri Riziki pia ameeleza kuridhishwa na namna Wanawake walivyojitokeza kushiriki katika maonesho hayo. 

Asilimia 87 ya idadi ya Wajasiriamali zaidi ya 300 wa Tanzania kwenye maonesho haya ni Wanawake, hali hii inadhirisha na uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan unatoa kipaumbele kwa wanawake kwa kuzingatia kuwa mwanamke ni kiungo thabiti katika maendeleo ya familia na nchi kwa ujumla, alisema Mhe. Waziri.

Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Robinah Nabbanja ambaye alimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni katika sherehe hiyo ya ufunguzi wa maonesho, ametoa wito kwa Serikali za Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuendelea kufanya mabadiliko muhimu ya sera za uchumi ili ziweze kuleta msukumo katika kuongeza uzalishaji wa bidhaa na kurahisha zaidi ufanyaji wa biashara katika Jumuiya. 

“Kundi la wajasiriamali wadogo na wakati linachangia asilimia 60 ya pato la Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, huku 99% ya biashara ndogo na kati zikimilikiwa na wazawa wa Afrika Mashariki, ni muhimu kukumbuka kuwa katika kila Waafrika 10; 6 kati ya hao wamejiajiri katika sekta ya biashara ndogo na kati, hivyo ni sawa na kusema kuwa, biashara ndogo na za kati zinazalisha wastani wa ajira 8 katika kila ajira 10 mpya,” alisema Mhe. Waziri Mkuu Nabbanja

Mheshimiwa Nabbanja alisisitiza kuwa endapo sera zitakuwa rafiki zaidi kiasi cha kutatua changamoto zinazowakabili wazalishaji wadogo italeta manufaa makubwa ya kiuchumi kwa Jumuiya, kwa kuwa asilimia 99 ya Wajasiriamali ni wazawa wa Afrika Mashariki hivyo maboresho hayo yatawanufaisha wao moja kwa moja na kuleta mchango mkubwa katika maendeleo ya viwanda na upatikanaji wa ajira za kutosha kwa Vijana na wanawake.

Mhe. Nabbanja amesema maonesho ya juakali ni jukwaa muhimu linalowawezesha Wajasiriamali kuonesha na kuuza huduma na bidhaa wanazozalisha, vilevile yanatoa fursa hadhimu kwa Wajasiriamali kuongeza wigo wa soko, kujifunza zaidi kuhusu ubunifu na kubadilishana uzoefu na teknolojia katika masuala mbalimbali kama vile kuongeza thamani ya mazao ya kilimo na mifugo.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Riziki Pembe Juma (wa kwanza kulia) akisalimiana na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Robinah Nabbanja (mwenye barakoa) kwenye sherehe ya ufunguzi wa maonesho ya 22 ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Wajasiriamali Wadogo na Wakati maarufu Juakali, iliyofanyika jijini Kampala, Uganda. 
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Riziki Pembe Juma akihutubia kwenye sherehe ya ufunguzi wa maonesho ya 22 ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Wajasiriamali Wadogo na Wakati maarufu Juakali, iliyofanyika jijini Kampala, Uganda. 
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Jamhuri ya Uganda Mhe. Robinah Nabbanja  akihutubia kwenye sherehe ya ufunguzi wa maonesho ya 22 ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Wajasiriamali Wadogo na Wakati maarufu Juakali, iliyofanyika jijini Kampala, Uganda. 
Viongozi na Watendaji wa Serikali, Sekretariati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Taasisi mbalimbali wakiwa kwenye picha ya pamoja kwenye ufunguzi wa maonesho ya 22 ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Wajasiriamali Wadogo na Wakati maarufu Juakali, iliyofanyika jijini Kampala, Uganda. 
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Riziki Pembe Juma na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Robinah Nabbanja wakiangalia bidhaa za mmoja wa wajasiriamali kwenye maonesho ya 22 ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Wajasiriamali Wadogo na Wakati maarufu Juakali, yanayoendelea jijini Kampala, Uganda. 
Mjasiriamali wa Tanzania alikimwonjesha mvinyo mteja kwenye maonesho ya 22 ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Wajasiriamali Wadogo na Wakati maarufu Juakali, yanayoendelea jijini Kampala, Uganda. 
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Riziki Pembe Juma (katika) akiwasili katika Viwanja vya Uhuru vya Kololo jijini Kampala, Uganda kushiriki ufunguzi rasmi wa maonesho ya 22 ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Wajasiriamali Wadogo na Wakati maarufu Juakali yanayoendelea nchini humo.

Tanzania na Oman Zainisha Maeneo ya Kushirikiana

Tanzania na Oman zimedhamiria kuchukua jitihada za makusudi kuimarisha ushikiano wa kiuchumi baina ya nchi hizo zenye uhusiano madhubuti wa kihistoria.

Hayo yamebainishwa na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi hizo, Mhe. Dkt. Stergomena L. Tax (Mb) na mwenyeji wake, Mhe.  Sayyid Badr Al Busaidi walipokutana pembezoni mwa Mkutano wa Pili wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Oman uliohitimishwa jijini Muscat tarehe 11 Desemba 2022.

Katika hotuba zao za kufunga Mkutano wa Pili wa JPC, Viongozi hao walieleza kuwa nchi zao zimekubaliana kuanzisha Kamati ya Pamoja ya Kufuatilia Utekelezaji wa Maazimio ya Mkutano huo ili kuwa na tija kwa pande zote mbili.

Kamati hiyo pamoja na mambo mengine, itahakikisha kuwa rasimu zote za mikataba na makubaliano zinakamilika na kutiwa saini ili kujenga mazingira ya kisheria ya kuimarisha uhusiano wa kindugu uliopo baina ya Tanzania na Oman.

Maeneo yaliyojadiliwa na ujumbe wa nchi hizo na kuwekewa mikakati ya utekelezaji ni pamoja na kilimo, elimu, nishati, biashara, uwekezaji, mawasiliano, mifugo na usafirishaji. Maeneo mengine ni uvuvi, utalii, michezo, utamaduni, madini, uhamiaji, fedha na udhibiti wa majanga ya moto.

Mkutano wa JPC kati ya Tanzania na Oman ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena L. Tax; Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Stephen Byabato; Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Prof. Jamal Katundu; Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab; Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati, Ndugu Kheri Mahimbali; na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Zanzibar, Ndugu Mwanahamisi Adam.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena L. Tax (Mb) na mwenyeji wake, Mhe.  Sayyid Badr Al Busaidi wakiwa katika mazungumzo pembezoni mwa Mkutano wa Pili wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Oman uliohitimishwa jijini Muscat tarehe 11 Desemba 2022.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena L. Tax (Mb) akiwa katika picha ya pamoja  na Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman, Mhe.  Sayyid Badr Al Busaidi waliipokutana pembezoni mwa Mkutano wa Pili wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Oman uliohitimishwa jijini Muscat tarehe 11 Desemba 2022.

Meza Kuu wakati wa Mkutano wa Pili wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Oman uliohitimishwa jijini Muscat tarehe 11 Desemba 2022.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena L. Tax (Mb) akibadilishana nyaraka zenye masuala yaliyoafikiwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman, Mhe.  Sayyid Badr Al Busaidi wakati wa Mkutano wa Pili wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Oman uliohitimishwa jijini Muscat tarehe 11 Desemba 2022.

 

Sunday, December 11, 2022

ZAIDI YA WAJASIRIAMALI 300 WASHIRIKI MAONESHO YA JUAKALI UGANDA


Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imefanikisha ushiriki wa Wajasiriamali zaidi ya 300 katika maonesho ya 22 ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Wajasiriamali Wadogo na Wakati maarufu Juakali yanayofanyika katika viwanja vya Uhuru vya Kololo jijini Kampala, Uganda kuanzia terehe 8 - 18 Disemba 2022.

Maonesho hayo yanayoongozwa na kauli mbiu “Nunua Bidhaa za Afrika Mashariki, ili kujenga Uchumi Stahimilivu na Endelevu wa Afrika Mashariki” yanalenga kutoa fursa kwa Wajasiriamali ya kuonesha huduma na bidhaa mbalimbali wanazozalisha na kubadilishana uzoefu, ujuzi na taarifa na wajasiriamali wenzao katika Jumuiya, sambamba na kukuza wigo wa masoko mapya.

Maonesho hayo ambayo yamevutia Wajasiriamali zaidi 1500 kutoka Nchi zote saba (7) Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, na ikikadiriwa 75% kati yao kuwa ni wanawake, yamesheheni bidhaa mbalimbali zenye asili ya Jumuiya. Kwa upande wa wajisiriamali wa Tanzania miongoni mwa bidhaa na huduma wanazozionesha ni pamoja na mavazi ya asili, bidhaa za baharini, bidhaa za kilimo zilizoongezewa thamani, mashine za kuzalisha bidhaa mbalimbali, madawa ya asili, vito vya thamani na madini, utalii, na bidhaa za ngozi kama vile viatu, mabegi na mikoba. 

Wakizungumza kwa nyakati tofauti Wajasiliamali wa Tanzania wameonesha kuridhishwa kwao na kupongeza juhudi na hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali ya Tanzania chini ya Uongozi madhubuti wa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuweka mazingira wezeshi ya biashara ikiwa ni pamoja na kuwawezesha kushiriki katika maonesho hayo. 

“Kutokana na gharama kubwa za kusafirisha bidhaa zetu hadi hapa nchini Uganda, wengi wetu tusingeweza kumudu, hivyo tusingeweza kuwa na uwakilishi wa kutosha katika maonesho haya. Hata hivyo kutokana na dhamira ya Serikali ya kutusaidia wajasiriamali kukua kibiashara kupitia kupata masoko mapya ya huduma na bidhaa tunazozalisha na kutuongezea ujuzi na uzoefu imeona ni vyema ituwezeshe katika maeneo mbalimbali ikiwemo kugharamia usafiri wa kutuleta hapa nchini Uganda na kuturudisha nyumbani baada ya maonesho”. Ameeleza Lilian Sambu mjasiliamali. 

Maonesho ya Juakali yalifanyika kwa mara ya kwanza mwezi Novemba 1999 jijini Arusha, ambapo yaliambatana na tukio la kihistoria la kusainiwa kwa Mkataba wa Uanzishwaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kutokana na mafanikio makubwa yaliyopatikana katika maonesho hayo, Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki walielekeza kuwa yafanyike kila mwaka kwa mzunguko kati ya Nchi Wanachama ili kuimarisha mtangamano wa jamii na uchumi wa watu wa Afrika Mashariki.
Bw. Joseph Ndunguru (kulia) mzalishaji wa bidhaa za vyakula kutoka mjini Mtwara akielezea bidhaa zake kwa mteja aleyetembelea banda lake kwenye maonesho ya 22 ya Juakali yanayoendelea katika viwanja vya Uhuru vya Kololo jijini Kampala, Uganda.
Wateja wakichangamkia bidhaa za mmoja wa wajasiriamali wa Tanzania (kulia) walipotembelea banda lake katika maonesho ya 22 ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Wajasiriamali Wadogo na Wakati maarufu Juakali yanayoendelea katika viwanja vya Uhuru vya Kololo jijini Kampala, Uganda.
Sehemu ya wajasiriamali wa Tanzania wakipanga bidhaa zao kweye maonesho 22 ya Juakali yanayoendelea katika viwanja vya Uhuru vya Kololo jijini Kampala, Uganda 
Wateja wakiangali bidhaa za mmoja wa wajasiriamali wa Tanzania (kulia) walipotembelea banda lake kwenye maonesho ya 22 ya Juakali yanayoendelea katika viwanja vya Uhuru vya Kololo jijini Kampala, Uganda.
Mkurugenzi Mtendaji wa Just Products Bi. Judith M. Lugembe akifuatilia taarifa ya biashara yake katika maonesho ya 22 ya Juakali yanayoendelea katika viwanja vya Uhuru vya Kololo jijini Kampala, Uganda
Naibu Katibu Mkuu wa Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Mipango, Miundombinu, Fedha na Utawala Mhandisi Steven Mlote akifuatilia maelezo ya mjasirimali alipotembelea banda la Tanzani kwenye maonesho ya 22 ya Juakali yanayoendelea katika viwanja vya Uhuru vya Kololo jijini Kampala, Uganda
Mkurungenzi wa Idara ya Ajira na Ukuzaji Ujuzi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi,Ajira,Vijana na Wenye Uemavu) Bw. Ally Msaki akizungumza na Naibu Waziri Mkuu wa Kwanza na Waziri anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki wa Uganda Mhe. Rebecca Alitwala Kadaga alipotembelea banda la Tanzania kwenye maonesho ya 22 ya Juakali yanayoendelea jijini Kampala, Uganda
Mkurugenzi Msaidizi wa Biashara, Uwekezaji na Sekta za Uzalishaji Bw. Athuman Nkungu akiangalia bidhaa ya mmoja wa wajasiriamali alipotembelea meza yake kweye maonesho 22 ya Juakali yanayoendelea katika viwanja vya Uhuru vya Kololo jijini Kampala, Uganda 
Sehemu ya wajasiriamali wa Tanzania wakimsalimia Naibu Waziri Mkuu wa Kwanza na Waziri anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki wa Uganda Mhe. Rebecca Alitwala Kadaga (yupo kwenye gari inayoonekana pichani) alipotembelea banda la Tanzania kweye maonesho 22 ya Juakali yanayoendelea katika viwanja vya Uhuru vya Kololo jijini Kampala, Uganda 
Naibu Waziri Mkuu wa Kwanza na Waziri anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki wa Uganda Mhe. Rebecca Alitwala Kadaga (mwenye chupa ya mvinyo mkononi) akipokea zawadi kutoka kwa mmoja wa wajasiriamali wa Tanzania kwenye maonesho ya 22 ya Juakali yanayoendelea jijini Kampala, Uganda

Wednesday, December 7, 2022

MHE. DKT. TAX AWAKARIBISHA WAWEKEZAJI KUTOKA VIETNAM


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax amewakaribisha wawekezaji kutoka Vietnam kuja nchini kuwekeza katika sekta ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano pamoja na Kilimo.


Mhe. Waziri Tax ameyasema hayo alipokutana kwa mazungumzo na Waziri wa Habari na Mawasiliano  wa Vietnam na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha nchi hiyo Mhe.  Nguyen Manh Hung alipomtembelea Ofisini kwake jijini Dodoma hivi karibuni.


Mhe. Dkt Tax amesema Tanzania inathamini ushirikiano kati yake na Vietnam ambayo imepiga hatua  kubwa katika maendeleo ya teknolojia ya habari na mawasiliano na kwamba kupitia ushirikiano huo Tanzania  imejipanga kunufaka katika sekta hiyo na nyingine zenye manufaa kati ya nchi hizi mbili.


Ameongeza kusema nchi hiyo ambayo tayari imewekeza kwenye sekta ya Mawasiliano hapa nchini kupitia Kampuni ya Simu ya Halotel, bado inakaribishwa kuwekeza zaidi katika sekta hiyo hususan kwenye miundombinu ya kidijiti na kwamba Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ili kuhakikisha wawekezaji wanafanikisha malengo yao lakini pia Taifa linanufaika kupitia uwekezaji.


“Tanzania inaendelea kujiimarisha katika Sekta ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kwa kushirikiana na wadau wa ndani na nje ya nchi. Kama ulivyosema Mhe. Waziri, Vietnam ni miongoni mwa nchi 10 duniani zilizopiga hatua kubwa katika sekta hiyo,  naendelea kuhimiza wawekezaji zaidi kutoka nchini kwako kuja kuwekeza kwenye sekta hiyo lakini pia na sekta nyingine kama Kilimo hususan kile cha biashara na usindikaji wa mazao ya kilimo” alisema Dkt. Tax.

 

Kwa upande wake, Mhe. Nguyen Manh Hung amepongeza jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali ya Tanzania katika kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji na kwamba nchi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania katika masuala mbalimbali yanachangia maendeleo ya wananchi.


Akizungumzia uwekezaji kupitia kampuni ya Viettel ambayo ni kampuni mama ya mtandao wa simu wa Halotel hapa nchini, amesema nchi yake imewekeza mtaji wa takribani Dola bilioni moja katika miundombinu ya mtandao huo ambao umejikita kuwahudumia zaidi wananchi wa vijijini na kwamba hadi sasa Mtandao huo umeajiri watanzania 1,000.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akiwa katika mazungumzo na Waziri wa Habari na Mawasiliano wa Vietnam na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha nchi hiyo Mhe. Nguyen Manh Hung alipomtembelea Ofisini kwake jijini Dodoma hivi karibuni.
Sehemu ya ujumbe ulioambatana na Mhe. Mahn Hung akiwemo Balozi wa Vietnam nchini Mhe. Nguyen Nam Tien (kulia) wakifuatilia mazungumzo
Sehemu ya ujumbe wa Tanzania ulioshiriki mazungumzo. Kushoto ni Bw. John Kambona, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki 

 

VACANCY ANNOUNCEMENT


 

Monday, December 5, 2022

WAZIRI AKUTANA KWA MAZUNGUMZO NA MABALOZI

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb) amekutana na kufanya mazungumzo na mabalozi wa Umoja wa Ulaya, Italia na Marekani na Uingereza katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.

Dkt. Tax amekutana kwa nyakati tofauti na Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Mhe. Manfredo Fanti, Balozi wa Italia nchini Mhe. Marco Lombardi, Balozi wa Marekani nchini, Mhe. Donald Wright pamoja na Balozi wa Uingereza nchini, Mhe. David Concar. 

Pamoja na mambo mengine, Dkt. Tax amejadili na mabalozi hao masuala ya kuimarisha ushirikiano baina ya Tanzania na nchi zao hususan katika kutekeleza diplomasia ya uchumi, sekta ya kilimo, elimu, miundombinu, nishati, utalii, ulinzi na takwimu.

Waziri Tax amewahakikishia mabalozi hao utayari wa Serikali ya awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan wa kuendelea kushirikiana na nchi zao kutukeleza diplomasia ya uchumi kwa maslahi ya pande zote mbili.

“Serikali ya awamu ya sita imetoa kipaumbele katika utekelezaji wa diplomasia ya uchumi pamoja na kuendeleza ushirikiano katika sekta mbalimbali zikiwemo sekta za kilimo, elimu, miundombinu, nishati, utalii, ulinzi,” alisema Dkt. Tax.

Kwa upande wake Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini, Mhe. Manfredo Fanti amesema Umoja wa Ulaya unaridhishwa na mazingira ya biashara nchini ambayo ni ishara kuwa wafanyabiashara kutoka nchi za umoja huo wataendelea kuwekeza Tanzania katika sekta mbalimbali kwa maslahi ya pande zote mbili. 

Kadhalika Balozi wa Italia nchini Mhe. Marco Lombardi amesema Tanzania ni nchi yenye utulivu na uchumi wake umeendelea kuimarika jambo ambalo linawafanya waitaliano kuendelea kuwekeza katika sekta mbalimbali. 

Balozi Lombardi ameongeza kuwa wawekezaji wengi wa Italia wako tayari kuwekeza katika sekta za kilimo, miundombinu, elimu, takwimu, uchumi wa bluu pamoja na kuwawezesha wanawake kiuchumi.

Naye Balozi wa Marekani nchni, Mhe. Donald Wright amesema serikali ya Marekani itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania na kuhakikisha Tanzania inatekeleza na kufanikisha vipaumbele vyake ilivyojiwekea kijamii na kichumi hususan biashara na uwekezaji, nishati na utalii.

Kwa upande wake Balozi wa Uingereza nchini, Mhe. David Concar, pamoja na mambo mengine, amesema serikali yake itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuendeleza na kuimarisha uhusiano wake na Tanzania na kutoa uzito kwa mambo ya kimkakati yanayotekelezwa na serikali hususan biashara na uwekezaji, utalii, kilimo na miundombinu.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akizungumza na Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini, Mhe. Manfredo Fantiwalipokutana kwa mazungumzo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akimsikiliza Balozi wa Italia nchini Mhe. Marco Lombardi walipokutana kwa mazungumzo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Balozi wa Marekani nchini, Mhe. Donald Wright akifafanua jambo kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax walipokutana kwa mazungumzo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akizungumza na Balozi wa Uingereza nchini, Mhe. David Concar walipokutana kwa mazungumzo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam


DKT. TAX: WANAWAKE KUJIAMINI, KUJITUMA NDIYO SIRI YA MAFANIKIO

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb) amewataka wanawake kujiamini, kujituma, kujiendeleza, kuwa waungwana na waadilifu wanapotekeleza majukumu yao kwani hiyo ndiyo siri ya mafanikio yao kijamii, kisiasa na kiuchumi.

Dkt. Tax ametoa wito huo alipofungua programu ya mafunzo ya uongozi kwa viongozi wanawake Tanzania, yanayotolewa na Taasisi ya Uongozi, Jijini Dar es Salaam.

Dkt. Tax ameongeza kuwa wanawake wanapswa kuimarisha uwezo wao, kutumia weledi, busara na werevu wa kushawishi, kutiana moyo, kujadili kwa umakini na kufanya maamuzi kwa umahiri na kujiamini, ili nafasi ya mwanamke katika uongozi ithaminiwe na kuthibitisha kuwa watoto wa kike na wanawake wanao uwezo.

Aidha, Waziri Dkt. Tax amesema kuwa uwakilishi wa wanawake katika nafasi za uongozi na ngazi za maamuzi umekuwa ukikua kwa kasi ndogo duniani kote licha ya jitihada mbalimbali za kitaifa na kimataifa zinazoendelea.  

Amesema Idadi ya wanawake viongozi katika taasisi za umma, asasi za kiraia na sekta binafsi imekuwa ikiongezeka ikilinganishwa na miongo iliyopita, lakini bado kasi ni ndogo.

“Tanzania imekuwa ya mfano katika suala hili kwani karibu kila sekta ina wanawake katika nafasi za uongozi na idadi imekuwa ikiongezeka. Tunao viongozi wanawake ambao wanatia hamasa kwa wanawake wanaochipukia katika masuala ya uongozi,” alisema Dkt. Tax 

Waziri Tax amesema ripoti ya Umoja wa Mataifa na Chama cha Mabunge Duniani inaonyesha kuwa hadi Januari 2021, nchi za Bara la Ulaya zikiwemo Norway, Finland, Iceland na Denmark, zinaongoza kwa kuwa na idadi ya wanawake viongozi kwa zaidi ya asilimia 50 kwenye nyadhifa za uwaziri na watendaji wakuu serikalini huku idadi ya wanawake wanaosimamia Wizara nchini Marekani imeongezeka kutoka asilimia 17 mwaka 2020 hadi asilimia 46 mwaka 2021. 

Kwa upande wa Tanzania, “takwimu zinaonesha kuwa tuna asilimia 26 ya wanawake viongozi. Idadi ya Mawaziri wanawake imeongezeka kutoka asilimia 21 mwaka 2020 hadi kufikia asilimia 35 mwaka 2022. Idadi ya Wakurugenzi wanawake imeongezeka kutoka asilimia 19 mwaka 2020 hadi kufikia asilimia 26 mwaka 2022. Idadi ya Majaji wanawake imeongezeka kutoka asilimia 39 mwaka 2020 hadi kufikia asilimia 40 mwaka 2022. Vilevile, idadi ya Wabunge Wanawake kwa mwaka 2022 ni asilimia 36.7 na walioteuliwa ni asilimia 57. Licha ya ongezeko hili, bado tuna kazi ya kuendelea kuwawezesha Wanawake katika sekta mbalimbali ili tuweze kufikia taifa lenye usawa wa kijinsia katika masuala ya Uongozi,” alieleza Waziri Tax .

Waziri Tax aliongeza kuwa Serikali itaendelea kuandaa na kuboresha, sera, sheria, kanuni na miongozo ambayo ni rafiki na wezeshi kwa jinsia zote ili kuiwezesha jamii hususan mwanamke kukabiliana na changamoto. 

Awali akiongea kabla ya ufunguzi wa mafunzo hayo, Balozi wa Finland nchini, Mhe. Theresa Zitting amesema kuwa Serikali yake itaendelea kushirikiana na Taasisi ya Uongozi kutoa elimu kwa jamii kuhusu masuala ya usawa.

“Taasisi ya uongozi bado ina jukumu la kufundisha zaidi watu wengi katika jamii za kitanzania hususan kuwajengea uwezo wanawake ili kuwawezesha kuondokana na unyanyasaji wa kijinsia, kuwapa nafasi ya kutoa maamuzi na kuwaweseha kutekeleza majukumu yao vyeme kwenye jamii zao,” alisema Balozi Theresa.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Shirika la Wanawake la Umoja wa Mataifa (UN – Women) nchini, Bi. Hodan Addou amesema mwanamke anahitaji msaada na mafunzo ya uongozi ili kumuimarisha na kumwezesha kufanya maamuzi sahihi katika jamii. 

“Ni matumaini yangu kuwa kupitia mafunzo haya mtapata ujuzi ambao utawafanya kuwa viongozi bora katika jamii na kuwawezesha kufika malengo yenu kwa weledi zaidi ya sasa,” alisema Bi. Hodan

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akitoa hotuba ya ufunguzi wa programu ya mafunzo ya uongozi kwa viongozi wanawake Tanzania, yanayotolewa na Taasisi ya Uongozi, Jijini Dar es Salaam

Balozi wa Finland nchini, Mhe. Theresa Zitting akielezea fursa na changamoto za uongozi kwa mwanamke katika programu ya mafunzo ya uongozi kwa viongozi wanawake Tanzania, yanayotolewa na Taasisi ya Uongozi, Jijini Dar es Salaam

Mwakilishi wa Shirika la Wanawake la Umoja wa Mataifa (UN – Women) nchini, Bi. Hodan Addou akielezea masuala ya wanawake katika mafunzo ya uongozi kwa viongozi wanawake Tanzania, yanayotolewa na Taasisi ya Uongozi, Jijini Dar es Salaam

Meza kuu ikiongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax katika picha ya pamoja na baadhi ya washiriki wa mafunzo ya uongozi kwa viongozi wanawake Tanzania, yanayotolewa na Taasisi ya Uongozi, Jijini Dar es Salaam 



Saturday, December 3, 2022

BALOZI FATMA ASAINI KITABU CHA MAOMBOLEZO UBALOZI MDOGO WA CHINA

Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab amesaini kitabu cha maombolezo katika Ubalozi wa Mdogo wa China uliopo Mazizini - Zanzibar, kufuatilia kifo cha Rais Mstafu wa Jamhuri ya Watu wa China, Jiang Zemin kilichotokea Novemba 30, 2022. 

Baada ya kusaini kitabu cha maombolezo, Balozi Fatma ametoa salamu za pole kwa Serikali ya Watu wa China na kuwasihi kuendelea kuwa wavumilivu wakati huu wa msiba wa kuondokewa na kiongozi wao mpenda amani, maendeleo na ustawi wa jamii yake.

Rais huyo wa zamani alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 96, Pia Jiang aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Kikomunisti cha China kuanzia 1989 mpaka 2002 alichukua madaraka kutoka kwa Zhao Ziyang. Jiang atakumbukwa kwa kuwa kiongozi hodari na kuwa mwanzilishi wa kutaka kufanya mapinduzi ya kiuchumi hatua ambazo zimezaaa matunda na kupatikana kwa China moja na yenye maendeleo.

Serikali ya Tanzania na Watanzania wake kwa ujumla wanaungana na Serikali ya Watu wa China kuombeleza musiba huo mzito.

Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab akisaini kitabu cha maombolezo katika Ubalozi wa Mdogo wa China uliopo Mazizini - Zanzibar, kufuatilia kifo cha Rais Mstafu wa Jamhuri ya Watu wa China, Jiang Zemin


Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab akizungumza na Balozi Mdogo wa Jamhuri ya Watu wa China anayefanyika Kazi zake Zanzibar Mhe. Zhang Zhisheng baada ya kumaliza kutia saini kitabu cha maombelezi kufuatilia kifo cha Rais Mstafu wa Jamhuri ya Watu wa China Jiang Zemin
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab katika picha ya pamoja na Balozi Mdogo wa Jamhuri ya Watu wa China anayefanyika kazi zake Zanzibar Mhe. Zhang Zhisheng pamoja na Mkurugenzi wa Ofisi za Mambo ya Nje Zanzibar, Bi. Mariam Mrisho baada ya kumaliza kutia saini kitabu cha maombelezi kufuatilia kifo cha Rais Mstafu wa Jamhuri ya Watu wa China Jiang Zemin





RAIS DKT. SAMIA AWATAKA WANAWAKE KUFANYA KAZI KWA BIDII

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amewasihi viongozi wanawake vijana kufanya kazi kwa bidii ili kufikia utekelezaji wa Ajenda 2030 ya Maendeleo Endelevu na Ajenda ya Umoja wa Afrika ya mwaka 2063. 

Mhe. Dkt. Samia ametoa wasaa huo wakati akifungua Kongamano la nne la Wanawake Vijana wa Mtandao wa Viongozi Wanawake Barani Afrika (AWLN) lililofanyika visiwani Zanzibar na kuwataka wanawake kufanya kazi kwa bidii ili kuendelea kuchangia maendeleo katika sekta mbalimbali kwenye jamii zao.

Pamoja na mambo mengine, Dkt. Samia amebainisha kuwa Tanzania inatambua na kuzingatia uwezo wa kitaaluma wa wanawake katika kufanya kazi na hivyo kupelekea idadi ya viongozi wanawake kuongezeka katika vyombo vya maamuzi (Bunge) kutoka asilimia 21.5 kwa mwaka 2005 hadi kufikia asilimia 37 mwaka 2020. 

“Idadi ya Majaji wanawake imeongezeka kutoka aslimia 34 mwaka 2005 hadi aslimia 39 mwaka 2022, Mabalozi wanawake na Makamishna Wakuu kutoka asilimia 3 mwaka 2005 hadi asilimia 21 mwaka 2022, Wakuu wa Mikoa Wanawake wamepanda kutoka aslimia 10 mwaka 2005 hadi asilimia 23 mwaka 2022, pamoja na Wakuu wa Wilaya Wanawake wameongezeka kutoka asilimia 19 mwaka 2005 hadi 29 mwaka 2022,” alisema Dkt. Samia

“Tunataka kuhakikisha kwamba wanawake wanaingia kwenye masoko ya kikanda na kuyatumia masoko hayo kama hatua ya kwenda mbali zaidi hadi kwenye masoko ya nje,” aliongeza Rais Dkt. Samia

Kwa Upande wake Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la watu wa Ethiopia, Mhe. Sahle-Work Zewde amesema kuwa ni wakati muafaka kwa Bara la Afrika kufanya mabadiliko ya uongozi kwa kuwapa nafasi za uongozi wanawake vijana ili waweze kuchangia maendeleo katika katika jamii zao pamoja na kuwahamasisha wengine kuwa wanawake wanaweza.

“Tunaamini kuwa wanawake vijana wakiendelezwa na kupatiwa mafunzo na ujuzi wa taaluma mbalimbali wataongoza vyema zaidi kuliko ilivyo kwa sasa, mfano wakipatiwa mafunzo ya usuluhishi wa migogoro watakuwa na msaada mkubwa wa kuchagiza amani katika jamii zetu,” alisema Mhe. Zewde

Awali akiongea katika kongamano hilo, Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini, Bw. Zlatan Milisic, amesema ni muhimu katika jamii wanawake kujumuishwa katika nafasi za maamuzi ili kupunguza migogoro katika jamii.

“Endapo wanawake vijana watashirikishwa katika hatua rasmi na zisizo rasmi za kufanya maamuzi ili kushughulikia changamoto mbalimbali katika jamii zetu itasaidia kuwajengea uwezo na kuwapatia maendeleo yao wenyewe,” alisema Bw. Millisci.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akitoa hotuba ya ufunguzi wakati wa  Kongamano la nne la Wanawake Vijana wa Mtandao wa Viongozi Wanawake Barani Afrika (AWLN) lililofanyika visiwani Zanzibar 

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la watu wa Ethiopia, Mhe. Sahle-Work Zewde akizungumza na washiriki wa Kongamano la nne la Wanawake Vijana wa Mtandao wa Viongozi Wanawake Barani Afrika (AWLN) lililofanyika visiwani Zanzibar  

Viongozi waandamizi wa Serikali wakifuatilia Kongamano

Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini (UN), Bw. Zlatan Milisic akiwasilisha salamu za UN kwa washiriki wa Kongamano la AWLN 





CFR YATAKIWA KUONGEZA WIGO WA PROGRAMU KUKIDHI MAHITAJI

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb) wakati wa mahafali ya 25 ya Chuo cha Diplomasia alipowatunuku vyeti wahitimu 990 katika ngazi ya Astashahada ya Juu, Shahada, Stashahada na Astashahada katika fani ya diplomasia yaliyofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam

 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb) (katikati) katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wa Chuo cha CFR wakati wa mahafali ya 25 ya Chuo hicho  yaliyofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam

 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb) (katikati) katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wa Chuo cha CFR na wahitimu wakati wa mahafali ya 25 ya Chuo hicho yaliyofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam


Baadhi ya Wahitimu wa Chuo cha Diplomasia (CFR) wakiimba Wimbo wa Taifa wakati wa mahafali ya 25 ya Chuo hicho yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam
Baadhi ya Wahitimu wa Chuo cha Diplomasia (CFR) wakiimba Wimbo wa Taifa wakati wa mahafali ya 25 ya Chuo hicho yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam
Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la Chuo cha Diplomasia (CFR) Balozi Ramadhan Mwinyi (aliyekaa) akiwa na wahitimu ambao walishinda tuzo za kuwa wanafunzi bora katika moja ya kozi zinazotolewa na chuo hicho wakati wa mahafali ya 25 ya chuo hicho yaliyofanyika jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (aliyekaa) akiwa na wahitimu ambao walishinda tuzo za kuwa wanafunzi bora katika moja ya kozi zinazotolewa na chuo hicho wakati wa mahafali ya 25 ya chuo hicho yaliyofanyika jijini Dar es Salaam
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (aliyekaa) akiwa na wahitimu ambao walishinda tuzo za kuwa wanafunzi bora katika moja ya kozi zinazotolewa na chuo hicho wakati wa mahafali ya 25 ya chuo hicho yaliyofanyika jijini Dar es Salaam
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb) akiaga wahitimu aliowatunuku vyeti wakati wa mahafali ya 25 ya Chuo cha Diplomasia baada ya kumalizika kwa mahafali hayo yaliyofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam

 

 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb) amekitaka Chuo cha Diplomasia (CFR) kuongeza wigo wa program zake ili kukidhi mahitaji ya sasa na ya baadae. 

Dkt. Tax ametaka ongezeko hilo la wigo lifanyike kwa kuwatumia wataalamu wa ndani na nje ya chuo ambao wana uwezo na maono mapana. 

Waziri Dkt. Tax ametoa kauli hiyo leo Jijini Dar es Salaam wakati wa mahafali ya 25 ya Chuo hicho ambapo aliwatunuku vyeti wahitimu 990 katika ngazi ya Astashahada ya Juu, Shahada ya kwanza, Stashahada na Astashahada katika fani ya diplomasia. 

 “Mahitaji ya utaalamu katika Diplomasia yanaendelea kupanuka, kulingana na mahitaji yanayoendelea kujitokeza Kitaifa na Kimataifa,hususan katika Diplomasi ya Uchumi. Hivyo ni muhimu kwa Chuo kupanua progamu zake ili kukidhi mahitaji ya sasa, na siku za usoni. Hatua hii iende sanjari na kuwatumia wataalamu ndani ya Chuo, na nje ya Chuo, wenye uwezo na maono mapana,” alisema Dkt. Tax. 

Dkt. Tax amekipongeza Chuo cha CFR kwa kazi nzuri wanayoifanya na kutoa wahitimu wenye ueledi na mahiri wanaotambulika kitaifa na kimataifa na kuwataka wahakikishe wanatekeleza mikakati yao kikamilifu na hivyo kukamilisha lengo la kuanzishwa kwa chuo hicho

Amewataka kuhakikisha wanashirikiana na taasisi nyingine ili kuongeza elimu na ujuzi na hivyo kunufaisha wanafunzi wao hasa ikizingatiwa kuwa dunia ya sasa inahitaji ushirikiano na taasisi nyingine. 

 Amesema CFR kimetoa wahitimu mahiri na ni matarajio ya Serikali kuwa kila mtumishi atatimiza wajibu wake kwa kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa na kuzingatia maadili ya kiutumishi ili kuendelea kutoa wahitimu wenye ubora wa kitaaluma wenye maadili mema na mwenendo mwema. 

Amewataka wanachuo wanaobaki kuendelea kujifunza kwa bidii na kuiga mfano wa wanaohitimu wa tabia njema na mwenendo mwema na kujituma katika masomo yao ili kuendelea kuilinda sifa nzuri ya chuo tangu kuanzishwa kwake. 

Amekitaka chuo kuongeza mafunzo ya strategia, kufanya tafiti mahsusi na kutoa ushauri kwa serikali na wadau wengine katika sehemu ya strategia na diplomasia na kuweka mikakati ya pamoja na kutoa ushauri kwa Serikali na wadau wake jinsi ya kuwa na mwelekeo sahihi wa kukabiliana na changamoto zinazoikabili Tanzania na dunia kwa ujumla. 

“Chuo lazima kiongeze mafunzo ya strategia, kifanye tafiti mahsusi na kutoa ushauri kwa serikali na wadau wengine katika sehemu ya strategia na diplomasia. Tafiti kama hizo zitachangia kuimarisha diplomasia na kuweka mikakati ya pamoja ya jinsi ya kukabiliana na changamoto zinazoikabili Tanzania na dunia kwa ujumla,’ alisema Dkt. Tax 

Amekitaka chuo cha CFR kuhakikisha kinaelimisha taifa kupitia mijadala na makongamano ili kupanua uelewa na kujenga uzalendo kwa kujumuisha jamii katika masuala ya strategia na diplomasia na kuongeza kuwa diplomasia na strategia ni vitu vipana, na vyote vinagusa kila eneo na kwamba ni vizuri Chuo kikajipanga kwendana na dunia inavyokwenda. 

“Chuo hiki hakina budi kuendelea kuelimisha taifa kwa mijadala na makongamano kwa lengo la kupanua uelewa kujenga uzalendo na kujumuisha jamii katika masuala ya strategia na diplomasia, haya hayako nje ya wigo wa shughuli zenu, diplomasia ni kitu kipana na strategia ni kitu kipana pia na vyote vinahusu karibu kila eneo, kwa hiyo ni vizuri tukaenda na dunia inavyokwenda, sasa tunaongelea diplomasia ya uchumi lakini pia ipo diplomasia ya ulinzi na katika maeneo mbalimbali, tujipange vyema kwa kujua dunia inaenda namna gani na mafunzo tunayotoa yanaendaje katika kukabiliana na changamoto tulizonazo katika eneo hili,” alisisitiza Dkt. Tax