Tuesday, November 15, 2011

TANZANIA YAISHUKURU JUMUIYA YA KIMATAIFA

Balozi Rajabu Gamaha,Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,akihutubia mwishoni mwa wiki mkutano wa Baraza kuu la 66 la Umoja wa Mataifa.

Katika Mkutano huo, Marais wa Mahakama za Kimataifa za Makosa ya jinai za Mauaji ya Kimbari Rwanda (ICYR) na Mauaji ya halaiki ya iliyokuwa Yugoslavia ya zamani ( (ICYT) waliwasilisha taarifa zao za mwaka mbele ya wajumbe wa mkutano huo. katika hotuba yake, Balozi Gamaha pamoja na mambo mengine aliishukuru Jumuiya ya Kimataifa kwa kuendelea kuiamini Tanzania kwamba inastahili kuwa mwenyeji wa Tawi la Mfumo wa Kimataifa wa kushughulikia umaliziaji wa mashauri ya masalia ya Mahakama ya Kimataifa ya Rwanda. Jukumu hilo linakwenda sambamba na uhifadhi na utunzaji wa nyaraka na kumbukumbu zote muhimu zinazohusu mahakama hiyo. Mahakama ya Kimataifa ya mauaji ya Kimbari ( ICTR) iliyoko Mkoani Arusha inatarajiwa kumaliza kazi zake mwaka 2014. Na mfumo huo wa kimataifa wakushughulikia umaliziaji wa mashauri ya masalia ambao tawi lake litakuwa pia Mkoani Arusha utaanza kazi 2012.

Na Mwandish Maalum

New York

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imeishukuru Jumuiya ya Kimataifa kwa kuiamini kwa mara nyingine, kwamba inastahili kuwa tawi la Mfumo wa Kimataifa wa kushughulikia Umaliziaji wa Mashauri ya Masalia ya Mahakama ya kimataifa ya mauaji ya kimbari ya Rwanda( ICTR).

Shukrani hizo zimetolewa mwishoni mwa wiki na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Rajabu Gamaha, wakati Mkutano Baraza Kuu la 66 la Umoja wa Mataifa ulipopokea na kujadili taarifa za mwaka za utendaji kazi wa Mahakama za Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari Rwanda (ICTR) na Mauaji ya halaki ya iliyokuwa Yugoslavia ya Zamani (ICTY).

Mwaka jana Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa, lilipitisha azimio namba 1966 la kuanzisha Mfumo wa Kimataifa wa kushugulikia umalizaji wa mashauri ya masalia ( International Residual Mechanism) ikihusisha pia uhifadhi wa nyaraka na kumbukumbu muhimu za mahakama hizo mbili.

Kupitia Azimio hilo, Arusha-Tanzania ambayo imekuwa Makao Makuu ya ICTR ndiyo inatakayoendelea na jukumu hilo na The Hague , Uholanzi itakuwa tawi la ICTY

Naibu Katibu Mkuu Balozi Rajabu Gamaha, akaeleza kwamba kutokana na jumuia hiyo kuendelea kuiamini Tanzania kubeba jukumu hilo. Tanzania imejiandaa na iko tayari kutekeleza wajibu huo.

“Kwa niaba ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na watu wake, ninatoa shukrani za dhati kwa jumuia ya kimataifa kwa kuiamini Tanzania kwa mara nyingine, kwamba tunastahili kulibeba jukumu hili, tumejiandaa na tuko tayari.” Akasema Balozi Gamaha.

Akaeleza kuwa Serikali ya Tanzania imekuwa ikifuatilia kwa karibu azimio lililopitisha kuanzishwa kwa mfumo huo, mfumo utakaohakikisha kwamba haki inatendeka na hukumu zinatolewa kwa watuhumiwa waliobaki.

Akasisitiza kwamba, serikali kama ilivyotoa ushirikiano kwa mahakama ya ICTR, itatoa ushirikiano wote wa kiutawala na kiutendaji kwa Mfumo huo unaotarajiwa kuanza kazi zake Julai mosi mwaka 2012.

Akizungumzia kipindi cha mpito kuelekea kumaliza kazi kwa mahakama hiyo na kuanza kazi kwa Mfumo. Naibu Katibu Mkuu ameelezea masikitiko ya Tanzania kuhusu suala zima la uondokaji wa wataalamu wenye uzoefu na ambao wameitumikia mahakama hiyo kwa muda mrefu.

Balozi Rajabu Gamaha, amesema uamuzi wa wafanyakazi wenye ujuzi wakiwa wamesheheni kumbukumbu na historia ya mahakama hiyo kuondoka kwenda kutafuta kazi sehemu nyingine siyo tu kutaathiri kipindi hiki cha mpito bali kutapoteza hazina na kumbukumbu walizonazo watumishi hao.

Akatumia fursa hiyo kuuomba Umoja wa Mataifa na jumuia ya kimtaifa kuendelea kutoa ushirikiano kwa mahakama hiyo ikiwa ni pamoja na kutafuta njia muafaka na kuendelea kuwa na watumishi wazoefu kuelekea kipindi cha mpito.

Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda inatakiwa kukamilisha kazi zake si zaidi ya Desemba 31, 2014

Awali akiwasilisha taarifa yake, Rais wa Mahakama ya Rwanda Jaji Khalida Rachid Khan, ameelezea baadhi ya changamoto zinazoikabili mahakama hiyo katika kipindi hiki cha mpito kuwa ni pamoja na kuondoka kwa wafanyakazi wanaokwenda kutafuta kazi za kudumu.

“ pamoja na mafanikio mengi yakiwamo ya kukamilisha baadhi ya kesi zikiwamo utoaji wa hukumu za kihistoria kwa watuhumiwa kadhaa katika kipindi hiki cha mwaka mmoja. Tuna tatizo kubwa la wafanyakazi kuondoka.”

Na kufafanua kwamba wafanyakazi hao wanaondoka kwenda kutafuta kazi za kudumu na zenye maslahi mazuri kwa kutambua kwamba mahakama hiyo inamaliza muda wake na hivyo kutokuwa na uhakika wa hatima yao ya baadaye.

Akaeleza changamoto nyingine kuwa ni ile ya kushindwa kuwafikishwa mbele ya mkondo wa sheria watuhumiwa tisa wa mauaji ya kimbari.

Miongoni mwa watuhumiwa hao, wapo watatu wanaosadikiwa kuwa ni watuhumiwa muhimu ambao wametajwa kuwa ni Felicien Kabuga, Protais Mpiranya na Augustin Bizimana.

Akatumia fursa hiyo kuzitaka nchi za Maziwa Makuu kutoa ushirikiano wa kuwakamata na kuwafikisha mahakamani watuhumiwa ambao wanasadikiwa kuwa katika nchi hizo.

Baadhi ya wazungumzaji wengine waliozungumza wakati mkutano huo, akiwamo Mwakililishi wa Jumuia ya Ulaya, wamesema watatoa ushirikiano wa karibu kwa Mfumo wa wa kimataifa wa kushughulikia umalizaji wa mashauri ya masalia ya mahakama ya Rwanda (ICTR) huku wakitoa msisitizo wa Nchi za Maziwa Mkuu kuwakamata wahutumiwa waliobakia.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.