Wednesday, June 13, 2012
Rais apokea Special Envoys kutoka DRC na Sudan Kusini
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumatano, Juni 13, 2012, amepokea ujumbe maalum kutoka kwa wajumbe maalum wa marais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Mheshimiwa Salva Mayardit Kiir wa Jamhuri ya Sudan Kusini.
Ujumbe wa Rais Kabila umewasilishwa kwa Rais Kikwete na Waziri wa Mambo ya Nje wa DRC na Mjumbe Maalum wa Rais Kabila, Mheshimiwa Raymond Tschibanda wakati ujumbe wa Rais Kiir umewasilishwa na Mheshimiwa Nhial Deng Nhial, Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan Kusini na Mjumbe Maalum wa Rais Kiir.
Rais Kabila katika ujumbe wake maalum kwa Rais Kikwete amemwelezea hali ya kiusalama ilivyo katika eneo la Kaskazini la Mkoa wa Kivu, Mashariki mwa DRC, kufuatia chokochoko na mapigano mapya yaliyoanzishwa na jambazi la kivita linalotafutwa kimataifa, Jenerali Bosco Ntaganda.
Mheshimiwa Tschibanda amemweleza Rais Kikwete jinsi vitendo cha Jenerali Ntaganda na wapiganaji ambao amesema awali idadi yao ilikuwa kati ya 200 na 250, lakini sasa imeanza kuongezeka, vinavyoleta hali ya wasiwasi na hofu mashariki mwa nchi hiyo hata kama shughuli za kikundi hicho zinaelezwa kuendeshwa katika eneo dogo lisilozidi kilomita za mraba kati ya tatu na tano.
“Mheshimiwa Rais, kwa jumla DRC imetulia kisiasa na kiusalama, lakini eneo la Kivu Kaskazini, mashariki mwa nchi yetu linaleta wasiwasi na hofu kubwa kwa sababu Jenerali Ntaganda ameanza tena chokochoko. Tuna ushahidi kuwa ameanza kupanua ukubwa wa kikundi cha wapigaji wake na amepata silaha kubwa,” Mheshimiwa Tschibanda amemwambia Rais Kikwete.
Naye Mheshimiwa Nhial amemweleza Rais Kikwete kuhusu mazungumzo ya karibuni kati ya Jamhuri ya Sudan Kusini na Sudan yaliyofuatia mapigano ya kugombea mpaka kati ya mataifa hayo mawili ambayo hadi mwaka jana yalikuwa nchi moja.
Katika ujumbe wake, Rais Kiir amemwomba Rais Kikwete kuunga mkono msimamo wa Sudan Kusini wa kutaka mzozo wa mpaka na rasilimali zilizoko katika eneo hilo la mpaka kati ya nchi hizo mbili upelekwe kwenye vyombo vya usuluhishi vya kimataifa kwa uamuzi wa mwisho.
Tanzania ni mwanachama wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika (AU) na Sudan Kusini ingependa kuona Umoja huo unapanga muda wa kuzungumzia hali ya mpaka kati ya nchi hizo wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa AU unaofanyika baadaye mwezi huu mjini Addis Ababa, Ethiopia.
……..Mwisho………..
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.