TAARIFA KWA VYOMBO VYA
HABARI
Waziri Mkuu wa
Thailand, Mheshimiwa Yingluck Shinawatra, anatarajiwa kuwasili jijini Dar es
Salaam kesho, tarehe 30 Julai, 2013 mchana kwa ziara ya siku tatu nchini
Tanzania kwa mwaliko wa Rais Jakaya Mrisho
Kikwete.
Bibi Shinawatra,
ambaye atatokea Msumbiji, atalakiwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Julius Nyerere na mwenyeji wake, Rais Kikwete, na kupigiwa mizinga 19 kwa heshima yake.
Wakati wa adhuhuri, Waziri
Mkuu wa Thailand atafanya mazungumzo rasmi na Rais Kikwete, Ikulu na baadaye kutia
saini mikataba mbalimbali ya ushirikiano kati ya Tanzania na Thailand.
Kabla ya kuhudhuria dhifa
ya Taifa itakayoandaliwa na mwenyeji wake, Ikulu, Bibi Shinawatra, ambaye anafuatana
na ujumbe wa wafanyabiashara takriban 70 wa Thailand, atahutubia mkutano wa Uwekezaji
wa Biashara kati ya Thailand na Tanzania kwenye Hoteli ya Hyatt Regency
Kilimanjaro, ambao utahudhuriwa na Wafanyabiashara na Wawekezaji kutoka
Thailand na wawekezaji wa ndani (Tanzania), Wanadiplomasia, Wasomi na Viongozi mbalimbali
kutoka serikalini. Katika mkutano huo, Waziri Mkuu wa Thailand ataelezea sera
ya uchumi ya nchi yake kwa Tanzania na Bara la Afrika. Baada ya hapo, Waziri Mkuu
huyo atazuru maonyesho ya biashara hotelini hapo.
Katika siku ya pili ya
Ziara yake, Mgeni huyo wa Taifa atatembelea Mbuga ya Wanyama ya Serengeti
mkoani Mara, ambako atajifunza namna Mamlaka za Tanzania zinavyosimamia na kutunza
Hifadhi za Taifa za Wanyamapori. Waziri Mkuu Shinawatra atakabidhi Vifaa mbalimbali
vya kupambana na majangili kwa Mamlaka ya Taifa ya Hifadhi za Wanyama (TANAPA).
Mgeni huyo atarejea
Dar es Salaam tarehe 1 Agosti na kuagwa na mwenyeji wake, Rais Kikwete kwenye Uwanja
wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, tayari kwa safari ya kuelekea nchini Uganda.
IMETOLEWA
NA: WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA,
DAR
ES SALAAM
Julai
29, 2013
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.