M23
yachakazwa
Na Habari Leo
KIKUNDI cha waasi cha M23 kinachopambana na jeshi la Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo (DRC), kimeripotiwa kupigwa vibaya na kutikisa nguvu za kikundi
hicho kutokana na baadhi ya wapiganaji wake kuripotiwa kupoteza maisha.
Mapigano baina ya M23 na Jeshi la Serikali ya DRC linalosaidiwa
na Kikosi Maalumu cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa (MONUSCO), yameibuka
upya ndani ya wiki hii.
Habari za kiintelijensia ambazo gazeti hili limezipata zinasema
kuwa, kutokana na shambulio hilo, Serikali ya Rwanda imelazimika kuingilia kati
kusaidia waasi hao kwa kupeleka bataliani mbili zenye jumla ya askari 1,700
huko DRC, ili waweze kukabiliana na nguvu ya majeshi ya DRC, Monusco na Brigedi
ya Majeshi ya Kulinda Amani ya Umoja wa Mataifa yenye mamlaka ya kujibu mapigo
(FIB).
Kwa mujibu wa vyanzo hivyo vya habari, Rwanda imepeleka bataliani
hizo mbili zenye askari 850 kila moja saa 24 zilizopita na kwamba wamevuka
mpaka kuingia DRC katika eneo la Kibumba, lakini wanashindwa kusonga mbele.
Habari zaidi zinasema sababu ya Rwanda kupeleka askari wake hao
ni kusaidia M23 ambao walipigwa sana Agosti 23 na 27, mwaka huu katika eneo la
vilima vya Kibati na haijulikani kama kweli waasi hao wako katika eneo hilo au wamekwishakimbia
kutokana na kipigo walikichopata.
“M23 walitandikwa sana Agosti 23 na 27 katika eneo la vilima
vya Kibati, na wala haijulikani kama wapo hai au vipi, ndio maana sasa hivi
Rwanda imepeleka batalioni zao kuwapa nguvu, lakini wanashindwa kusonga mbele
maana hawajielewi kwa sababu ya kipigo walichopata,” kilisema chanzo kimoja cha
habari.
Kwa mujibu wa vyanzo hivyo vya habari, eneo la Kibati ndilo
eneo kubwa la M23 ambalo wamekuwa wakitumia kuhifadhi silaha zao za kivita,
lakini wakati wa mapambano majeshi ya DRC, MUNUSCO na FIB yalisambaratisha kabisa
ngome hiyo ya waasi.
FIB inaundwa na askari wengi wa Afrika Kusini na Tanzania. Habari
zaidi zinasema kwa sasa majeshi ya DRC, Monusco na FIB yanawasubiri kwa hamu
askari hao wa Rwanda kuingia uwanja wa vita ili kukabiliana nao kama walivyokabiliana
na waasi wa M23.
“Taarifa tulizonazo hivi sasa Rwanda inajiuliza iwapo isonge mbele
kupambana au irudi nyuma, ikifikiria pia kipigo walichopata M23,” kilisema
chanzo kimoja cha habari.
Inaelezwa kwamba, kutokana na kipigo walichopata M23 siku chache
zilizopita kimepelekea Rwanda kujikuta ikikiri na kusema ukweli juzi kuwa
inakisaidia kikundi hicho cha waasi.
Vyanzo hivyo vya habari viliendelea kusema kuwa, mwaka jana mwezi
Mei, Baraza la Usalama la UN katika ufuatiliaji wake lilibaini majeshi ya
Rwanda kushiriki vurugu zinazoendelea ndani ya DRC, hali iliyosababisha Nchi za
Maziwa Makuu kuingilia kati ili kuleta suluhu bila kuishirikisha Rwanda ambayo
ilionekana kuwa na maslahi ndani ya mgogoro huo.
Katika hatua nyingine, taarifa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa zilisema, Waziri Bernard Membe alikutana na Mabalozi
wa Mataifa matano ambayo ni wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
ili kujadili masuala mbalimbali ya Kikanda na hasa mgogoro wa DRC.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, Waziri Membe alipokutana na mabalozi
hao alishukuru Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kutoa tamko la kulaani
vikali tukio la kuuawa kwa mlinzi wa Amani wa Tanzania na kutuma salamu za pole
kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na familia ya marehemu.
Waziri Membe pia aliomba baraza hilo kuitaka Rwanda kuacha
kuingiza majeshi yake DRC kwa nia ya kusaidia waasi wa M23 na kuongeza kuwa
linapokuja suala la FIB wito wao ni “akishambuliwa mmoja, wameshambuliwa wote.”
Mabalozi aliokutana nao Waziri Membe ni kutoka Urusi,
Uingereza, Ufaransa, Marekani na China, nchi ambazo zinajulikana kama wajumbe
wa kudumu wa Baraza hilo la Usalama.
Wakati huo huo, Waziri Membe alisema Rais Yoweri Museveni ameitisha
kikao cha dharura cha Nchi za Maziwa Makuu, mjini Kampala ili kujadili mgogoro huo
wa DRC kitakachofanyika Septemba 4 na Septemba 5, mwaka huu. Alisema Septemba 4
utakuwa mkutano wa Mawaziri na Septemba 5 utakuwa mkutano wa Marais wa nchi
hizo.
Katika hatua nyingine, jeshi la Afrika Kusini limetamba kuwa lipo
tayari kuongeza nguvu kwa wapiganaji wa Monusco kwa kuwa wanaamini wana jeshi
imara lenye uwezo wa kuchakaza `wakorofi’.
Kauli hiyo imetolewa na Luteni Jenerali wa Jeshi la Afrika
Kusini, Derrick Ngwebi alipozungumza na wapiganaji katika kambi ya Thaba Tshwane,
jijini Pretoria. “Tuko imara na tayari kwa lolote huko DRC. Hatuna chembe ya shaka,”
alisema na kuongeza kuwa, Umoja wa Mataifa umewaomba Afrika Kusini kuongeza
zana za kivita huko Mashariki kwa DRC.
“Kikosi cha mizinga kinatoka Tanzania na kimeshatua DRC. Kwa
upande wa helikopta za kivita Umoja wa Mataifa ulituomba tujiandae, nasi
tumefanya hivyo na nawahakikishieni, kazi itafanyika,” alisema Ngwebi na
kuongeza kuwa, imeshatanguliza askari na helikopta tatu za kivita wakati
ikijipanga kupeleka helikopta zaidi na za kisasa za kivita.
Wiki iliyopita, Rais Jacob Zuma aliliambia Bunge la Afrika
Kusini kuwa nchi yake imeshapeleka askari 1,345 huko Mashariki na DRC.
Kwa hisani ya: www.habarileo.co.tz
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.