Mhe. Naibu Waziri akikagua shughuli za wajasiriamali
Watanzania katika soko la Comesa. Kulia kwa Naibu Waziri ni Mhe.
Grace Mujuma, Balozi wa Tanzania nchini Zambia na kushoto ni Bw. Mboweto, Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Soko la Comesa ambaye ni Mtanzania.
Naibu Waziri azungumza na Wajasiriamali wa Kitanzania, Lusaka
Mhe. Mahadhi Juma Maalim (Mb.),
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania amewatembelea Wajasiriamali ambao ni Raia wa Tanzania wanaoishi na kufanya
shughuli zao nchini Zambia katika maeneo ya Viwanja vya COMESA. Katika ziara
hiyo iliyofana, Mhe. Naibu Waziri aliambatana na Mhe. Grace Mujuma, Balozi wa
Tanzania nchini Zambia pamoja na Maofisa wengine wa Wizara ya Mambo ya Nje.
Baada ya kutembelea mabanda mbalimbali na kukagua shughuli zinazofanywa na
Watanzania hao, Mhe. Naibu Waziri alipata fursa ya kubadilishana nao mawazo.
Watanzania hao walielezea furaha yao kwa kutembelewa na kiongozi wa Serikali ya
Tanzania na kubainisha kufarijika kwao kwa namna Serikali yao inavyowajali.
Waliomba juhudi zifanyike kupanua barabara katika eneo la Tunduma ili kupunguza
msongamano wa magari katika eneo hilo. Aidha, waliomba mashauriano yafanyike
ili kituo cha mpaka cha Tunduma/Nakonde kifanye kazi kwa masaa 24. Walisema
hatua hiyo itasaidia kuondoa msongamano, kuongeza kasi ya biashara, kupunguza
vitendo vya jinai na kuiongezea mapato Serikali.
Kwa upande wake, Mhe. Naibu Waziri aliwapongeza Watanzania hao kwa kuamua kufanya shughuli
zinazoweza kuwapatia kipato cha halali na kujenga taifa lao. Aliwataka wahakikishe
kwamba wote wanaishi kisheria na kufuata taratibu zilizowekwa na mamlaka za
Zambia ili kuepusha usumbufu kwao na kwa Serikali. Aidha, aliwataka
wasijihusishe na vitendo vyovyote vya jinai ili kuepusha kuchafua sifa
nzuri za taifa la Tanzania.
Mhe. Naibu Waziri yupo nchini Zambia akiongoza ujumbe wa Tanzania katika
mkutano wa kimataifa kuhusu Mkataba unaolenga Kutokomeza matumizi ya Mabomu ya
kusambaa (Convention on Cluster Munitions). Kabla ya kutembelea wajasiriamali,
Mhe. Naibu Waziri alikutana na kuzungumza na Watanzania wa rika na kada
mbalimbali wanaoishi nchini Zambia, mazungumzo ambayo yalifanyika katika
Ubalozi wa Tanzania, Lusaka
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.