----------------------------------------
MKUTANO WA 12 WA MAWAZIRI WA MAMBO YA NJE WA JUMUIYA YA MADOLAWAFANYIKA
MJINI NEW YORK.
Waziri wa Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe ameshiriki Mkutano wa 12
wa Mawaziri wa Mambo ya Nje kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola uliofanyika
Mjini New York sambamba na Kikao cha 68 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa
kujadili masuala mbalimbali muhimu kuhusu Jumuiya hiyo.
Wakati wa Mkutano huo,
Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo Mhe. Kamalesh Sharma alitoa taarifa kwa Mawaziri
kuhusu kupitishwa kwa Mpango Mkakati wa miaka minne kuanzia mwaka 2013/2016 ulioandaliwa na
Sekretarieti ya Jumuiya hiyo ili kuiwezesha kukidhi mahitaji ya nchi
wananchama. Mpango Mkakati huo umezingatia masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja
na kuhakikisha nchi wanachama zinafuata utawala wa sheria, zinaimarisha
demokrasia, zinaheshimu haki za binadamu pamoja na kuzingatia usawa wa
kijinsia.
Katika maelezo yake,
Mhe. Sharma alisema kuwa, Sekretarieti ya Jumuiya ya Madola inaendeleza
jitihada zake kuzisaidia nchi wanachama kuimarisha demokrasia na maendeleo
endelevu ambapo pamoja na mambo mengine waangalizi katika chaguzi mbalimbali
zinazofanyika katika nchi wanachama wamekuwa wakipelekwa ikiwa ni pamoja
chaguzi zilizofanyika hivi karibuni katika nchi na Ghana, Maldives na Sri
Lanka.
Aidha, Mawaziri hao walipata fursa pia ya kupitia
utekelezaji wa mapendekezo yaliyotolewa na Jopo la Watu Mashuhuri wa Jumuiya
hiyo (EPG) kuhusu mageuzi katika Jumuiya hiyo. Vile vile ilielezwa kuwa, Katika
kutekeleza mapendekezo hayo, Sekretarieti ya Jumuiya ya Madola imeanzisha
mipango mbalimbali ikiwa ni pamoja na
kuunda Kikundi cha Wataalam kwa ajili ya kutafuta fedha ili kuiwezesha Sekretarieti kuzisaidia nchi
wanachama zilizoathiriwa na mabadiliko ya tabianchi na zile zinazoendelea.
Katika hatua nyingine,
Mawaziri hao walipokea taarifa kuhusu maandalizi ya Mkutano wa Wakuu
wa Nchi na Serikali (CHOGM) unaotarajiwa kufanyika mjini Colombo, nchini Sri
Lanka mwezi Novemba, 2013.
Akizungumza kuhusu
maandalizi ya mkutano huo wa CHOGM ambao hufanyika kila baada ya miaka miwili,
Waziri wa Mambo ya Nje wa Sri Lanka, Mhe. G.L. Peiris alisema kuwa, nchi yake
imekamilisha maandalizi yote muhimu kwa ajili ya mkutano huo na kuwahakikishia
Mawaziri hao kuwa hali nchini kwake ni ya amani na usalama tofauti na taarifa
zinazotolewa na baadhi ya nchi kuwa hali si shwari nchini humo.
Tanzania ni miongoni
mwa nchi wanachama 54 wa Jumuiya ya Madola ambayo Kiongozi wake Mkuu ni Malkia
Elizabeth II wa Uingereza.
-Mwisho-
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.