Mhe. Bernard K. Membe (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa akiongea na waandishi wa habari mapema leo kwenye ukumbi wa mkutano wa Wizara ya Mambo ya Nje, jijini Dar es Salaam. Kulia ni Balozi Rajabu Gamaha, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje.
Waandishi wa habari waliokusanyika kumsikiliza Mhe. Waziri Membe.
Uongozi wa Wizara ya Mambo ya Nje ukijumuisha Balozi Irene Kasyanju (kushoto), Mkurugenzi wa Kikengo cha Sheria, Balozi Simba Yahya (wa pili kushoto), Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati, Balozi Mbelwa Kairuki (wa tatu kushoto), Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia na Balozi Dora Msechu (wa nne kushoto), Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika.
Wengine waliohudhuria Mkutano huo ni Bw. Mkubwa Ally (kushoto), Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali cha Wizara ya Mambo ya Nje, Bw. Thobias Makoba (katikati) na Bw. Togolani Mavura (kulia), Wasaidizi wa Mhe. Waziri Membe.
Kwenye Mkutano pia alikuwepo Bw. Kaaya (wa pili kulia), Kaimu Mkurugenzi Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa
Mmoja wa waandishi wa habari kutoka gazeti la The Citizen, Bw. Mkinga Mkinga akiuliza swali kwa Mhe. Waziri Membe.
Mhe. Waziri Membe akifafanua ombi la Kenya kuhusu uhalali wa kuwafikisha Viongozi Wawili wa juu wa Serikali ya Kenya kwenye Mahakama ya Kimatafa (ICC) kujibu Makosa ya Jinai. Kulia ni Balozi Rajabu Gamaha na kushoto ni Balozi Vincent Kibwana, Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Wakurugenzi wakisikiliza kwa makini maswali mbalimbali yaliyokuwa yakiulizwa na waandishi wa habari (hawapo pichani). Kulia ni Bw. Mndeme, Mkurugenzi wa Idara
ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu, na Bw. Ligaganya, Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango.
Mhe. Waziri Membe akihojiwa na Bw. Erick David Nampesya, Mwandishi/Mtangazaji kutoka Shirika la Habari la BBC.
Membe: Hakuna Kiongozi wa
Afrika kupelekwa ICC
Na TAGIE DAISY MWAKAWAGO
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Mhe. Bernard K. Membe (Mb), akutana na waandishi wa habari leo kujadili uhalali
wa kuwafikisha Viongozi Wawili wa juu wa Serikali ya Kenya kwenye Mahakama ya
Kimatafa kujibu Makosa ya Jinai. Mazungumzo hayo yalifanyika katika ukumbi wa
mikutano wa Wizara ya Mambo ya Nje, jijini Dar es Salaam.
Waziri Membe alikuwa akielezea yaliyojiri kwenye
Kikao cha dharura cha Viongozi Wakuu wa Nchi za Umoja wa Afrika (UA)
kilichomalizika mjini Addis Ababa, nchini Ethiopia jana tarehe 12 Oktoba,
2013. Kikao hicho kilihudhuriwa pia na
Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.
Mfalme Mswati wa III, Rais wa Swaziland, na Viongozi Wakuu na Watendaji Wakuu
wa Serikali barani Afrika.
Kikao hicho kiliitishwa kutokana na ombi la
Serikali ya Jamhuri ya Kenya ya kutaka UA kujadili mahusiano yaliyopo kati ya
nchi za Afrika na Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) na iwapo ni
sahihi kwa Viongozi Wakuu wa Nchi za Afrika kufikishwa katika Mahakama hiyo
kujibu mashtaka wakati wakiwa madarakani.
“Viongozi hao wa Afrika waliazimia mambo makuu
matano,” alieleza Waziri Membe, huku akiyataja mawili kuwa hakuna Kiongozi
yoyote kutoka barani Afrika atakayepelekwa ICC au Mahakama yoyote kujibu mashtaka
wakati akiwa madarakani hata akiwa anashika nafasi ya kukaimu.
Mengine ni kuwa mashtaka yanayomkabili Kiongozi
yoyote barani Afrika yasubiri hadi Kiongozi huyo atakapomaliza muda wa uongozi
wake. Aidha, Mhe. Waziri alieleza
kusikitishwa kwa Viongozi wa Afrika na namna Mahakama ya ICC inavyoendesha
shughuli zake kwa kile walichokiita “kuwaandama Viongozi wa Bara la Afrika
kuliko Viongozi wa Mataifa mengine hata pale panapokuwa na ushahidi wa Viongozi
hao wengine kufanya makosa ya Jinai.”
Waziri Membe alihoji inakuwaje kwamba kati ya kesi
30 zilizopelekwa ICC tangu mwaka 2004, ishirini na saba (27) zinatoka barani
Afrika. “Haya yote yalijadiliwa kwa
kina, pamoja na pendekezo la kujitoa kwenye uanachama wa Mahakama ya ICC,”
aliongeza Waziri Membe.
Alisema suala la kujitoa uanachama wa ICC
limeachiwa kila nchi kuamua, ingawaje linategemewa kujadiliwa tena katika kikao
cha Mawaziri wa Mambo ya Nje na Mawaziri wa Sheria wa nchi wanachama wa
mahakama hiyo kitakachofanyika tarehe 29 Novemba mwaka huu nchini Uholanzi.
Hivi sasa kuna nchi thelathini na nne (34) barani Afrika ambazo ni wananchama
wa Mahakama hiyo.
Akiendelea kuzungumza katika Mkutano wake wa leo na
waandishi wa habari ambao pia ulihudhuriwa na Uongozi wa Wizara ya Mambo ya Nje
na Ushirikiano wa Kimataifa, Waziri Membe amesema kuwa Umoja wa Afrika
umepeleka ombi lake rasmi kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC)
kuahirisha kesi inayowakabili viongozi hao wa Kenya.
Wakati huo huo, Mhe. Waziri Membe alitumia fursa ya
mkutano wake na waandishi wa habari kutoa salamu za pole kwa Bibi Ufoo Saro,
Mwandishi/Mtangazaji wa kituo cha televisheni ITV, na familia yake, kufuatia
taarifa iliyomfikia kuwa Bibi Saro amelazwa hospitali akiwa mahututi
baada ya kupigwa risasi na kujeruhiwa vibaya. Mama yake mzazi, Anastazia Saro
na mtoto wake waliuwawa katika shambulio hilo.
Taarifa zinasema mtuhumiwa ni
mchumba wa Bibi Saro, ambaye anadaiwa kufyatua risasi kwa familia hiyo
na hatimaye kujipiga risasi na kufa.
Sambamba na taarifa hiyo, Mhe. Waziri Membe pia
aliwatakiwa wananchi sikukuu njema ya Kumbukumbu ya Hayati Baba wa Taifa
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ambayo itaadhimishwa Kitaifa kesho tarehe 14
Novemba 2013.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.