Mhe. Bernard K. Membe (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa akizungumzia ushiriki wa Tanzania katika operesheni
za kulinda amani za Umoja wa Mataifa popote pale duniani.
Waziri Membe akiendelea na mahojiano yake na Mwandishi Fredy Mwanjala wa Kituo cha Televisheni cha Channel Ten ofisini kwake leo, jijini Dar es Salaam.
Waziri Membe akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya mahojiano na mwandishi Fredy Mwanjala (kushoto) na mpiga picha Bi. Fauzia Yusuph (kulia), wote wanatoka Kituo cha Televisheni cha Channel Ten.
Membe: Vifo vya Askari ni chachu kwa Watanzania
Na TAGIE
DAISY MWAKAWAGO
Tanzania itaendelea
kushiriki operesheni za kulinda amani za Umoja wa Mataifa popote pale duniani.
Msimamo huo wa
Tanzania uliwekwa wazi na Mhe. Bernard K. Membe (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa katika mahojiano maalum na Mwandishi Fredy Mwanjala wa
Kituo cha Televisheni cha Channel Ten, yaliyofanyika
leo ofisini kwake jijini Dar es Salaam.
Katika mazungumzo yao
yaliyolenga kutaka kufahamu msimamo wa Tanzania kufuatia vifo vya askari wake
huko Darfur, Sudan na hivi karibuni huko Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia
ya Watu wa Kongo (DRC), Waziri Membe alisema moja ya Sera ya Mambo ya Nje
katika awamu ya nne ya Mhe. Rais Jakaya Mrisho Kikwete ni ulinzi na amani.
Hivyo, Tanzania
itaendelea kushiriki katika operesheni hizo za kulinda amani ambazo zimeiletea
Tanzania heshima kubwa katika medani ya kimataifa.
Waziri Membe alisema
inawezekana kuwa wanajeshi wa Tanzania wanalengwa na kundi la waasi la M23, kwa
kuwa Tanzania ni mwiba mkali kwa kikundi hicho kutokana na umahiri wake
unaofahamika vyema katika nchi za Maziwa Makuu.
“Umwagikaji wa damu Mashariki
mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Kongo (DRC) ni chachu kwa Watanzania dhidi
ya kikundi cha waasi cha M23,” alisema Mhe. Bernard Membe, Waziri wa Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Hivi karibuni mwezi
Agosti, kikosi cha M23 kilishambuliwa na kuteketezwa kwa mujibu wa taarifa za
kiitelijensia zilizoripotiwa na vyombo vya habari. Lakini inasemekana kuwa kuna kundi lingine limezuka
tena hivi karibuni kwa jina hilo hilo la M23 kama vile chem-chem ya maji, alieleza
Waziri Membe.
“Ni muhimu ieleweke
kuwa Tanzania haitosita kamwe kuendelea kuwa mstari wa mbele katika kupambana
na hizi vita za nchi jirani zisizoisha,” alisema Waziri Membe. Aliongeza na kusema kuwa Tanzania imekuwa
kinara cha medali za kimataifa katika kutetea na kulinda amani na usalama wa
nchi yetu na barani Afrika.
“Sisi ni taifa ambalo
liko tayari kujitolea kupigana na kumwaga damu katika kutetea amani na kutatua
migogoro ya majirani zetu,” alisema Waziri Membe. Alieleza kuwa Tanzania imeshiriki kwa namna
moja au nyingine katika vita vya ukombozi wa amani barani Afrika katika nchi za
Msumbiji, Afrika Kusini, Zimbabwe, Comoro, Uganda, Mashariki ya Kongo-DRC na
nchi nyingine nyingi.
Akizungumzia kupoteza
maisha kwa Askari wa Tanzania nchini Kongo-DRC, Waziri Membe alisema kuwa ni msiba
mkubwa wa Kitaifa na wa Umoja wa Mataifa.
Alieleza kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepokea
salamu za rambirambi kutoka Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Umoja wa
Ulaya (EU), Serikali ya Kongo, Serikali ya Angola, Serikali ya Afrika ya Kusini
na nchi nyingine duniani.
Tanzania ni mojawapo
ya nchi zinazounda Brigedi Maalum ya umoja wa mataifa (MONUSCO) kulinda na
kusimamia amani huko Mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Kongo
(DRC). Kuna batalioni moja yenye askari
zaidi ya 1,270 ambao wanaunda sehemu ya Brigedi hiyo Maalum ya MONUSCO.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.