Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon ametuma salam za rambirambi kwa Familia na kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufuatia kifo cha Mlinzi wa Amani Mtanzania ambaye amepoteza maisha siku ya jumapili baada ya kushambuliwa na kundi la waasi la M23 katika eneo la Kiwanja- Rushuru kilimita 25 magharibi ya mji wa Goma. katika shambulio hilo, Mlinzi mwingine ambaye pia ni Mtanzania amejeruhiwa. kumekuwapo na mapigano kati ya Majeshi ya Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (FARDC) na Kundi la M23.
Luteni Rajabu Ahmad Mlima Enzi ya Uhai Wake
Na Mwandishi Maalum
Kwa mara nyingine Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, amelaani vikali tukio la kuuawa kwa mwanajeshi wa kitanzania aliyekuwa akihudumu katika Misheni ya Umoja wa Mataifa ya Kutuliza Amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (MONUSCO).
Kifo cha mwanajeshi huyo mtanzania kimetokea jana jumapili baada ya kushambuliwa na kundi la M23 ambalo linapigana na majeshi ya Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya KONGO ( FARDC).
Katika salamu zake rambirambi kwa familia ya marehemu na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa, ameelaani vikali mauaji hayo na kuahidi kwamba Umoja wa Mataifa utaendelea kutekeleza majukumu yake ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua zote muhimu kuwalinda raia wa DRC.
“Ninalaani vikali mauaji ya mlinda amani kutoka Tanzania ambaye alishambuliwa na kundi la M23 katika eneo la Mashariki ya DRC, ninatoa salamu zangu za rambirambi kwa familia ya marehemu, na kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ” ananukuliwa Katibu Mkuu akisema.
Kwa mujibu wa taarifa zilizoufikia Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, siku ya jumapili , zinaeleza kwamba Mlinzi huyo wa amani aliyepoteza maisha na ambaye jina lake linahifadhiwa kwa sasa anacheo cha Luteni na kwamba alishambuliwa wakati kikosi chake kikiwa katika harakati za kutoa ulinzi wa raia katika eneo la Kiwanja- Rutushura kilomita 25 kutoka Magharibi mwa mji wa Goma.
Katika mashambuli hayo mlinzi mwingine wa amani ambaye pia ni mtanzania amejeruhiwa.
Aidha taarifa iliyotolewa na msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, inaeleza kwamba Umoja wa Mataifa utachukua hatua zote muhimu kwa mujibu wa Azimio namba 2098 ( 2013 ) kutimiza wajibu wake .
Ni kupitia Azimio hilo ambalo lilipitishwa mwezi Marchi mwaka huu, Baraza Kuu la Usalama liliridhia kuanzishwa kwa Brigedi Maalum ( FIB) ambayo pamoja na mambo mengine imepewa jukumu la kutumia nguvu pale inapobidi ikiwa ni pamoja na kuwapokonya silaha makundi ya wanagambo wenye silaha likiwamo kundi hilo la M23 na makundi mengine ambayo yamekuwa yakiendesha mapigano na machafuko katika DRC.
Mapigano yanayoendelea hivi sasa kati ya majeshi ya serikali ya Kongo na kundi la M23 yamefuatia kuvunjia hivi karibuni kwa mazungumzo ya Kampla yaliyokuwa yakiendelea kati ya pande mbili. Hali inayolifanya eneo hilo la Mashariki ya Kongo kuzidi kuwa tete.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.