Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb) amesisitiza umuhimu wa Tanzania kuridhia uraia wa nchi mbili ili Watanzania wanaoishi ughaibuni waweze kufaidika na fursa za kiuchumi na kijamii zinazotolewa kwa raia katika nchi wanazoishi.
Mhe. Waziri alitoa kauli hiyo katika ufunguzi wa kongamano lililoandaliwa na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) na kufanyika katika Hoteli ya JB Belmont jijini Dar es Salaam tarehe 22 Januari, 2014. Kongamano hilo ambalo linawakutanisha wawakilishi kutoka Serikalini, wanazuoni, asasi za kiraia na watafiti mashuhuri lina lengo la kujadili njia mbalimbali ambazo wanadiaspora wanaweza kuzitumia kuchangia maendeleo ya nchi yao kwa mazingira ya Tanzania.
Mhe. Waziri aliwambia wajumbe wa kongamano hilo kuwa hoja ya uraia wa nchi mbili itawasilishwa na kutetewa katika Kikao Maalum cha Bunge la Katiba ambacho kinatarajiwa kufanyika katika siku za karibuni. “Endapo uraia wa nchi mbili utaridhiwa, Watanzania wanaoishi ughaibuni wataweza kupata kazi nzuri na kukopa benki katika nchi wanazoishi, hivyo kipato chao kitaongezeka ambacho watakitumia pia kuwekeza nyumbani. Mhe. Waziri alisikika akisema.
Mhe. Membe alitolea mfano wa nchi zilizoweka mazingira mazuri ya wanadiaspora katika kuchangia maendeleo ya nchi zao kuwa ni pamoja na Nigeria, Ghana na Kenya.
Awali, akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo, Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Uhamiaji hapa nchini Bw. Damien Thuriaux alisema kuwa, kongamano hilo ambalo litafanyika kuanzia tarehe 22 hadi 29 Januari 2014 lina lenga kuhamasisha uratibu wa masuala ya Uhamiaji na Diapora kwa kuzishirikisha Wizara na Taasisi mbalimbali. Aidha katika kushirikiana na Serikali ya Tanzania, Bw. Damien alisema kuwa Shirika lake litasaidia uundwaji wa Tovuti maalum kwa ajili ya watu waishio Nje (Diaspora) na masuala mengine yanayohusu uhamiaji.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.