Bw. Bujiku Sakila, Afisa Mambo ya Nje akimweleza jambo Bi. Zuleikha Tambwe, Afisa Mambo ya Nje mara baada ya ufunguzi wa Mkutano wa Baraza la Mawaziri.
Na Rosemary Malale, Addis Ababa
Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU) imetoa rai kwa nchi za Afrika kuongeza uzalishaji na uwekezaji katika kilimo kwa vile kinachangia kwa kiasi kikubwa Pato la Taifa kwa nchi Barani Afrika.
Rai hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Dkt. Nkosazana Dlamini-Zuma wakati akifungua Mkutano wa 24 wa Baraza la Mawaziri wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) ulioanza leo tarehe 27 Januari, 2014 Mjini Addis Ababa, Ethiopia.
Dkt. Dlamini-Zuma alisema kuwa, kwa Afrika kuhakikisha ukuaji wa pato la taifa kwa asilimia 7 na zaidi ni vema kilimo kiwe kipaumbele kwa nchi wanachama, kwa vile kinachangia kwa kiasi kikubwa pato la Taifa kwa nchi zao. Alisema kuwa kwa mwaka huu wa 2014 ni muhimu kuongeza uwekezaji katika kilimo, uzalishaji, kuboresha miundombinu na ujuzi ikiwa ni pamoja na kuwekeza katika tafiti za kilimo.
Alisisitiza kuwa Kamisheni yake kwa mwaka huu imejipanga kuchukua hatua madhubuti katika kuboresha kilimo ikiwa ni pamoja na kuwawezesha wanawake ambao ndio kundi kubwa linaloshughulika na kilimo na chakula kwa kuwapatia mafunzo, mitaji na kuwasaidia kuanzisha vikundi vya ushirika na masoko kwa bidhaa za kilimo. Pia, alieleza kuwa imefika wakati sasa kwa Afrika kuwa na kauli katika kupanga bei ya mazao na bidhaa zitokanazo na kilimo.
Aidha aliongeza kuwa, ili kufikia malengo hayo, Kamisheni ya Umoja wa Afrika itashirikiana na Taasisi nyingine za Kimataifa kama UNECA, Benki ya Maendeleo ya Afrika, Nchi Wanachama, Vyama vya Kiraia na Jumuiya za Kikanda za Kiuchumi.
Dkt. Dlamini-Zuma alieleza kuwa Mkutano wa mwaka huu wenye kaulimbiu isemayo “Mwaka 2014 ni mwaka wa Kilimo na Usalama wa Chakula; Kuadhimisha miaka 10 ya Mpango wa Maendeleo ya Kilimo Afrika (CAADP)” unalenga kuweka mikakati madhubuti katika kuhakikisha kilimo kinakuwa ni mkombozi wa Watu Barani Afrika kiuchumi na kwa usalama wa chakula.
Katika hatua nyingine, Dkt. Dlamini-Zuma ametoa wito kwa Waafrika wote kutoa michango na mawazo yao kuhusu Muundo wa Agenda 2063 ambayo inalenga katika kujenga Afrika Tunayoitaka katika kipindi cha miaka 50 ijayo kuanzia mwaka 2014.
Aidha, aligusia migogoro inayoendelea kusumbua baadhi ya nchi za Afrika kama vile Sudan Kusini na Jamhuri ya Afrika ya Kati ambapo alisema kuwa Umoja wa Afrika, Jumuiya za Kikanda za Kiuchumi na Jumuiya ya Kimataifa zitaendelea kushirikiana ili kuzisaidia nchi hizi kupata suluhisho la kudumu katika migogoro yao.
“Mwezi Mei mwaka uliopita wakati wa kuadhimisha miaka 50 ya Umoja wa Afrika tuliahidi kwa watu wetu kuwa hatutavirithisha vizazi vijavyo vita na migogoro bali tuliapa kufanya kazi bila kuchoka kuhakikisha migogogro Barani humu inamalizwa kabisa hadi kufikia mwaka 2020” alisema Dkt. Dlamini Zuma. Vile vile, Dkt. Dlamini-Zuma alizipongeza nchi za Mali, Madagascar na Somalia kwa hatua waliyofikia katika kushughulikia migogoro yao.
Mkutano wa Baraza la Mawaziri ambao utamalizika tarehe 28 Januari, 2014 ni matayarisho ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika ambao utafanyika mjini hapa tarehe 30 na 31 Januari, 2014. Ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa Baraza la Mawaziri unaongozwa na Mhe. Bernard K. Membe (Mb.), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
-mwisho-
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.