Mhe. Salum, kulia akitoa neno baada ya shughuli za kusaini Mkataba kukamilika. Anayemsikiliza ni Waziri wa Biashara na Viwanda wa Malawi, Mhe. Gwengwe. |
Maafisa wa Tanzania na Malawi wakifanya maandalizi kabla ya Mawaziri kuwasili kwa ajili ya shughuli ya uwekaji saini Mkataba |
Maneno aliyosema Waziri wa Fedha baada ya uwekaji saini
Na Ally Kondo. Lilongwe
Nchi za Afrika zimehimizwa kufanya biashara baina yao ili
kujiletea maendeleo, badala ya kusubiri misaada isiyokuwa na uhakika kutoka
nchi wahisani. Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa Fedha, Mhe. Saada Salum (Mb)
wakati wa hafla ya uwekaji saini Mkataba wa kuanzisha Kituo cha Pamoja cha
Uhamiaji na Ushuru wa Forodha cha Songwe – Kasumulu kati ya Serikali ya
Tanzania na Serikali ya Malawi.
Uwekaji saini huo
ulifanyika Lilongwe, Malawi siku ya Jumatatu tarehe 10 Machi, 2014 ambapo Mhe
Salum aliwela saini kwa niaba ya Serikali ya Tanzania, wakati Waziri wa
Biashara na Viwanda, Mhe. Sosten Gwengwe
aliweka saini kwa niaba ya Serikali ya Malawi.
Mhe. Salum alieleza kuwa kuanzishwa kwa kituo hicho,
kutasaidia, sio tu kupunguza gharama za kufanya biashara kati ya Tanzania na
Malawi bali pia kutaimarisha uhusiano baina ya watu wa nchi hizi mbili ambao
kimsingi wana utamaduni unaofanana.
Mhe. Waziri aliwataka wataalamu wa pande zote mbili kuandaa
mpango kazi wa kutekeleza Mkataba huo haraka iwezekanavyo ili wananchi na
Serikali waone matunda yake badala ya kuishia katika makaratasi.
Alipoulizwa na wanahabari kutoa maoni kuhusu utekelezaji wa
Mkataba huo, Mhe Wazri aliwahakikishia wananchi wa Malawi na Tanzania kwa
ujumla kuwa kituo hicho kitafanya kazi kama ilivyokusudiwa na hakuna tishio
lolote la kuvurugika kwa uhusiano kati ya nchi hizi mbili.
Kwa upande wake, Mhe. Gwengwe alifarijika na uanzishwaji wa
kituo hicho, kwa kuwa kitarahisisha usafirishaji wa bidhaa kwa haraka kutoka
Tanzania kuingia Malawi ambayo haina Bandari.
Uwekaji saini wa Mkataba huo umeenda sambamba na mkutano wa
Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC)
ambapo Mhe. Salum anaongoza ujumbe wa Tanzania. Mkutano huo ulioanza na vikao
vya Makatibu Wakuu unatarajiwa kukamilika tarehe 11 Machi, 2014.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.