Mhe. Bernard Membe, Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania kwenye mazungumzo na Mabalozi wa Nchi za Kiafrika Wanachama wa Jumuiya ya Madola Jijini London, Uingereza. |
Mhe. Bernard Membe (Mb.),
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ametoa wito kwa Nchi za
Kiafrika Wanachama wa Jumuiya ya Madola kuunganisha nguvu na kuwa na sauti moja
itakayotetea maslahi ya nchi za kiafrika kwenye jumuiya hiyo.
Mhe. Membe aliyasema hayo
alipokutana na Mabalozi wa Nchi 12 za Kiafrika wanaowakilisha nchi zao kwenye
Jumuiya ya Madola pembezoni mwa Mkutano wa Kikosi Kazi cha Mawaziri cha jumuiya
hiyo kilichofanyika Jijini London Uingereza tarehe 13-14 Machi 2014.
Kwenye mazungumzo yao Mhe.
Membe aliwakumbusha Mabalozi hao chimbuko la jumuiya hiyo na ushiriki wa nchi
za kiafrika ili kutetea maslahi ya Waafrika na hatimaye kuvuna matunda ya
ushiriki wa Waafrika kwenye Jumuiya ya Madola.
“Kama wanachama kutoka Bara
la Afrika, ni wajibu wetu kushikamana na hata pale mwanachama mmoja anapotolewa
au anapowekewa vikwazo vya ushiriki, tuungane na kuhakikisha mwanachama huyo
anaondolewa vikwazo na hatimaye kurudi kwenye jumuiya. Tusipofanya hivyo hata
sisi tutakuwa na tatizo” alisema Mhe. Membe.
Aliwaasa kuwa na sauti moja
katika kutetea haki za ushiriki wa nchi za Kiafrika ndani ya jumuiya hiyo.
Alisema namba ya nchi za Afrika kwenye jumuiya hiyo ni kubwa na hivyo ushiriki
wa Waafrika lazima uwe wa kushindo.
Alisisitiza kuwa na sauti
moja ya Waafrika kutakemea masuala yanayokuja kama shinikizo kutoka wanachama
wa Nchi za Magharibi kama vile ndoa za jinsia moja, ambayo yanagusa dini,
tamaduni, mila na desturi za Kiafrika. Alisema upepo wa shinikizo hilo unavuma
kwa kasi kana kwamba kukubaliana na masuala hayo kutaondoa umaskini barani
Afrika. Nchi za Kiafrika kwenye Jumuiya hiyo zina wajibu wa kushiriki
kikamilifu kwa kusimamia agenda zitakazoleta maendeleo barani Afrika.
Ili kufanikisha wajibu huo,
Mhe. Membe aliwahimiza Mabalozi hao kushiriki kwenye chaguzi mbalimbali za jumuiya, kutoa
taarifa kwa Wakuu wa Nchi na Serikali zao kutoka Makao Makuu ya Sekretarieti ya
Jumuiya hiyo yaliyopo London Uingereza na mwisho kuhakikisha wanashiriki
kikamilifu na kutoa sauti ya pamoja kwenye shuguli mbalimbali za Jumuiya badala
ya kusubiri wengine wafanye maamuzi kwa niaba yao.
Kwa upande wao, mabalozi
hao walimpongeza Mhe. Membe kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kikosi Kazi cha
Mawaziri cha jumuiya hiyo kwa kipindi cha miaka miwili. Aidha walisifu jitihada
za Tanzania kutetea maslahi ya nchi za Kiafrika wanachama wa jumuiya hiyo.
Kwa upande mwingine walilalamikia
uongozi wa Sekretarieti ya Jumuiya ya Madola kwa kutoshirikiana na mabalozi hao
hususan kwenye maandalizi ya Vikao vya Wakuu wa Nchi na Serikali wanachama au
baada ya vikao hivyo. Waliongeza kuwa kero za kiutendaji zinafanyiwa kazi juu
juu tu na badala yake zinazua kero kubwa zaidi. Hivyo walimuomba Mhe. Membe kuwasaidia
kwa kupitia Vikao vya Kikosi Kazi cha Mawaziri kuondoa changamoto hizo.
Ndani ya Jumuiya ya Madola
kuna nchi za Kiafrika 18 ambapo 12 kati ya hizo zilizoshiriki kwenye mkutano
huo ni; Mauritius, Cameroon, Seychelles, Namibia, South Africa, Uganda, Kenya,
Mozambique, Ghana, Lesotho, Zambia na Tanzania. Jumuiya ya Madola ina jumla ya
nchi 53.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya
Serikali kwa Umma
Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.