Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) atapokea
tuzo ya Africa’s Most Impactful Leader of the Year kwa niaba ya Mhe.
Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamahuri ya Muungano wa Tanzania mjini
Washington D.C, Marekani tarehe 09 Aprili, 2014.
Tuzo hiyo
ambayo hutolewa kila mwaka na Taasisi ya Uchapishaji ya African Leadership Magazine yenye makazi yake nchini Marekani kwa
viongozi wa Afrika wanaofikia vigezo vilivyowekwa na Taasisi hiyo ikiwa ni
pamoja na kuzingatia utawala bora, demokrasia na kuheshimu haki za binadamu kwa
Mwaka 2013 inatolewa kwa Mhe. Rais Kikwete.
Kwa mujibu wa
Taasisi ya African Leadership Magazine,
Tuzo hiyo inatolewa kwa Mhe. Rais Kikwete kutokana na namna ya pekee ya uongozi
wake wenye matokeo yanayopimika kiutawala bora hususan kwa mwananchi wa kawaida
wa Tanzania. Aidha, uongozi wake umeiletea Tanzania heshima kubwa kimataifa na
kuiweka Tanzania kama chaguo muhimu kwa wawekezaji kutokana na ukuaji uchumi na
maboresho ya sera.
Tuzo hiyo
tayari imewahi kutolewa kwa Marais na Viongozi wengine mbalimbali wa Afrika
wakiwemo Mhe. Ellen Johnson Sirleaf, Rais wa Liberia, Mhe. James Michel, Rais
wa Shelisheli na Rais Mstaafu wa Ghana, Mhe. John Kuffor.
Ujumbe wa Mhe.
Membe utamhusisha Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Bw. Salvatory Rweyemamu,
Waandishi wa Habari na Maafisa wa Serikali. Mhe. Membe atarejea nchini tarehe
11 Aprili, 2014.
Imetolewa
na: KITENGO CHA MAWASILIANO YA SERIKALI, WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO
WA KIMATAIFA, DAR ES SALAAM.
8
APRILI, 2014
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.