Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) |
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Serikali ya Uingereza
imemwalika Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K.
Membe (Mb.) kuhudhuria Mkutano wa Kimataifa kuhusu Ukomeshwaji wa Udhalilishaji
wa Kijinsia kwenye Maeneo yenye Migogoro (“End Sexual Violence in Conflict”) utakaofanyika
mjini London, Uingereza kuanzia tarehe 10 hadi13 Juni, 2014.
Mwaliko huo unakuja
kufuatia mchango mkubwa wa Tanzania katika kufanikisha kuwepo kwa Tamko la
Umoja wa Mataifa linalohusu suala hilo (Declaration of Commitment to End Sexual
Violence in Conflict).Vile vile itakumbukwa kuwa, Tanzania imekuwa mstari wa
mbele katika kuchangia vikosi vya kulinda amani katika maeneo yenye migogoro
Barani Afrika ambayo pia yana wahanga wengi wa udhalilishwaji wa kijinsia.
Pamoja na masuala
mengine, Mkutano huo utajadili hatua za kuchukua ili kumaliza tatizo la
udhalilishaji wa kijinsia katika maeneo yenye migogoro; mchango au nafasi ya
vijana katika kupambana na udhalilishaji wa kijinsia katika maeneo yenye migogoro;
kiwango cha udhalilishaji wa kijinsia unatokea katika maeneo yenye migogoro na
kuweka makubaliano ya kimataifa ya namna ya kutekeleza mikakati iliyomo katika maazimio ya G8 na
Umoja wa Mataifa; na kusikia matatizo na athari za udhalilishaji wa kijinsia
katika migogoro moja kwa moja kutoka kwa Wahanga.
Pia washiriki watajadili
changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na udhaifu unaotokana na kutoadhibiwa kwa
wanaofanya vitendo hivyo.
Mkutano huo
utazikutanisha nchi zilizoathiriwa na migogoro, nchi wahisani, Umoja wa
Mataifa, Asasi zisizo za Kiserikali, Mashirika ya Kimataifa na Taasisi za
Kijamii na wadau wengine.
Aidha, wakati wa
ziara hiyo, Mhe. Membe atakutana kwa mazungumzo na Waziri wa Uingereza
anayeshughulikia masuala ya Afrika, Mhe. Mark Simmonds. Miongoni mwa masuala
watakayozungumza ni kuimarisha ushirikiano baina ya Tanzania na Uingereza.
IMETOLEWA
NA: WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA, DAR ES SALAAM
10
JUNI, 2014
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.