Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Iran Dkt. Asghar Fashad akizungumza.
===========================================
Mhe. Omar Mjenga, Balozi Mdogo wa
Tanzania- Dubai, leo amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa
Hospitali ya Iran ya Dubai, Dr. Asghar Fashad. Katika mazungumzo, Mhe. Mjenga
alimuomba Dr asghar kuangalia uwezekano wa kuwa na makubaliano kati ya
hospitali yake na Ubalozi Mdogo kwa ajili ya kutoa huduma za afya kwa
Watanzania kwa gharama nafuu ukilinganisha na gharama zake za sasa.
Baada ya mazungumzo na mashauriano ya
muda wa saa moja, Uongozi wa Juu wa Hospitali, ulikubali ombi la Mhe. Mjenga la
kupunguza gharama za matibabu kwa Watanzania kwa asilimia 40 (40%). Mwanzo,
Uongozi ulipendekeza asilimia 20, ambayo Mhe. Mjenga aliwaeleza kuwa bado
ilikuwa ni punguzo dogo na bado ingekuwa ni mzigo mkubwa kwa Watanzania.
Hatmaye, ndio maafikiano hayo yakafikiwa ya asilimia 40.
Mpango wa huu utajumuisha Watanzania
wote waishiyo UAE na wale wanaoishi nje ya UAE ikiwa ni pamoja na wale
wanaoishi Tanzania. Hospital ya Irani ni moja ya hospitali zenye huduma za hali
ya juu kwa hapa Dubai na UAE kwa ujumla.
Uongozi wa Hospitali umekubali kuanza
kutoa Vitambulisho Maalum kwa ajili ya Watanzania wote kuanzia Jumapili tarehe
1 Septemba. Mkataba wa Makubaliano haya utatiwa saini Jumatatu tarehe 2
Septemba.
Aidha, Mhe. Mjenga, amemuomba
Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali hii, kuangalia uwezekano wa kujenga Hospitali
kubwa yenye hadhi kama hii, nchini Tanzania. Kimsingi, Mkurugenzi Mkuu
amekubali ombi hili, na ameahidi kumuomba Rais wa Hospitali kufanya ziara
nchini Tanzania mwezi ujao ili kuona na uongozi husika na kuanza mazungumzo ya
kuanzisha Hospitali kama hiyo. Ameeleza kuwa Tanzania na Iran na nchi marafiki
wa siku nyingi, na hivyo Iran inafarijika sana kuwa karibu na Tanzania
kimahusiano.
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.