Na Ally Kondo, Addis Ababa
Wakuu wa Nchi za Afrika wamekumbushwa kuwa, Mwaka 2015 umeingia lakini Bara la Afrika bado linakabiliwa na changamoto nyingi ambazo kama hazitapatiwa ufumbuzi ustawi wa bara hilo utaendelea kudumaa. Kauli hiyo ilikuwa inarudiwa mara kwa mara na viongozi waliopata fursa ya kuhutubia wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika jijini Addis Ababa siku ya Ijumaa tarehe 30 Januari 2015.
Changamoto hizo ni pamoja na mabadiliko ya tabianchi, ugaidi, migogoro ya kutumia silaha, ukatili wa kutisha, biashara haramu ya binadamu, umasikini na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola. Walishauri katika mwaka wa 2015 lazima matatizo hayo yajadiliwe kwa kina kwa madhumuni ya kuyatafutia ufumbuzi wa kudumu.
Alipokuwa anahutubia mkutano huo, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Mhe. Nkosazana Zuma alisema kuwa, licha ya changamoto hizo, Bara la Afrika linapiga hatua kimaendeleo na kwamba Agenda 2063 inayowasilishwa katika Mkutano huo inatoa wito kwa Serikali na sekta nyingine kushirikiana kwa pamoja ili kukuza uchumi kwa kuweka mkazo kwenye ubunifu katika sekta ya kilimo, usindikaji wa mazao na ujenzi wa miundombinu.
Mhe. Zuma alisisitiza umuhimu wa kutumia fedha za ndani kwa ajili ya kugharamia miradi ya kipaumbele ambayo imezingatiwa katika Mpango wa Maendeleo wa Miaka 10 ambao nao utawasilishwa katika mkutano huo. Alieleza kuwa Sekretarieti imefanyia kazi pendekezo la kutafuta vyanzo mbdala vya fedha ambapo Mawaziri wa Fedha walijadili na ripoti yao itawasilishwa wakati wa mkutano huo. Umoja wa Afrika pia umeanzisha Mfuko Maalum utakaozinduliwa wakati wa mkutano huo kwa ajili ya kuhifadhi fedha hizo.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mhe. Ban Ki-moon alieleza kuwa mwaka 2014, AU na UN zilishirikiana kutafuta amani katika nchi zenye migogoro. Alisema mafanikio makubwa yalipatikana na hivyo kusisitiza kuwa pande zilizosaini mikataba ya amani lazima zitekeleze vipengele vya mikataba hiyo. Alitoa mfano wa Mkataba wa Arusha na kusema kuwa pande zinazohusika zitekeleze makubaliano ya kugawana madaraka. Aidha, alisisitiza umuhimu wa kukitokomeza kikundi cha waasi cha FDLR kinachoendesha uasi wake Mashariki mwa DRC.
Mhe. Ban Ki-moon pia aliwakemea viongozi wa Afrika wanaong’ang’ania madaraka. Aliwashauri viongozi hao waache tabia hiyo na kuruhusu demokrasia ichukue mkondo wake.
Rais wa Kikao cha 69 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda, Mhe. Sam Kutesa pamoja na mambo mengine, alizungumzia mabadiliko ya mfumo katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Alisema katika uongozi wake atafanya jitihada kuhakikisha kuwa mfumo wa Baraza hilo, chombo ambacho alikitaja kama kisichokuwa na demokrasia kuliko vyombo vyote duniani unafanyiwa mabadiliko.
Viongozi hao pia walihimiza juhudi za kutafuta tiba na chanjo ya ugonjwa wa Ebola na kusisitiza kuwa kampeni ifanywe ili nchi zilizoathirika na ugonjwa huo zisamehewe madeni.