Rais wa Baraza Kuu la Makanisa ya Sabato Duniani, Askofu Wilson akimpongeza Waziri Membe mara baada ya kumaliza kuwahutubia Waumini wa kanisa hilo waliokusanyika Uwanja wa Taifa kwa ajili ya Kongamano la Kimataifa lilililofikia kilele leo. |
Waumini wakishangilia na kufurahia hotuba nzuri iliyotolewa na Waziri Membe |
Kikundi cha watoto kikitoa burudani katika maadhimisho hayo. |
Waziri Membe akizungumza na Askofu Wilson kabla ya kuhutubia |
Mazungumzo yakiendelea |
Waziri Membe (Katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Askofu wilson na Mkewe (wapili kutoka kushoto), na wa pili kutoka kulia ni Mchungaji Blasius Luguri na mkewe.
Waziri Membe atoa rai kwa madhehebu kuombea uadilifu kwa viongozi
Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard Membe ametoa rai kwa waumini wa Kanisa
la Waadiventista Wasabato nchini kushiriki kikamilifu katika kutengeneza
viongozi bora wa Serikali wanaozingatia misingi ya uadilifu, upendo na unyenyekevu.
Waziri Membe ameyasema hayo wakati
akitoa hotuba ya kufunga Kongamano la Kimataifa la Utume la Kanisa la
Waadventista Wasabato lililofanyika katika Uwanja wa Taifa, Jijini Dar es
Salaam tarehe 07 Februari, 2015.
Mhe. Membe alisema kuwa Dini na
madhehebu yanayo nafasi kubwa katika kujenga jamii yenye maadili na hofu ya Mungu
wakiwemo viongozi na hivyo kupelekea taifa kuwa na amani, upendo na mshikamano.
Alieleza kuwa kama Waziri wa Mambo ya Nje, amejifunza kuwa diplomasia na hofu
ya Mungu vikifanya kazi pamoja hakuna changamoto yoyote isiyoweza kukabiliwa.
“Dini na Diplomasia vina husiana
pale masuala ya amani, ulinzi na usalama yanapoguswa. Hivyo nawaomba mshiriki
katika kutengeneza viongozi bora katika jamii zetu kwa misingi ya uadilifu
ambao watasimamia amani na kujiepusha na vitendo viovu ikiwemo rushwa,” alisema
Mhe. Membe.
Aidha, alilipongeza Kanisa hilo
kwa kuwa mfano mzuri wa ustahimilivu na uvumilivu wa kidini hapa nchini. Alieleza
kwamba kamwe hajawahi kusikia Kanisa la Waadiventista Wasabato limeingia katika
mgogoro na Serikali, dhehebu au dini nyingine na hilo ni funzo kubwa kwa
Watanzania, kwamba kutofautiana kiitikadi, kidini, kikabila au rangi si sababu
tosha ya kuwagombanisha na kuvuruga amani ya nchi.
“Nalipongeza Kanisa lenu kwa kuwa
mfano mzuri wa uvumilivu wa kidini na imani, mnaendesha mambo yenu kwa
uvumilivu mkubwa na kushirikiana na dini
zote na hili linatufundisha kuwa kutofautiana kwetu sio sababu tosha ya kugombana”
alisisitiza Membe.
Pia, Mhe. Membe alilihakikishia
Kanisa hilo dhamira ya Serikali ya kuendelea kushirikiana nalo kwa ajili ya
ustawi wa nchi na kufafanua kuwa Serikali itaendelea kulinda uhuru wa kuabudu
kwa dini zote kama inavyoelezwa kwenye Katiba ya nchi. “Serikali inao wajibu wa
kusaidia dini na madhehebu kufanyakazi
kwa uhuru. Bahati nzuri Katiba inayopendekezwa imezingatia kulinda uhuru
huo hivyo tuiunge mkono” alifafanua Waziri Membe.
Vilevile alilisifu Kanisa hilo kwa
kuanzisha miradi ya huduma zikiwemo Shule15 za Sekondari na Msingi, Chuo Kikuu
na Hospitali mbili ambavyo vinatoa mchango mkubwa kwa Serikali na Wananchi kwa
ujumla.
Awali akimkaribisha Waziri Membe
kufunga Kongamano hilo, Rais wa Baraza Kuu la Makanisa ya Sabato Duniani,
Askofu Ted Wilson alisema kuwa anawaombea
Viongozi wa Tanzania waendelee kuwa na maono kwa ajili ya kuwatumikia
wananchi na kwamba wakimtumaini Mungu
atawawezesha kupata maono mapya kwa ajili ya kulitumikia Taifa hili.
Kwa upande wake, Mwenyeji wa
Mkutano huo, Mchungaji Blasius Luguri aliipongeza Tanzania kwa kudumisha amani ambayo
imepelekea Tanzania kuchaguliwa kuwa mwenyeji wa Kongamano hilo ulioyashirikisha
Mataifa zaidi ya 20. Aidha, alimwomba Mhe. Membe kufikisha ujumbe kwa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa wana imani na Tanzania kuwa ni nchi ya
amani, usalama na utulivu.
Kanisa la Sabato ni Kanisa
linalokua duniani likiwa na Waumini milioni 307 huku Waumini milioni 30 wakiwa
Afrika na takriban milioni 5 wakiwa Tanzania.
-Mwisho-
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.