Saturday, May 16, 2015

Rais wa Msumbiji kufanya ziara ya kitaifa nchini


Rais wa Msumbiji, Mhe. Filipe Nyusi 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Msumbiji, Mhe. Filipe Jacinto Nyusi anatarajiwa kuwasili nchini tarehe 17 Mei, 2015 kwa ziara ya Kitaifa ya siku tatu nchini kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete.

Mhe. Rais Nyussi atapokelewa na mwenyeji wake Mhe. Rais Kikwete mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere. Mhe. Rais Nyusi atakagua Gwaride la Heshima na kupigiwa mizinga 21.

Baada ya mapokezi hayo, Mhe. Nyusi atafanya mazungumzo ya faragha na Rais Kikwete yakifuatiwa na mazungumzo ya kuimarisha ushirikiano baina ya Tanzania na Msumbiji.

Baadaye siku hiyo ya Mei 17, Mhe. Rais Nyusi atakutana kwa mazungumzo na Mabalozi kutoka Nchi za Afrika waliopo hapa nchini mkutano utakaofanyika katika Hoteli ya Hyatt Regency, Jijini Dar es Salaam na kushiriki Dhifa ya Kitaifa itakayoandaliwa na mwenyeji wake Mhe. Rais Kikwete, Ikulu.

Mhe. Rais Nyusi ambaye ataongozana na Viongozi Waandamizi kutoka Serikali ya Msumbiji atahutubia Kongamano la Biashara litakalowakutanisha Wafanyabiashara wa nchi hizi mbili ambalo litafanyika tarehe 18 Mei, 2015 kwenye Hoteli ya Hyatt Regency Jijini Dar es Salaam.

Aidha, siku hiyo ya tarehe 18 Mei, Mhe. Nyusi atapata fursa ya kukitembelea Chuo cha Diplomasia kinachotambulika kama “Tanzania-Mozambique Centre for Foreign Relations” kilichopo Kurasini ambacho kilianzishwa mwaka 1978 kama mradi wa ubia ili kuendeleza mahusiano ya kindugu ya muda mrefu kwa lengo la kutoa mafunzo ya diplomasia na masuala ya kimataifa kwa manufaa ya wananchi wa nchi hizi mbili.

Mhe. Nyusi atakutana na Raia wa Msumbiji waishio hapa nchini kabla ya kuelekea Zanzibar ambako atafanya mazungumzo rasmi na Mhe. Dkt. Ali Mohammed Shein, Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na pia kuzungumza na raia wa Msumbiji waliopo Zanzibar.

Akiendelea na ziara yake hapa nchini, Mhe. Rais Nyusi ataondoka Zanzibar tarehe 19 Mei, 2015 kuelekea Dodoma. Akiwa Mkoani humo atatembelea Makao Makuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na kuzungumza na Mwenyekiti wa CCM, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Aidha, Mhe. Rais Nyusi atalihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na baadaye kutembelea Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).

Mhe. Rais Nyusi anatarajiwa kumaliza ziara yake hapa nchini tarehe 19 Mei, 2015 na kuondokea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kurejea Msumbiji.


Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali kwa Umma,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Dar es Salaam.
16 Mei, 2015



No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.