Picha na Reginald Philip.
==============================
Waziri
Membe aongoza Mkutano wa Dharura wa Baraza la Mawaziri wa EAC
Mkutano wa Dharura wa
Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) umefanyika leo Jijini
Dar es Salaam kwa ajili ya kuandaa agenda za Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi
wa Jumuiya hiyo utakaofanyika tarehe 13 Mei, 2015 kujadili
hali ya usalama nchini Burundi.
Akifungua Mkutano
huo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ambaye pia ni
Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa EAC, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) alisema
kuwa nchi ya Burundi inapita kwenye wakati mgumu wakati ikijiandaa kwa uchaguzi
mkuu utakaofanyika hivi karibuni, hivyo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ameitisha mkutano huo wa dharura
kujadili suala hilo na kutafuta ufumbuzi.
Waziri Membe alieleza
kuwa, hali ya usalama nchini humo kwa sasa si shwari huku kukiwa na mfululizo
wa maandamano ya wananchi na tayari zaidi ya Wakimbizi 50,000 wamekimbilia nchi jirani ikiwemo Tanzania, Rwanda na Uganda.
“Lengo mojawapo la
Jumuiya ya EAC ni kuhakikisha nchi zote wanachama zinakuwa katika hali ya
amani, usalama na utulivu hivyo ni wakati muafaka mkutano huu kufanyika”
alisisitiza Waziri Membe
Mhe. Membe aliongeza
kuwa Mkutano huo ambao umehudhuriwa na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi wanachama
wa EAC yaani Kenya, Rwanda, Burundi na Uganda pamoja na mambo mengine utapokea
na kujadili Taarifa ya Timu ya Watu Mashuhuri (Eminent Persons) walioteuliwa
kufuatilia hali ya usalama nchini Burundi kutoka EAC na Jumuiya ya Soko la
Pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika (COMESA) inayoongozwa na Waziri Mkuu
Mstaafu wa Tanzania, Jaji Joseph Sinde Warioba.
Aidha, Mkutano huo
pia utapokea na kujadili Taarifa ya Mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje
waliotembelea Burundi hivi karibuni kwa ajili ya kupata taarifa za ndani za
hali ilivyo nchini humo; Taarifa ya Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja
wa Mataifa, Eneo la Maziwa Makuu; Taarifa ya Kamishna wa Baraza la Amani na Usalama
la Umoja wa Afrika na Taarifa ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Burundi.
Mkutano wa Wakuu wa
Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki chini ya Uenyekiti wa Rais Kikwete
utafanyika Jijini Dar es Salaam tarehe 13 Mei, 2015 na utahudhuriwa na Marais wan
chi wanachama wa Jumuiya hiyo akiwemo Mhe. Yoweri Kaguta Museveni, Rais wa Uganda,
Mhe. Paul Kagame, Rais wa Rwanda, Mhe. Pierre Nkurunziza, Rais wa Burundi na
Mhe. Uhuru Kenyatta, Rais wa Kenya.
Viongozi wengine walioalikwa
kushiriki Mkutano huo ni pamoja na Rais wa Afrika Kusini, Mhe. Jacob Zuma ambaye
atawakilishwa na Naibu Rais, Mhe. Cyril Ramaphosa, Kamishna wa Umoja wa Afrika,
Mhe. Bibi Nkosazana Dlamini Zuma, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa
Mataifa, Ukanda wa Maziwa Makuu, Bw. Said Djinnit; Katibu Mtendaji wa Sekretarieti
ya Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR), Prof. Ntumba Luaba, Kamishna wa Baraza la
Amani na Usalama la Umoja wa Afrika na Wawakilishi wa Umoja wa Ulaya (EU).
-Mwisho-
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.